*Maelezo ya Jaji Ramadhani, Luanda moto

*Ripoti ya Ikulu nayo yataka waondolewe

*Lissu ataka wapime, kumshitaki Kikwete

*Amtaka Jaji Kiongozi Fakih Jundu ajiuzulu

 

Mhimili wa Mahakama umetikisika baada ya kuwapo ushahidi wa wazi kwamba Rais Jakaya Kikwete amevunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kwa kuwaongezea mikataba ya kazi baadhi ya majaji na kumpandisha cheo mwingine.

Sasa kuna shinikizo la kitaaluma la kuwataka majaji waliopata ajira kwa mikataba na wale waliokuwa na kashfa kabla ya kuteuliwa, ama wajiuzulu wenyewe au waondolewe na mamlaka iliyowapa mamlaka hayo.

 

Miongoni mwa walengwa ni Jaji Kiongozi Fakih Jundu, ambaye licha ya kustaafu, si tu aliongezewa mkataba bali pia alipandishwa cheo na kushika wadhifa huo alionao sasa. Kuna taarifa kwamba Ikulu pamoja na kutambua kosa hilo la kikatiba, Julai 29 mwaka huu, ilimwongezea Jaji Kiongozi Jundu mkataba mwingine wa miaka miwili.

 

JAMHURI imekuwa gazeti la kwanza nchini kuchapisha kwa kina kashfa zinazoukabili Mhimili wa Mahakama. Pamoja na kuwapo majaji wasiotambulika kikatiba, wapo wengine ambao ni watuhumiwa wa rushwa wakati wakiwa mahakimu na wengine wakiwa mawakili. Toleo lililopita tulichapisha baadhi ya majina ya majaji hao. Taarifa zaidi zinapatikana kwenye tovuti ya www.jamhurimedia.co.tz. JAMHURI imepata nyaraka zinazothibitisha hayo.

 

Baadhi ya wananchi ambao hukumu za kesi zao zimetolewa na majaji wasiotambulika kwa mujibu wa Katiba, sasa wanajiandaa kufungua kesi. Hali hiyo inatarajiwa kuleta tafrani kwani kuna kesi nyingi zilizotolewa uamuzi na majaji hao ambao kuwapo kwao kumekiuka ibara 111 na 121 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

 

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, amezungumza na JAMHURI na kusema kwamba baadhi ya majaji hawana elimu ya chuo kikuu kama inavyotamkwa kwenye Katiba, wengine ni wagonjwa ambao hawajawahi kusikiliza na kutoa hukumu tangu wateuliwe, na wengine wanakabiliwa na kashfa mbalimbali kabla hawajateuliwa kuwa majaji.

 

Lissu anasema uteuzi mwingi umefanywa “kishikaji” ili kuwawezesha baadhi yao kujiandalia mafao baada ya kustaafu. Anatoa mifano ya majaji kadhaa walioteuliwa ilhali wakiwa wamebakisha miezi michache kabla ya kustaafu utumishi wa mahakama.

 

GHARAMA ZA MAFAO YA JAJI MSTAAFU

 

Hadi mwaka 2008, Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu alikuwa akilipwa mshahara wa Sh 1,782,000 kwa mwezi. Pensheni yake ilitakiwa iwe asilimia 80 ya mshahara wake kwa mwezi.  Gharama zote za pensheni, mafuta, dereva, gari, matengenezo ya gari kwa miaka minne iligharimu Sh 187,388,800. Kiasi hicho ni pamoja na gharama za gari.

 

Kwa upande wa Jaji wa Mahakama ya Rufaa, kwa mahitaji yote hayo kwa kipindi cha miaka minne, pamoja na gari analopewa, ni Sh 192,841,600. Jumla kuu bila gharama ya gari ni Sh milioni 98. Mafao anayopata Jaji wa Mahakama Kuu aliyeko madarakani ni Sh milioni 125 kwa mwaka.

