Mradi wa uendelezaji viwanja viwili vilivyoko Mtaa wa Ohio (Plot 775/39 na 776/39) vya Shirika la Tija la Taifa (NIP), unaonekana kuwa ni ‘hewa’ kutokana na kutokamilishwa kwa mujibu wa makubaliano ya wabia wawili waliojitokeza kuendeleza viwanja hivyo kwa nyakati tofauti.

Ujenzi wa mradi huo ulilenga kujenga ghorofa 35 ambazo ujenzi wake ungegharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 50 (ambazo ni sawa na Sh bilioni 109.6). Jengo hilo lilitakiwa kukamilika katika kipindi cha miaka mitatu, ambayo imeishia mwaka jana.

Ujenzi wa jengo hilo haujaanza kwa takribani miaka minne, na fedha zimeshatumika kinyume na mkataba. Kiasi cha dola za Marekani 1,116,158.25, ambazo ni sawa na Sh 2,446,618,884 (kwa mujibu wa gharama za ubadilishaji fedha kutoka Benki Kuu) ‘zimeliwa’.

Fedha hizo zilitumika kuanzia Agosti, 2011 mpaka Februari, 2015. Wabia waliojitokeza kwa nyakati tofauti ni pamoja na Kitmeer Real Estate Developers Limited (KRED), ambaye mkataba wake ulivunjwa kutokana na kutofanya chochote katika siku 90 za makubaliano. Alitafutwa mwekezaji mwingine ambaye ni Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambaye pia hajaendelea na ujenzi kutokana na sababu mbalimbali.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo JAMHURI imeziona, barua yenye kumbukumbu Na. TYC/T/200/627/09, iliyoandikwa Septemba 21, 2012, kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, aliwataka Shirika la Tija la Taifa kuzingatia taratibu na sheria za mali za shirika la umma.

“Nia ya Msajili wa Hazina si kutelekeza mashirika yenye uwezo mdogo kumezwa na yale makubwa, hasa ikiwa viwanja vya NIP (Shirika la Tija la Taifa) vipo katika ‘prime area’. Kinachotakiwa ni kuiendeleza NIP iwe 

‘consulting firm’ madhubuti kama Ernst and Young, PwC,” inasomeka sehemu ya barua hiyo.

Katika barua hiyo, Ofisi ya Msajili wa Hazina inaeleza kwamba NIP iangalie uwezekano wa kuviendeleza viwanja hivyo kwa ushirikiano na NSSF ama vinginevyo na NIP iwe mbia mwenye mamlaka (majority shareholder) au equal shareholding (wabia sawia).

Akizungumza na JAMHURI, Mwenyekiti wa Bodi ya NIP, Prof. Samwel Wangwe, anasema kumekuwa na masuala yenye kuhitaji ushauri kutoka taasisi mbalimbali za Serikali, na tayari Bodi yake imeshawasiliana na taasisi hizo.

“Kuna masuala hapa, kwa mfano mwongozo wa ubia wa mashirika ya umma hautakiwi kuwa chini ya asilimia 50. Suala hilo kwenye mkataba wa NIP na NSSF tumelipeleka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuomba ushauri wake. Kuna masuala ya manunuzi, hayo tumewasiliana na Mamlaka ya Ugavi na Ununuzi (PPRA),” anasema Prof. Wangwe.

Prof. Wangwe anasema Bodi yake imeshauri mazungumzo yaendelee baina ya NIP na NSSF, mashirika ambayo yako chini ya Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana, Wazee na Walemavu.

Barua ya Katibu Mkuu, Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana, Wazee na Walemavu, iliyoandikwa Februari 17, 2016 yenye kumbukumbu Na. CAB.41/275/01 kwenda kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NIP, Prof. Wangwe, imeelekeza Bodi ya NIP kuchukua hatua stahiki haraka kama ilivyopendekezwa.

Taarifa ya Bodi ya Wakurugenzi wa NIP ya Machi 2, 2016, ambayo JAMHURII imepata nakala yake, inasema hakukuwa na idhini ya waziri mwenye dhamana na NIP kuhusu uwekezaji huo na barua zilizoandikwa wizarani hakuna ushahidi iwapo zilijibiwa.

