Mpenzi msomaji wa JAMHURI,  katika toleo lililopita Madaraka Nyerere, ambaye ni mtoto wa Mwalimu Nyerere alielezea masuala mbalimbali kuhusu Mwalimu, familia yake na kutoa mtazamo wake juu ya hali ya maisha ya sasa ya Watanzania baada ya kifo cha baba wa Taifa. Ifuatayo ni sehemu ya mwisho ya makala hiyo… 

Nimewahi kusikia taarifa ambazo siwezi kuthibitisha zinazosema kuwa kuna watu wanasubiri Mama Maria afariki ili waanze kuchimba hiyo dhahabu. Kufanya hivyo kwa sasa akiwa hai kunaweza kuibua changamoto za kisiasa ambao zitaleta matatizo badala ya neema.

 

Watanzania tunapenda sana kuongea, kwa hiyo haya ya kumtakia maisha mafupi Mama Maria yanaweza kuwa siyo ya kweli. Lakini kama ni ya kweli, na ukiongezea ukweli kuwa Mwalimu Nyerere ananyang’anywa ardhi ambayo alipewa, basi ujue maadili, hekima na busara ambavyo vilitawala enzi zake, leo hii vimetoweka na tumebaki na jamii na viongozi ambao wanatumia nafasi zao kujinufaisha kwanza na kuangalia masilahi ya wengine inapolazimika, lakini siyo kama madhumuni ya msingi ya uongozi.

 

Labda muhimu pia kugusia kuwa Mwalimu Nyerere alifahamu taarifa za kitafiti kuonesha kuwa hilo eneo linayo dhahabu, lakini nimeambiwa kuwa kauli aliyotoa ni kuwa suala la kilimo na uhakika wa chakula lilikuwa muhimu kuliko uchimbaji dhahabu.

 

Kwa maoni yangu ni kuwa eneo lote la Kijiji cha Butiama na Kijiji cha Buturu, libaki eneo la kumbukumbu chini ya Sheria ya Mambo ya Kale ili lilindwe dhidi ya miradi yoyote ya uchimbaji madini.

 

Niliwahi kumsikia afisa mwandamizi wa kampuni ya Anglo Gold aliyetembelea Butiama akisema kuwa eneo hilo lina dhahabu, lakini siyo ya kiasi kikubwa sana kiasi cha kuibua nia ya kampuni kubwa kama Anglo Gold kukusudia kuchimba dhahabu pale. Ni dhahabu kidogo ambayo kampuni ndogondogo tu ndiyo zitaona kuwa ni mali, lakini siyo Anglo Gold.

 

Kwa maana nyingine, Serikali haiwezi kukosa mapato makubwa kwa kulitangaza lile eneo kama eneo maalumu la kumbukumbu kwa heshima ya Mwalimu Nyerere aliyelitumia kama eneo la kilimo akisisitiza umuhimu wa kilimo na uhakika wa chakula na akitahadharisha ukomo wa shughuli za uchimbaji madini.

 

Hata hivyo, kwa sera ambazo tunazo sasa hivi Serikali ilishajitoa kwenye shughuli zote za uchumi na kuacha nafasi kwa sekta binafsi kusimamia shughuli hizo.

 

Kwa maana hiyo, mradi wowote wa uchimbaji dhahabu katika eneo la Mwibanza utatoa nafasi kwa watu wachache tu kunufaika na rasilimali hiyo na siyo umma wa Watanzania.

 

Kama uongozi wetu wa sasa na hata wa miaka ijayo unayo dhamira ya kweli ya kuthamini mchango wa Mwalimu Nyerere katika kuendeleza kilimo, basi hapa wanayo fursa nzuri ya kufanya hivyo.

 

Labda Serikali inaweza kutoa nguvu, taaluma na mtaji kuonesha mfano mzuri wa utekelezaji wa Sera ya Kilimo Kwanza kwenye shamba hili.

