Juzi, tarehe 14 Oktoba 2012, tumetimiza miaka 13 tangu kufariki Mwalimu Julius Nyerere, kiongozi wa kwanza wa Tanganyika huru, na baadaye Tanzania.

Tangu kufariki kwake na kila tunapoadhimisha siku aliyofariki kunaibuka mjadala mkubwa kuhusu uongozi ikizingatiwa kuwa Mwalimu Nyerere bado anaheshimika kama aliyekuwa muadilifu, na ambaye aliweka masilahi ya Taifa mbele. Uadilifu huu unatokana na sera alizoziasisi zilizotanguliza umuhimu wa walio wengi kufaidika na rasilimali na maendeleo kwa ujumla, lakini pia katika mwenendo wake wa uongozi.


Ukweli unabaki kuwa kiongozi anaweza kuwa na sera zinazohitaji masilahi ya Taifa na masilahi ya wengi, lakini bado akawa ni mfano mbovu kabisa wa uadilifu na mtu anayetanguliza masilahi yake binafsi na kuacha mahitaji ya wengi yakitapatapa kwenye mawimbi na kina cha bahari yakitafuta pa kuhemea.


Imekuwa desturi tangu kufariki kwake kutafakari maisha ya utumishi wa Mwalimu Nyerere kwa umma kila tunapoadhimisha kifo chake. Na mimi naona sina budi kufanya hivyo, haswa kwa kuzingatia kuwa mawazo yanayotolewa na kila mmoja wetu yanaweza kuchangia mjadala kuhusu changamoto za kisiasa na kijamii ambazo nchi yetu na watu wake wanakabiliana nazo sasa na wakati huo huo kuchangia mawazo kuhusu namna ya kukabiliana na baadhi ya changamoto hizo.

Uamuzi wa kuzikwa Butiama

Mwalimu Nyerere tunamkumbuka kama mtu ambaye alikuwa na misimamo thabiti. Alifanya uamuzi kwa kufanya tafakari za kina na siyo kwa masuala makubwa tu yaliyokabili Taifa, bali hata kwa uamuzi ambao ulihusu maisha yake binafsi.


Wakati akiugua saratani ya damu, Mwalimu Nyerere aliarifiwa na daktari wake kuwa, kwa kawaida ya magonjwa ya aina hiyo, jitihada za tiba hufikia kikomo na hatimaye hazisaidii katika kurefusha maisha ya mgonjwa.


Alipopewa hii taarifa Mwalimu Nyerere alitoa maagizo ni wapi angetaka azikwe na kuonesha sehemu alipozaliwa kwenye eneo la Mwitongo, kijijini Butiama. Ni sehemu ambako alikulia kabla hajaanza kusoma akiwa na umri wa miaka 14. Mwitongo ndipo sehemu aliyoifahamu katika hatua za kwanza za maisha yake, akiwa mmoja wa watoto wa Mtemi Nyerere Burito aliyeongoza kabila la Wazanaki wa eneo la Butiama, na ambaye alikuwa na wake 22. Mama yake Mwalimu, Mgaya wa Nyang’ombe, alikuwa ni mke wa tano wa Nyerere Burito.


Ulizuka mjadala baada ya kifo chake kwa baadhi ya Watanzania ambao walipenda Mwalimu Nyerere azikwe eneo la Tanzania tofauti na Butiama. Baadhi walitaja Dar es Salaam wakati wengine walipendekeza Dodoma, na hoja ilikuwa maeneo hayo yangewezesha Watanzania wengi zaidi kuweza kuzuru kaburi lake. Butiama iko pembezoni kwa Watanzania wengi na siyo rahisi kufika huko.

 

Wengi wetu hutafakari sababu ambayo ilimshawishi Mwalimu kuzikwa Butiama na tunaamini kuwa ulikuwa ni uamuzi sahihi. Kuna mijadala mikali ambayo huzuka nchini Zimbabwe mara anapofariki kiongozi na unapochukuliwa uamuzi wa ama kukubali, au kukataa asizikwe kwenye eneo ambalo linaitwa Heroes Acre, eneo ambalo limetengwa kwa madhumuni ya kuzika mashujaa wa Zimbabwe . Uamuzi wa nani ni shujaa yanafanywa na Kamati Kuu ya chama cha Zanu-PF, chama ambacho kimeongoza serikali ya Zimbabwe tangu kupatikana uhuru wao mwaka 1980, na baadhi ya watu wanalamikia uamuzi huo, wanasema unapendelea zaidi wale waliokiunga mkono chama hicho.


