Wakati sheria ya madini namba 14 ya mwaka 2010 ikizuia watoto kufanya kazi katika maeneo ya machimbo, hali imekuwa tofauti katika eneo la kijiji cha Ikandilo kata ya Nyaruyeye Halmashauri ya wilaya ya Geita.

Katika eneo hilo watoto wamekuwa wakifanya shughuli mbalimbali katika machimbo ya dhahabu na kusababisha kushuka kwa mahudhurio shuleni kwa asilimia hadi zaidi ya 40.

Shughuli zinazofanywa na watoto hao kwenye machimbo hayo ni pamoja na kubeba maji, hasa kwa watoto wa kike, huku watoto wa kiume wakitumika kuponda na kusaga mawe kwa ajili ya uchenjuaji wa dhahabu.

Kuwapo kwa watoto hao katika eneo hilo kumechangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa mahudhurio ya wanafunzi kwenye shule zilizoko jirani na migodi hiyo ya uchimbaji dhahabu.

Shule ya Msingi Ikandilo, iliyopo kilomita moja hivi kutoka kwenye eneo la mgodi wa Baraka uliopo Nyaruyeye, inao wanafunzi 336. Kushuka kwa mahudhurio hayo kunatokana na baadhi ya wazazi kuambatana na watoto wao kwenda kufanya shughuli za kuongeza kipato cha familia kwa kufanya biashara mbalimbali ikiwamo ya kuuza maji na kuponda mawe.

Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo ya msingi Ikandilo iliyopo katika Kata ya Nyaruyeye kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Geita, wamesema wanalazimika kufanya kazi za migodini wakati wa masomo ili kutafuta pesa kwa ajili ya mahitaji ya shule na nyumbani kutokana na familia zao kutokuwa na uwezo.

Kutokana na hali hiyo,wanafunzi hao wanasema hali hiyo imewaathiri kimasomo kutokana na kutokuhudhuria masomo yao ipasavyo, baada ya kuathiriwa na shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu.

Mmoja wa wanafunzi hao, Ndalahwa John (14), anayesoma darasa la tano, katika shule ya msingi Ikandilo, anabainisha anavyolazimika kufanya shughuli ya uchimbaji.

“Kwa kweli tunapata tabu sana kutokana na wanafunzi wengi kutokea kwenye familia duni na kama unavyosikia shughuli za uchimbaji madini zilivyo ngumu huwezi kumudu kusoma na kuchimba,’’anasema John.

Akizungumzia hatua za uchimbaji dhahabu, John anasema, “kuna aina mbili za uchimbaji dhahabu – ya kwanza ni ile ya vikole ambayo yenyewe inapatikana kwenye ardhi ya mchanga laini…Lakini pia ipo ile inayopatikana kwenye mwamba mgumu na baadaye unalazimika kutumia madini ya zebaki. 

“Dhahabu ya aina hii unapitia hatua ngumu sana kuipata maana tunatumia sururu kama mwanda wake ni laini ndiyo unapata unafuu kidogo, lakini kama mwamba huo ni mgumu huwa tunatumua baruti.

“Tukimaliza hatua zote kuchimba, kusaga na kuosha na kukamua ile dhahabu kwa kutumia kitambaa baadaye tunaenda kuichoma na kupata dhahabu yenye rangi ya  shilingi mia moja, tunakwenda sokoni kuuza,” anasema John.

John anasema pesa anayoipata kutokana na shughuli za uchimbaji madini, humsaidia kununua mahitaji ya shule ikiwamo sare za shule, pamoja na mahitaji mengine ya nyumbani.

Anasema maisha duni ya familia yake, ndiyo hasa sababu ya kuamua kuanza majukumu makubwa katika umri mdogo. Anasema anatambua kwamba Serikali imetangaza elimu ni bure, lakini yeye anaamini kwa kiwango kikubwa anawajibika kukidhi mahitaji mengine ili aweze kusoma.

“Ninafahamu kwamba kazi ninayoifanya ni hatarishi kwa afya yangu, lakini haya yanasababishwa na dhiki iliyoko katika familia yangu…bila hivyo nisingefanya kazi hizi ngumu,” anasema John. 

Kwa upande wake, Joseph Renard (14), mwanafunzi anayesoma katika Mpango wa Elimu ya Msingi Kwa Walioikosa (MEMKWA) anasema amekuwa mzoefu na shughuli za madini kutokana na kuzianza katika umri mdogo.

“Tunahangaika sana kupata dhahabu na hata ukiipata unauza hela ndogo japo umeihangaikia kuipata…hebu jiulize, unachimba mchanga au mawe ndani ya shimo baada ya hapo unapakia kwenye mfuko unafunga kamba na kuanza kuivuta kwa lengo la kutoa ule mzigo wa mawe ndani ya shimo,’’ anasema Joseph. 

