Waziri wa Ujenzi, Dk. John MagufuliAfya ndiyo msingi wa uwepo wa maisha ya binadamu. Kwa mujibu wa  ufafanuzi uliotolewa na kutangazwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) katika mkutano wake wa Juni 19-22, 1946 na kusainiwa na wawakilishi wa nchi 61 duniani. ‘Afya ni hali ya mtu kuwa vizuri kimwili, kiakili na kijamii na si tu kutokuwa na ugonjwa au udhaifu.’

Ufafanuzi huo ulianza kutumika Aprili 1948 na hadi hii leo maana hiyo ya afya haijabadilika. 

Ufafanuzi huo unamaanisha kwamba tunaposema mtu ana afya si tu tunakusudia kuwa mwili wake hauna maradhi, upungufu au udhaifu, bali pia mtu huyo anatakiwa asiwe na matatizo ya kimwili, kiakili na hata kijamii.

Kwa mujibu wa tafsiri hiyo pana ya neno ‘afya’, tunaona kuwa watu wengi wanaamini kuwa afya imegawanyika katika makundi mawili muhimu ambayo ni afya ya kimwili na afya ya kiakili. 

Afya ya mwili kwa binadamu ina maana kuwa na mwili wenye afya usiokuwa na maradhi, afya ambayo kwa kawaida hutokana na kuupa mwili mazoezi ya mara kwa mara, lishe bora na mapumziko ya kutosha. 

Afya ya akili au uzima wa kiakili ni utambuzi wa mtu na uzima wake kisaikolojia. Mtu ambaye ana afya nzuri ya kiakili hana matatizo ya kiakili au kichaa. 

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ‘afya ya akili ni pale mtu anapoweza kufahamu uwezo wake na kustahamili mfadhaiko (stress) unaotokana na dhiki au matatizo ya kawaida ya kimaisha, aweze kufanya kazi yenye kuleta mafanikio na kuchangia masuala tofauti katika jamii yake.’

Tunaweza kusema kuwa afya ya akili inajumuisha masuala kadhaa kama vile uwezo wa kuishi kwa furaha, uwezo wa kuvumilia shida na kurejea katika hali ya kawaida baada ya kupatwa na matatizo, uwezo wa kuwa na uwiano katika maisha,  uwezo wa kubadilika kwa urahisi na kuzoea mazingira mapya, kujihisi salama na kujitambua.

Msingi wa hoja hii ni kutokana na watu walio wengi kuendelea kuduwaa bila kujua wa kumsaidia wanapokuwa na matatizo ya kiafya, kwani kila upande unashangaa hata wale tunaodhani ni watekelezaji nao wamekuwa wa kushangaa.

Mtu anapokosa dawa hospitali, kwa akili ya kawaida, anaweza kukimbilia kuwalaumu madaktari. Baadhi ya wananchi wamekuwa wakiwalaumu hata wenye kumiliki au kuendesha hospitali na vituo vya afya.

Mfano, imekuwa kawaida kukosa dawa katika hospitali za Serikali lakini dawa hiyo hiyo ni rahisi sana kupatikana kwenye maduka ya dawa ya watu binafsi. Haiingii akilini lakini mwenye kujibu hilo naye bado utamkuta anashangaa kwa nini dawa hazipatikani katika hospitali za Serikali.

Hivi karibuni katika kampeni za kuwania urais, tumeshuhudia na wote ni mashahidi kuwa Dk. John Pombe Magufuli ambaye kwa sasa ni Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, amekuwa akishangaa kama walivyo watu wa kawaida na kujiuliza maswali kama watu wa kawaida kuwa kwa nini dawa hazipatikani hospitalini!

Ni aibu, lakini maadam tumemwamini na kumchagua kuwa rais wetu, tunaamini tatizo hili litabaki historia katika nchi hii.

Siku moja baada ya kuapishwa kwa rais, uongozi wa Hospitali teule ya Nyakahanga iliyopo wilayani Karagwe, Kagera, ilifanya mkutano wa wazi na wadau wa afya wilayani.

Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Andrew Charles Cesari, alikutana na wadau wa afya walioambatana na waandishi wa habari, viongozi wa vyama vya siasa pamoja na asasi za kiraia. Mkutano huo ulibaini changamoto mbalimbali zinazoikabili hospitali hiyo.

