Umri wa kati ni mtihani. Huu ni umri kati ya miaka 35 hadi 59. Ni umri kati ya ujana na uzee. Ni umri ambao mtu anaingia katika kipindi cha pili cha mchezo wa maisha.

“Katika umri wa kati moyo hauna budi kufunguka kama ua la waridi na si kufunga kama kabeji,” alisema John A. Homes. Kwa wanandoa ni kipindi ambacho mke anakuwa mwenzi (si ‘bibi’ tena), sababu kipindi cha uzeeni mke anakuwa kama nesi.

Lillian Gordy Carter anaainisha umri huu kama umri wa mtu kuzima zima taa kwa sababu za kiuchumi na si nyinginezo. Namna ya kujua kama umeingia umri wa kati ni pale unaporudi chuoni uliposoma na kugundua wanafunzi ni wadogo kuliko ulivyokuwa. Kwa misingi hii umri wa kati ni mtihani.  

Umri wa kati ni umri ambao mtu si kijana wala si mzee. Kadiri ya Kamusi ya Collins, umri wa kati ni kati ya miaka 40 hadi 60. Kadiri ya Kamusi ya Oxford, umri wa kati ni kati ya miaka 45 hadi 65. 

Umri huu unategemea upo nchi gani na wastani wa watu kuishi ni upi.  Kuna upande mzuri wa umri wa kati. “Bila shaka umri wa kati ni kipindi cha furaha sana katika maisha, hisia kali za ujana zinakuwa zimepoa na udhaifu unaotokana na umri unakuwa haujaanza; ni kama tunavyoona vivuli, asubuhi na jioni vinakuwa virefu, lakini ni kama vinapotea adhuhuri,” alisema Eleanor Roosevelt.

Ujana ni asubuhi ya maisha. Umri wa kati ni adhuhuri ya maisha. Uzee ni jioni ya maisha. Kivuli cha hisia za ujana ni kirefu na kivuli cha udhaifu wa mwili sababu ya uzee ni kirefu.

“Miaka inaweza kufanya ngozi yako kuwa na mifunyo, lakini kutokuwa na shauku ya kitu chochote kunafanya roho iwe na mifunyo. Wewe ni mdogo kama imani yako, na mzee kama mashaka yako; ni kijana kama kujiamini kwako, ni mzee kama kukata tamaa kwako.

“Katika kitovu cha kila moyo kuna chumba cha kurekodi. Kikipokea ujumbe wa uzuri, matumaini, furaha na ujasiri unakuwa kijana. Moyo wako ukifunikwa na theluji ya kutazamia mabaya na  barafu ya wasiwasi hivyo na hivyo tu unazeeka,” alisema Douglas MacArthur.

Lisha akili yako na mawazo mazuri na fikra ya matumaini, ndoto za maendeleo na mipango yenye kuleta furaha. Confucius alisema binadamu wanatawaliwa na tamaa ya mwili wakati wa ujana na majivuno wakati wa umri wa kati na uchoyo wakati wa uzeeni.

Mtihani wa umri wa kati ni majivuno. Kusema kweli ukimeza majivuno yako hautavimbiwa. Ni katika umri wa kati mwenye majivuno anauliza mwongoza magari kwenye sherehe:

“Watu ambao huwa wanajaza tenki mafuta kwenye magari yao wanaegesha wapi magari?” Majivuno yanajidhihirisha katika kuchukua sifa ya watu wengine. Si honi inayosukuma gari moshi ingawa inasikika kuliko injini. Mwenye majivuno hayuko tayari kufanya mambo madogo madogo.

Yeye ambaye ni mkubwa sana kiasi cha kutofanya mambo madogo ni mdogo kuweza kukabidhiwa mambo makubwa. Umri wa kati ni umri wa kujiendeleza na kuendeleza. Umri wa kati ni nabii wa umri wa uzeeni.  

“Umri wa kati wenye juhudi, nafikiria ni mtangulizi wa umri wa uzeeni wenye furaha,” alisema Vida D. Scudder. Katika umri wa kati, yaani wa kipindi cha pili cha mchezo wa maisha, chagua mambo mawili au matatu ambayo uliyafanya vizuri kipindi cha kwanza cha mchezo wa maisha uyaendeleze. 

By Jamhuri