Kampuni ya Tandahimba Quality Control System, iliyoshinda kwa utata zabuni ya kuendesha maghala ya Muungano wa Vyama vya Ushirika Wilaya za Tandahimba na Newala (TANECU), inahaha ngazi za juu ili ikabidhiwe maghala hayo.

Kampuni hiyo inatafuta njia za mkato, ikiwezekana kwa kumtumia Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, ili ikabidhiwe shughuli hiyo yenye ukwasi mkubwa.

Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Leseni za Maghala, Fidelis Temu, ameiandikia Tandahimba Quality Control System barua ili ijibu hoja za pingamizi zilizotolewa na wadau kadhaa kwa maandishi.

Kwa upande wake, Temu ameulizwa na JAMHURI na kusema; “Kweli tumepokea pingamizi, tumewaandikia barua tukitaka wajibu hoja zilizotolewa na watoa pingamizi, lakini hawajajibu.”

Kwa mujibu wa Sheria Namba 10 ya mwaka 2005, kampuni hiyo imepewa siku saba iwe imejibu hoja hizo. “Tulishawapa barua, lakini hawajajibu. Siku saba zitakamilika Jumatatu ijayo (Septemba 29, 2014),” amesema Temu.

Lakini kuna habari zisizo rasmi ambazo zinadai kwamba wenye kampuni hiyo ya Tandahimba wamefanya kila waliloweza ikiwamo kuwasiliana na Ofisi ya Waziri mwenye dhamana ili ushindi wao uendelee kutambuliwa.

Hata hivyo, Temu amekanusha vikali madai hayo kwa kusema “Ni uongo, sijapokea shinikizo lolote linalotaka niwape leseni kampuni ya Tandahimba Quality Control System, nakuhakikishia huo ni uongo; Waziri hajanipa shinikizo. Kwanini nidanganye? Hii haitakuwa kampuni ya kwanza kuinyima leseni, zipo nyingi ambazo zimenyimwa.

“Tunaangalia vigezo vilivyowekwa kisheria, kama havijafikiwa na kampuni husika, hatutoi leseni. Hii ni shughuli ya mamilioni ya shilingi, kwa hiyo lazima tuwe makini kwa kufuata sheria.”

Hata hivyo, sheria husika inatamka bayana kuwa mwenye uamuzi wa mwisho wa kutoa au kutotoa leseni ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika ambaye kwa sasa ni Chiza. Ni kwa mantiki hiyo, na kwa mamlaka aliyonayo kisheria; kumekuwapo habari kwamba waziri ameshaamuru Tandahimba ipewe leseni.

Alipotafutwa Waziri Chiza kuzungumzia shinikizo lake la kutoa kibali, alisema: “Jamani mimi nina mwisho wa mipaka yangu ya kazi. Sifahamu lolote kuhusu vibali hivyo, sijaviona na wala sihusiki kushinikiza.” Ingawa JAMHURI lina taarifa za uhakika kwamba viongozi wa  kampuni hiyo walimfuata Waziri kushinikiza matakwa yao.

Hayo yakiendelea, imebainika kuwa watu wengi waliotajwa kuwa ndiyo wamiliki wa Kampuni ya Tandahimba Quality Control System, hawapo. Habari za kiuchunguzi zinaonesha kuwa majina ya watu hao ‘hewa’ yalikabidhiwa kwa Mweyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Tandahimba, Bakari Fumao, Septemba 23, mwaka huu.

Lengo lilikuwa kumtaka mwenyekiti huyo asaidie kujua kama kweli wenye Tandahimba Quality Control System wapo, au ni majina tu yaliyotungwa kwa lengo la watu kujipatia fedha kupitia maghala hayo ya wananchi. Kwenye maombi ya zabuni, Tandahimba Quality Control System Limited wamiliki wake wametajwa kuwa ni Abdallah Ally Nyange na wenzake; wa SLP 93, Tandahimba, Mtwara; Khalida Abdala Mwataha wa SLP 93, Tandahimba, Mtwara; Hassan Dadi Nassoro wa SLP 93 Tandahimba; na Juma Salumu Mkata wa SLP 93, Tandahimba, Mtwara.

Hata hivyo, majina hayo yamezua mjadala huku baadhi ya maelezo yakidai kwamba hakuna wenye majina hayo, wengine wakisema yameunganishwa majina ya watoto na ya wazazi wa baadhi ya viongozi na watendaji wa TANECU.