 

LISSU ATISHIA KULISHAWISHI BUNGE KUMNG’OA JK

 

Lissu anasema endapo Rais Kikwete atasita kuwaondoa majaji wote waliopo kinyume cha Katiba, katika mkutano wa Bunge wa Oktoba 30, mwaka huu atawasilisha hoja ya kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kumchunguza Rais Jakaya Kikwete.

 

“Hatuwezi kujaziwa mahakama na watu kama hawa (waliopo kinyume cha Katiba), hukumu zote walizotoa ni batili kwa sababu hawana sifa,” amesema Lissu.

 

Amesema Jaji Kiongozi Jundu anatakiwa ajiuzulu mwenyewe kwa sababu kwa hali ya mambo ilivyo, hata kama aking’ang’ania nafasi hiyo, hawezi kuwa na heshima mbele ya majaji.

 

“Ajiuzulu mwenyewe, kama hataki, basi aondolewe na aliyempatia nafasi hiyo kwa sababu yupo kwenye wadhifa huo kinyume cha Katiba. Aliyemteua asipomwondoa, tutamwondoa yeye kwa kutumia vifungu vya Katiba.

 

“Wote wanaotajwa kuwa wapo kwenye ujaji kinyume cha Katiba wajiuzulu, hili si jambo la ajabu, hivi karibuni nchini Kenya majaji zaidi ya 10 waliondolewa kwa mambo kama haya.

 

“Ikulu (Taarifa ya Kikundi Kazi), wasomi wa kisheria, majaji waliobobea. Jaji Luanda na Jaji Ramadhani – kila mmoja anasema hawa majaji wa mikataba hawafai, itakuwa ajabu kuona Mheshimiwa Rais Kikwete ananyamaza na kufumbia macho uvunjaji huu wa Katiba wa waziwazi,” amesema Lissu.

 

UTARATIBU WA KUMWONDOA RAIS MADARAKANI

 

Utaratibu huo umeainishwa katika Kanuni ya 121 ya Kanuni za Kudumu za Bunge (toleo la mwaka 2007). Kanuni hiyo inasema, “Mbunge yeyote anaweza kuwasilisha kwa Spika taarifa ya Hoja ya kumshtaki Rais kwa madhumuni ya kumwondoa Rais madarakani kupitia Azimio la Bunge kwa mujibu wa Ibara ya 46A ya Katiba ikiwa inadaiwa kwamba Rais: –

(a) ametenda vitendo ambavyo kwa ujumla vinavunja Katiba au Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma;

(b) ametenda vitendo ambavyo vinakiuka maadili yanayohusu uandikishwaji wa vyama vya siasa yaliyotajwa katika ibara ya 20(2) ya Katiba; au

(c) amekuwa na mwenendo unaodhalilisha Kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano. Isipokuwa kwamba, hoja ya namna hiyo haitatolewa, ndani

ya miezi kumi na miwili tangu ilipotolewa na kukataliwa na Bunge.

122.-(1) Bunge halitajadili wala kushughulikia hoja ya kumshtaki Rais, isipokuwa tu kama: –

(a) taarifa ya maandishi, iliyowekwa saini na kuungwa mkono na Wabunge wasiopungua asilimia ishirini ya Wabunge wote itatolewa;

(b) taarifa hiyo itawasilishwa kwa Spika siku thelathini kabla ya kikao ambapo hoja hiyo inakusudiwa kutolewa Bungeni;

(c) taarifa hiyo pia itafafanua makosa aliyoyatenda Rais; na

(d) taarifa hiyo vile vile itapendekeza kuwa Kamati Maalumu ya Uchunguzi iundwe ili ichunguze mashtaka yaliyowasilishwa dhidi ya Rais.

(2) Wakati wowote baada ya kupokea taarifa iliyowekwa saini na Wabunge na kujiridhisha kuwa masharti ya Katiba kwa ajili ya kuwasilisha hoja hiyo Bungeni yametimizwa, Spika atamruhusu mtoa hoja kuiwasilisha hoja hiyo Bungeni.

