Bukombe ni moja ya wilaya zinazopatikana katika Mkoa wa Geita. Wilaya hii inakadiriwa kuwa na ukubwa wa kilometa za mraba 8,055.59 huku asilimia 21.9 likiwa ni eneo la makazi (km. 1,766.59), eneo linalobaki ambalo ni kilometa za mraba 6,289 ni pori la hifadhi ya misitu na Hifadhi ya Kigosi Muyowosi.

Wilaya hii pia inalo jimbo moja la uchaguzi ambalo ni Bukombe lenye tarafa tatu ambazo ni Ushirombo, Siloka na Bukombe. Kata zilizopo Jimbo la Bukombe ni 17,  ambazo ni Katome, Bulega, Bugelenga, Butizya, Bukombe, Bulangwa, Katene, Igulwa,  Runzewe Mashariki, Busonzo, Iyogelo, Lyambamgongo, Ng’anzo,  Namonge, Runzewe Magharibi,  Ushirombo na Uyovu.

Idadi ya wakazi wa wilaya hii inaelezwa kuwa ni  watu 396,423; hii ni kutokana na sensa iliyofanyika mwaka 2012, ambao wanajishughulisha na shughuli za kilimo, ufugaji, ulinaji wa asali, uchimbaji wa madini na ujasiriamali.

Mbunge wa Jimbo la Bukombe ni Dotto Biteko (CCM), ambaye pia ni Waziri wa Madini. Jimbo hilo lina jumla ya madiwani 21, ambao kati yao 16 ni madiwani wa kata kupitia CCM, mmoja kutoka Chama cha upinzani – Chadema, huku wanne wakiwa ni madiwani wa Viti Maalumu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Dionis Myinga, amesema utekelezaji wa miradi ya maendeleo umefanyika kwa kiwango kikubwa kutokana na ushirikiano mzuri wa viongozi waliopo madarakani.

Myinga amesema kwamba viongozi wa wilaya kwa kushirikiana na mbunge wameweza kutekeleza ahadi zote zilizotolewa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

“Jambo linalofanyika hapa ni kila kiongozi kuwa mtumishi wa wananchi. Huku kwetu hakuna kiongozi ambaye hajivunii kutekeleza wajibu wake, kwani tunakaa na kufanya kwa pamoja huku tukiwashirikisha wananchi. Ushirikiano na mbunge wetu ni mkubwa, kwani tunayo bahati sasa ni Waziri wa Madini na huku kwetu kunachimbwa madini pia,” amesema.

Amesema kutokana na wilaya hiyo kuwa na mbunge ambaye ni mnyenyekevu na msikivu kwa wapiga kura wake, muda mwingi wamekuwa naye katika shughuli za maendeleo ya wilaya huku akiwa akitoa kipaumbele katika ujenzi wa shule, zahanati na vituo vya afya.

“Pamoja na kushirikiana katika shughuli za maendeleo na mbunge wetu, pia tumekuwa tukikutana kula na kunywa pamoja katika sherehe za mwaka mpya, jambo ambalo linazidi kuongeza undugu na ushirikiano katika Wilaya yetu ya Bukombe,” amesema.

Myinga amesema utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, 2015-2020 umefanikiwa kwa kiwango kikubwa kutokana na ushirikiano uliopo kati ya uongozi wa halmashauri ya wilaya na Serikali Kuu.

Bukombe ina zahanati saba mpya huku ikiwa na vijiji 52 ambavyo vinahudumiwa na zahanati hizo. Akizungumza kuhusu wananchi kupatiwa vitambulisho vya taifa, amesema wakazi wa wilaya hiyo wamekuwa wakirahisishiwa kwa kusogezewa huduma hiyo jirani zaidi.

“Tumekuwa na utaratibu wa kuwafuata maeneo yao ili iwe rahisi kwao kupata huduma hii muhimu, mafanikio ni makubwa katika zoezi hili ingawa zipo changamoto za hapa na pale kutokana na nyaraka kutakiwa kupelekwa Chato kwa ajili ya kupata kitambulisho,” amesema.

Amesema wilaya hiyo inalo tatizo la mtandao wa mawasiliano huku wakitegemea kampuni moja tu ya simu iliyoweza kuweka mitambo yake. “Tumewasiliana na TTCL ili waweze kusogeza huduma zao tuweze kufanyia kazi agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kutumia mtandao wa taifa. Wameahidi kufika kabla ya mwezi wa kumi,” amesema.

Wilaya yetu imeongeza madarasa katika shule zote wilayani ili kuendana na kasi ya ongezeko la wanafunzi pamoja na kwamba idadi ya wanafunzi bado ni kubwa sana. Tumekuwa tukiwatumia wajenzi wanaopatikana katika wilaya yetu ili kufanya matumizi yenye tija.

