Madiwani Biharamulo washtukia ufisadi

Madiwani wa Halmashari ya Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, wameshitukia harufu ya ufisadi katika matengenezo ya gari la Mtendaji Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Nasib Mmbagga. Mkurugenzi huyo amewasilisha mapendekezo ya Sh milioni 67 kwa ajili ya matengenezo ya gari lake lilosajiliwa kwa namba STK 5499 aina ya Toyota Land Cruiser GX V8.

Halmashauri hiyo kupitia mkurugenzi wake huyo, iliwasilisha hoja hiyo katika Baraza la Madiwani kuomba kuidhinishiwa kiasi hicho cha fedha kugharamia matengenezo hayo. Katika taarifa yake kwa Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo, Mmbagga amesema kuwa gari hilo liliishiwa mafuta ghafla likiwa wilayani Nzega, Mkoa wa Tabora.

 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Madiwani wa Halmashauri hiyo, wamesema walitaka kujua bei halisi ya vipuri vitakavyotumika kutengenezea gari hilo.

 

Walimwagiza mkurugenzi huyo kutuma mhandisi na mafundi wa halmashauri hiyo, kutafuta bei halisi ya vipuri vya gari hilo na gharama halisi ya matengenezo ndani ya siku 14, wakiwa na fomu za kulinganisha bei (Quotation form) katika kikao cha baraza lijalo.

 

Mjumbe wa Kamati ya fedha, Mipango na Uongozi, wa Halmashauri hiyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyabusosi, Msuya Bitanambona, alimtuhumu Katibu wa kikao hicho,  Amina Kiwanuka, kuwa ameficha nyaraka za bei ya vipuri vya gari hilo.


Mmbagga alipoulizwa kuhusu kutenga kiasi hicho kikubwa cha fedha kwa jili ya kutengeneza gari lake, amesema hawakuomba fedha hizo kwenye Baraza la Madiwani, bali waliwasilisha taarifa ya mapendekezo ya Wakala wa Kampuni ya Toyota.


“Toyota ni mzabuni wetu, anataka kutengeneza gari hilo kwa kiasi hicho cha fedha.

“Wakala wa Toyota alifungua gari na akaleta maombi ya kulitengeneza kwa fedha hiyo na akataka anibane kwenye mkataba lakini nilikataa kusaini, niliona  kiasi cha Sh milioni 67 ni kikubwa sana ni bora ukaongezea fedha kidogo ukanunua gari jipya kama Hilux. Mimi sijasaini mkataba wa matengenezo na kama gharama ni hiyo sitasaini mkataba,” amesema.

 

Alipoulizwa kuhusu fedha kiasi gani inalipwa kwa ajili ya gari hilo kuhifadhiwa kwenye yadi ya Toyota, Mkurugenzi amesema, “Hakuna gharama yoyote kwa sababu yule ni mzabuni wetu, linakaa pale bila gharama yoyote.”

 

“Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkurugenzi wetu ametutia wasiwasi, alileta katika kamati ya fedha nyaraka za bei ya vipuri vya kutengenezea gari la Mkurugenzi, lakini nyaraka hizo zimenyofolewa hazikuletwa kwenye baraza hili pamoja na makabrasha ya madiwani, kitendo hiki kinanipa wasiwasi mkubwa kama kweli kiasi hicho kilichoombwa ni sahihi,” amesema.

 

Diwani wa Viti Maalumu, Justina Pereus (Chadema), ameiambia JAMHURI kuwa anashangazwa na halmashauri hiyo kutokuwa na ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato, huku watumishi wake wakipanga mipango ya kufuja fedha za walipakodi.

 

Alitoa mfano wa bajeti ya mapato ya ndani ya halmashauri hiyo mwaka wa fedha 2012/2013 ilikuwa ni 1,639,176,000/-, lakini bajeti ya mwaka huu wa fedha 2013/2014 halmashauri hiyo itakusanya mapato ya ndani 1,329,361,000/- ikiwa na pungufu ya asilimia 19 ya bajeti inayoishia Juni 2013. Pereus alimlaumu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Apolinary Mugarura, kufumbia macho matumizi mabaya ya fedha za umma, huku na yeye binafsi alitumia nafasi yake kukwamisha jitihada za halmashauri hiyo kuongeza mapato ya ndani.

 

“Mwenyekiti wetu anafumbia macho matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi, sijui anapata maslahi gani, lakini hata yeye kwa faida yake  binafsi anashiriki kukwamisha ukusanyaji wa mapato ya ndani. Kwa mfano, katika Kata yake ya Nyakahura kuna soko kubwa lakini halikuwekwa kwenye orodha ya masoko ya kukusanya mapato, na tulipouliza kwenye baraza alitumia mamlaka yake kuzima hoja hiyo,” amesema diwani huyo.

Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo imepanga kutumia Sh 19,314,305,420/- kwa mwaka wa fedha 2013/2014.