 

Familia ya Mwalimu, uhusiano na serikali

 

Pamoja na maneno yanayoashiria uhusiano mbaya kati ya familia ya Mwalimu Nyerere na Serikali, ukweli ni kuwa uhusiano ni mzuri. Jukumu la Serikali, kwa mujibu wa sheria, ni kutoa stahili kwa mjane wa Rais mstaafu, Mama Maria Nyerere. Na hilo jukumu inalifanya vizuri tu na hata wakati mwingine kwa kuvuka mipaka.

 

Tathimini ya enzi za Mwalimu na sasa

Hata hivyo, katika mtizamo mpana zaidi wa kitaifa tunaona kuwa kuna baadhi ya upungufu unaojitokeza tunapoadhimisha kifo cha Mwalimu Nyerere. Inakuwa vigumu kuepuka kulinganisha hali ya maadili, utaifa, uzalendo, uchumi wa kujitegemea, umoja na mshikamano vilivyopo sasa na wakati wa uhai wake.


Maadili

Inatosha tu kusema kuwa maadili ya kijamii na ya kisiasa yemeshuka kwa kiwango kikubwa sana. Unapoona mshiriki na mshindi wa Big Brother Africa ambaye akiwa ndani ya jengo la mashindano Afrika Kusini alifanya vitendo ambavyo kimaadili havifanyiki hadharani, anapopokewa kama shujaa anaporudi Tanzania , ujue kuna kasoro kubwa ndani ya jamii yetu.

 

Ukiona kuwa matumizi ya pesa kwenye uchaguzi wetu wa kutafuta uongozi yamekuwa ni jambo la kawaida na hayupo mtu wa kukemea hali hii kwa sababu wa kukemea nao wanazo kasoro zile zile ambazo zinahitaji kukemewa, basi ujue kuwa nchi imetumbukia ndani ya shimo la uchafu ambalo kihistoria tunaona linaweza kupata suluhisho kutoka kwenye mapinduzi tu kwa sababu tukio kama hilo linasafisha uozo wote na kuanza upya na maadili mapya.

 

Lakini taratibu zote za kidemokrasia zinapingana na taratibu za mapinduzi kwa hiyo suluhisho kwa kweli ni gumu sana . Ungefikiri kuwa suluhisho ni kufundisha kada mpya yenye maadili mapya, lakini unaweza kweli kuweka matumaini kwa mwalimu afundishe maadili mapya wakati mwalimu kamuuzia mzazi mtihani, na mwanafunzi anafahamu kuwa mzazi wake kamnunulia mtihani?

 

Kuporomoka kwa maadili nafikiri kuna chanzo fulani. Mimi nafikiri chanzo kikuu ni kudharau au kupuuza mila na desturi zetu ambazo zote zinaonekana hazifai wakati ni dhahiri ndani ya mila na desturi hizo kulikuwa na mafundisho ambayo yalizingatia kulinda maadili yetu kwa vijana waliyokuwa wanaelekea rika ya kuwa watu wazima.

 

Nafikiri kinachotokea ni kuwa wale ambao wamekuwa kwenye mazingira yasiyo na miongozo ile ya kimaadili ambayo baba zetu walipitia sasa wamefikia utu uzima na wanashika nyadhifa mbalimbali za uongozi ndani ya jamii. Ni sawa na kumfanya mtoto awe baba ndani ya nyumba. Ni dhahiri kuwa mambo mengi yataanza kwenda kombo, siyo kwa makusudi, ila ni kwa kutokuwa na mifano na mafunzo ya jambo gani ni sahihi na jambo gani ambalo halistahili kuvumiliwa.

 

Utaifa

Taifa linaloundwa na viongozi na raia wasiyo waadilifu linaathiriwa na hatari ya kudhoofu kwa misingi ya utaifa ambayo iliwasukuma wazalendo walioungana zaidi ya miaka hamsini iliyopita kudai Uhuru wetu.