“Tunatumia mafundi wetu wa ndani (wa kawaida), hatutumii makandarasi (kampuni binafsi), mhandisi wa wilaya anasimamia miradi yote ya ujenzi, utaratibu huu unatusaidia kuokoa kiasi kikubwa cha fedha. Serikali inatoa Sh milioni 40 kwa madarasa mawili lakini sisi tunatumia Sh milioni 12 kwa kila darasa, hivyo tunaokoa Sh milioni sita mpaka nane.

“Fedha inayobaki tumekuwa tukiomba idhini tuitumie kwenye eneo jingine, hii ni katika kuokoa fedha na kuboresha utendaji kazi wa kila siku.

“Wilaya yetu inayo miradi 15 ya maji ambayo ni maji ya visima iliyogharimu kiasi cha Sh bilioni 10.77 huku miradi tisa imekamilika na usambazaji wa maji unaendelea. Mradi wa visima katika vijiji vitano vya Iyogero, Businda, Namsera, Lyambamgongo na Namburahera umetengewa Sh milioni 130.5, mkandarasi akiwa ni PVR Services Ltd. Pia uchimbaji wa visima katika vijiji sita vya Bugerenga, Ng’anzo, Msonga, Namonge, Msasa na Butinzya unaendelea huku mkandarasi akiwa ni Seba Construction and Drilling Co. Ltd.

“Tunatambua juhudi za serikali katika upatikanaji wa maji nchi nzima lakini huku kwetu ukombozi wa kudumu utapatikana iwapo tutaanza kupata maji kutoka Ziwa Victoria, kwa sababu visima vinavyochimbwa maji hupungua kadiri siku zinavyokwenda, huku vingine vikikauka. Tunaendelea kufanya mawasiliano na wizara husika ili ombi letu hilo liweze kupata muafaka wa kudumu.

“Kwenye sekta ya afya, serikali imetoa Sh bilioni 3.17 kwa mwaka 2018, ambazo zimesaidia katika sekta ya afya wilayani kwetu.

“Katika bajeti ya mwaka 2019/20, serikali imetenga Sh bilioni 1.6 huku Sh milioni 650 zimeshatolewa kwa ajili ya ujenzi wa barabara huku kilometa 83.2 zikiwa za changarawe na Sh milioni 950 za ujenzi wa kilometa mbili za lami hapa mjini.

“Kwa sasa tunafuatilia kutekeleza ahadi ya rais ya ujenzi wa kilometa tano za lami na tumeshapokea Sh milioni 500, tutakamilisha mapema iwezekanavyo, kwani aliahidi kuja kuangalia utekelezaji wa ahadi hiyo,” amesema Myinga.

Myinga anabainisha kwamba Wilaya ya Bukombe ni moja ya wilaya ambazo zimepewa kipaumbele katika sekta ya umeme, kwani nguzo za umeme tayari zimesambazwa kila kijiji na ifikapo mwaka 2020 vijiji vyote vitakuwa vina umeme.

Pia amesema kuwa halmashauri imefanikiwa kujenga jengo binafsi kwa ajili ya soko la madini kutokana na wilaya hiyo kuwa moja ya wilaya zinazochimba madini ya dhahabu.

“Sisi kwetu ni kusema na kutenda, tunasema kuhusu soko la madini na kutenda kwa kujenga jengo la soko la madini, hii itaongeza pato la serikali pamoja na kuwa na uhakika wa soko kwa wachimbaji wadogo,” amesema.

Mbunge wa Bukombe, Dotto Biteko, amesema kwa mujibu wa Ilani ya CCM, Kifungu cha 51 kinachohusu elimu, ameweza kushirikiana na watendaji waliopo kuboresha elimu jimboni kwake.

“Kwa kuzingatia matakwa ya ilani katika sekta ya elimu nimetekeleza yafuatayo katika idara mbili ambazo ni elimu ya msingi na elimu ya sekondari:

Elimu ya msingi

Shule zote za msingi nyingi zimeboreshwa katika kipindi cha miaka minne huku nyingi zikiwa zimeboreshwa kupitia mfuko wa jimbo na fedha nyinginezo kutoka taasisi mbalimbali ili kufikia azima yetu ya kuboresha elimu katika jimbo letu kama ambavyo niliahidi kwenye uchaguzi.

Shule ya Msingi Ibamba 

Tumejenga vyumba vinane vya kisasa vya madarasa pamoja na madawati, ujenzi wa vyoo matundu 20 ambavyo vyote vimeghalimu Sh milioni 93. Ujenzi umekamilika na vyote vinatumika katika kuboresha elimu ya watoto jimboni.

Shule ya Msingi Nyakonga

Upatikanaji wa Sh milioni 35 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vinne na ofisi moja katika Shule ya Msingi Nyikonga. Ujenzi huu utasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule hii, pia itasaidia kuongeza ufaulu kwa shule zetu.