(3) Hoja hiyo itakapowasilishwa Bungeni, Spika atalitaka Bunge, bila ya kufanya majadiliano yoyote, lipige kura ya siri ili kupata uamuzi juu ya hoja hiyo.

JAMHURI inaona kwa hali ya siasa za nchi hii ilivyo kwa sasa ndani ya ukumbi wa Bunge kura ya siri ya kumg’oa Rais inaweza kutoa matokeo yasiyotarajiwa na wahusika.

 

UKIUKAJI KATIBA

Mwaka 2008, Ikulu iliunda Kikundi Kazi kwa Ajili ya Kuchambua na Kushauri Kuhusu Ajira ya Majaji Baada ya Kustaafu. Kikundi hicho kilichokuwa na wajumbe sita, kiliongozwa na Frederick Mmbanga kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma. JAMHURI inayo ripoti hiyo yenye kurasa zaidi ya 200 na vielelezo vyake.

 

Kikundi Kazi kilipomaliza shughuli hiyo kiliikabidhi Ikulu. Baada ya kupitia Katiba, Sheria na nyaraka mbalimbali, Kikundi Kazi kilijiridhisha pasi na shaka kwamba mikataba ya majaji, kama ilivyokuwa ikifanywa na marais wa Jamhuri ya Muungano, akiwamo Rais Jakaya Kikwete, imekuwa ikivunja Katiba.

 

Sehemu ya 9.1 ya mapendekezo ya Kikundi Kazi inasema, “Kwa kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 ndiyo inayotumiwa kumteua Jaji/inayotawala ajira ya Jaji, MIKATABA ILIYOPO HIVI SASA IKO KINYUME CHA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, 1977.

 

“Hii ina maana kwamba majaji hao wanafanya kazi ya Jaji kinyume cha Katiba hivyo kazi zote ambazo wamezifanya na wanaendelea kuzifanya wakiwa chini ya ajira mpya za mikataba hazina uhalali wowote kisheria. Kazi hizo ni sawa kama vile zimefanywa na mtumishi mwingine yeyote asiye na madaraka ya Jaji.

 

“Rais ASHAURIWE KUIFUTA MIKATABA hiyo mara moja kwa vile ina madhara makubwa kwa jamii na katika uteuzi wa majaji wapya kuchukua nafasi zao. Majaji waliofutiwa mikataba waendelee na pensheni zao kama kawaida.”

 

Sehemu ya 9.2 ya taarifa ya Kikundi Kazi inasomeka hivi, “Kwa majaji ambao wako kazini na wanakaribia kufikia umri wa kustaafu kwa lazima, Rais ashauriwe kuwaongezea muda wa kazi (extension) iwapo watahitajika na siyo kuwapa ajira za mkataba kama utaratibu ulivyotumika katika kumuongezea muda wa kazi Jaji V.K.D. Lyimo (angalia kiambatanisho).”

 

JAJI AUGUSTINO RAMADHANI APINGA MIKATABA

 

Jaji Mkuu mstaafu Augustino Ramadhani ni miongoni mwa wasomi mahiri wa sheria nchini ambao wamepinga dhana ya majaji kupewa mikataba. Jaji Ramadhani aliweka mtazamo wake katika maandishi na kumpelekea Jaji Mkuu wa wakati huo, Barnabas Samatta. Akasambaza mtazamo wake kwa majaji L. Makame, Jaji D. Lubuva, Jaji J. Mrosso, Jaji E. Munuo, Jaji H. Nsekela, Jaji J. Msofe na Maji S. Kaji.