 

Uzalendo ni kama suala ambalo ni kichekesho siku hizi. Kuna watu hawaamini kuwa wapo Watanzania ambao wako tayari kujitoa mhanga kulinda utaifa kwa kusukumwa na uzalendo.

 

Uchumi wa Kujitegemea

Tunasikia mara kwa mara kuwa hakuna sababu yoyote ya Tanzania kuwa nchi masikini; na kwamba kuna vyanzo vya kutosha kuweza kuleta maendeleo makubwa. Lakini kwa sera hizi za ubinafsishaji na utukuzaji wa sekta binafsi, sidhani kama jitihada hizi za kujenga uchumi usiyo tegemezi zinaweza kuleta mafanikio na maendeleo ya haraka.

 

Taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali nazo zinaashiria kuwa usimamizi mzuri wa mapato na matumizi ya Serikali vinaweza kuwa mchango mkubwa wa kusukuma maendeleo yetu.

 

Mimi siku zote ninaamini kuwa, kuacha ung’ang’anizi wa kiitikadi tu, haipo sababu ya msingi ambayo inaweza kushikilia hoja ya Serikali kujitoa kwenye shughuli za kiuchumi. Tunapoitoa Serikali kumiliki hisa kwenye shughuli kuu za kiuchumi tunafanikisha masuala mawili ya msingi na yote ambayo hayana manufaa yoyote kwa masilahi ya umma. Kwanza , tunaipunguzia Serikali vyanzo vya mapato ambayo yatatumika kwa manufaa ya wote; pili, tunatoa fursa kwa mashirika au watu wachache kunufaika na rasilimali zetu na kuwanyima wengi nafasi ya kunufaika na rasilimali hizo kupitia hisa ambazo zingeshikwa na Serikali.

 

Hivi karibuni mzozo wa mpaka na Malawi ulizua hisia kuwa Tanzania ingeweza kupigana vita na Malawi. Kwa bahati nzuri, tumesikia Rais Kikwete akisema kuwa hatuwezi kufikia hatua ya kupigana vita kwa sababu anaamini kuwa mzozo huu utatatuliwa kwa njia za kidiplomasia. Kwa sera ambazo tunazo sasa hivi, na kama siyo kwa busara hizo za kuepuka vita, ingewezekana kabisa kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania kupigana vita kali na kuleta hasara ya mali na maisha, halafu rasilimali zote ambazo zimezusha vita zikapewa mwekezaji kwa manufaa yake na ya kampuni yake na sisi kuambulia chini ya asilimia 5 ya mapato ya yule mwekezaji!

 

Hizi vita bado zinapiganwa kwa jina la Tanzania ingawa siyo kwa kutumia silaha, na faida zake kwenda kwa kampuni chache au watu wachache. Mimi nafikiri umewadia wakati wa kurudisha, siyo kwa nadharia tu, lakini kwa vitendo, umiliki wa dhati wa rasilimali za nchi kwa watu wake ili wote tunufaike nazo na siyo genge la watu wachache ambao wanatuimbia wimbo usioisha kuwa sekta binafsi ndiyo mwarobaini wa kila kitu.

 

Serikali haipaswi kushiriki katika kila mradi wa kiuchumi, lakini yanaweza kuchanguliwa maeneo nyeti ambayo Serikali itakuwa na hisa za kutosha na kuacha sehemu ya hisa hizo kumilikiwa na sekta binafsi.

 

Sekta binafsi iwepo na ifanye kazi pamoja na Serikali, lakini huu uongo kuwa Serikali haina nafasi katika shughuli za kiuchumi unatoa fursa kwa wachache kunufaika na rasilimali na wengi kulishwa takwimu tu kuwa uchumi wetu unakua kwa kasi nzuri.

 

Umoja na mshikamano

Mimi naamini kuwa suala la umoja na mshikamano limepata pigo kubwa sana katika miaka ya hivi karibuni na kwa kweli inawezekana kuwa ukiitisha kura ya maoni Watanzania wa upande wa Zanzibar watachagua kutupilia mbali Muungano.

