Serikali imewekeza zaidi ya Sh bilioni 300 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya usafiri ndani ya Ziwa Victoria, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas, amebainisha.

Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 150 zinatumika kwa ajili ya ujenzi wa meli kubwa na chelezo.

Akizungumza baada ya kufanya ziara ya kukagua maendeleo ya miradi mbalimbali inayohusisha Ziwa Victoria, Dk. Abbas amebainisha kuwa meli inayojengwa kwa ajili ya kufanya kazi katika Ziwa Victoria itakuwa kubwa kuliko zote katika eneo la Afrika Mashariki.

“Kununuliwa kwa meli kubwa kwa ajili ya kuhudumia ndani ya Ziwa Victoria ni ahadi iliyodumu kwa muda wa miaka 23, lakini hivi sasa inatekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli,” amesema Dk. Abbas baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa meli hiyo.

Pamoja na ujenzi wa meli na chelezo,  serikali imetoa fedha pia kwa ajili ya ujenzi wa vivuko, ukarabati wa meli zilizopo na ujenzi wa magati katika maeneo mbalimbali kuzunguka ziwa hilo.

Ujenzi wa meli hiyo kubwa itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200 umefikia asilimia 33 na kazi hiyo inatarajiwa kukamilika mwaka 2021.

Aidha, Dk. Abbas alishuhudia ukarabati unaoendelea katika meli ya MV Victoria, ambayo baada ya kukamilika itasaidia kutoa huduma bora za usafiri kwenye ziwa hilo kubwa kuliko yote barani Afrika.

Amesema kuwa hivi karibuni serikali itasaini makubaliano ya utekelezaji  wa miradi  ya ujenzi wa  meli katika Ziwa Tanganyika na uundaji wa meli tatu mpya na za kisasa katika eneo la Ziwa Nyasa.

Alizitaja baadhi ya meli hizo kuwa ni meli mbili za mizigo – MV Ruvuma na meli kubwa ya kisasa ya abiria ya MV Mbeya II. Kazi ya ujenzi wa meli hiyo tayari imeshaanza.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli, Eric Hamis, amesema kuwa ujenzi wa meli hiyo mpya unaendelea vizuri na Septemba 30, mwaka huu vifaa mbalimbali kwa ajili ya ujenzi vilianza kuletwa na sasa kazi ya uunganishwaji wa vyuma imekwisha kuanza.

Ameongeza kuwa ujenzi wa chelezo umefikia asilimia 53 na ifikapo Machi mwakani chelezo kitaanza kutumika kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya.

Aidha, Hamis ameishukuru serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi hiyo miwili ya ujenzi wa meli mpya na ukarabati wa MV Butiama na MV Victoria.

Amesema serikali imekwisha kutoa Sh bilioni 70.8  kati ya Sh bilioni 150 zinazohitajika katika miradi hiyo.

By Jamhuri