 

Katika maoni yake, Jaji Ramadhani anasema, “Katika mada niliyoitoa kwa waheshimiwa wabunge niliongelea juu ya Dhana ya Uhuru wa Mahakama na nilisema mojawapo ya dhana hiyo ni majaji kuwa huru kwa dola (Executive). Nilisema kuwa uhuru huu hukingwa kwa ‘security of tenure’ na kwa majaji kulipwa mishahara moja kwa moja kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina (Consolidated Fund).

 

“Sasa sina hakika kama mikataba haiathiri dhana ya Uhuru wa Mahakama inapofanya kazi ya ujaji iwe ‘negotiable’. Dhahiri kwangu kuwa kama ujaji ni wa mkataba basi sheria za kawaida kuhusu mikataba zitatumika na siyo ‘security of tenure’. Doesn’t this compromise security of tenure?’

 

JAJI WA RUFAA KUPEWA MKATABA

 

Akiwa anajiandaa kutoa mada kwa wabunge, ndipo Jaji Ramadhani alipata fursa ya kipekee ya kuchunguza ibara ya 120 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Ibara ya 120(1) inasema: Kila Jaji wa Rufani atalazimika kuacha kazi yake atakapotimiza umri wa miaka sitini na tano, lakini masharti ya ibara hii ndogo yatatumika bila kuathiri masharti yafuatayo…

 

Ibara ndogo ya (3) inasema: Iwapo Rais ataona kuwa kwa ajili ya manufaa inafaa Jaji wa Rufaa aliyetimiza umri wa miaka sitini na tano aendelee kufanya kazi, na Jaji huyo wa Rufani anakubali kwa maandishi kuendelea kufanya kazi, basi Rais aweza kuagiza Jaji huyo wa Rufani aendelee kufanya kazi kwa muda wowote utakaotajwa na Rais (msisitizo wangu).

 

Tafsiri yangu hapa ni kuwa Rais anasema: “Jaji XYZ badala ya kustaafu ukitimia umri wa miaka sitini na tano nakuongezea miaka ABC uendelee kufanya kazi na utastaafu umri wa miaka OPQ. Hii haina maana kuwa Jaji wa Rufaa anayehusika atastaafu akitimiza miaka sitini na tano na kupata marupurupu yake halafu aajiriwe kwa mkataba. Tafsiri yangu kuwa aendelee na kazi mfululizo na aje kustaafu baada ya hicho kipindi cha ziada alichopewa. Akistaafu na kupata haki yake haendelei na kazi bali anaanza ajira mpya ya mkataba.”

 

Jaji Ramadhani ambaye ni mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mwenye cheo cha Brigedia Jenerali, anaongeza, “Labda tafsiri yangu inashawishiwa na hali ilivyo jeshini nitokako. Kule, mathalani, umri wa lazima wa kustaafu kwa wenye cheo cha kuanzia Brigedia Jenerali hadi Jenerali ni miaka 57. Lakini Amiri Jeshi Mkuu (Rais) anaweza kumuongezea afisa muda wa miaka kadhaa aendelee na utumishi. Hivyo yule afisa hatostaafu akitimiza umri wa miaka 57 bali atastaafu baada ya kipindi chake alichoongezewa.

 

“Hii imesababisha maafa. Kwa mfano marehemu Meja Jenerali Francis Louis aliongezewa muda ikawa angestaafu akitimiza umri wa miaka 60. Bahati mbaya alikufa akiwa bado miezi miwili au mitatu kufikia miaka 60. Kisheria alikosa haki za pensheni. Jeshi waliniomba niwape mapendekezo ya marekebisho ya sheria.”

 

JAJI MKUU KUPEWA MKATABA

Jaji Ramadhani anasema kutokana na tafsiri yake, Jaji wa Rufaa kustaafu na kupewa mkataba badala ya kuendelea na utumishi na kuja kustaafu akiwa amepindukia umri wa miaka 65, inafuatia kuwa siyo sahihi kwa Jaji Mkuu kustaafu na kupewa mkataba kuendelea na wadhifa huo kupindukia umri wa miaka 65.

