Mhariri wa JAMHURI nimevutiwa kwa kiwango kikubwa baada ya kusoma toleo lenu Na 39 la Agosti 14-20, 2012 lililoongozwa na habari yenye kichwa kisemacho ‘Majaji Vihiyo Watajwa’. Mara tu niliposoma habari hii, nikaona ni vyema nifunge safari na kuja hapo ofisini kwako nieleze kilio changu. Wengi wa majaji waliotajwa wameshiriki kwa namna moja au nyingine kukandamiza haki yangu.

Mwaka 1996 nikiwa mwajiriwa wa kampuni ya Dragon Security Services Ltd, kampuni iliamua kunifukuza kazi kwa uonevu. Sababu ya kunifukuza ilikuwa ni utaratibu aliouanzisha mwajiri nje ya mkataba wa kufanya kazi bila kutupa malipo ya ziada. Mimi nilizungumza na wenzangu kuwa tuupinge utaratibu huu, na iliposikika nikaadhibiwa kwa kufukuzwa kazi.

 

Niliamua kwenda kwenye Bodi ya Usuluhishi iliyopo chini ya Wizara ya Kazi na Ajira, kueleza malalamiko yangu na huko mwajiri alishindwa. Mwajiri aliposhindwa aliamua kukata rufaa kwa Waziri wa Kazi na Ajira kupinga uamuzi wa Baraza la Usuluhishi. Tulipofika mbele ya Waziri pia nikashinda kesi na Waziri akaagiza nilipwe stahili zangu.

 

Uamuzi wa Waziri No. KZ/U.10/FR/7766/7 ulitoka rasmi Mei 20, 1999. Baada ya kwisha siku 28 bila kupata malipo yangu kutoka kampuni ya Dragon Security Services Ltd, niliomba kupeleka shauri hilo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa nia ya kukazia hukumu.

 

Niliwasilisha ombi la kukazia hukumu ambako ilikuwa nadai gharama za usafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Tabora Sh 511,000, mishahara ya kati ya Aprili 8, 1997 hadi Agosti 10, 1999 jumla ya Sh 658,000, posho ya likizo Sh 6,000 na posho ya kujikimu kwangu na kwa mke wangu kwa kiwango cha Sh 7,800 kila mmoja wetu tangu siku niliyoachishwa kazi.

 

Pia kwa kuheshimu uamuzi wa Waziri wa kumzuia mwajiri kunifukuza kazi, badala yake kuniachisha kazi, watoto wangu wanne kila mmoja naye apatiwe Sh 3,900 kila siku tangu siku nilipoachishwa kazi kwa kuonewa.

 

Katika kukazia hukumu hiyo, niliomba pia kuwa nipewe riba ya asilimia 30 kwa malipo hayo kwa muda wote utakaopita bila kupatiwa malipo yangu. Pia niliomba mahakama inipe nafuu yoyote itakayoona inafaa. Afisa wa Kazi, E. F. Urasa, aliniandikia maombi yangu haya niyapeleke Kisutu kwa ajili ya kukazia hukumu.

 

Kwa mshangao nilipofika Kisutu, Hakimu aliyepangiwa kesi, Pelagia B. Khaday ambaye sasa ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, kinyume kabisa na Kifungu cha 24 (1) (d) cha Sheria ya Kazi ya Mwaka 1964, badala ya kukazia hukumu kama sheria inavyotaka – kwani uamuzi wa Waziri ni sawa na uamuzi wa Mahakama – yeye akaanza kuisikiliza upya.

 

Nilishuhudia mambo ya ajabu kupitia karani wake kwenye chumba cha mahakama siku ya kutoa hukumu. Khaday aliahirisha kusoma hukumu baada ya mawasiliano yasiyo ya kawaida… kati yake na mlalamikiwa. Kesi iliahirishwa tukaambiwa hukumu itasomwa saa nane mchana. Kwa niliyoyashuhudia nilijua fika nitashindwa, na kweli hukumu iliposomwa na Hakimu Khaday nikashindwa.

