Wiki iliyopita nilifika katika mmoja ya mifuko ya pesheni kujiandikisha kwa ajili ya utaratibu wa kujiwekea akiba kwa mpango wa kuchangia kwa hiari. Baada ya kutoka katika ofisi za mfuko huo wa pesheni nikiwa na fomu na makabrasha mengi, nikakutana na mtu mmoja ambaye maongezi kati yangu na yeye ndiyo yaliyonisukuma kuandika makala haya.

Rafiki yangu huyu ambaye ni mfanyakazi, alishikwa na bumbuwazi kuona ninaeleza habari za mfuko wa jamii. Swali lake kubwa lilikuwa ni hili, “Je, mifuko ya hifadhi ya jamii inahusika na wajasiriamali?” Haraka haraka nikabaini tatizo lake anafahamu kuwa mifuko ya kijamii ni kwa ajili ya wafanyakazi walioajiriwa ama na serikali, mashirika, au kampuni kubwa pekee.

 

Kutokana na maarifa na ufahamu nilionao kuhusu mifuko hii ya hifadhi ya jamii, nilipata wasaa mzuri wa kumwelekeza rafiki yangu huyu kwa kina kuhusu mifuko ya hifadhi ya jamii na namna inavyowagusa Watanzania wote bila kujali wapo serikalini, kwenye sekta binafsi ama katika sekta isiyo rasmi.

 

Wajasiriamali ni sehemu ya nguvukazi ya jamii. Kile kinachowapata wale walioajiriwa kwa maana ya kuchoka kiumri na kiafya, kutakiwa kupumzika baada ya miaka mingi ya kazi pamoja na maandalizi ya maisha ya baadaye; vivyo hivyo kinawahusu pia wajasiriamali.

 

Ndiyo maana baada ya kumaliza mazungumzo na rafiki yangu huyu nikabaini kuwa nina haja ya kushirikishana na wajasiriamali wenzangu, kuhusu dhana nzima ya umuhimu wa mifuko ya hifadhi ya jamii, na umuhimu wa mjasiriamali kujiandaa kustaafu ujasiriamali.

 

Ni vema tukafahamu kuwa mifuko ya hifadhi ya jamii ina histoia ndefu nchini Tanzania. Awali kulikuwapo mifuko isiyo rasmi ya hifadhi ya jamii (informal safety nets) ambayo ilikuwa ni vijana kusaidia wazee ama ukoo kusaidiana.

 

Kuanzia mwaka 1942, wakoloni wakaja na utaratibu rasmi ambapo GEPF ilikuwa ya kwanza ikifuatiwa na NPF (NSSF)-1964, PPF-1978, PSPF-1999 kwa kutumia Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 1954.

 

Lakini mwaka 2008 kuliundwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambapo utaratibu wa kuchangia kwa hiari ulianzishwa. Hata hivyo, sheria hii ilitanguliwa na Sera ya Hifadhi ya Mamii ya mwaka 2003.

 

Lengo la sera hii lilikuwa kuweka mazingira mazuri ya taratibu za hifadhi za jamii, kuruhusu mwanachama kuhama kutoka mfuko mmoja kwenda mwingine na stahili zake pamoja na kuanzisha mifumo ya uchangiaji wa ziada kwa hiari.

 

Ni kutokana na sheria na taratibu zilizoboreshwa ndipo kumekuwapo na fursa ya Mpango wa Uchangiaji wa Hiari ambapo watu mbalimbali kutoka serikalini, sekta binafsi na katika sekta isiyo rasmi wanapata fursa ya kuwa wanachama katika mifuko hii ya kijamii.

 

Hivyo utabaini kuwa mjasiriamali yeyote anayo nafasi ya kujiunga na mfuko wa hifadhi ya jamii na kuanza kujiwekea akiba. Ni muhimu sana wajasiriamali kutafakari kwa kina maisha ya baadaye badala ya kujisemea “Atajua Mungu”. Maisha ya sasa na baadaye kwa mjasiriamali yamo katika uamuzi wa mjasiriamali mwenyewe. Unachoamua leo ndicho utakachopata kesho.

 

Nimekuwa nikieleza mara kwa mara katika chambuzi zangu kupitia safu hii; kuhusu athari za mabadiliko ya kibiashara kwa wajasiriamali. Nimepata kueleza kuwa biashara za sasa zinahitaji akili nyingi, ubunifu mwingi na kuona mbali kwa tofauti sana.

 

Hii ina maana kuwa wewe mjasiriamali upende usipende kuna wakati biashara zinaweza kukoma. Kukoma huku kuna namna mbili.

 

Mosi ni kukoma mwendo wa kibiashara kutokana na mabadiliko ya kimzunguko. Hapa ni pale unapojikuta biashara iliyokupa faida jana leo imegoma na haina faida tena.

 

Pili ni kukoma kwa biashara kwa maana ya wewe mjasiriamali kuishiwa uwezo wa kuendelea na biashara.

Kuna wakati umri utakuwa umeenda sana, afya inaweza kuwa matatani au akili yako mjasiriamali kuchoka kabisa kiasi kwamba hakuna namna isipokuwa kuachana na biashara.

 

Jawabu kwa kukoma kwa namba mosi ni wewe mjasiriamali kubadilisha biashara ama kuingiza mbinu mpya katika hiyo biashara iliyokoma. Jawabu la kukoma kwa pili ni wewe mjasiriamali kustaafu.

 

Hapa kwenye kustaafu ndipo ambapo wajasirimali wengi hawajui. Kimsingi kama ilivyo kwa watu walioajiriwa, ndivyo ilivyo kwa mjasiriamali ya kuwa kuna wakati utafika na utalazimika kustaafu katika ujasiriamali.