Inawezekana kuwa wazo la kumzika Mwalimu sehemu nyingine zaidi ya Butiama lingeibua mijadala ya aina hiyo na badala ya kumfanya apumzike kwa amani, lingekuwa linamhagaisha huko aliko. Tayari kuna makundi ya watu yanayodai kuwa mchango wake katika kuleta Uhuru wa Tanganyika ulikuwa ni mdogo kuliko historia inavyoeleza na inawezekana kuwa makundi ya aina hiyo yangezua mjadala mkubwa kuhusu kuwapo nchini Tanzania kwa eneo maalumu la kuzikwa viongozi wa kitaifa.


Uamuzi wake wa kuzikwa Butiama unafanana na uamuzi wake wa kurudi Butiama baada ya kustaafu mwaka 1985 na kijiendeleza na shughuli za kilimo. Kwa hakika kwa yeye Butiama ni nyumbani, katika uhai na katika kifo chake, na hili linadhihirishwa na uamuzi wake wa kuzikwa alipozaliwa.


Uamuzi wangu wa kuishi Butiama

Baada ya Mwalimu kuzikwa Butiama tarehe 23 Oktoba 1999 mimi nilichukuwa uamuzi wa kubaki Butiama na nimekuwa nikiishi huko tangu wakati huo.


Kwangu ilikuwa rahisi kuchukua uamuzi wa kuhamia Butiama kwa sababu familia yangu ilikuwa nje ya nchi, na nilidhani kuwa ilikuwa muhimu kwa mmoja wetu yaani mmoja wa watoto wake, aweze kuwa karibu na Mama Maria. Kwa hiyo nikabaki hapa baada ya mazishi ya Mwalimu ingawa haukuwa uamuzi rahisi kuutekeleza.


Unapokuwa na mazoea ya kuishi Dar es Salaam inakuwa vigumu sana kuishi sehemu nyingine ya Tanzania na kwa kweli mwanzoni nilikuwa najikuta nikisafiri mara kwa mara kwenda Dar es Salaam, lakini sasa hivi nimeshazoea kuishi Butiama na hufika Dar es Salaam mara moja moja.

Tofauti ya sasa na alipokuwa hai kwa familia

Ni dhahiri kuwa, kwa kawaida, kuondokewa na kiongozi wa familia kunaacha pengo kwa familia yoyote na haikuwa tofauti kwa familia ya Mwalimu Nyerere. Lakini labda tushukuru kuwa mwanadamu ameumbwa kukabili mabadiliko yanayoandama maisha yake na kadiri miaka inavyozidi kupita. Hali ya kukosekana kwa kiongozi wa familia inajisawazisha yenyewe na unaibuka uhusiano mpya ambao unaakisi hiyo hali mpya.


Siwezi kusema familia yake imezoea kutokuwapo kwa Mwalimu, lakini labda ni sahihi tu kusema kuwa maisha yanaendelea kwa kadri ya wale waliyopo wanavyoyasukuma, kila mmoja akiwa anachangia anavyoweza majukumu yake ya kifamilia.


Lakini naweza kukiri kuwa yeye alituunganisha kama familia, na kutokuwapo kwake kunasababisha kuibuka kwa matawi yake ambayo kila moja linatafuta nafasi yake katika ulimwengu huu na katika maisha kwa ujumla. Sisemi kuwa kufariki kwake hakujatutenganisha kama familia ila kuondoka kwake ni hatua tu ambayo familia nyingi zinapitia. Yeye mwenyewe alikabiliana na hali hiyo baba yake alipofariki dunia mwaka 1942 na kuanza kuchukua jukumu la kusimama mwenyewe na kuunda familia yake miaka kumi baadaye, na sisi pia tunapitia mzunguko wa aina hiyo kama sehemu ya kukabiliana na mabadiliko.


