Madudu mengine TTCL

*Wasaini mkataba wa ulaji wa Sh milioni 740 kwa mwaka

*Walishirikiana na maofisa kuweka ‘walinzi hewa’ lindoni

Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), imeingia mkataba wenye utata na kampuni moja ya ulinzi wenye thamani ya Sh milioni 742 kwa mwaka. Utadumu hadi mwaka 2015.

Utata wa mkataba huo unatokana na idadi ndogo ya walinzi wanaoshiriki ulinzi kwenye vituo wanavyopangiwa, tofauti na ile inayoonyeshwa kwenye mkataba.


Ulisainiwa Mei 14, mwaka huu, kati ya Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO), Said Amir, akiwakilisha TTCL; na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo yenye anuani inayoonesha kuwa ipo Dar es Salaam na Mwanza.


Mkataba huo unaonyesha kuwa ulipaswa kuanza Mei Mosi, 2012 na kwisha muda wake Aprili 30, 2015.


Utata unajitokeza kwenye idadi ya walinzi ambao kampuni hiyo inapaswa kuwaweka kwenye vituo kama walivyofikia makubaliano na TTCL.

 

Kwa mujibu wa mkataba huo, kila ‘kichwa’ kinapaswa kulipwa na TTCL Sh 180,000 kwa mwezi.


Imebainika kuwa katika vituo kadhaa, idadi ya walinzi si ile iliyoelezwa kwenye mkataba, hiyo ikiwa na maana kwamba kampuni hiyo inalipwa fedha nyingi kwa “walinzi hewa”.


Baadhi ya vituo ambavyo vinaonyeshwa kwenye mkataba kwamba wakati wa mchana vinapaswa kuwa na walinzi wawili, imebainika kuwa ni mlinzi mmoja tu anayefanya kazi hiyo. Kwa usiku, baadhi ya vituo vinavyoonyeshwa kwenye mkataba kuwa na walinzi wanne, mara nyingi kampuni hiyo imekuwa ikipeleka mlinzi mmoja au wawili.


Kwa upande wa silaha, imebainika kuwa Mkataba unaitaka kampuni hiyo iweke walinzi 113 kwa mgawo kulingana na kanda tatu za Dar es Salaam Kati, Dar es Salaam Kaskazini na Dar es Salaam Kusini.


Kwa mchanganuo huo, malipo kwa Dar es Salaam Kati yanapaswa kuwa Sh 99,000,000 (walinzi 15); Dar es Salaam Kusini Sh 212,760,000 (walinzi 32); na Dar es Salaam Kaskazini Sh 431,280,000 (walinzi 66).


Kwa idadi hiyo, malipo yanapaswa yafanywe kwa askari 113, lakini JAMHURI imejiridhisha pasi na shaka kuwa kampuni hiyo haina idadi hiyo ya askari wanaopelekwa kwenye malindo.


Hii ina maana kwamba fedha nyingi zimekuwa zikiishia mikononi mwa kampuni hiyo ya ulinzi pamoja na maofisa kadhaa wa TTCL.


Said Amir wa TTCL, alipoulizwa hakutaka kuzungumzia wizi huu, badala yake ametaka JAMHURI iwasiliane na Mkuu wa Kitengo cha Fedha TTCL, Mrisho Shabani.

 

JAMHURI iliwasiliana na Mrisho mara kadhaa, ambapo ametaka nakala ya mkataba aweze kujiridhisha. Pamoja na kupewa nakala na maswali kadhaa, hadi tunakwenda mitamboni, Mrisho hakuwa tayari kujibu.


Mara ya mwisho alipopigiwa simu, alijibu kwa ujumbe wa maandishi akisema, “Tuko mkutano wa wafanyakazi wote na mwenyekiti wa bodi.”