majaliwaWiki iliyopita kwa mshangao mkubwa nimesoma maelezo ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul  Makonda. Makonda amesema mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwa lipo kundi la watu 10 lilitaka kumhonga Sh 5,000,000 kila mmoja kwa maana ya Sh milioni 50 kwa mwezi asiendelee na mpango wa kuzuia uuzaji wa dawa za kulevya aina ya Shisha.

Makonda amewatuhumu Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Naibu Kamishna Suzan Kaganda, kuwa huenda wamekutana na hao wataalam wa kutoa Sh milioni 5 kuruhusu utumiaji wa Shisha. Kwa kujipendekeza, Makonda akamwomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa awawajibishe Sirro na Kaganda.

Sitanii, Namshukuru Waziri Mkuu Majaliwa kwa kutuliza kiherehere cha Makonda. Nasema kiherehere kutokana na kauli ya Waziri Mkuu Majaliwa kumweleza Makonda kuwa akishindwa kusimamia usitishwaji wa matumizi ya Shisha katika Jiji la Dar es Salaam, basi yeye hatasita kumwajibisha. Akamtaka Makonda afanye kazi yake.

Makonda kwa wadhifa wake, ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Jiji la Dar es Salaam. Rais John Pombe Magufuli alipomteua Makonda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, baadhi ya watu walitilia shaka uteuzi huu. Nikiri mapema kuwa mimi nilikuwa mmoja wa waliotilia shaka uteuzi huu.

Hoja ya kutilia shaka uteuzi wake si umri tu, bali hata uwezo. Naamini Rais Magufuli aliyemteua na wasaidizi wake, wanafuatilia kwa karibu matendo ya Makonda. Kimsingi, nampa heshima asiyostahili Makonda kumjadili katika safu hii. Hata hivyo, nalazimika kumjadili kutokana na matendo na wadhifa alionao, yanayoelekea kutoboa kitovu cha utawala bora katika nchi hii.

Sitanii, hatujasahau kauli ya Makonda dhidi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, mbele ya Rais John Magufuli wakati wa uzinduzi wa daraja la Kigamboni. Rais Magufuli naye, pengine kwa kumwamini kupita kiasi Makonda, alitoa kauli kuwa amemtumbua Kabwe. Baada ya muda mfupi, Kabwe akafariki dunia.

Makonda alikwenda msibani na mtoto wa Kabwe akakataa kumpa mkono. Tunaweza kuliona suala la kutopewa mkono kuwa ni dogo, lakini kidiplomasia ni ujumbe mkubwa mno. Makonda huyu, sina uhakika kama anajitambua. Huko mitaani yako maneno ya kutisha. Wapo watu wanaotilia shaka mwenendo wake. Wakati akiwatuhumu akina Sirro na Kaganda, yeye anatajwa kwa mabaya zaidi.

Uliza gari lake likiharibika nani huwa wanampa msaada kwenye tuta? Uliza, ukarabati wa ofisi yake Kinondoni na ofisi ya Mkuu wa Mkoa nani kaufanya na kwa fungu lipi la Serikali? Tabia ya Makonda ya kuwachogea wenzake si tu imekera jamii, naamini hata aliyemteua inamkera. Mkoa wa Dar es Salaam tunajua alichokifanya Makonda katika uchaguzi wa Kinondoni.

Sitanii, kwamba Makonda alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Konondoni, ni kweli. Kwamba wilaya ya Kinondoni yote ilichukuliwa na upinzani katika uchaguzi wa mwaka 2015, ni kweli. Kwamba Makonda alifanya  mbinu zisizokubalika kuwezesha mtoto wa Sitta kuwa Meya wa Kinondoni, ambapo mawaziri wanne waliazimishwa akili yake, wengi wanalifahamu hili.

Binafsi sidhani kama najitendea haki kumjadili kijana huyu mwenye umri karibu na nusu ya miaka niliyoisha duniani. Nrudia, kwmaba hata hivyo, kwa anayoyatenda ya kutuhumu vyombo vya dola, naamini sina budi kumjadili. Kwamba anawatuhumu Sirro na Kaganda ni hatari. Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Robert Boaz, amesema wameanza kuwachunguza Kaganda na Sirro.

Si nia yangu kuingilia uchunguzi unaoendelea, bali nataka haki itendeke. Kwamba Makonda ahojiwe ataje majina ya hao watu 10 waliotaka kumhonga Sh milioni 50. Aeleze, jinsi Sirro na Kaganda anaowatuhumu kula rushwa alivyopata taarifa. Mheshimiwa Majaliwa, ikiwa Makonda atashindwa kubainisha hili la Shisha, itatulazimu kuhoji Makonda katudanganya mangapi kama taifa?

Sitanii, naomba kuhitimisha kwa kauli nzito. Tuhuma dhidi ya vyombo vya dola kuwa vimekula rushwa, ni kubwa mno. Serikali Kuu inapaswa kuchunguza na ikithibitika kuwa Sirro au Kaganda wamekula rushwa ya Shisha, basi waondolewe kwenye nyadhifa wanazozishikilia haraka na kushitakiwa. Hata hivyo, ikithibitika kuwa Makonda kafyatua, sawa na alivyofanya kwa Kabwe, basi Serikali imchukulie hatua mara moja.

2573 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!