Changamoto hizo ni pamoja na upungufu wa dawa na vifaa tiba, Serikali kuchelewesha fedha za ruzuku na wakati mwingine kutochangia kabisa, upungufu wa wataalamu na vifaa tiba, vitanda, wodi za wazazi pamoja na miundombinu mibovu ya maji na umeme hospitalini hapo.

Ruzuku ndogo kutoka serikalini pia ni kikwazo kinachokwamisha huduma hospitalini hapo kama alivyoeleza Dk. Cesari.

Hali hii inayoonekana katika Hospitali teule ya Nyakahanga, haina tofauti na hospitali nyingi nchini. Licha ya Serikali kujitwika gunia la misumari kwenye upara kwa kuing’ang’ania hospitali hiyo ibaki chini ya halmashauri, bado watumishi wa Serikali wameshuhudiwa wakiendelea kuhubiri kuwa zahanati na vituo vya afya vina dawa za kutosha na kuwa tatizo lipo kwa wataalamu katika vituo hivyo.

Deodatus Kinawilo ni Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, ambaye alinukuliwa akisema kuwa Serikali inatoa fedha nyingi sana (hakutaja kiasi) kwa ajili ya dawa na vifaa tiba katika vituo vyote vya afya, huku akiwatupia lawama watumishi wanaoihujumu Serikali.

Swali hapa ni, je, mkuu huyo kabla ya kuuambia umma hivyo alifanya tathmini na kujiridhisha kuwa fedha zimefika kweli katika vituo hivyo? 

Wakati hayo yote yakiendelea kuhusu sintofahamu hizo, mwananchi mwenye kipato cha chini kabisa ndiye anayeendelea kuumia kwa kukosa huduma na wakati mwingine wananchi wengine wakipoteza maisha baada ya kusubiri kwa muda mrefu bila kupatiwa huduma.

Pia mivutano ya itikadi za vyama imechangia kwa kiasi kikubwa kudorora kwa huduma za afya wilayani Karagwe, huku wadau wakitolea mfano Kituo cha Afya Kayanga ambako Diwani wa Kata hiyo, aliyekuwa anatoka Chama cha Wananchi (CUF), Adventina Kahatano, aliyekuwa akiishinikiza Serikali kufungua huduma za upasuaji kituoni hapo bila mafanikio, licha ya kuwa ni zaidi ya mwaka mmoja sasa tangu kukamilika kwa wodi hiyo na vifaa vyake.

Maoni ya wadau waliohudhuria mkutano huo ni kuwa tatizo hili litafutiwe mwarobaini wa kulitibu moja kwa moja. Wananchi wamechoka na maneno yasiyo na vitendo katika nchi hii. Maisha bora kwa kila Mtanzania waliyoahidiwa na awamu iliyopita hayajaonekana.

Akina mama bado wanajifungulia sakafuni kwa kukosa vitanda katika wodi ya wazazi. Kaulimbiu ya sasa isemayo ‘Hapa kazi tu’ haina budi ibainishe nani wa kuwajibishwa kati ya watumishi wanaodaiwa ni wazembe na Serikali inayoonekana kutotoa vitendea kazi.

Ikumbukwe kuwa Hospitali ya Nyakahanga ina zaidi ya miaka 100 sasa tangu kuanzishwa kwake. Ilijengwa na wamisionari Wajerumani mwaka 1912 na ikiwa inamilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania.

Mwaka 1972 ilitaifishwa na kuwa hospitali teule ya wilaya na hivi sasa iko mbioni kubadilishwa kutoka hospitali teule ya wilaya na kuwa hospitali ya Halmashauri ya Wilaya.

Ziara ya ghafla ya Rais Dk. Magufuli katika Hospitali ya Taifa Muhimbili imeweka wazi kile kinachoendelea kote nchini. Kwa hali ilivyo, rais hahitaji kuvamia katika hospitali yoyote hapa nchini. Atoe taarifa na aende tu, atakuta hali ni ile ile aliyoikuta Muhimbili kwa sababu sekta ya afya inatumia fedha nyingi zaidi katika semina kuliko dawa na vitendea kazi.

 

[email protected]

By Jamhuri