Na Phabian Isaya

Katika toleo lililopita tuliishia katika aya isemayo: “Simuoni siku kadhaa sijui amepotelea wapi? alisema kijana wake aliyekuwa na dharau kwa kijana Noel. Alikuwa hamuamini kwa lolote na alimuona kama bango bovu lililofutika maandishi. Sasa endelea….
“Mmmh! Vijana bhana, kwa hiyo anategemea ata… siku moja katika umaskini alio nao? alisema baba mwenye nyumba hiyo naye akiwa afikirii kama Noel anaweza kutoka kimaisha kupitia kitu kile alichokuwa anakipenda maishani mwake.
Maongezi yalikuwa yakiendelea, familia ya kina Noel ilikuwa haithaminiki, watu waliowazunguka waliiona ni familia iliyo kuwepo tu isiyo na mbele wala nyuma.
“Ni kweli siku mbili, tatu hizi haonekani, alisema mama wa nyumba hiyo.
Usiku huo eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika hosteli za wanachuo, Gilbeth pamoja na binti Anthonia waliyesoma na Noel pamoja na Gilbeth walikuwa wamekaa katika mgahawa wa chuo wakiwa wanaongea. “Dah! Noel sijui yuko wapi? alisema Anthonia akiwa amemkumbuka Noel.
“Sijui yuko wapi, sijui yuko Mwanza, alikuwa anapata ugumu kuweza kufahamu Noel alipokuwa, maana hakuwa na uhakika wowote ule.
“Nasikia alikuwa akitangaza redioni…. walikuwa wakikumbuka mengi juu ya Noel ambaye waliamini huenda atakuwa katika maisha yasiyokuwa na matumaini.
“Ndoto yake ya kuandika vitabu itakuwa ndiyo imeishia hapo, alisema Gilbeth. Kwa maneno yake alikuwa akiamini huenda Noel hapo ndiyo ukawa mwisho wa maisha yake.
“Sisi tuliobahatika tusome kuja kusaidia wenzetu, alikuwa akiongea kwa kumaanisha Anthonia, binti ambaye alikuwa amebadilika. Alikuwa akiishi maisha yenye matumaini. Anthonia na Gilbeth wote walikuwa wanasoma shahada ya kwanza ya sheria chuoni hapo.
 “Jamani eeeh! Tusimuwazie sana Noel, tuangalie maisha yetu kwanza, alisema Gilbeth kutokana na kufika kwake chuoni alikuwa amemtenga Noel kwa kiasi fulani. Mitihani ya kuhitimisha muhula wa chuo ilikuwa nayo imekaribia, ulikuwa umesalia mwezi mmoja tu kuweza kuanza kwa mitihani hiyo.
 “Tukimaliza mitihani nitakwenda Mwanza nionane na Noel, nione yuko katika hali gani, alisema Gilbeth. Mfumo wa maisha ya chuo kwa kiasi fulani ulikuwa umeanza kumbadilisha Gilbeth.
Lilikuwa juma moja tu limepita baada ya wanafunzi wa chuo kuingiziwa fedha za kujikimu kimaisha katika akaunti zao binafsi, wanafunzi walikuwa na pesa, maisha yaliwaendea wengi wao vema.
Gilbeth akiwa anaongea na Anthonia mara akaja rafiki yake ambaye aliyekuwa akisoma naye kitivo kimoja, akasalimiana nao, kisha akaja na wazo tofauti.
“Jamani tuko vizuri sana, kwa nini tusiende Maisha Club kuburudika kidogo walau kwa leo tu?” Anthonia na Gilbeth wanakabaliana na wazo alilokuwa amelitoa mwenzao.
“Ni kweli, hasa kuhusu mihangaiko ya hapa chuoni, alisema Anthonia akiwa anasimama akionyesha utayari wa kwenda klabuni. Walifanya kila liwezekanalo, kisha wakaondoka.
Walikuwa ni watu waliobadilika, tabia na mienendo yao ilikuwa ni tofauti na walivyokuwa wamefika chuoni hapo, walitaka kuendana na hali halisi ya Jiji la Dar es Salaam.


