Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limedhamiria kueneza uelewa, na kukuza matumizi ya viwango na kanuni za udhibiti wa ubora katika sekta za viwanda na biashara.

Hatua hiyo ya TBS inakuja huku kukiwa na wimbi kubwa la kuzagaa kwa bidhaa zinazozalishwa nje na ndani ya nchi na kuuzwa katika kila upande wa Tanzania.

 

Dhamira hiyo ya TBS inatiwa chachu na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda, baada ya kuzindua Bodi mpya iliyojaa ari na nguvu mpya katika utendaji wake.

 

Bodi hiyo imepewa miezi sita kuhakikisha soko na bidhaa za  afya ya mtumiaji vinakuwa salama na shirika hilo kurudisha heshima yake kama zamani.

 

Walioteuliwa katika Bodi hiyo ya TBS ni Geofrey Simbeye,  Mwakilishi  kutoka TPSF, Fatma Riami Diwani (Viwanda Vidogo na Vya Kati), Michael Kamba (Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali), Dkt. Pamela L. Sawa (Wizara ya Afya), Magdallena Utouh (Tume ya Ushindani), Jasson B. Bagonza (Wizara ya Fedha).

 

Wengine ni Juma Rajabu, mwakilishi Umoja wa Wajumbe wenye uelewa wa masuala ya viwango, Rashid A. Salum (Umoja wa Wajumbe wenye uelewa wa masuala ya viwango, Zanzibar), Profesa Ntegua Mdoe (Vyuo vya Elimu ya Juu), Dkt. Fidea L. Mgina (Wizara ya Viwanda na Biashara) na Joseph Masikitiko (Kaimu Mkurugenzi Mkuu).

 

Pia Bodi hiyo imemteua Joseph Masikitiko kuwa Kaimu Mkurugenzi wa TBS. Kabla ya uteuzi huo, Masikitiko alikuwa Mkurugenzi wa Huduma za Shirika.

Aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi, Leandri Kinabo, anaendelea na nafasi yake ya Mkurugenzi wa Utayarishaji Viwango, ambapo Emanuel Itelia na aliyekuwa Ofisa Mipango, anakuwa Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Shirika. Wote watafanya kazi kwa uangalizi wa miezi sita.

 

Tayari Bodi, kwa kushirikiana na manejimenti ya shirika hilo, imeonesha matumaini ya kutokomeza bidhaa hizo. TBS imevifungia kwa muda usiojulikana viwanda vinne hadi sasa vinavyozalisha nondo.

 

Viwanda vilivyofungiwa ni Metro Steel Mills kilichoko Vingunguti, Dar es Salaam; Quaim Steel Mills kilichopo Chang’ombe wilayani Temeke, na Am Steel na Dar Steel vyote vya Mbagala Zakhem.

 

Hatua hiyo imekuja baada ya kubainika kwamba vimekuwa vikizalisha na kuuza nondo zisizokuwa na ubora unaotakiwa, na vingine vikizalisha nondo bila kuwa na kibali cha TBS, jambo ambalo ni kosa kutokana na sheria namba 2 ya mwaka 2009.

 

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungiwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Quaim, Hassan Amir, alisema kiwanda chake kilianza kuzalisha nondo mwaka 2006.

 

Mwanasheria wa TBS, Baptista Bitao, amesema shirika lake linafanya kazi kwa kuzingatia sheria inayompa mamlaka inspekta wa shirika hilo kukifungia kiwanda kinachokiuka sheria ya namba 2 ya viwango ya mwaka 2009.

 

“Hatua ya kusimamisha uzalishaji wa bidhaa ni ya kwanza kisha barua inatakiwa ifuate katika kipindi cha siku tatu, hawa wamefungiwa ili waweze kufuata utaratibu ikiwa ni pamoja na kuzalisha bidhaa zenye ubora, wakikiuka watawafikisha mahakamani,” amesema.Amsema kufanya hivyo ni kukiuka sheria ya viwango namba 2 ya mwaka 2009.

 

Meneja wa Kiwanda cha Metro, Onesmo Ngondo, alitoa lawama kwa TBS akidai kuwa haitoi elimu kwa wananchi na hasa wawekezaji, ili waweze kutambua umuhimu wa kupeleka bidhaa zao kuchunguzwa na kuthibitishwa kabla ya kuuzwa.

 

Akizungumzia kuhusu hatua hiyo, Ofisa Uhusiano wa TBS, Roida Andusamile, anasema imetekelezwa baada ya TBS kuchukua sampuli ya vipande kadhaa vya nondo na kuvipima kwenye maabara yake. Katika uchunguzi huo, ilibainika kuwa nondo hazikuwa na ubora unaotakiwa.

 

Amesema hatua hiyo ya TBS ni mwendelezo wa kusaka bidhaa zinazozalishwa zikiwa chini ya kiwango.

 

TBS ilimeanza kuzisaka nondo feki kwenye baadhi ya kampuni za usambazaji wa bidhaa hizo, na kusimamisha uuzaji wa zaidi ya tani 1,350. Viwanda vilivyofungwa kwa kuzalisha nondo bila kuwa na kibali kutoka katika shirika hilo ni Am Steel na Dar Steel.

 

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ukaguzi, Mwanasheria Mkuu wa TBS, Bitaho, amesema wameamua kufunga viwanda hivyo baada ya kujiridhisha na ukaguzi kuwa vinafanya kazi ya kusambaza bidhaa sokoni bila kupewa leseni ya ubora wa viwango kutoka shirika hilo.

