Upo ukweli unaopendwa kutumiwa na watu wengi sana. Ukweli huo unasema hivi; “Kazi ya Mungu haina makosa.’’ Ni ukweli kwamba hujaumbwa kwa makosa wala kwa bahati nasibu. 

Mwanasayansi Albert Einstein anasema,“Mungu hachezi bahati nasibu.’’ Mshairi Russel Kelfer anasema, ‘Wewe ni wewe kwa kusudi. Wewe ni sehemu ya mpango wa ajabu. Wewe ni wa thamani na chombo maalumu kikamilifu. Unaitwa mtu mwanaume au mwanamke maalumu wa Mungu.” Biblia Takatifu inasema, “Umeumbwa kwa namna ya ajabu.’’

Maneno ‘kwa namna ya ajabu’ ni mazito hayafafanua kwa ufahamu wetu wa kibinadamu. Lakini maneno ‘kwa namna ya ajabu’ kwa sehemu yangu na uelewa wangu naweza kuyafafanua kwa namna ifuatayo: Binadamu ni kiumbe aliyepewa upendeleo wa aina yake katika uumbaji; kiumbe huyu ana uwezo wa kujenga au kubomoa, ana uwezo wa kufikiri, kutenda na kuamua, ana uwezo wa kubadili kile anachokiona na ana uwezo wa kutawala viumbe wengine kwa kutaja machache. 

Sifa nyingine ya binadamu ni kubadilika; binadamu siyo kama gogo ambalo linaweza kukaa miaka mingi kwenye maji lakini lisibadilike hata siku moja na kuwa mamba. Binadamu anabadilika na anabadili. 

Na yote katika yote ni kwamba mwanadamu amepewa upendeleo wa aina yake, wa kuumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kuumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ni zawadi. Ni muujiza. Ni maajabu. Hujaumbwa kwa bahati mbaya. Umeumbwa kwa malengo. Hivyo basi furahia namna ulivyoumbwa. Furahia namna walivyoumbwa wengine. Furahia namna dunia ilivyoumbwa kwa ustadi mkubwa. Furahia kuitwa raia wa taifa lako. 

Yape maisha yako mhuri wa malengo. Yape maisha yako mhuri wa utakatifu. Yape maisha yako mhuri wa upendo. Yape maisha yako mhuri wa msamaha. Yape maisha yako mhuri wa uadilifu. Yape maisha yako mhuri wa unyenyekevu. Yape maisha yako mhuri wa bidii katika kazi, bidii katika kumtumikia Mungu aliyekupa zawadi ya uhai. Kila siku amka na malengo ya juu. 

Amka na mbinu mpya, mawazo mapya, ushauri mpya. Usiwe mtu wa kufikiri kwa karibu. Amini unaweza kuyatimiza malengo yako. Usikate tamaa. Methali ya Kichina inatutia moyo kwa maneno haya, “Dunia ni ya wale ambao wanavuka madaraja mengi katika kufikia kwao kabla ya wengine kuona daraja hata moja.’’ Dunia ni ya watu wasiokata tamaa. Uliwekwa duniani kutoa mchango wako. 

Mabadiliko yanaanza na wewe. Mafanikio yanaanza na wewe. Anza kwa kuonesha njia. Penye nia pana njia. Vipaumbele vinatuagiza kuhesabu visivyohesabika. Kuwekea muda kinachoishi milele. Kuwekea umbo kisichoweza kuumbika. Kutafuta thamani ya kisichopimika. Kuwekea mipaka kisichokuwa na mwisho. Kuwekea taswira kisichoweza kuwa na sura. Kuanzisha kisicho na mwanzo. 

Barack Obama, Rais wa Marekani, anasema, “Mabadiliko hayawezi kutokea kama utamsubiri mtu mwigine au muda fulani. Sisi ndiyo mabadiliko tuliyoyasubiri muda mrefu.’’ Kila kukicha mwanadamu anakabiliwa na zoezi la kufanya uchaguzi fulani. 

Ulimwengu huu hauna nafasi kwa watu wanaopuuzia maarifa ya muhimu. Kila kukicha yeyote anaalikwa kuukaribisha utajiri na kuuaga umaskini, au kuuaga utajiri na kuukaribisha umaskini. Lakini yote katika yote tunahitaji kuandika upya historia mpya ya maisha yetu na taifa letu. Tuyatazame mazingira yetu tunayoishi kwa jicho la ushindi. Tuutazame huu ulimwengu kwa jicho la ushindi. Wahenga walipata kunena, “Penye nia pana njia.’’

Hannibal[183-247], mgunduzi wa silaha za kivita, anatushauri hivi, “Lazima tuone njia, kama haipo tuitengeneze.’’ Ni wakati sasa wa kuitengeneza upya njia! Kwa sababu huko nyuma tumekuwa tukiishi kama wanyama. Hatuwezi kubadili kilichotokea kwani ni historia tayari. Na sasa tufungue macho yetu tuzione fursa zinazotuzunguka.

Mwandishi wa Kihispania Anais Nin anasema, “Hatuoni vitu kama vilivyo, tunaviona kama tulivyo’’. Huu ni wakati wa kuviona vitu vilivyo na siyo wakati wa kujiona tulivyo. Kila mtu sasa na ajihisi kama mvumbuzi, mtafiti na mtatuzi wa matatizo yanayoikabili jamii yetu. Uhodari wa kuishi si uhodari wa kuishi miaka mingi, la hasha. 

Ni uhodari wa kuwa msaada katika jamii inayokuzunguka na ulimwengu kwa ujumla wake. Tutafanikiwa kiroho, kimaadili, kisiasa, kijamii na kiuchumi endapo kila mtu atawajibika kufanya kazi kwa maadili mema kwa nafasi yake aliyopo. Mafanikio yako yanategemeana na uamzi wako uliofanya. 

James Allen anasema hivi, “Leo uko pale ambapo mawazo yako yamekuleta, kesho utakuwa pale ambapo mawazo yako yamekupeleka. Jenga leo yako vizuri ili kesho yako iwe nzuri zaidi.  

Mchezaji wa mpira, Jerry Rice, anasema, “Leo nitafanya ambayo wengine hawatataka kufanya ili kesho niweze kutimiza ambayo wengine hawataweza kutimiza.’’

1366 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!