Taarifa hiyo inanukuu barua yenye kumbukumbu Na. NIP/C/MTL/PR/90 ya Juni 29, 2012 na NIP/C/MTL/PR/91 ya Julai 19, 2012. 

Inasema hakukuwa na kibali kutoka kwa Msajili wa Hazina kuruhusu uwekezaji huo, mkataba ulikuwa kinyume na maelekezo ya Serikali ya asilimia 50/50 kwa mujibu wa barua ya Msajili wa Hazina.

JAMHURI imebaini kuwa sehemu ya fedha zilizolipwa na NSSF katika akaunti ya NIP kiasi cha dola za Marekani 566,400 sawa na Sh bilioni 1.241 alilipwa dalali. Fedha iliyobaki ilitumika kuendesha ofisi za NIP kwa matumizi ya utawala.

Bodi ya Wakurugenzi wa NIP ilitoa maoni jinsi fedha iliyotolewa na kutumika kihalali inarudishwa kwa NSSF, bila kuhusisha fedha alizolipwa dalali. Inaonesha kwamba mpaka Machi, 2016, kulikuwa na kiasi cha dola za Marekani 400,000 kwenye akaunti ya NIP sawa na Sh milioni 876. “Iliyobaki ambayo ilitumika kwa matumizi mengine tofauti na yaliyokusudiwa, kiasi cha dola za Marekani 636,158.25 (ambazo ni sawa na Sh bilioni 1.394) zitarudishwa kutoka kwenye mradi utakapomalizika na kuanza kuzalisha,” inasema sehemu ya taarifa ya Bodi ya NIP.

Kaimu Mkurugenzi  Mkuu NIP, Novatus Masau, akizungumza katika mahojiano na JAMHURI, amesema kwa sasa kuna hatua ambazo  zinachukuliwa na Serikali, hivyo hawezi kuzungumzia suala hilo kutokana na yeye kuwa mtu mdogo.

Anasema Serikali inafanya kazi kuhusiana na suala hilo na kwamba viongozi wa juu ndiyo wenye mamlaka ya kulizungumzia kwa sasa kutokana na uchunguzi unaoendelea.

Mkurugenzi wa Fedha wa NIP, Rafael Laizer, alipoulizwa kuhusiana na matumizi ya fedha hizo na kiasi kilichobaki mpaka sasa, amesema hawezi kuzungumzia suala hilo mpaka litakapokuwa limefanyiwa kazi na vyombo ya dola.

JAMHURI ilitaka kufahamu iwapo kiasi cha dola za Marekani 400,000 zilizobaki katika akaunti ya NIP zimetumika, Laizer amekataa kuzungumzia fedha hizo kwa sasa. “Unauliza maswali ya msingi sana, lakini nasikitika kwa upande wangu siwezi kuongelea masuala hayo kwa sasa, labda usubiri mpaka pale tutakapokuwa tayari kueleza hili kwa vyombo vya habari, ila sasa siyo wakati wake. Tukiwa tayari tutakuita na kukufahamisha kila kitu unachotaka kukifahamu,” amesema Laizer.

Februari 2011, NSSF na NIP walisaini mkataba wa kuendeleza viwanja hivyo. Mkataba ulisainiwa bila ya kuwapo kwa upembezi yakinifu (feasibility study) wenye kuonesha makadirio ya gharama za mradi.

Pia, hapakuwa na kumbukumbu zozote zinazoonesha kwamba mkataba wa uwekezaji wa ubia kati ya NSSF na NIP ulipata idhini ya Bodi ya NIP pamoja na waziri mwenye dhamana.

Mkataba huo kwa upande wa NIP ulisainiwa na Leonidas Rwejuna na Mary Matteru, na kwa upande wa NSSF alisaini Dk Ramadhan Dau.

Afisa Mwandamizi wa NSSF, ameiambia JAMHURI kwa sharti la kutotajwa gazetini, kuwa nia ya Shirika hilo ilikuwa ni kunusuru hali na hivyo anaamini bado nia njema hiyo ikitumiwa vyema majengo husika yanaweza kujengwa.

1599 Total Views 5 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!