 

Kilichonishangaza, nimeshindwa kesi ingawa huyo aliyekuwa mwajiri wangu hakupata kufika mahakamani hata siku moja. Nilikata rufaa Mahakama Kuu CA Na 126 ya 2006. Baada ya kuwasilisha utetezi wangu, Jaji Othman alitoa hukumu kuwa Mahakama ya Kisutu chini ya Hakimu (Jaji) Khaday ilikosea kusikiliza kesi hii upya. Jaji Mohamed Chande Othman ndiye Jaji Mkuu wa Tanzania kwa sasa.

 

Jaji Chande aliweka wazi kuwa chini ya Kifungu cha 28 (1) (a) na (b) cha Sheria ya Usalama wa Ajira, Sura ya 387 (2002), uamuzi wa Waziri ni wa mwisho. Hivyo uamuzi alioutoa Waziri wa Kazi Mei 20, 1999, hakuna mahakama yenye nguvu kisheria kuubadili, isipokuwa kuutekeleza. Aliagiza nikakazie hukumu Kisutu.

 

Nipofika Kisutu kukazia hukumu, waliniambia nilishalipwa na wakaniambia mambo mengine yaliyonishangaza… Hapo ilikuwa Jaji mwingine, Shangwa, aliyetoa hukumu ya kusitisha utekelezaji wa amri ya Mahakama ya kukamata na kuuza mali za Kampuni ya Dragon Security Services Ltd. Dalali Jibrea aliyekuwa afanye kazi ya kukamata mali za  mwajiri huyu mkorofi na kuziuza, alipata amri ya Mahakama kutoka kwa Jaji Shangwa akikataza uuzaji huu. Nilimwandikia Jaji Kiongozi, Novemba 10, 2008 kupinga hatua hii ya Jaji Shangwa.

 

Huwezi kuamini kwanza. Baada ya kupata nakala ya Uamuzi/Amri hii ya Mahakama nilikwenda moja kwa moja kwa wakili wangu, Chabruma kuomba ushauri nifanyeje, naye aliniagiza niende kwa karani mhusika (Nd. Abeid) na kuomba nipewe nakala ya Chamber Summons ambayo Dragon Security Service Ltd walidai wameiwasilisha mahakamani.

 

Sikuamini masikio yangu nilipoambiwa na karani Abed kwamba hapakuwa na Chamber Summons yoyote ndani ya jalada husika, na kwamba maombi yaliyopelekwa kwa Jaji Shangwa yalikuwa ya mdomo. Ni dhahiri kwamba huu si utaratibu bali ni fujo.

 

Mbali na kwamba maombi yaliwasilishwa siku 38 baada ya kutolewa Amri ya Mahakama ya Kisutu kuruhusu kuuza mali za mwajiri wangu, Jaji Shangwa alisikiliza upande mmoja siku ya tarehe 30/10/2008 na yalikubaliwa siku hiyo hiyo, yakachapishwa siku hiyo hiyo, yakatiwa saini siku hiyo hiyo na nakala ikawasilishwa kwa dalali siku hiyo hiyo.

 

Nilimwambia Mheshimiwa Jaji Kiongozi hii ni kasi ya ajabu ambayo sijapata kuishuhudia katika maisha yangu, hasa ukizingatia kwamba Mahakama Kuu ni mahali penye kazi nyingi sana na muhimu. Kibaya zaidi, wajibu maombi waliandikwa ‘absent’ kama vile waliitwa wakakataa. Mimi naamini huu si ustaarabu unaokubalika kisheria na umechangia kuninyima haki zangu kisheria na kikatiba kwa kuninyima fursa ya kusikilizwa.

 

Baada ya yote hayo, nimepeleka upya maombi katika Kamati ya Malalamiko ya Mahakama Kuu, inayoongozwa na Jaji Msoffe na Kamati hii imeahidi kuyafanyia kazi malalamiko yangu mwezi Julai mwaka huu, ambapo sijapewa jibu. Ukiweka na riba sasa deni hilo limekua hadi Sh bilioni moja na zaidi. Naomba Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete aingilie kati suala langu.

 

Nimehangaika kiasi cha kutosha hadi familia yangu imeyumba kwa muda wote huu. Yeyote anayetaka kunipa msaada wa kuniwezesha kupata haki yangu, anaweza kuwasiliana name kwa simu Na. 0652 332229. Naishi kwa tabu hapa Dar es Salaam.

 

Edward Msago (62) ameeleza kuwa ni msomaji mzuri wa JAMHURI na anaomba wasamaria wamsaidie. Mhariri.


1584 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!