 

Aidha, kuna masuala ya kisiasa na dini ambayo sasa yanaanza kuwatenganisha Watanzania. Mwalimu Nyerere alisema kuwa unapoona kiongozi anaanza kutumia udini au ukabila kutafutia umashuhuri, basi ni dhahiri kuwa kiongozi huyo hana hoja za msingi na anatafuta kura za huruma zisizohitaji tathimini ya kweli ya mpiga kura.

 

Kutangazwa makao mapya ya wilaya mpya ya Butiama

Mimi nakiri kuwa ni mmoja wa watu ambao sikufurahia uamuzi wa Butiama kutangazwa kuwa makao makuu ya wilaya mpya ya Butiama kwa sababu niliamini kuwa kuja kwa wilaya kutaleta pia athari kadhaa.

 

Kwanza, inafahamika kuwa makao ya wilaya yanahitaji maeneo yenye ukubwa mahususi ya kujenga makao yenyewe rasmi ya wilaya, ikiwa ni pamoja na ofisi na taasisi mbalimbali ambazo zinaambatana na uamuzi huo. Na mimi naamini kuwa ardhi ya Butiama ni ndogo kiasi kwamba italeta matatizo katika kuainisha maeneo hayo ya kuweka hayo majengo na taasisi bila kuathiri wakazi wa Butiama.

 

Hata hivyo, naamini kuwa limechaguliwa eneo sasa ambalo halina wakazi wengi na ambalo pengine litapunguza huu mgongano ambao nauzungumzia.

 

Pili, kuna uasilia ambao unaambatana na eneo fulani kuwa kijiji na uasilia huu unaambatana na desturi fulani ambazo zinapambanua eneo moja la Tanzania na jingine. Ujio wa wilaya na halmashauri unakuja pia na mambo ya kimjini mjini ambayo, kwa desturi yake, hufuta uasilia wa eneo husika, na utaifanya Butiama badala ya kuwa kijiji chenye desturi mahususi kuwa kama eneo lingine lolote la mji la Tanzania .

 

Watu wengine wanasema kukubali wilaya ni suala la kwenda na wakati, lakini kwa kuwa mimi najihusisha na uratibu wa asasi ya jamii inayosimamia uendelezaji wa tamaduni chini ya Mpango wa Utalii wa Utamaduni unaosimamiwa na Bodi ya Utalii Tanzania, nina wasiwasi kuwa kuja kwa wilaya kunazua changamoto nyingine katika kulinda na kutunza mila na desturi za Wazanaki na kutadhoofisha hii azma ya kulinda tamaduni ambazo tayari zimeshaanza kupotea kutokana na kasi ya mawasiliano mapya na nguvu ya utandawazi.

 

Siyo suala la kujenga ukabila, ila ni suala tu la kutunza na kulinda asili ya eneo husika.

Nimesikia mmoja wa viongozi wetu akisema kuwa faida za kuwa na wilaya ni kuwa Serikali itaweza kutenga fedha kwa ajili ya kuendeleza miundombinu kama vile upatikanaji wa maji safi na salama, mawasiliano na barabara. Hayo, bila shaka yakija, yatakuwa na manufaa kwa wote.

 

Labda baada ya miaka 50 itakuwa rahisi watu kutathimini kama Butiama itakuwa imenufaika kwa kuwa wilaya au itakuwa imeathiriwa kwa uamuzi huo. Kila jambo lina faida na hasara zake, na hili litabaki hivyo kwa uamuzi huu pia.

 

Wageni wa Butiama

Nikiwa kama Mratibu wa asasi ya kijamii inayojulikana kama Butiama Cultural Tourism Enterprise (BCTE) tumekuwa tunasimamia sehemu ya kazi ya kupatangaza Butiama kama kivutio cha kihistoria na kiutamaduni, tukishirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania .

 

Kwa wastani tunapata wageni 450 kwa mwezi na kwa kawaida mwezi huu wa Oktoba ndiyo tunapata wageni wengi zaidi kwa kuwa Oktoba 14, siku ambayo alifariki Mwalimu Nyerere, tunakuwa na idadi kubwa ya watu wanaozuru Butiama.

 

Sehemu kubwa ya wageni hawa ni Watanzania, lakini tunapata wageni pia toka nchi za jirani za Kenya na Uganda na baadhi ya nchi za nje.

 

Butiama iko karibu sana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti  kwa hiyo baadhi wa wageni wanaokwenda au kutoka huko hupita Butiama.

 

Tuhuma za kuuawa kwa Mwalimu Nyerere

Binadamu wengi wanapenda sana kuamini kuwa kila jambo likitokea, basi kuna mkono wa mtu unahusika. Na hivi karibuni kifo cha Mwalimu Nyerere kimehusishwa na njama mahususi za kumuua.

 

Kwa desturi za Kizanaki hakuna mtu ambaye anakufa kwa sababu ya ugonjwa au uzee, lazima yuko mtu miongoni mwa wale waliobaki hai ambaye amesababisha kifo chake kwa njia za uchawi. Kwa mfano, Bibi Christina Mgaya wa Nyang’ombe, mama mzazi wa Mwalimu Nyerere, mara baada ya kifo cha mume wake Mtemi Nyerere Burito tarehe 30 Machi 1942, alitimuliwa Butiama na kuhamia kwa ndugu zake katika kijiji jirani cha Muryaza baada ya kutuhumiwa kuwa alisababisha kifo cha mume wake.

 

Kwa hiyo, hakurithiwa kama ilivyo desturi za wakati ule za mila za Kizanaki na aliishi kwa jamaa zake hadi Mwalimu Nyerere alipotoka masomoni Uingereza na kudai arudi nyumbani na akarudi, ingawa baadhi ya ndugu zake hawakufurahia kurudi kwake Butiama.

 

Kwa hiyo basi, ni kawaida kabisa kwa hisia kama hizi kuwapo ndani ya jamii. Lakini kusema hivi haina maana kuwa haiwezekani kuwa tuhuma hizo ni za kweli. Lakini mtu yoyote muungwana hawezi kuanza kutoa shutuma nzito kama hizi bila kuwa na ushahidi usiotiliwa shaka na ambao hauna dosari.

 

Lakini naweza kuelewa kwanini baadhi ya watu ambao wanashikilia hizi tuhuma kuwa zinaweza kuwa ni kweli. Tunamfahamu Mwalimu Nyerere kuwa, hata baada ya kustaafu, hakukalia kimya uamuzi au matukio ambayo aliamini yanaathiri baadhi ya msingi ambayo yeye aliiona kuwa ni nguzo inayoshikilia nchi yetu. Baadhi ya haya ni uadilifu ndani ya uongozi, umoja, uzalendo na sera zenye kujali masilahi ya wengi badala ya sera zinazokuza na kulinda nafasi kwa wachache kujinufaisha.

 

Na kwa kweli ukichunguza baadhi ya matukio kwenye nyanja ya siasa katika kipindi hiki ambacho amefariki, yametokea mengi ambayo tunaamini kuwa kama angekuwa hai asingenyamaza na angeyazungumzia kuyapinga na kuyakemea au kuyatungia kitabu pale ambapo ujumbe wake aliona unapuuzwa. Kwa hiyo, mtu yeyote ambaye anafuatilia hali ya uongozi nchini, na watu wengi wanasema hivi, ni kuwa Mwalimu Nyerere angekuwapo labda baadhi ya uamuzi na mienendo ya baadhi ya viongozi wetu ungekuwa tofauti kwa kuogopa kauli yake au kuandikiwa kitabu ambacho kitajenga hoja inayopingana na uamuzi wa viongozi. Na pengine baadhi ya uamuzi ambao umefanyika usingefanyika.