Kule katika studio za redio alikokuwa akifanyia kazi Noel na kufukuzwa kutokana na upotevu wa vifaa, wakawa katika udhohofu, hususan katika kipindi alichokuwa akikiendesha Noel.
Siku zote mwenye chake atabaki kuwa mwenye chake. Aliyekuwa akiendesha kipindi alikuwa akiendesha pasipokuwa na weledi sawa na ule aliokuwa nao Noel.
Mkurugenzi wa redio aliingia katika mawazo sana. Wakati wa usiku alikuwa akiumiza kichwa huku akishauriana na mwenzake ambaye alikuwa meneja uzalishaji wa vipindi. “Dah! Kuna pengo limeanza kuonekana, alisema huku akiwa anatikisa kichwa chake.
“Pengo la kitu gani? mkurugenzi akamuelezea kwa ufupi: “Kipindi alichotengeneza Noel kimepwaya, ni lazima tulitazame hilo.
Wakainamisha vichwa chini kufikiri namna ya kufanya. “Jambo la msingi tumtafute Noel walau kama ni kumlipa fedha kidogo tuwe tukimlipa, alisema mkurugenzi akiwa ameona umuhimu wa uwepo wa Noel. 
“Tutampata vipi? Mkurugenzi akakumbuka siku moja alikuwa akisoma gazeti fulani akaona makala aliyokuwa ameandika Noel. Akamuita dada aliyekuwa mapokezi. “Niitie Mariamu mara moja. Meneja uzalishaji wa vipindi akasimama na kutoka ofisini ili kwenda kumuita dada wa mapokezi.
Mkurugenzi alikuwa akiwaza Noel atakuwa wapi. “Lakini yule kijana ana kipaji katika hii tasnia ni vema aendelee kuwepo hapa ili kipindi kiweze kusonga, alikuwa akiwaza.
Wakati akiwa katika mkanganyiko huo, muda huu ulikuwa ni wa kile kipindi cha Noel ambacho alikuwa amekibuni kurushwa hewani.
Wale Wakorea waliofunga safari wakati wa nyuma kuja Mwanza kwa ajili tu ya utangazaji mzuri wa Noel, nao walikuwa wanasikiliza wakiwa Dar es Salaam, wakawa wakijadiliana kuhusu yule aliyekuwa akitangaza.
“Mbona hatangazi kama Noel! Walikuwa wakishangaa. “Hamna, Noel nimegundua ana uwezo mzuri.” Walikuwa wakijenga kila hoja Wakorea hao ambao walikuwa mezani muda huo wakila. 
“Ni kweli dah! Tutamkumbuka kwa sauti yake nzuri. Mchungaji alisema amekwenda kusoma wapi? 
Walikuwa wamekumbuka namna Noel alivyokuwa mahiri. “Mchungaji alisema amekwenda nchini Urusi kaika Chuo Kikuu cha Mosow kusoma, ” mmoja wao alisema.
Katika maongezi wakajikuta wanapata hamasa ya kuweza kumpigia mchungaji ili kujua mambo yalikwendaje. Simu ya mchungaji iliita kisha akapokea.
“Haloo! Habari za huko, aliongea mchungaji kwa sauti ya chini. “Nzuri mchungaji, hivi Noel anaendeleaje huko Moscow? Mchungaji akawapa maneno ya faraja.
“Anaendelea vema, tumuombee sana kijana huyu. Maneno yao juu ya Noel yalikuwa ni maneno yaliyojaa baraka zilizo halisi kutoka ndani ya mioyo yao. “Atafanikiwa, tunaomba namba yake ili tuwasiliane naye,” alisema mmoja wao. Mchungaji akawatajia namba ya Noel, kwa maana alikuwa ameikariri.
Yule dada wa mapokezi akaingia ofisini kwa mkurugenzi, kisha mkurugenzi akasema: “Lile gazeti lililokuwa na makala aliyoandika Noel ninaliomba. Akatoka kwenda kulisaka lilipo. Mkurugenzi hakutaka kusema kusudio lake lilikuwa nini hasa. Akafika pale mapokezi akaangaza na kuliona, kisha akalichukua na kumpelekea bosi ofisini kwa mwendo wa haraka. 
“Bosi hili hapa. Wakasimama wale wawili kuangalia ni nini hasa mkurugenzi alichokuwa akitaka kukifanya. Akalifungua gazeti kisha akafika ukurasa uliokuwa na makala ya Noel, akakutana na kila kitu cha Noel kikiwa pale, akashusha pumzi yake na kusema:
“Afadhali, ngoja nichukue mawasiliano yake, kisha nitampigia kesho nikiwa nimetulia.” Akalifunga gazeti. Hivyo wale watu wawili wakafahamu maana ya mkurugenzi kuulizia gazeti lile.
Mkurugenzi alipanga kuongea na Noel amfurahishe kwa malipo madogo yoyote ili kusudi kile kipindi kiweze kuendelea, akijua Noel atakuwa mtaani akihangaika kutafuta mkate wake wa kila siku.
“Hata nikimpa laki moja Noel atakubali, si mbaya, lakini kipindi kiweze kuendelea, alisema mkurugenzi akiwa anamwambia yule meneja wa vipindi.
Wakorea wale wakiwa mezani wakila walikuwa wakiendelea kula huku wakiongea kwa mitizamo chanya juu ya Noel. “Huko Urusi anaweza kufanya mambo mazuri pia, alisema Mkorea mmoja ambaye alikuwa anauamini uwezo wa Noel.
“Ni kweli, lakini unajua Mungu huwa anakusudi fulani na maisha yetu, walikuwa wakimtazama Noel kwa jicho la tatu. “Pengine anaweza kuwa ndiye mtu atakayeleta mapinduzi ya heshima katika tasnia ya uandishi, mmoja wao alisema. Walikuwa wamepanga mara kutakapokucha waweze kufanya naye mazungumzo na kumshauri mambo kadha wa kadha.


