Mhubiri wa Injili, Israel Ayivor, alipata kusema kwamba yule aliyekusaidia kuzungumza mambo mabaya kuhusu mwenzako ndiye atakayemsaidia mtu mwingine kuzungumza uovu juu yako. Wema ni akiba.

Tenda wema uende zako, usisubiri malipo. Kumbuka kwamba watu uliowatendea mema wanaweza kukugeuka lakini Mwenyezi Mungu hawezi kukugeuka.

Mtu aliyekuwa sababu ya furaha yako anaweza kuwa sababu ya majonzi yako, lakini kumbuka Mungu ndiye sababu ya furaha yako daima.

Mtu aliyekusudia kukuinua ukiinuka anaweza kukuonea wivu, lakini yule ambaye hawezi kukuonea wivu ni Mungu peke yake.

Mwandishi Dresch Messenger anasema: “Maadui wako ni rasilimali yako ya thamani kama haulipi kisasi kwa sababu wanakufanya uwe macho na kuchapa kazi, vinginevyo ungebweteka.”

Mwandishi mwingine aitwaye, Sidney Sheldon, anasema kufanikiwa unahitaji marafiki na kufanikiwa sana unahitaji maadui.

Mwandishi wa habari, David Brinkley, naye anasema kwamba mtu aliyefanikiwa sana ni yule ambaye anaweza kuweka msingi imara kwa tofali zile ambazo wengine humrushia kumpiga nazo.

Maisha yanaweza kukurushia tofali nyingi, zidake na zitengenezee msingi ambao utakuwezesha kusonga mbele. Maadui zako pia ni warushaji wa mawe. Daka mawe yao na jenga ngazi.

Usiruhusu mambo hasi yanayotokea katika maisha yako yakufanye na wewe uwe ‘hasi’. Yageuze kuwa kitu chanya na yatumie kama msingi wa hatua inayofuata. Yatumie maneno wanayokusema watu kama mawe ya kuvukia ng’ambo ya pili ya mafanikio yako. 

Machi 3, 2011 saa mbili usiku rafiki yangu alinitumia ujumbe kwenye simu yangu ya kiganjani, ujumbe huo ulikuwa unasomeka kama ifuatavyo: “Usiangalie jana kwa hasira wala kesho kwa woga. Itazame leo kwa hekima na busara huku ukijipanga kusonga mbele kwa kumtanguliza Mungu kwa kila jambo.”

Usiogope maneno ya wanaokusema vibaya maana maneno ni HERUFI tu zilizounganishwa na kupewa sauti. Lawama na maelezo mengi ni mali ya walioshindwa, lakini walioshinda wana maneno mawili tu: ‘MALENGO na JITIHADA.’

Tusiwachukie wanaotuchukia, tuwapende ili waone wema na upendo wa Mungu kupitia kwetu. Adui ni wa kumuombea mazuri ili yale mazuri anayopata na kukutana nayo yambadilishe kuwa mtu mzuri.

Hilo linawezekana, ukimchukia anayekuchukia unakosea.

Athisthenes – Mwanafalsafa wa Kigiriki aliwahi kusema: “Wasikilize maadui zako kwa sababu ni wa kwanza kugundua makosa yako.”

Methali ya kabila la Wafipa inasema hivi: “Mvua ya Mungu huwanyeshea hata washirikina.” Martin Luther King, Mwanaharakati mweusi alipata kusema kwamba giza haliwezi kutokomezwa na giza, bali hutokomezwa na mwanga tu. Vivyo hivyo chuki haiwezi kutokomezwa na chuki, bali ni upendo tu unaoweza kufanya hivyo.        

Tuwafundishe maadui zetu moyo wa upendo, tuwafundishe maadui zetu moyo wa msamaha. Tutambue kwamba tunaishi kwenye jamii ambayo pia inahitaji kufundishwa namna ya kuuchuchumilia wokovu, ni wajibu wa wabatizwa kuwa chambo cha kuwanasa wahitaji walio na kiu ya kusikia habari za wokovu na matunda yake.

Tubadili tabia chafu zilizokithiri katika jamii yetu na tuzalishe amani na upendo miongoni mwa jamii, tusisubiri kuhubiriwa ndipo tuamue kutenda ama kuwajibika. Kila mmoja mahali alipo awe mjumbe na mpatanishi wa habari njema.

1679 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!
Show Buttons
Hide Buttons