 

Wakati wafanyakazi hupangiwa muda wa kustaafu, mjasiriamali unatakiwa ujipangie muda wa kustaafu. Kwa mfanyakazi; tafsiri ya kustaafu ni pale ambapo taifa linaona kuwa mtu amelitumikia vya kutosha hivyo yafaa apumzike.

 

Kwa upande wa wale wafanyakazi walioajiriwa na serikali ama mashirika, inapofika wakati wa kustaafu walau mwajiri na serikali wanakuwa wamejiridhisha kuwa huyu mstaafu anayo akiba itakayomtosha kuishi katika maisha yake yaliyobaki hadi kufa. Akiba hii ndiyo kile kinachoitwa mafao na pensheni.

 

Nafahamu changamoto inayowakumba wataafu wengi kuhusu pensheni ndogo wanayoendelea kulipwa kila mwezi baada ya kustaafu; lakini lengo na mpango wa mtu kustaafu kwa sheria za ajira za hapa nchini ni kumsaidia kuishi maisha mazuri hata baada ya kustaafu kwake.

 

Kwa kuwa nia yangu ni kusemezana na wajasiriamali juu ya hatima yao ya kustaafu; naomba niachane na hayo ya walioajiriwa bali nijikite kwa wajasiriamali wenzangu. Kama nilivyotangulia kusema ni kuwa katika ujasiriamali kuna kustaafu na kama hutaki kustaafu kwa hiari biashara zitakustaafisha kwa lazima.

 

Swali hapa linalokuja ni hili: Je, mjasiriamali utaishije ukistaafu? Nimesema kuwa umri wa kustaafu kwa mjasiriamali anajiamulia mwenyewe. Unaweza kustaafu ukiwa na miaka 30, 45, 50, 60, 70 au katika umri wowote ule utakaojiamulia wewe mwenyewe.

 

Kama mjasiriamali ukiamua kustaafu ukiwa na miaka 30 na tuchukulie umri wa kuishi wa Mtanzania ni miaka 60+ (nimetumia kigezo cha ustaafu wa serikalini); ina maana utakuwa umebakiza miaka 30 mbeleni. Je, katika miaka 30 ijayo utaishije? Vivyo hivyo ikiwa utastaafu ukiwa na miaka 40, utakuwa na miaka 20 mbele.

Ukistaafu na miaka 50, utakuwa na miaka 10 mbele. Kubwa ninalotaka mjasiriamali ujiulize ni kwamba utaishije ukifika wakati ambao biashara haziendi ama ule muda utakaokuwa umechoka kiumri na kiafya kuweza kumudu biashara?

 

Tumeona kuwa wenzetu walioajiriwa huendelea kula pensheni yao hata baada ya kustaafu. Je, mjasiriamali una mpango gani? Ni vema nizitaje fursa zote alizonazo mjasiriamali kujiandaa mapema kwa ajili ya kustaafu.

 

Kwanza, mjasiriamali anaweza kuwekeza katika vitegauchumi vya muda mrefu ili vimsaidie atakapokuwa hawezi tena kufanya biashara (kustaafu).

 

Pili, anaweza kusomesha watoto kwa lengo la kuja kumsaidia baadaye, tatu anaweza kuweka hisa ama kuwa na biashara katika mifumo rasmi, zitakazoweza kumfaa kwa miaka mingi baadaye. Fursa nyingine (ambayo ni ngeni kwa wajasiriamali wengi) ni hii ya kuweka akiba katika mifuko ya hifadhi ya jami.

 

Hata hivyo, kwa mazingira ya ujasiriamali wa Kitanzania si wengi wanaoweza kumudu kuwekeza kwenye vitegauchumi vikubwa vya kuwasaidia miaka na miaka baadaye. Pia si wengi wanaoweza kuwekeza katika hisa na biashara za mifumo rasmi.

 

Sasa, wajasiriamali wa kawaida wanafanyaje kujihami na maisha baada ya kustaafu katika ujasiriamali? Suluhu inapatikana kupitia fursa ya kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Kwa kuwa mwanachama katika mmoja ya mifuko hii inakupa wasaa mjasiriamali hata mwenye mtaji mdogo kabisa kujiwekea akiba kidogo kidogo kwa ajili ya mafao ya kustaafu kwako.

 

Taratibu, sera na kanuni za namna ya kujiunga zinatofautiana kwa mfuko mmoja hadi mwingine sambamba na aina ya mafao yanayotolewa. Hata hivyo, kuna mifuko ambayo ina mafao mazuri mno kwa ajili ya wajasiriamali.

 

Mathalan mifuko hii ina faida mbalimbali ikiwamo mafao ya ujasiriamali (mtaji) pamoja na mikopo ya kibiashara kupitia Saccos.

 

Mbali ya faida za kibiashara, mifuko hii inakupa wasaa wa kutoogopa kuhusu familia na afya yako mjasiriamali kwa sababu wana mafao ya matibabu, mikopo ya nyumba, samani, mafao ya elimu na mafao ya uzazi.

 

Nitoe wito kwa wajasiriamali wote nchini mjaribu kutembelea mmoja kati ya mifuko hii ya kijamii iliyo karibu nanyi ili kupata maelekezo na namna ya kujiunga. Furaha yangu itakamilika pale nitakapoona wajasiriamali wadogo na wakubwa wengi iwezekanavyo wakijiunga na mifuko hii ya hifadhi ya jamii kwa ajili ya usalama wa ujasiriamali wao.

 

stepwiseexpert@gmail.com, 0719 127 901

2457 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!