Noel akiwa chumbani kwake anafungua begi lake mara baada ya kumaliza kusali na kusoma kile kitabu. Anagundua hawezi kukimaliza kwa usiku ule, hivyo anaamua kufungua begi lake kuangalia mawasiliano ya wale jamaa wawili kutoka nchi ya Zimbabwe na Afrika Kusini.
Watu hao alipanda nao gari moja kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, ambao walikuja Tanzania kufanya utafiti. Mmoja alikuwa raia wa Zimbabwe na mwingine wa Afrika Kusini.
Walikuwa ni wahadhiri wa chuo kikuu, mmoja kati yao akiwa profesa na mmoja akiwa ni daktari wa falsafa. Aliyekuwa profesa ndiye alimchangamkia sana Noel na kumuachia mawasiliano yake. Noel akapata zile namba pamoja na barua pepe zao alizokuwa ameandikiwa na yule profesa.
Akachukua namba na kumpigia usiku huo huo. Noel alitaka kujenga uhusiano mzuri ambao utasababisha yeye kutengeneza marafiki nje ya taifa lake, kwa kuwa alikuwa na mambo mengi aliyoyalenga kwa mtazamo mpana zaidi. 
Akaipiga ile namba ikaita, kisha yule profesa raia wa Zimbabwe akapokea: “Haloo!! aliitikia profesa huyo Mzimbabwe. “Mimi ni yule kijana tuliyekutana pindi tunaelekea uwanja wa ndege kutokea hotelini nchini Tanzania, alijieleza vema Noel. Kisha akamkumbuka, wakaongea maneno mengi yenye kufarijiana.
 “Sawa Noel, hii namba yako nitaitunza katika simu yangu.” Maongezi hayakuishia hapo waliendelea kuongea. “Nimefika katika Jiji la Moscow, alisema. Ilikuwa ni furaha kwa profesa kusikia kijana amefika salama. “Sasa wewe kazana, hakikisha unatengeneza wigo wa watu wengi wenye tija, alimsihi Noel katika hilo.

Itaendelea

By Jamhuri