Mkazi wa Newala, Ahmed Hassan, katika barua yake ya pingamizi kwa Temu, anasema, “Tafadhali rejea tangazo lako ulilolitoa tarehe 27 Agosti 2014. Nawasilisha pingamizi la Ms Tandahimba Quality Control Systems Ltd kupewa leseni ya kuendesha Ghala Na. 1&2 Malopokela Block ‘A’ (TANECU Warehouse) kwa sababu zifuatazo:

“Kampuni ya Tandahimba Quality Control Systems Ltd iliyoomba kwenu leseni ya kuendesha ghala Na. 1&2 (TANECU Warehouse) baadhi ya wamiliki wake walioorodheshwa ni wafanyakazi wa TANECU ingawa wametumia majina ambayo si rahisi kujua ni wao.”

Hassan anatoa mfano wa majina hayo kuwa ni la Hassan Dadi Nassoro wa SLP 93 Tandahimba ambaye jina lake halisi anadai kuwa ni Hassan Dadi Chipyangu, na kwa jina maarufu la Udede. Huyu, anadai ni Meneja wa Tawi la TANECU Tandahimba. Aidha, kazi aliyopewa Famao imekuwa ngumu kwani baadhi ya simu za watu wanaodaiwa kuwa ndiyo wamiliki wa Tandahimba Quality Control System zimekuwa hazipatikani, jambo linalozidi kuthibitisha kuwa huenda kweli majina hayo ni ‘hewa’ na pengine kampuni yenyewe ina utata kama kweli ipo kihalali.

Kati ya wamiliki wa kampuni hiyo, mmoja (jina tunalo) imebainika ndiye aliyepo, lakini kwa miezi kadhaa sasa anatibiwa jijini Dar es Salaam. Hofu ya maghala hayo kukabidhiwa kwa kampuni ambayo wamiliki wake hawajulikani imewaingia wananchi wengi, hasa kutokana na historia ya kupotea kwa mazao yao na hivyo kupata hasara kubwa.

Wakati haya yakiendelea, wakulima na watu wanaoweka pingamizi, wanasema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara haijaonesha dhamira ya kuwasaidia ili wasiingie mikononi mwa watu wasio waaminifu wanaoweza kuwaliza wakulima. Kampuni ya Tandahimba Quality Control System inadaiwa kuwa wamiliki wake ni ama viongozi wa TANECU, au watoto na ndugu zao; na kwamba majina mengine yanayotajwa yametungwa ili kuficha ukweli.

Biashara ya kuhifadhi mazao maghalani ina ukwasi mkubwa kwani kila mkulima hukatwa Sh 14 kwa kila kilo moja ya korosho inayohifadhiwa humo kwa miezi mitatu. Baada ya muda huo, gharama hizo huongezeka. Sheria ya Stakabadhi Ghalani inawataka wamiliki wote wa maghala kusajili na kuthibitishwa maghala hayo ili yaingie kwenye biashara ya kutunza mali za wakulima. Kwa Tandahimba na Newala, maghala mengi ni kwa ajili ya kuhifadhia korosho.

Kwa kuwa TANECU ni kati ya wamiliki wa maghala makuu, na kwa mujibu wa Sheria ya Ushirika, Juni 5, mwaka huu walitangaza zabuni ili kupata waendeshaji wa maghala hayo. Kampuni nane zilipeleka zabuni lakini mshindi akawa Tandahimba Quality Control System Limited, inayodaiwa kuwa na nasaba na viongozi wakuu wa TANECU.

Mwenyekiti wa TANECU, Yusuph Nannila, akizungumza kwa simu na JAMHURI hivi karibuni, alisema yeye si msemaji wa chama hicho.

“Siwezi kufanya kazi kwenye meseji au simu, mimi ni kiongozi tu, mtafute GM (Meneja Mkuu). Anaitwa Mpakate. Hayo ni masuala ya kiutendaji na si ya kiutawala,” alisema Nannila.

Kwa upande wake, Mpakate anakiri kuwa ni kweli kampuni ya Tandahimba Quality Control System Limited imeshinda zabuni hiyo, lakini akasema si wajibu wake yeye kama Meneja au TANECU kuwajua wamiliki wa kampuni hiyo.

Akizungumza kwa ukali, Mpakate alisema, “Hilo la kampuni waulize BRELA (Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni). Sisi tunaangalia karatasi, hatuangalii majina ya watu kama wapo au hawapo. Hiyo ni kazi ya BRELA.

“Sasa unauliza kama wenye majina hayo wapo au hawapo ina maana una mashaka (shaka) na Serikali? Vigezo tulivyoweka vimetimia, suala la nani ni nani kwenye kampuni hilo si letu,” alisema na kuongeza: “Nasema siyo kazi yangu hiyo. Unadhani naweza kumfuata kila mtu aliyeomba kumjua ni nani? Kampuni zilikuwa nane ambazo ziliomba, wote nitawajua? Sisi tunaangalia karatasi tu, basi.”

By Jamhuri