Yanga-leo-72Tanzania kwa sasa inabebwa na Yanga katika anga za michuano ya kimataifa, kutokana na uwezo ambao wamezidi kuuonesha kwenye eneo hilo na ligi la hapa nyumbani. Hilo halina ubishi.

Hiyo imekuja baada ya Yanga kufuzu kwa hatua ya makundi ya michuano Kombe la Shirikisho Afrika wiki mbili zilizopita. Yanga imefuzu hatua hiyo baada ya kuitupa nje Sagrada Esperanca ya Angola kwa jumla ya mabao 2-1, ikipigwa ugenini 1-0 lakini ushindi wa 2-0 walioupata nyumbani uliwabeba Wanajangwani hao.

Mara baada kutinga hatua hiyo, kumeibuka minong’ono ya hapa  na pale kuhusu uwakilishi wa Tanzania mwakani kwenye michuano ya klabu – inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Sintofahamu hiyo iliyoanza kuzuka, ni kuwa labda Simba inaweza kushiriki michuano hiyo mwakani kupitia mgongo wa Yanga wa kufika hatua hiyo kwenye michuano ya CAF.

La hasha! minong’ono hii ni sawa na ndoto za Ali Nacha kutokana na kanuni za michuano hiyo kuibana Tanzania na nchi zote za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) isipokuwa Sudan tu, ambayo ndiyo imekuwa mkombozi wa ukanda huo kwa kuwa na rekodi ya kufanya vizuri.

Najua unataka kujua nini hicho hasa kinachoibana Tanzania na nchi za Cecafa kwa ujumla isipokuwa Sudan? Jibu ni moja tu –  hakuna hata nchi moja iliyoweza kufikisha pointi 12 au kuendelea zinazohitajika ili taifa fulani liweze kuongezewa timu kutoka moja hadi mbili katika kila michuano ya CAF ngazi ya klabu.

Hiyo inatokana na timu za wawakilishi za ukanda huo kutokuwa na rekodi ya kufanya vizuri kwenye ya michuano hiyo; mara nyingi zikiishia raundi za awali ambazo hazina pointi, kwa mujibu wa viwango vipya vilivyotolewa na CAF kuanzia mwaka 2010 hadi 2014.

Na viwango vijavyo vya miaka mitano mingine ijayo, vitatolewa 2018 na hivi vitaangalia zaidi matokeo ya klabu zetu za hapa Tanzania katika michuano hiyo mikubwa.

Hivyo basi, hatuna budi kukaza buti ili ndoto zetu za kuwakilishwa na klabu nne katika michuano hiyo mikubwa barani Afrika mwaka 2018. 

Rekodi ya viwango hivyo vya CAF inauumbua ukanda wa Cecafa kwani hakuna hata nchi moja – ukiiondoa Sudan – iliyoweza kujinyakulia hata pointi moja kutokana na kufanya vibaya kwenye michuano hiyo.

Sudan yenyewe imekuwa ikibebwa na timu kongwe za huko za El Merreikh na Al Hilal, ambazo zimeifanya nchi hiyo kufikisha jumla ya pointi 33 wakiwa nafasi ya tano kwa mujibu wa viwango vya CAF na hiyo ni kutokana na kufanya vizuri kwa timu zake hizo.

Kwa Yanga kuingia hatua ya makundi (robo fainali) ya Kombe la

Shirikisho Afrika mwaka huu, sasa kunaihakikishia Tanzania kuandika pointi moja na sasa ikidaiwa pointi nyingine 11 ili iweze kuongezewa timu moja moja katika kila michuano hiyo mikubwa ya klabu barani Afrika.

Endapo Yanga ikifanya vizuri mwaka huu na mwakani ikizidi

kufanya pamoja na Azam FC, basi bila shaka mwaka 2018 kuna uwezekano Tanzania tukawakilisha timu mbili Ligi ya Mabingwa na mbili Kombe la Shirikisho.

Hiyo itatokana na Yanga endapo ikiingia hatua ya nusu fainali ya

michuano hiyo, basi itakuwa na uhakika wa kuifanya Tanzania kuwa na alama mbili na ikifika fainali, basi nchi hiyo itajikusanyia pointi tatu kama timu hiyo itapoteza fainali, na pointi nne kama Wanajangwani hao wakiibuka mabingwa.

Kwa Afrika ni nchi 12 pekee ambazo zimejihakikishia nafasi ya kuingiza timu mbili mbili katika kila michuano hiyo CAF – Tunisia ikiwa kinara, ikifuatiwa na Misri, Congo DR, Algeria, Sudan, Ivory Coast, Morocco, Cameroon, Congo Brazzaville, Mali, Nigeria na Afrika Kusini iliyoanza kufanya vizuri kwa miaka ya hivi karibuni.

Ni mtihani mkubwa sana kwa Tanzania na nchi za Cecafa inayotakiwa kuhakikisha inaufanya, ili nchi wanachama ziweze kuongezewa uwakilishi katika michuano hiyo na ni lazima zijitutumue sana kuweza kufikia mafanikio waliyofikia timu hizo 12.

Kwani ili ujihakikishie ubora wewe mwenyewe na nchi yako kufika huko, ni lazima uweze kupambana vilivyo na mataifa hayo 12 yanayoongoza kwa ubora katika ngazi ya klabu barani Afrika, la sivyo kila mwaka tutaishia kupeleka timu moja moja.

Kimahesabu ndani ya miaka miwili ijayo kwa upande wa Tanzania, ili tuweze kupeleka timu mbili mbili katika kila michuano ni lazima Yanga mwaka huu ihakikishe inaingia fainali na kuchukua kombe la michuano hiyo ili iihakikishie nchi pointi nne.

Na pia mwakani Yanga (Ligi ya Mabingwa) na Azam FC (Kombe la Shirikisho) zitakazoliwakilisha Taifa katika michuano hiyo, zihakikishe zinachukua makombe ya michuano hiyo.

Yanga imepangwa Kundi A na timu za TP Mazembe ya DRC Congo, MO Behaia ya Algeria na Madeama kutoka Ghana.

Endapo Yanga itachukua kombe hilo itaondoka na kitita cha dola 625,000 (sh. bilioni 1.3), mshindi wa pili dola 432,000 (sh. milioni 907) na timu itakayoshika nafasi ya pili na tatu katika kila kundi zitapata dola 239,000 (sh. milioni 500).

Hivyo basi, tunahitajika kuiombea Yanga ifanye vizuri katika michuano hiyo, ili tuweze kutimiza ndoto za kuwakilishwa klabu nne kama ilivyokuwa kwa mataifa ya Kiarabu.

By Jamhuri