 

“Hata kama tafsiri yangu ina walakini, Ibara 118(2) inasema, katika sehemu zinazohusika kama ifuatavyo: …[Jaji Mkuu] atashika madaraka ya Jaji Mkuu mpaka atakapotimiza umri wa kustaafu kama Jaji wa Rufani…

 

“Hivyo Jaji Mkuu anapaswa kustaafu akitimiza umri wa miaka 65, ambao ni umri wa kustaafu wa Jaji wa Rufani, na siyo umri ule wa Jaji wa Rufani anapoacha kazi baada ya kumaliza mkataba,” anasema Jaji Ramadhani.

HITIMISHO

Jaji Ramadhani anasema, “Nimeandika haya baada ya kutafakari kwa kina na kujihoji sana. Mimi mwenyewe, kunako majaaliwa, nitakuja kutimiza umri wa miaka 65. Na kama Mungu atanijaalia siha yangu kuendelea kama ilivyo, je, sitataka mkataba? Wahenga wanasema ‘lililompata peku na ungo litampata’. (Peku ni ungo mkuukuu). Hivyo nami yatanikumba hayo.

 

“Pamoja na hayo nimeleta maoni haya kwa madhumuni makuu mawili; Kwanza, sisi ni majaji wa upeo wa juu kabisa katika nchi hii. Tutakaloamua kama ni sawa au siyo sawa ndilo hilo mpaka ama majaji wengi wa Rufani wawe na mawazo tofauti au Bunge litunge sheria kutengua maamuzi yetu. Hivyo tuna wajibu wa kujichunguza (soul searching) na kuona kama tuko sawa tusingoje Bunge kutukosoa.

 

“Nia na madhumuni yangu ni kuwa masuala haya tuyajadili. Tukubaliane tafsiri iliyo sahihi. Lakini hata kama tukitoa tafsiri inayokubaliana  na tunavyotenda hivi sasa, swali linakuja, je, hakuna mwanya wa mashaka? Kama upo, that is, if there is ambiguity, hatuwezi kuweka vifungu vikawa bayana kabisa vyenye tafsiri ambayo haina shaka yoyote? Like Caesar’s wife we should be above board.

 

“Hivyo, madhumuni ya pili ni kuangalia nini cha kufanya ili tuweke mambo dhahiri bashiri bila kuwapo wasiwasi wowote na kuwapa fursa wale ambao wametimiza umri wa miaka 65 na ambao wana haja ya kuendelea waweze kufanya hivyo bila kuhatarisha kukosa kaa na gando…” Mwisho, Jaji Ramadhani alimaliza mtazamo wake kwa kusema, “Kama kuna yeyote niliyemkwaa namuomba radhi”.

 

JAJI BERNARD LUANDA ATOBOA: MIKATABA INAVUNJA KATIBA

Agosti 9, 2005 Jaji Bernard Luanda wakati huo akiwa Jaji Mfawidhi Bukoba, alimwandikia barua Jaji Kiongozi akieleza maoni yake juu ya hatua ya majaji kupewa mikataba. Kwenye utangulizi wa taarifa yake, Jaji Luanda aliweka bayana mtazamo wake juu ya jambo hilo.

 

Alisema, “Suala la majaji kupewa mikataba nadhani linaendeshwa kinyume cha Katiba, pamoja na barua hii, nafungasha maelezo ya kina kuhusu suala hili.” Barua yake kwa Jaji Kiongozi aliipa kichwa kisemacho, “Uhalali wa Kikatiba kwa Majaji Kufanya kazi kwa Mkataba baada ya Kustaafu”.

 

Anaanza kwa kusema, kwa mujibu wa Katiba ya Nchi, Majaji wa Mahakama Kuu watimizao miaka 60 wanalazimika kuacha kazi. Kwa upande wa Majaji wa Mahakama ya Rufani ni miaka 65. Hayo yameelezwa kwenye Ibara ya 110(1) na 120(1).