Nakumbuka maneno ya Mzee Kingunge Ngombale-Mwiru, tuliyekuwa naye London siku Mwalimu alipofariki. Aliniambia mimi na kaka yangu Makongoro kuwa kifo cha Mwalimu kinatufanya sisi sasa kuwa watu wazima kwa sababu tunabeba majukumu ambayo hatukuwa nayo hapo awali. Alisema, “Watu walipofika nyumbani walikuwa wanamuulizia Mwalimu. Lakini leo hii wakifika nyumbani watakuulizia Madaraka au Makongoro.” Na wengine, ambao hakuwataja Mzee Kingunge.

Maisha yake wakati wa uongozi

Mwalimu alikuwa ni mtu aliyefuata ratiba kwa umakini mkubwa. Baadhi ya walinzi wake wa zamani wanakumbuka kuwa akiambiwa ratiba inaanza saa fulani, basi kama ni safari kwa hakika atakuwa tayari kuondoka saa ile ile bila kupoteza dakika.


Alikuwa na desturi ya kila siku kuamka mapema sana, kusikiliza taarifa za habari za nje ya nchi na za nchini pia za Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ya wakati ule. Alitumia muda pia kufanya mazoezi ya viungo na alihudhuria ibada kila siku kabla ya kuelekea kazini Ikulu, wakati huo tukiwa tumehamia kwenye makazi yake yaliyopo eneo la Msasani ambalo siku hizi linaitwa Mikocheni.


Kuna baadhi ya wageni walifika Msasani kumuona, lakini wengi waliishia Ikulu. Ofisi yake ya Msasani ilikuwa kwenye ghorofa ya chini na huko ndiko alipoonana na wageni, au kwenye sebule iliyopo ghorofa ya chini.


Kwenye ghrofa ya juu ilikuwa sebule ya juu, na chumba chake cha kulala. Alipohamia sebule ya juu tulitambua kuwa shughuli zake za kikazi zilikuwa zimeisha na huko tulipata fursa ya kuongea naye kama mzazi na mwanafamilia.


Kwa kawaida yake hakupenda kuchanganya familia yake na shughuli zake za kikazi. Kwa hiyo ilikuwa ni nadra sana kwa wageni wake kufika kwenye ghorofa ya juu na kuonana na wanafamilia au wanafamilia kuteremka chini na kuchanganyika na wageni wake rasmi.


Mara chache ambapo aliamua kutuita chini kuonana na wageni wake ni alipofika Rais mstaafu wa Zambia, Dk. Kenneth Kaunda. Mgeni mwingine ambaye tulionana naye alikuwa Rais wa India wa nyakati zilizopita ambaye sikumbuki jina lake. Aidha, alipompokea Malkia Beatrice wa Uholanzi, akiwa katika ziara rasmi nchini, Mwalimu alituiita Ikulu kukutana naye na familia yake.


Ratiba ya Mwalimu Nyerere alipokuwa Butiama inaweza kugawanywa katika vipindi viwili; alipokuwa Rais wa Tanzania na alipostaafu uongozi wa nchi.


Akiwa Rais, Mwalimu Nyerere aliweka utaratibu wa kusafiri kwenda Butiama kwenye mapumziko kila mwisho wa mwaka. Lakini ingawa alikuwa huko kwa mapumziko alitumia muda mwingi wa likizo yake akujishughulisha na kilimo kwa kusirikiana na wanakijiji wengine.


Pamoja na kuwa mapumzikoni, kwa kuwa alikuwa kiongozi wa nchi, basi ilikuwa kawaida kwa watu mbalimbali wenye matatizo kufika kumuona ili kuomba awasaidie kutatua hayo matatizo.


Alipotoka shambani na katika muda wake wa mapumziko alitumia muda mrefu kujisomea baadhi ya vitabu vyake. Alipofariki mwaka 1999 aliacha maktaba ya vitabu vyake zaidi ya 8,000 ambavyo karibia vyote aliweza kuvisoma. Hivi ni vitabu alivyoanza kuvikusanya alipoanza kusoma katika ngazi ya chuo, lakini pia kuna vitabu ambavyo aliendelea kununua au alivyozawadiwa na waandishi tofauti wa vitabu, au watu mbalimbali ambao walimtumia vitabu ambavyo waliamini angependa kusoma.


