Majipu huanza kama chunusi Zanzibar!

seifMiaka 15 iliyopita, nikimaanisha mwaka 2000 katika mwezi wa Novemba, nilifanya mahojiano na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Tanzania Bara, Wilfred Muganyizi Lwakatare. Katika mahojiano hayo, nilimuuliza juu ya sintofahamu ya kisiasa iliyokuwa inaendelea Zanzibar baada ya kuwa CUF wamekataa matokeo ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba.

Lwakatare, ambaye sasa ni Mbunge wa Bukoba Mjini kwa tiketi ya CHADEMA, aliniambia mambo mengi, lakini kati ya yote alisema: “CUF inatoa siku 90 uchaguzi uwe umerudiwa Zanzibar, vinginevyo watatutambua sisi CUF ni akina nani.” Hapa CCM walikuwa wametangazwa washindi. CUF wakataka uchaguzi Zanzibar urudiwe.

Nikumbushe tena kidogo. Mwaka 1995 ilikuwa umefanyika Uchaguzi wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi Tanzania, ambapo kituo cha televisheni cha DTV kilitangaza kuwa Maalim Seif Shariff Hamad ameibuka mshindi. DTV walipigwa faini, lakini bado matokeo yakatangazawa na Seif akatangazwa kupata asilimia 49.8 huku Komandoo Dk. Salmin Amour akitangazwa kupata ushindi kwa asilimia 50.2.

Sitanii, kwa bahati mbaya waliokuwa wanajumulisha hizi kura walisahau kuwa kuna kura zilizoharibika. Kwa maana hiyo, katika historia ya Zanzibar uchaguzi huu tulishuhudia washindi wakitangazwa kwa kura halali tu, bila kuelezwa zilizoharibika zilikuwa asilimia ngapi. Kwa Wakatoliki, wanasema “Hili ni fumbo la imani.”

Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Na 11 ya Mwaka 1984 kama ilivyorekebishwa mwaka 2010, Kifungu cha 42 (5) kinasema mtu yeyote au taasisi itakayotangaza matokeo ya uchaguzi kabla ya Tume itapigwa faini ya Sh 500,000 au kwenda jela miaka 5 au vyote viwili. Maalim Seif Shariff Hamad ametangaza matokeo kabla ya Tume mwaka huu.

Kwa mshango wangu, Seif hakupigwa faini ya Sh 500,000, hakuhukumiwa kwenda jela miaka 5 au kupewa adhabu zote mbili. Badala yake, Mwenyekiti wa Tume Jecha Salim Jecha akafuta matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar na akatangaza kinyume na sheria kuwa uchaguzi utaitishwa baada ya siku 90. Masikini utawala wa bora!

Enzi za Mkoloni nchi ilikuwa inaendeshwa kwa matamko. Mkoloni alipokuwa anaona hali fulani haimfai, anatoa tamko lenye mazingira ya kumnufaisha. Haki za binadamu zinapatikana kwa kuheshimu utawala wa sheria. Utawala wa sheria unapatikana kwa kuheshimu misingi ya Katiba na sheria za nchi. Leo, tunashuhudia yanayoendelea Zanzibar.

Sitanii, pengine nichepuke kidogo. Nimemfahamu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana kitambo sasa. Ni mtu asiyependa kusikia upuuzi. Ni mtu anayesimamia haki. Kwa bahati mbaya, katika hili sijasikia vyema sauti yake. Naisikia zaidi sauti ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar Vuai Ali Vuai.

Nikiendeleza mchepuko wa mawazo kidogo, nitanue kinachoendelea Zanzibar na maeneo mbalimbali katika nchi hii. Niliamini uchaguzi umekwisha. Sijui kama ni mpango wa CCM au wapambe wachache wenye kufanya haya, ila tunatetelesha demokrasia nchini. Tumeyasikia yaliyoendelea Tanga. Mshindi wa umeya anatangazwa kwa nguvu.

Tumeyasikia ya Kyerwa, Kyela, mamluki Dar es Salaam na mwingineko. Madiwani wa vyama vya upinzani wanakamatwa na kuwekwa ndani. Wanabambikiwa kesi, hapana shaka baada ya uchaguzi watafutiwa kesi husika na maisha yataendelea. Najua hili la Zanzibar limeandikwa kitambo. Jecha hawezi kusimama si mbele ya mke wake tu, bali hata watoto wake kueleza alipata wapi mamlaka ya kufuta uchaguzi.

