Mabaraza ya Kata yamesahaulika

Mhariri

 

Mabaraza ya Kata yameanzishwa kwa mujibu wa Sheria Na. 7/85 lakini halmashauri zinazosimamia mabaraza haya zimeyatelekeza kabisa. Mimi ni Katibu wa Baraza la Kata Kwashemshi. Tangu tuteuliwe mwaka jana hakuna mafunzo yoyote yaliofanyika, kitendo ambacho ni hatari sana. Mabaraza haya yamepunguza sana mlundikano wa kesi katika Mahakama za Mwanzo na Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya. Napenda niishauri Serikali yangu kwamba elimu kwa wajumbe hawa ni muhimu sana, kwani ni sehemu nyingi wajumbe wanalalamika kwamba wametelekezwa. Tatizo hili halipo kwa Baraza la Kata Kwashemshi tu bali mabaraza mengi nchini malalamiko ni haya haya.

Tangu kuteuliwa kwetu mwaka jana hakuna hata vitini vya sheria za Mabaraza ya Kata ambayo tungeletewa na Halmashauri kupata maelekezo ya kazi au kumuita Mwenyekiti wa Baraza Katika Halmashauri kwenda kupewa majukumu yake. Yote haya hayajafanyika Korogwe na kwingineko ambako nimeuliza. Wajumbe hawa wanalalamika sana. Nchi hii ina semina nyingi sana kila kukicha, sasa naomba baadhi ya semina zifutwe ili zielekezwe kwa wajumbe wa Mabaraza ya Kata na Mabaraza ya Vijiji pamoja na wenyeviti wa vitongoji.

 

Hawa ni watu muhimu sana kama Katiba ya nchi inavyosema katika Ibara ya 145. Inasema kutakuwa na vyombo vya Serikali za Mitaa, Mikoa, Wilaya na Kijiji. Ibara ya 146 (1) inasema madhumuni ya kuwapo Serikali za Mitaa ni kupeleka madaraka kwa wananchi na vyombo vya Serikali za Mitaa vitakuwa na haki na mamlaka ya kushiriki na kuwashirikisha wananchi katika mipango yao.

 

Hapa Katiba imefafanua vizuri sana, ndiyo maana ninapendekeza mafunzo haya wapewe wenyeviti wa vijiji na vitongoji pamoja na wajumbe wa Mabaraza ya Kata na Vijiji kwa sababu wananchi tunaosikiliza mashauri yao wanatoka kwenye hivyo vijiji na vitongoji vyao. Unakuta sehemu nyingine za vijiji wenyeviti wanaweza wakagawa ardhi kwa mtu bila kuwapo kwa wajumbe wa Serikali ya Kijiji na Mkutano Mkuu wa Kijiji kama sheria inavyoelekeza. Kwa dosari hii, migogoro ya ardhi imekuwa mingi sana sehemu mbalimbali nchini.

 

Migogoro ya ardhi kwa kiasi kikubwa inasababishwa na viongozi hawa wa kuchaguliwa au maofisa watendaji wanaoamua kugawa ardhi peke yao, bila kufuata sheria inayotaka viongozi wa vijiji washirikishwe. Nazishauri halmashauri zote nchi nzima zisipuuze haya mawazo yangu kwani ni muhimu sana. Mimi ni Katibu wa Baraza la Kata. Ninapopeleka mafaili katika Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya Korogwe ninakutana na makatibu wenzangu wa kata na wilaya mbalimbali. Kilio ni hicho hicho cha kukosa mafunzo elekezi kwa kazi zao. Wilaya hizo ni Korogwe, Lushoto, Handeni na Kilindi.

 

Mussa Kipepe.

Katibu wa Baraza la Kata ya Kwashemshi,

Simu: 0714538960