Katika kipindi cha kustaafu kwake akiwa Butiama aliendelea kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na akawa pia na wadhifa wa Mwenyekiti wa Tume ya Kusini na msuluhishi wa mazungumzo ya amani ya Burundi . Kwa sababu ya kazi hizi, majukumu yake yalihusisha kufika Butiama kwa baadhi ya wageni ambao walihusika na kazi za Tume ya Kusini, pamoja na usuluhishi wa Burundi.


Kuna wageni kutoka maeneo mbalimbali ya dunia na Bara la Aafrika ambao pia walifika Butiama kuonana naye kwa masuala mbalimbali. Kuna mmiliki mmoja wa hoteli ya mjini Musoma anayekumbuka kumuona kwenye hoteli yake marehemu Laurent Kabila, kabla ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, akiwa hotelini mjini Musoma kwake kwa siku kadhaa akisubiri kuelekea Butiama kuonana na Mwalimu Nyerere. Wageni wa aina hii ni wengi ambao walifika Butiama kuonana na Mwalimu Nyerere.

Mwalimu kama mzazi na kiongozi wa familia

Kama ambavyo naamini ni hali ya kawaida katika familia yoyote, Mwalimu akiwa kama baba na kiongozi wa familia, alikuwa na upendo wa kawaida tu kwa familia yake. Kwenye familia za Kibantu, tofauti na katika jamii nyingine, hatuwezi kuzungumzia matukio mahususi ambayo yanamtanabahisha mzazi kuonesha mapenzi kwa familia yake. Sisi tunaamini kuwa alikuwa na mapenzi ya kawaida tu kwa familia yake.


Lakini tunakumbuka kuwa alikuwa ni mzazi ambaye alipenda kuunganisha ukoo wake kila ilipotokea fursa na aliacha msingi imara uliyounganisha ukoo wa baba na babu yake.

Mandhari ya Mwitongo

Nikizungumza kama mkazi wa Mwitongo na mdau wa shughuli za kupaendeleza Mwitongo kama eneo la kihistoria na la utamaduni wa kabila la Wazanaki, napenda kusema kuwa tunajitahidi kuweka vizuri mazingira ya eneo hilo ili lipendeze kama Mwalimu alivyokusudia kwa kuwa na mazingira yanayovutia.


Tunakusudia kuendeleza mradi wa upandaji miti ambao yeye aliuanzisha, lakini ambao hatujapata fursa ya kuuendeleza mpaka sasa. Changamoto kubwa ni kuwa baadhi ya wakazi wa Butiama huvamia huu msitu alioupanda na kukata miti bila idhini. Aidha, kuacha mipango hii, hakuna jitihada mahususi za kupanda miti katika eneo la Butiama.

Mwalimu na kilimo, changamoto za leo

Shughuli za kilimo alizoendeleza Mwalimu ni kama zimesimama kwa sasa na kuna wanafamilia wachache tu ambao wanajihusisha na kilimo, lakini kwa kiwango kidogo kulinganisha na kilimo alichoendesha Mwalimu.

Kwangu mimi jambo mojawapo linaloathiri

Jambo moja ambalo linaathiri mipango ya muda mrefu ya kuendeleza kilimo ni kuwa baadhi ya yale maeneo ambayo Mwalimu Nyerere alikuwa analima hayakuwa maeneo yake binafsi, bali yalikuwa na mpaka sasa ni maeneo yaliyopo chini ya mamlaka ya Kijiji cha Butiama. Yeye aliazimwa tu na kijiji kulima. Na hata pale wapimaji kutoka serikalini walipoendesha upimaji maeneo hayo na kutaka kumpa miliki, alikataa na kusisitiza kuwa ni maeneo ya kijiji.