Sitanii, nimeanza na historia jinsi nilivyoandika habari ya CUF watoa siku 90. Baada ya habari hiyo, aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Omary Mahita akasema kama CUF ni Ngangari, basi polisi nao ni Ngunguri. Hii maanake ni nini. Mahita alikumbuka mchezo wa kujifunza kuandika wa nga, nge, ngi, ngo, ngu. Kwa hiyo akaona kama nga haiwezi kuwa zaidi ya ngu!

CCM nao kwa upande wao walitangaza kuwa kama CUF ni Ngangari, basi wao ni Nginjangija. Sitakaa nisahau. Baada ya  hiyo habari yangu, vyombo vya habari vya ndani ya nje vikaidakia. Waandishi na wanasiasa wakaanza kuhesabu siku kila kukicha wakipunguza moja. Zikashuka hadi nane, hakika joto likaonekana wazi. Iliposalia siku moja kabla ya 90, Januari 25, kama kionja mchuzi vile, wakauawa watu wawili.

Siku iliyofuata, Januari 26, wananchi wakalipiza kisasi kwa polisi. Kwa ukatili kabisa huko Pemba wakachinja askari wawili. Narudia, si tu kwamba walifanya kosa kuua hao askari, bali unyama wa hali ya juu kwa kutenganisha kichwa na kiwiliwili. Katika hatua hii, askari walijibu mapigo. Wananchi wakataharuki, wakakimbia hovyo.

Kwa mara ya kwanza Tanzania ikazalisha wakimbizi wakakimbilia Shimoni Kenya. Maisha ya Watanzania 31 yakapotea, ingawa taarifa zisizo rasmi zinasema ni zaidi ya hao. Kuanzia wakati huo, uhasama Zanzibar ukawa zaidi ya miaka ya 1950. Mwaka 2001 Zanzibar walifikia hatua wakawa hawazikani tena. Zanzibar walifikia hatua hawashirikiani harusi.

Tulishuhudia milipuko ya mabomu ya kila aina na aibu za aina yake kwani kuna nyakati visima vikawa vinawekwa kinyesi kwa sababu ya itikadi za kisiasa. Ilifika mahala Wazanzibari wakakumbuka kaulimbiu ya enzi za ukoloni za “Gozi Zuia Fedha.” Hii maana yake ni kuwa Waafrika weusi wasinunue bidhaa kwenye maduka ya Waafrika wenye asili ya Kiarabu.

Sitanii, nimesoma mateso makubwa ya kihistoria waliyopata Wazanzibari. Nafikiria makovu ya kisaikolojia waliyonayo Wazanzibari kabla ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964. Ni kwa bahati mbaya sana, kwamba Zanzibar haijapata fursa ya kufanya maridhiano. Afrika Kusini walipita katika kipindi kigumu sawa na Zanzibar, lakini mara baada ya uhuru waliunda Tume ya Maridhiano iliyoongozwa na Askofu Desmond Tutu.

Tume hii ilizikutanisha pande zilizokuwa zikisigana. Pande hizi zilielezana ukweli na kusameheana. Kwa Zanzibar suala hili halijapata kufanyika. Nakumbuka aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola wakati wa uongozi wa Rais Benjamin Mkapa, Chifu Emeka Anyauko alipata kuwasuluhisha Zanzibar kufikia Mwafaka wa Kwanza mwaka 1998. Hata hivyo, mwafaka huu ulikuwa wa kufunika kombe mwanaharamu apite.

Mwaka 2001 CUF na CCM waliingia Mwafaka wa Pili, lakini nao haukuzaa matunda kwani baada ya uchaguzi wa mwaka 2005 CUF walikataa kutambua matokeo. Kilichotokea mwaka 2009, Maalim Seif Shariff Hamad alizungumza na Rais mstaafu Amani Abeid Karume, kama sikosei ilikuwa Novemba 9, kisha wakatoka na tamko lililozaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Hadi leo, ukiwauliza kada pana ya Wazanzibari kwamba mazungumzo kati ya Karume na Seif hadidu rejea zake zilikuwa zipi, sina uhakika kama wanazidi 10 wenye kufahamu kilichozungumzwa na nini hasa yalikuwa makubaliano. Mwaka 2010 tuliona mambo yanafanyika kwa kasi ya upepo. Ikabadilishwa Katiba ya Zanzibar kwa kiwango cha kuvunja Katiba ya Muungano.

