Picha ya Waziri MagembeHifadhi ya Taifa ya Milima ya Mahale itatumia kiasi cha Sh. bilioni 1.2 katika kuboresha miundombinu ya barabara, ili watalii waweze kuifikia hifadhi hiyo kwa urahisi kuliko hali ilivyo sasa.

Akizungumza na JAMHURI, Kaimu Mhifadhi wa Hifadhi hiyo, Gadiel Moshi, anasema Shirika la Hifadhi za Taifa limekuwa linatenga bajeti ya kutengeneza madaraja yanayokwamisha usafiri wa nchi kavu na kusababisha utalii katika Hifadhi hiyo kuwa ghali. Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limetenga fedha za kutosha kujenga madaraja manne. 

Anasema madaraja mawili ambayo ujenzi wake unagharimu kiasi cha Sh. milioni 500 unaendelea, wakati madaraja mengine makubwa mawili yakisubiri fungu katika bajeti hii ya 2016/17.

Moshi anasema katika mwaka wa fedha 2015/16 kuna miradi miwili mikubwa ya ujenzi wa madaraja katika vijiji vya Rukoma na Igarula, ujenzi unaendea na 2016/17, Hifadhi ya Mahale imepanga kujenga madaraja mengine mawili katika vijiji vya Nkonkwa na Kabezi.

Mhandisi wa madaraja hayo, Marango Ngose, anasema ujenzi wa madaraja hayo umeanza Juni mwaka huu na ujenzi wake unatarajiwa kukamilika baada ya miezi sita. 

“Mradi huu umeanza Juni mosi, mradi huu unatarajiwa kukamilika baada ya miezi sita… Tumekutana na changamoto ya maji katika ujenzi wa madaraja, lakini tutajitahidi kuhakikisha kwamba mradi unakamilika kwa wakati,” anasema Ngose.

Mhifadhi Moshi anasema katika Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Mahale kuna idadi ya sokwe 2,600 hapa katika Hifadhi ya Mahale, 800 wakiwa ndani ya hifadhi, na wengine nje ya hifadhi. Anasema sokwe wengine wako katika mapori yaliyoko chini ya vijiji. 

“Sokwe wengi wako nje ya hifadhi, nadhani wanahitaji kulindwa na wenye mamlaka ya kuwalinda sokwe hao pamoja na wanyama wengine ni Shirika la Hifadhi za Taifa…kuna aina 120 wa samaki, ni eneo unaloweza kupata uhalisia wa hifadhi hii,” anasema Moshi.

Mhifadhi Moshi anasema kumekuwa na ongezeko la watu katika mapori yaliyoko jirani, watu wanahama kutoka Kasulu na Kibondo kwenda katika mapori yaliyoko jirani na Hifadhi. 

“Wanakuja huku kwa ajili ya kulima, wengine wanavuna misitu, hali inayotishia uwepo wa sokwe katika Hifadhi ya Taifa ya Mahale. Kumekuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi, kupima ardhi ya vijiji ili kulinda misitu yao inayopakana na Hifadhi,” anasema Moshi.

Anasema kwamba Hifadhi imejipanga kuimarisha ulinzi katika Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Mahale. Anasisitiza kwamba ujenzi wa barabara kutoka Mpanda utapita kwenye ardhi ambayo haijapimwa, ardhi ambayo pia kuna sokwe wanaohitaji kulindwa. 

1229 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!