Hata hivyo, kuna taarifa kuwa, kwa kutambua kwamba hakuwa na ardhi, uongozi wa kijiji jirani cha Buturu ulimpa eneo Mwalimu Nyerere, lakini jambo la kushangaza ni kuwa baadhi ya viongozi wa hivi karibuni wa kijiji hicho wanasema hawakumbuki au hawana habari na hizo taarifa ya kupewa ardhi Mwalimu Nyerere. Kusema hawakumbuki inawezekana kuwa ni kweli kwa sababu wengi wao wana umri mdogo na siyo rahisi kuwa na kumbukumbu hizo kichwani.


Kwa hiyo, kinachotokea sasa ni mmoja wa viongozi hao wa zamani kuendelea kukalia hilo eneo na kuligawa kwa kuwakodishia watu wengine.


Mwalimu Nyerere alipokuwa akiendesha shughuli za kilimo baadhi ya wasaidizi wake walikuwa wanalima kwenye eneo hilo ambalo sasa limeporwa, na wanathibitisha kuwa ni eneo ambalo Mwalimu Nyerere alipewa na Kijiji cha Buturu.


Ni dhahiri leo hii zikitoka taarifa kuwa familia ya Mwalimu Nyerere imenyang’anywa ardhi na kiongozi wa zamani wa Kijiji cha Buturu desturi ya siku hizi ni kuamini kuwa siku zote ni viongozi na familia zao ndiyo wanayo tabia ya kupora mali za wananchi. Ukweli unaweza kuthibitishwa, lakini kwa mlolongo mrefu ambao unamshuku zaidi yule mwenye jina kuliko yule ambaye hana jina.

 

Baadhi yetu ndani ya familia tunatambua kuwa suala hili lina athari kubwa za kisiasa. Mwalimu Nyerere asingekuwa kiongozi muadilifu, leo hii familia yake ingekuwa inamiliki ardhi hata yenye ukubwa wa Mkoa wa Mara.


Lakini unaanzaje kudai haki dhidi ya wahusika ambao wao wenyewe wana masilahi ndani ya shauri hilo hilo? Kwa maneno ya siku hizi tunaita kupeleka kesi ya kenge kwa mamba. Kwa mfano mimi niliitwa kwenye kikao kimoja cha uongozi wa Kijiji cha Buturu na kuombwa nitoe uthibithso wa umilikiswaji wa lile eneo kwa Mwalimu Nyerere. Ni kweli kuwa Kijiji cha Buturu kina kumbukumbu sahihi za uamuzi wake wote kwa miaka 25 au 30 iliyopita? Sidhani. Na iwapo wangekuwa wanazo, wangezitoa kweli hadharani wakati watu wale wale ambao wanashikilia hayo maeneo wako kwenye uongozi wa kijiji? Sidhani.


Eneo la Mwalimu Nyerere la Mwitongo linajulikana kwa mwenyeji yoyote wa Butiama kuwa ni eneo lake. Lakini ukiomba kupata nyaraka za kuthibitisha miliki hiyo ukweli ni kuwa hazipo. Lakini haibadilishi ukweli kuwa ni eneo la Mwalimu Nyerere. Serikali ya Kijiji cha Butiama inaweza kuthibitisha hilo kwa taarifa ambazo inaweza kuziandaa leo hii, lakini uwezekano wa serikali hiyo hiyo kufanya hivyo wakati baadhi ya viongozi wake wa hivi karibuni wana njama za kujitwalia maeneo hayo ya Mwitongo inakuwa vigumu. Hili ndilo tatizo lililopo Buturu sasa hivi, lakini ni kiashiria kizuri cha aina gani ya viongozi ambao tunao sasa hivi. Na haya kama yanamtokea Mwalimu Nyerere, basi hakuna kizingiti chochote cha kuathiri haki kwa mwananchi wa kawaida.


Kuna taarifa kuwa eneo lote hilo, lile ambalo la Kijiji cha Butiama na lile ambalo alipewa Mwalimu Nyerere, lina madini ya dhahabu kwa hiyo tatizo hapa linaweza kuwa ni dhahabu na siyo ardhi ya kulima.


Unaweza kuwa unafikiri unapambana na wanakijiji ambao wanatafuta eneo la kulima, kumbe ni suala pana zaidi ya hapo.


ITAENDELEA

By Jamhuri