 

Kwa mantiki hii unaweza kuanza kujenga hoja kuwa baadhi ya wale waliyofanya uamuzi unaoonekana unaenda kinyume au na maadili ya uongozi, au unapingana na masilahi ya umma, walitafakari kuwa njia rahisi ya kurahisisha mipango yao ni kumouondoa huyu mzee mapema.

 

Hiyo unaweza kusema, lakini haitakuwa sahihi kufanya hivyo bila kuwa na ushahidi. Nimewahi kusikia tuhuma kuwa Rais Kikwete anatuhumiwa kuwa ndiye mtu aliyetumwa na nchi za Magharibi kukimaliza Chama Cha Mapinduzi (CCM). Nilivyosikia tuhuma hizi niliona kichekesho, lakini ukiangalia baadhi ya matukio katika uongozi wake ambayo yanaweza kuashiria hoja hiyo unaweza kuyapata.

 

Enzi za Mwalimu Nyerere waliotuhumiwa kwa makosa mbalimbali ya uongozi waliitwa pembeni na kuambiwa wajiuzulu. Miaka ya hivi karibuni wale ambao walikabiliwa na tuhuma za aina hiyo waliombwa kutafakari wao wenyewe uamuzi sahihi wa kuchukua. Uamuzi mgumu haufanyiki, upinzani wanapata mada ya kuzungumzia kwenye mkutano wao ujao, na CCM inazidi kudhoofu. Kama nilivyosema hakuna ushahidi wa wazi, lakini kuna viashiria tu.

 

Nafikiri njia nzuri ya kufunga mjadala huu ni kuzungumza kama wanasheria wanavyosema; hakuna ushahidi mpaka sasa unaothibitisha hizo tuhuma juu ya njama za kumuua Mwalimu Nyerere.

 

Hoja kuwa uchunguzi ufanyike kubaini kama aliuawa sioni kama zitaleta faida yoyote kwa sababu ameshafariki tayari na hakuna uchunguzi ambao utarudisha uhai wake.

 

Mwalimu Nyerere tunamkumbuka kwa maandishi na matamshi yake. Na naamini kuwa katika uhai wake aliandika na kutamka masuala yote ambayo aliamini ni ya msingi kwake na kwa jamii.

 

Kuna kiongozi mmoja ambaye amewahi kusema iwapo kuna wazo la msingi ambalo binadamu amelisema katika uhai wake, basi hilo wazo litadumu hata kama aliyelisema hayuko tena duniani.

 

Badala ya kutafuta wachawi sasa hivi mimi nafikiri wale wote ambao wanaamini kuwa Mwalimu Nyerere alitoa mchango mkubwa kwa nchi hii watumie muda wao kutafakari kazi aliyofanya na kujumuisha fikra zake na matendo yake kupima yale ambayo bado yanaweza kuwa suluhisho dhidi ya baadhi ya changamoto zinazoikabili Tanzania sasa hivi.

 

Iwapo hoja zake zina nguvu katika mazingira ya sasa, basi hazihitaji yeye mwenyewe kuzisemea.

 

Wanaoziamini wazichambue na wazitumie kama silaha ya kupambana na upungufu ambao tunauona leo katika nyanja mbalimbali. Lakini pia ni muhimu kwa vijana kujitafutia elimu kuhusu hayo yaliyopita ili kupata mifano mizuri ya uongozi ambayo iliweka masilahi ya Taifa mbele na kuzuia kabisa hizi hoja za siku hizi za kumpa kila mtu fursa ya kufanya anavyotaka.

 

Zinazungumzwa fursa za mwananchi, lakini ukweli ni kuwa baadhi ya viongozi wanapigana vikumbo na wananchi hao hao kutafuta fursa zao binafsi.

Madaraka Nyerere ni mmoja kati ya watoto wanane wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Tangu kifo cha Mwalimu, amekuwa akiishi Butiama akiwa Mratibu wa asasi ya kijamii ya Butiama Cultural Tourism Enterprise (BCTE) inayotangaza Butiama kama kivutio cha kihistoria na kiutamaduni kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania .

By Jamhuri