pg 1Uhusiano kati ya Tanzania na Rwanda umeimarika kwa kiwango cha hali ya juu na sasa Rais wa Rwanda, Paul Kagame amekubaliana na Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Mafuli mizigo yote ya nchi hiyo ianze kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI, umebaini kuwa makubaliano haya yalifikiwa wakati wa ziara ya kwanza ya Rais Mafuli aliyoifanya nje ya nchi tangu achaguliwe Oktoba 29, mwaka 2015 ambapo Aprili 6, 2016 Rais Mafufuli alifanya ziara ya kwanza nje ya nchi na kuanzia nchini Rwanda.

Katika kurejesha ukarimu, Rais Kagame alikubaliana na Rais Magufuli kuwa washirikiane kujenga miundombinu ya kisasa hasa reli, inayoweza kusafirisha mizigo mikubwa. Benki ya Exim ya China imekubali kutoa mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani bilioni 7.6 zaidi ya Sh trilioni 16 za Kitanzania kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa mradi huo mkubwa wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa unaotarajiwa kuanza katika mwaka huu wa fedha.

Ujenzi wa reli ya Kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge) utaziwezesha nchi za Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kuitumia reli hiyo kusafirisha mizigo ikiwamo madini ya shaba yanayopatikana kwa wingi katika Jimbo la Katanga nchini Congo yanayoweza kupakiwa kupitia Kigoma.

Rais wa Benki ya Exim ya China Liu Liang amemueleza Rais wa Tanzania Dk. Magufuli katika Ikulu ndogo ya Chamwino mkoani Dodoma kuwa pamoja na kutoa fedha hizo zitakazofanikisha ujenzi wa kilometa 2,190 za reli ya kati, benki hiyo itashirikiana na Tanzania katika kubadilishana uzoefu na utaalam katika ujenzi na uendeshaji wa reli hiyo.

“Jumanne ijayo (leo) tutakuwa Rwanda kufungua ofisi kubwa ya TPA, ambapo kwa makubaliano yaliyopo tutahakikisha hata kikombe kinachosafirishwa kutoka Rwanda kwenda nje ya nchi au kutoka nje ya nchi kwenda Rwanda kinapitia katika Bandari ya Dar es Salaam… tayari timu nzito ya wataalam imetangulia Rwanda na mimi nakwenda Jumatatu (jana) kuhakikisha tunafungua ofisi nzuri na kubwa itakayotoa huduma bora kwa taifa hilo liweze kusafirisha mizigo yake kupitia Bandari ya Dar es Salaam,” Injinia Deusdedit Kakoko, Mkurugenzi Mkuu wa Bandari ameliambia JAMHURI mwishoni mwa wiki.

Injini Kakoko amesema tatizo la kuchelewesha mizigo ya wateja sasa linafikia ukomo, na anataka mteja mzigo wake ukifika Bandari yoyote iliyopo chini ya TPA utolewe ndani ya siku mbili au tatu na si zaidi ya hapo. “Tunaimarisha huduma, na huduma zetu ndizo zitakazorejesha na kuongeza wateja, si vinginevyo,” amesisitiza.

Mkurugenzi huyo ambaye ana miezi miwili sasa tangu ameteuliwa kuwa DG wa TPA, amesema uchunguzi alioufanya amebaini ulikuwapo mtandao hatari uliokuwa unakwamisha mambo kwani baadhi ya wafanyabiashara wao ni waagizaji wa mizigo, wanamiliki kampuni za uwakala wa kupakia na kupakua mizigo bandarini (clearing agency) na wanamiliki bandari kavu (ICDs).

Anasema huo ni mgongano wa masilahi wa wazi, hivyo kuanzia sasa hakuna atakayeruhusiwa kufanya kazi zaidi ya moja bandarini. Anaongeza kuwa katika kuhakikisha Bandari haiwi mateka wa wafanyabiashara kama alivyozuia magari kupelekwa kwenye ICD kabla ya mizigo kujaa bandarini, vivyo hivyo watasaini mikataba mipya kuzuia makontena yasipelekwe ICD hadi kutokee ufinyu wa nafasi bandarini.

Injini Kakoko amesema kwa sasa tayari wamiliki wawili wa ICDs wamekubali kusaini mkataba mpya, na wengine bado wanasema wakae wazungumze, ila yeye anasema haoni sababu ya kuzungumza zaidi ya kuboresha utendaji kazi wa Bandari ikaweza kupokea na kusafirisha mizigo mingi kwa wakati na kwa uaminifu wa hali ya juu.

Amezitaka idara nyingine zinazohusika na mizigo inayoingia bandarini kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) nazo kuhakikisha zinaweka viwango vitakavyowahisha uondoshaji wa mizigo bandarini, kwa kuondoa urasimu kama upo.

“Jumanne ya Agosti 16, nitakaa na wahariri wakuu wa vyombo mbalimbali vya habari kueleza tuliyofanya ndani ya miezi miwili. Kikubwa tunataka kushika soko la Rwanda kwa asilimia 100. Tunataka nchi za Malawi, Zambia na nyingine nazo zipitishe mizigo yao Tanzania,” amesema na kuongeza kuwa kazi hiyo ameikabidhi kwa Idara ya Masoko inayopaswa kuwasiliana na kila mteja aliyepata kupitisha mzigo Bandari ya Dar es Salaam au Bandari yoyote nchini ikiwa hapitishi tena mizigo kumuuliza nini kilimkwaza, na kama bado kipo kitatuliwe.