Hili lilifanyika kwa hasira eti kwa sababu tu, aliyekuwa Waziri Mkuu wa wakati huo, mtoto wa mkulima, Mizengo Pinda alitoa kauli bungeni kuwa “Zanzibar siyo nchi.” Wakubwa wakaamua walipize kisasi. Wakaona bora wajitenge na kuwa na Zanzibar yao huru. Lakini yale yale tuliyoyashuhudia miaka iliyopita, ndiyo tunayoyashuhudia mwaka huu.

Sitanii, heshima ya Tanzania kwa uchaguzi wa Zanzibar mwaka huu imetetereka. Tusidanganyane. Haiwezekani kura za Muungano zikawa halali, za Zanzibar zikawa haramu. Tume iliyosimamia ni moja. Napata shida tunatokaje hapa. CCM kwa kuwa Maalim Seif alisema wameshindwa, wanataka uchaguzi urudiwe na Maalim Seif anasema hakuna cha kurudia uchaguzi. Mazungumzo yanaendelea, hatupewi taarifa juu ya kinachojiri, tunabaki kusikilizia kupitia dirishani.

Tuliyoyashuhudia Zanzibar mwaka 2001 au tunayoyashuhudia Burundi leo kutokana na viongozi kutamani uongozi wa kimabavu, sitashangaa yakijitokeza Zanzibar tena miezi michache ijayo. Mbaya zaidi, hata Maalim Seif hajawaondolea Wanzibari na Watanzania wasiwasi. Wakati dunia inapambana kuungana, Maalim Seif anataka kuvunja Muungano.

Ukimuuliza atapata nini katika utengano, anakwambia mamlaka kamili kwa Zanzibar. Ukiuliza kwa nini Mamlaka Kamili, ikitokea mpo chumba kimoja atakwambia kupigiwa mizinga 21 na akapata heshima kama Rais. Haangalii ni Wapemba wangapi wapo Kigoma, Bukoba, Mtwara, Tabora na kwingineko kuwa Muungano huu ukivunjika mapande ya ardhi wanayomiliki yanarejeshwa.

Si hilo tu, Seif na wezake wanahusishwa na Sultan wa Omani. Kwamba wapo Wazanzibari walikimbia baada ya Mapinduzi Matukufu waonaishi kama wakimbizi Uingereza na Omani na wanasubiri wakati wowote kurejea Zanzibar. Tena, ninaozungumza nao hawaoni aibu kusema Zanzibar ya akina Maalim Seif wanataka Mkuu wa Nchi ya Zanzibar arejee kuwa Sultan wa Oman!

Sitanii, kila upande una hofu. Wale wafuasi wa ASP hawaamini kama ekari tatu walizogawiwa na Mzee Karume wataendelea kuwa nazo iwapo CUF itapewa nchi. Ni katika misingi hiyo nasema Zanzibar kuna zaidi ya tatizo. Wakubwa wanapaswa kukaa wakakubali busara iliyotumika Afrika Kusini ikaja hapa kwetu. Ni vyema kabla ya chochote kiwacho, iundwe Tume ya Maridhiano Zanzibar.

Kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa au la si hoja. Watu hawa wanahitaji kujengewa mazingira ya kuaminiana. Waliokuwa wafuasi wa Hizbu wafike mahala waamini kuwa hawakuporwa na waliokuwa wafuasi wa ASP wafike hatua waone hata CUF wakitawala, hawatanyang’anywa mashamba yao na kugeuzi raia daraja la pili.

Sitanii na nahitimisha kwa kusema kuwa kinachoendelea Zanzibar ni jipu lililoanza kama chunusi. Rais John Pombe Magufuli amekwishasema yeye ni mtumbua majipu. Naomba sasa kama nilivyopata kusema kwenye moja ya makala zangu atumbue jipu hili. Kwa Kiingereza wanasema “akagunju kalafa tikaulila nzamba.” Zanzibar ni jipu, hatuna budi kulitumbua. Mungu ibariki Tanzania.