Anaongeza, “Baada ya hapo unapondaponda yale mawe saizi ya kokoto… baada ya hapo unaipeleka kwenye mashine ya kusaga kokoto.”

Anasema baada ya kupitia katika hatua zote ngumu, hatimaye dhahabu hupembuliwa kwa kutumia zebaki, kazi ya madini hayo ni kutafuta dhahabu na kuikamata ndiyo ukachome na kuiuza.

Baadhi ya wazazi waliozungumza na JAMHURI ni Veronika Francis, ambaye anakiri kwamba baadhi ya watoto kijijini hapo wamekuwa wakitoroka masomo na kwenda kujihusisha na shughuli za uchimbaji madini. 

Diwani wa Kata ya Nyaruyeye, Samson Saguda, ametangaza mpango wa kuanza oparesheni dhidi ya wanafunzi wanaokimbilia migodini na kuacha masomo.

Anasema operesheni hiyo itafanyika kwa kumshirikisha Mratibu wa Elimu Kata, Joel Muganyizi, lengo la kuanza kwa operesheni hiyo likiwa ni kuhakikisha watoto wote wanarudi shule na kuendelea na masomo.

“Haiwezekani Serikali imeondoa ada kwa wanafunzi kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha nne halafu unakuta mtoto haendi shule kwa kisingizio cha ugumu wa maisha.

“Tutahakikisha mimi pamoja na mratibu elimu tunaanza msako wa nyumba kwa nyumba kubaini ni akina nani wameacha shule kwa ajili ya kuchimba dhahabu, na kama yupo mzazi ambaye anajua mtoto wake ameacha shule kutokana na shughuli za madini ni bora amrudishe shule kabla operesheni haijaanza,”  anasema Saguda.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Onesmo Gold Mine Project, iliyofadhili ujenzi wa darasa na ofisi ya walimu shuleni hapo, Onesmo Malugu, anasema ushirikiano mzuri kwa jamii ni kitu pekee kilichomvutia kujenga miundombinu hiyo.

“Mwenyekiti wa kamati ya shule ni rafiki yangu…kuna siku aliniita nikatembelee shule yake, nilipofika nilishangaa kuona ndani ya dhahabu kuna shule chakavu, nikajitolea kujenga darasa moja na ofisi ya mwalimu, tunaomba wadau wengine watuunge mkono ili tuwajengee watoto wetu moyo wa kupenda shule,’’ anasema Malugu.

Baadhi ya wanafunzi akiwamo Ginuga Masunga (14), mwanafunzi wa darasa la sita, aliiomba Serikali kuwajengea matundu ya vyoo, nyumba za walimu, pamoja na kuboresha mazingira ya shule hiyo.

“Wanafunzi hawahudhurii kwa wingi shuleni kwa sababu ya wazazi hawahimizi watoto kuja shuleni, mimi ninakuwa wa kwanza darasani si kwa sababu wazazi wangu wana mwamko wa elimu.

‘’Ninaomba Serikali iboreshe mazingira ya shule na ijenge nyumba za walimu pamoja na madarasa ili wanafunzi wafurahie kusoma…namshukuru Malugu kwa kuanza kutoboreshea mazingira ya shule,” anasema Masunga. 

Zainabu Salumu (14), mwanafunzi wa darasa la nne, aliunga mkono hoja ya kujengewa vyoo pamoja na Serikali kuwaletea walimu wa kike kwa kuwa wanapopata matatizo ya hedhi inabidi waende nyumbani na kuathiri muda wa masomo.

Akizungumza na JAMHURI, kuhusu changamoto zinazoikabili shule hiyo tangu ilipoanzishwa mwaka 1991, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Elias Aselema, anasema  kuna upungufu wa vyumba vitano vya madarasa, nyumba sita za walimu, pamoja na samani za ofisi.

“Tunaomba msaada wa hali na mali ili kutatua changamoto zinazokabili shule yetu kutoka kwa wadau mbalimbali wa elimu walioko katika hafla hii na na wengine watakaoguswa na changamoto hizi,’’ anasema mwalimu mkuu.

Kuhusu hali ya ufaulu, anasema tangu amekabidhiwa shule hiyo kama mkuu wa shule, hali ya ufaulu imebadilika na ufaulu umepanda.

“Hali ya taaluma imekuwa ikienda vizuri katika shule hii, tunajitahidi kuwadhibiti wanafunzi watoro kwa kutumia kamati ya shule na walimu ili wasiende kwenye machimbo wakati wa masomo,” anasema Aselema. 

“Jamii haiwezi kuwa na wataalamu bila kuwekeza katika elimu na itapoteza nguvu kazi ya Taifa…tangu tuanze kuwadhibiti imekuwa tofauti, changamoto ni wazazi kuhama na watoto bila kufuata taratibu za kiofisi wanahama usiku…mnapokuwa mnaita majina mnaambiwa wamehama na mkifanya utafiti hamjui walikohamia,’’ anasema Aselema.

2336 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!