 

Bitaho amesema viwanda vilivyofungiwa ni pamoja na Dar Steel na AM Steel and Iron, kilichosajiliwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) mwaka 2002 na kupata leseni Manispaa ya Temeke mwaka 2004. Mwaka 2007 kilianza uzalishaji wa nondo chini ya msimamizi ambaye pia ni mmiliki wake, Sunil Patel.

 

Anasema walipofika kwa ajili ya ukaguzi ndani ya kiwanda hicho, walikuta nondo tani 60 ambazo zilikuwa tayari kupelekwa sokoni, lakini zilirudishwa sambamba na kiwanda kufungwa.

 

Bitaho amesema Kiwanda cha Dar Steel ambacho kilisajiliwa mwaka 2002, kilipatiwa leseni ya biashara mwaka 2005 pamoja na kuanza uzalishaji mwaka 2012, kilikutwa na nondo tani saba zikiwa tayari kupelekwa sokoni. Hata hivyo, zilizuiwa, ambapo Meneja Uzalishaji wa kiwanda hicho, Modest Ndaga, alipewa agizo la kufungwa kwa kiwanda hicho.

 

Naye Mkaguzi wa TBS, Yona Afrika, anasema viwanda vilivyofungiwa vinatakiwa viandike malalamiko yao ndani ya siku saba, ili waweze kukaguliwa na wakizidisha ndani ya siku 14, TBS watazikagua bidhaa hizo na kuziteketeza.

 

Amesema kwa sasa wameanza ukaguzi wa viwanda kwa Mkoa wa Dar es Salaam na kwamba ukaguzi huo utaendeshwa nchi nzima. Kutokana na Kanuni ya Viwango namba 25 ya mwaka 2012, viwanda visivyo na ubora vinapaswa kufungiwa.

 

Anasema kanuni hiyo inalitaka shirika hilo lijiridhishe na ubora wa viwanda, endapo watakuwa wanazalisha chini ya viwango faini yake ni Sh milioni 50 hadi Sh milioni 100 ama uongozi kupelekwa jela miaka miwili.

 

“Kama wataonekana wanazalisha bidhaa bora, tutawapa cheti na kuwaruhusu waendelee na uzalishaji, kwani tulitangaza muda mrefu wote waje watoe taarifa ili wakaguliwe kabla ya kuzalisha, lakini tunashangaa wengine wameanza uzalishaji,” anasema Afrika.

 

Mbali na kuvifungia viwanda hivyo, TBS imeharibu betri za magari zipatazo 985 kati ya 1,393 zilizoingizwa nchini mwaka jana, baada ya kubaini kuwa hazikidhi matakwa ya kiwango cha kitaifa namba TZS 144:2011.

 

Roida amesema, kwa majibu ya ripoti ya upimaji iliyotolewa na TBS, betri hizo zilifeli uwezo wa kuchaji (rating capacity).

 

“Betri inapofeli uwezo wa kuchaji, ufanisi wake huwa ni mdogo, hivyo kumsababishia hasara mtumiaji.

 

Bidhaa hizo zenye thamani ya Sh. 55,256,000 ziliagizwa kutoka Indonesia na Kampuni ya Noble Azania Auto Spares.

 

Shirika la Viwango Tanzania (TBS)

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 3 ya mwaka 1975 na kuanza kazi rasmi Aprili 16, 1976, kisha kuundwa upya kwa Sheria Na. 2 ya mwaka 2009 iliyoifuta sheria ya kwanza. Sheria mpya imelipa Shirika uwezo mkubwa zaidi wa kusimamia shughuli za utayarishaji wa viwango na udhibiti wa ubora.

 

Sheria mpya ya viwango imebainisha hatua zifuatazo zitakazochukuliwa inapobainika kuwapo kwa bidhaa hafifu:- Kuondoa bidhaa hafifu zilizopo sokoni; kufuta leseni; kuweka utaratibu wa marejesho au fidia; kuweka taratibu za kuharibu bidhaa duni au kuzirudisha zilikoagizwa; kutoza faini.

 

Sheria hii imeambatana na kanuni nne za utekelezaji ambazo ni: Kanuni za usimamizi wa alama ya ubora; kanuni za Ithibati ya Ubora (Certification Regulations); kanuni za Upimaji wa Bidhaa (Tested Products Regulations); pia kanuni za Ithibati ya Ubora wa Shehena (Compulsory Batch Certification of Imports Regulations); kanuni za Ubora na Usalama wa Chakula (Food Quality and Safety Regulations).

 

Majukumu ya TBS

Kwa mujibu wa Sheria ya Viwango Na. 2 ya mwaka 2009, TBS ina majukumu yafuatayo:

Kuweka, kurekebisha na kusimamia viwango vyote vya kitaifa, udhibiti wa ubora wa bidhaa za ndani na nje, kutoa ushauri viwandani juu ya uzalishaji wa bidhaa bora, kupima na kuhakiki vipimo vinavyotumika viwandani.

 

Majukumu mengine ni kuelimisha umma juu ya masuala ya viwango, kutoa leseni za matumizi ya alama ya ubora kwa bidhaa za ndani na nje zilizokidhi viwango stahili.

Kwa ujumla, jukumu la jumla la Shirika ni kukuza matumizi ya viwango, na kuinua ubora wa bidhaa na huduma nchini ili kupanua na kuimarisha soko la ndani na nje.

1505 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!