Wivu unaona tabasamu lako hauoni machozi yako

 

Wivu ni mtihani. Mwenye wivu haonekani mzuri anapokufanya uonekane mbaya. “Baadhi ya watu watakukataa, kwa sababu tu unameremeta sana kuwazidi. Hiyo ni sawa, endelea kumeremeta,” alisema Nandy Hale. Wivu unaona tabasamu lako, hauoni machozi yako.

Wivu unaona kicheko chako, hauoni huzuni yako. Wivu unaona pesa yako, hauoni matumizi yako. Wivu unaona baraka zako, hauoni mateso yako. Wivu unaona kampuni yako, hauoni changamoto zako. Wivu unaona kisomo chako, hauoni jasho lako. Wivu unaona bahari, hauoni miamba. Wivu unaona mabonde, hauoni milima. Kwa kifupi anayekuonea wivu anajitukana kuwa macho yake ya akili hayaoni.

 Unapowaonea wengine wivu unatangaza udhaifu wako. Kuonea watu wengine wivu ni kujitukana kwamba wewe haujiamini, haujui vipaji vyako. “Katika wivu kuna kujipenda kuliko upendo kwa wengine,” François de La Rochefoucauld.

Kuwaonea wengine wivu ni kutangaza kuwa hauna upendo kwa jirani. “Ni afadhali kuonewa wivu kuliko kuhurumiwa,” alisema Herodutus.  Mafanikio yanazaa maadui wenye wivu. “Chuma kinatafunwa na kutu, na wenye wivu hivyo hivyo wanatafunwa na wivu,” alisema Antisthenes.

Upande mzuri wa kuonewa wivu ni kukumbushwa vipaji ulivyonavyo, nguvu ulizonazo na uwezo ulionao. Wanaokuonea wivu wamehesabu baraka zako, vipaji vyako, mali zako na matunda yako. “Wivu ni ufundi wa kuhesabu baraka za mwingine badala ya baraka zako,” alisema Harold Coffin. Wanaokuonea wivu wanatangaza ukubwa wako. “Anayemwonea mwingine wivu anakiri ukubwa wake,” alisema Samuel Johnson. Wivu hauingii katika nyumba zilizo tupu (Methali ya Kidenishi). Unapoonewa wivu ina maana nyumba yako ina kitu kizuri.

Wivu ni kuumia kwa sababu ya mafanikio ya wengine. “Wivu ni heshima ambayo akili ya kawaida hutoa kwa akili isiyo ya kawaida,” alisema Askofu Fulton Sheen wa Marekani. Unapowaonea wengine wivu, wivu unaongea. Unaongea juu ya jambo unalolitaka, unalolipenda na unalolichukia.

Ungejifunza kutoka kwa mtu unayemwonea wivu kama usingetiwa upofu na chuki. Ukiwaonea wengine wivu, wivu unadokeza ambacho hauna katika maisha yako. “Unaweza kuwa mwezi na bado ukazionea wivu nyota,” Gary Allan. Unapoonewa wivu, jua ukweli huu, watu wanachodharau katika maisha yako wanakipenda na wangetamani kuwa nacho.

Juu ya wivu na husuda Papa Francisco alikuwa na haya ya kusema: “Wivu unaua. Hauvumilii wengine kuwa na kile ambacho sina. Na kila mara ukiwa na husuda unateseka, kwa sababu moyo wa mwenye husuda au mwenye wivu huteseka. Ni moyo unaoteseka. Ni mateso ambayo yanatamani kifo cha wengine. Ni mara ngapi katika jumuiya zetu – na hatupaswi kutazama mbali kuona hili – watu wanauawa kupitia wivu kwa kutumia ulimi? Watu wanamwonea wivu huyu au yule na wanaanza kusengenya – na masengenyo yanaua.”

Kwa wanandoa wivu kiasi unahitajiwa. Nimesema “kiasi.” Maji yasizidi unga, na wala usiunguze. “Wivu katika mapenzi/ndoa ni kama chumvi kwenye chakula. Chumvi kidogo inaboresha utamu, lakini ikizidi sana inaharibu utamu, na katika mazingira fulani inahatarisha maisha,” alisema Maya Angelou.

Yote yakishasemwa, tunahitaji busara kuishi na watu. “Usimelemete kuliko bwana wako,” aliandika Robert Green katika kitabu chake cha 48 Laws of Power. Usimwaibishe mkubwa wako wa kazi mbele ya watu. Tunapambana na husuda na wivu kwa njia ya matashi mema, unyenyekevu, kujiachilia chini ya maongozi ya Mungu. Lazima kukubali katika maisha kuwa hata vidole havilingani.

439 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!