Shule ya Msingi Bulumbaga

Tayari tumepata fedha Sh milioni 10.3 kwa ajili ya

ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa pamoja na ofisi moja ya walimu, ujenzi upo katika hatua za mwisho ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya shule.

Shule ya Msingi Namonge

Ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na matundu sita ya vyoo ni kielelezo cha namna tunavyotekeleza. Tumefanikiwa kujenga majengo hayo kwa Sh milioni 66.

Elimu ya sekondari

Katika kipindi cha miezi mitatu tumeweza kujenga mabweni vyumba 20 pamoja na bwalo. Hii ni katika kuboresha elimu ya sekondari wilayani kwetu pamoja na mkakati wa kupata kidato cha tano na cha sita.

Mwaka 2020 tutakuwa na shule mbili ambazo zitakuwa za kidato cha tano na cha sita, ambazo ni Bukombe na Businda. Tayari maandalizi yamefanyika huku Shule ya Businda ikiwa na mabweni mawili kwa ajili ya wasichana na Bukombe ina mabweni mawili na bwalo.

Shule ya Sekondari Businda

Ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa, ofisi moja ya walimu na vyoo majengo matatu yenye matundu 24 umepunguza changamoto ya upungufu wa madarasa. Ujenzi huu umekamilika na majengo yote yanatumika, ikiwa ni pamoja na maandalizi ya awali kwa shule hii kutumiwa na wanafunzi wa kidato cha tano mwaka 2020.

Majengo haya yamejengwa na kukamilika kwa Sh milioni 110.

Shule ya Sekondari Busonzo

Ujenzi wa maabara katika shule hii kwa kiasi kikubwa umefanikiwa kutokana na nguvu za wananchi, jumla ya Sh milioni 40.1 zilipatikana na zilikamilisha maabara. Umuhimu wa shule hii haupimiki kwa sababu unawaondolea usumbufu wanafunzi wa Kata ya Busonzo ambao husafiri umbali mrefu na aidha shule hii inaongeza idadi ya sekondari jimboni kwetu.

Shule ya Sekondari Ushirombo

Sh milioni 60 zimetumika kujenga madarasa matatu ya mfano huku madarasa haya yakiwa moja ya madarasa/mradi ambayo baadhi ya wilaya huja kujifunza kutokana na kujengwa kwa ustadi mzuri zaidi.

Shule ya Sekondari Igulwa 

Shule hii ni moja ya shule zinazotegemewa katika kusaidia

kupunguza idadi kubwa ya wanafunzi katika shule za Katente, Ushirombo na Businda. Tayari imepauliwa kwa gharama ya Sh milioni 6.9 huku mazingira bora ya shule yakiendelea kuboreshwa ili iwe shule rafiki kwa wanafunzi. 

Shule ya Sekondari Iyogelo

Benki ya Dunia imetoa fedha kiasi cha Sh milioni 391 ambazo zimetumika kujenga nyumba moja ya walimu inayokaliwa na familia sita, vyumba vitatu vya madarasa, majengo matatu yenye matundu kumi ya vyoo pamoja na matenki mawili ya maji.

Ujenzi huu umepunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa madarasa na upungufu wa nyumba za walimu, pia tumepeleka mtambo wa umeme wa Rex Solar Energy shuleni hapo ambao unawasha madarasa yote, hivyo kuwasaidia wanafunzi kupata muda wa ziada wa kusoma huku giza kuwa historia shuleni hapo wakati tukisubiri umeme wa REA.

Shule ya Sekondari Katome

Kata ya Katome inayo shule hii moja tu ya sekondari, hivyo ni shule tegemezi zaidi, shule hii imeendelea kuboreshwa mazingira yake ya elimu ikiwa ni pamoja na majengo yanayohitajika. Serikali kwa kushirikiana na ofisi ya mbunge itaendelea kuboresha elimu pamoja na huduma zote muhimu kwa wananchi ili waweze kuishi maisha bora.

Shule ya Sekondari Namonge 

Benki ya Dunia imetoa kiasi cha Sh milioni 289.8 ambazo zimesaidia kujenga nyumba moja ya watumishi ya kukaa familia sita, vyumba vinne vya madarasa pamoja na majengo ya vyoo matundu kumi. Majengo yote yamekamilika na tayari yanatumika.

Kukamilika kwa mradi huu kumesaidia kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa walimu na watoto.

Tunaendelea kuboresha mazingira katika shule zetu, kwetu tuna kaulimbiu ya kusema na kutenda. Tunasema lakini tunatenda zaidi, hii Bukombe unayoiona si ile ya wakati ule. Tumeazimia kuwa na Bukombe ya mfano,” amesema Biteko.

Itaendelea toleo lijalo…

By Jamhuri