Anasema mapato yatakayopatikana yatawekezwa katika Bandari kuhakikisha inakuwa na teknolojia ya kisasa na kuwa chaguo la wateja namba moja katika miaka 20 ijayo na zaidi.

 

Malori ya Dangote kuzuiwa

Injinia Kakoko amesema Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania imejadili kwa kina hatari inayoikabili Barabara ya Mtwara – Dar es Salaam iwapo mfanyabiashara Aliko Dangote ataendelea kutumia malori kusafirisha saruji kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam. Amesema malori 500 aliyonunua yataharibu barabara katika muda mfupi na kuiingiza Serikali katika gharama kubwa ya kujenga upya barabara.

“Sisi Dangote tutamwezesha kwa meli maalum, asafirishe saruji kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam kwa meli na hata ikibidi kujenga bandari kadhaa kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi hadi Tanga kuwezesha meli kutia nanga kushusha saruji tutafanya hivyo, ila malori haya kuyaruhusu yataharibu barabara vibaya mno,” amesema Injinia Kakoko.

Amesema asilimia 97 ya mizigo inasafirishwa kwa malori nchini, lakini sasa wanataka kufanya kinyumbe ambapo kiasi hicho cha mizigo kisafirishwe kwa meli na reli na asilimia tatu au chini ya hapo ndiyo pekee isafirishwe kwa malori kwa nia ya kuokoa barabara na kuongeza ufanisi kwa kupunguza gharama za usafirishaji.

Akizungumza na JAMHURI hivi karibu, Dangote amesema anafahamu hatari ya malori kuharibu barabara, ila akaongeza: “Barabara zimejengwa ili zitumike, ziharibike, zijengwe tena, hilo ni jambo la kawaida na sioni tatizo lolote malori kuharibu barabara kama yanaingiza pesa itakayotumika kujenga hizo barabara.”

 

Mhanga, Magesa wasimamishwa

Katika hatua nyingine, uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa kwa nia ya kuboresha ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam wiki iliyopita maafisa 20 wakiwamo Kaimu Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Hebel Muhanga, aliyepata kuwa Mkurugenzi wa ICT, Phares Magesa (ambaye pia ni mjumbe wa NEC – CCM), wanasheria watatu na maofisa wengine wa Bandari wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi.

Katika safisha safisha hiyo wajumbe wa Kamati ya Zabuni ya Bandari, iliyokuwa inaongozwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala, Peter Gawile na akiwamo aliyekuwa Msaidizi Maalum wa aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Bandari, Madeni Kipande, kijana Christian Chiduga nao wamesimamishwa kazi kwa tuhuma za kufanya madudu katika zabuni.

Kati ya mambo yaliyomsimamisha kazi Mhanga, ni pamoja na habari zilizoandikwa na Gazeti la JAMHURI, kuonyesha alivyoshindwa kudhibiti uingizaji wa vibarua hewa Bandari, ambapo baadhi ya kampuni zikiongozwa na Baga na Hai Sub Suppliers zilikuwa zinaingiza vibarua hewa hadi 1,400 kwa mwezi.

Nakala za malipo ambazo JAMHURI lilizipata zinaonyesha kuwa baada ya Injinia Kakoko kuingia TPA idadi ya vibarua imeshuka kutoka wastani wa vibarua 450 kwa siku hadi 28. Kakoko amelithibitisha JAMHURI kuwa vigogo hao wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi, ambapo kama hawatakutwa na hatia watarejeshwa kazini, lakini wakikutwa na hatia wajiandae kwenda kwenye Mahakama ya Mafisadi.

 

Vyeti bandia Bandari

Taarifa zilizolifikia JAMHURI na kuthibitishwa na Kakoko ni kuwa kwa sasa TPA imeanzisha msako wa watumishi wenye vyeti bandia, ambapo takwimu za awali zimebaini karibu watumishi 1,500 wenye vyete bandia au wanaotumia majina yasiyo yao.

Msako huo unahusisha idara zote na hivyo chanzo cha habari kinasema hadi kazi hiyo inakamilishwa idadi inaweza kufikia watumishi 3,000. “Tena mimi nasema mwenye cheti bandia bora ajiondoe mapema kazini. Kila mwenye cheti chenye mashaka nitamfukuza,” amesema Kakoko.

Bandari ya Dar es Salaam ipo katika harakati za kufufua utendaji wake baada ya kubainika siku za nyuma kuwa kulikuwapo wizi wa makontena, ufanisi ulishuka na mizigo ikapungua kufikia asilimia 50 ya mzigo iliyokuwa inapitishwa awali huku baadhi ya watumishi wasio waadilifu wakitumia mwanya huo kuhamisha mizigo ambayo ingesimamiwa na Bandari kwenye ICD na kuingiza vibarua hewa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikwenda bandarini na kubaini uozo mara kadhaa, ambapo kwa kupewa nguvu na Rais Magufuli kwa makusudi wameamua kuimarisha utendaji wa Bandari nchini. Injinia Kakoko mtu mwenye msimamo mkali wa utumishi wa kizalendo, alihamishiwa TPA kutoka Tanroads kwa nia ha kudhibiti hali hiyo na tayari ameanza kufanikiwa.

Ndani ya miezi miwili ameanza kuongeza mapato ya Bandari kwa kuzuia magari yasipelekwa ICD ambapo sasa ana mpango wa kuzuia hata makontena yasipelekwa ICD hadi isiwepo nafasi bandarini hali inayoongeza mapato ya Bandari. Anasema anataka kuboresha bandari zote hata za maziwa ya Tanganyika, Victoria na Nyasa, suala litakaloongeza mapato ya TPA.

By Jamhuri