 

Anasema, “Kwa muda sasa wamekuwapo majaji wa Mahakama Kuu na Rufani wanaopewa mikataba ya kufanya kazi ya miaka miwili baada ya kustaafu. Wapo walioongezewa baada ya mkataba wa kwanza kwisha. Majaji hao huwa wanaingia mkataba kwa maandishi na Ofisi ya Rais (Utumishi).

 

“Swali kubwa la kikatiba ambalo linaweza kuibuka ni: Je, ajira hizi za mikataba kwa majaji ni sahihi? Upo uwezekano mkubwa ya kwamba Rais anapokubali Jaji Mstaafu apewe mkataba anafanya hivyo akidhani anatumia Ibara ndogo ya (3) za Ibara 110 na 120 ya Katiba.

 

Ibara hizo zinatamka: 110(3) Iwapo Rais ataona kuwa kwa ajili ya manufaa ya umma inafaa Jaji aliyetimiza umri wa miaka sitini aendelee kufanya kazi, na huyo Jaji mwenyewe anakubali kwa maandishi kuendelea kufanya kazi, basi Rais aweza kuagiza kuwa Jaji huyo aendelee kufanya kazi kwa muda wowote utakaotajwa na Rais.

 

Ibara ya 120(3) Iwapo Rais ataona kuwa kwa ajili ya manufaa ya umma inafaa Jaji wa Mahakama ya Rufani aliyetimiza umri wa miaka sitini na tano aendelee kufanya kazi, na huyo Jaji mwenyewe wa Mahakama ya Rufani anakubali kwa maandishi kuendelea kufanya kazi; basi Rais aweza kuagiza kuwa Jaji huyo wa Mahakama ya Rufani aendelee kufanya kazi kwa muda wowote utakaotajwa na Rais.

 

Jaji Luanda anaendelea kujihoji kwamba swali la kujiuliza ni maneno “aendelee kufanya kazi” yana maana gani?

“Ukisoma kwa makini utaona si sahihi kutoa tafsiri ya kuwa kwanza Jaji huyo astaafu halafu apewe mkataba. Tafsiri sahihi ni kwamba jaji huyo hapaswi kustaafu kwanza. Jaji huyo ataendelea na kazi mpaka muda aliotamka Rais kwisha ndipo atastaafu. Hivyo utaona kuna ‘continuity’.

 

Kwa kufanya hivyo Jaji huyo anayeendelea atalindwa na Katiba katika masuala ya ajira yake, kiapo chake, maslahi yake na kadhalika. Tofauti na Jaji Mstaafu aliyepewa mkataba. Ajira yake ya mkataba inaweza kufutwa wakati wowote. HALINDWI NA KATIBA. Hiyo ndiyo hali halisi. Kwa bahati mbaya sana hili halijaonekana!

 

“Lingine la kuliangalia ni hili. Kwa kuwa jaji amestaafu, basi kiapo chake nacho kimeondoka. Kwa bahati mbaya hawaapishwi ili washike kazi hizo za ujaji. Angalia Ibara 111 na 121 ya Katiba.”Ibara 111 ya Katiba inasema, “Jaji wa Mahakama Kuu hatashika madaraka yake ila mpaka awe ameapishwa kwanza kiapo cha uaminifu na pia kiapo kingine chochote kinachohusika na utendaji wa kazi kitakachowekwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge.”

 

Ibara 121 ya Katiba inasema, “Jaji wa Mahakama ya Rufani hatashika madaraka yake ila mpaka awe ameapishwa kiapo cha uaminifu na kiapo kingine chochote kinachohusika na utendaji wa kazi kitakachowekwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge.”

 

Jaji Luanda anahitimisha maelezo yake kwa kusema bayana, “Ni hoja yangu kwamba majaji waliostaafu na kupewa mikataba si majaji kwa mujibu wa Katiba.”

 

1888 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!