Juzi nimesoma habari inayohusu utajiri wa kutisha, wa baadhi ya viongozi wa madhehebu ya kikristo. Viongozi wanaotajwa, wengi wao ni hawa wa madhehebu yanayoibuka na kusajiliwa kila siku. Nilifurahi kusoma habari hiyo kwa sababu imebeba kile ambacho mara zote nimekiamini.

Habari hiyo imenikumbusha kisa kimoja nilichosimuliwa na rafiki yangu hivi karibuni. Rafiki huyo aliniambia kwamba katika eneo la Manzese, Dar es Salaam, kumetoka kisa cha aina yake. Watu wanaojifanya maombi yao ni makali kiasi cha kuweza kuwafufua wafu waliifuata familia moja iliyokuwa na mgonjwa mahututi.

 

Baada ya kutambua kuwa mgonjwa yule kashindikana kupona, wakasema wao wangeweza kumponya kwa maombi. Wakaingia chumbani alimokuwa. Wakaanza na kuendelea kusali kweli kweli. Baada ya dakika kama 15 hivi wakawaomba wanandugu waende nje ili waweze “kuwasiliana na Yesu” moja kwa moja.

 

Baada ya dakika kama 30 za maombi, mmoja akatoka nje akiwa amejiinamia. Kwa masikitiko makubwa akawaeleza wale ndugu na jamaa waliokuwa nje ya nyumba kwa kusema; “Tunasikitika kwamba mgonjwa amefariki dunia.” Ndugu wakaanza kulia. Akawaambia, “Msilie maana tunauchukua mwili wake na kwenda nao kanisani kwa ajili ya maombi zaidi maana tumepata maono kuwa atafufuka.”

 

Kweli, wale ndugu wakatulia. Baada ya muda wakamchukua yule “marehemu” na kumpeleka kanisani kwao kwa ajili ya maombi yenye uwezo wa kuvunja nguvu zote za mwovu ibilisi!

 

Walipofika kanisani maombi yaliendelea usiku kucha. Asubuhi wakawatangazia kuwa yule marehemu kafufuka kutokana na nguvu za maombi! Habari hizo zikatikisa kweli kweli. Wapo walioamini lakini wengine walipinga. Walioamini wakawa wengi.

 

Ukweli wa mambo. Kumbe walichofanya matapeli hao kwa kivuli cha kanisa ni kumdunga ‘nusu kaputi’ yule mgonjwa kiasi cha kumfanya aonekane kweli kafariki dunia. Kule kukesha kanisani kulilenga kumfanya atokwe na ile “nusu kaputi”. Alipoanza kurusha mikono na kupepesa macho, wale matapeli wa kiroho wakataka umma uamini kuwa maombi ndiyo yaliyomfufua, na kwamba wao wana nguvu hizo za kimungu.

Kisa hiki ni cha kweli. Nimekitoa kama njia ya kuonesha ni kwa namna gani wananchi hasa wenye shida wanavyohadaiwa. Ongezeko la madhehebu ya kilokole si jambo la kuachwa hivi hivi bila kuhojiwa. Kwa kuwa baadhi ya wanahabari wameanza kulifuatilia jambo hili, matarajio ya wengi ni kuona wanaingia ndani zaidi ili kupata ukweli wa mambo.

 

Neno la Mungu sasa limegeuzwa kuwa biashara ya kuwatajirisha baadhi ya watu katika nchi yetu. Mambo haya tulizoea kuyasikia katika nchi za Nigeria, Zambia na kwingineko lakini sasa yameingia kwa kasi mno nchini mwetu.

 

Pamoja na kuamini kwangu kwamba Mungu yupo, sidhani kama kweli aina hii ya ibada ya njia za mavuno inayofanywa na baadhi ya “wachungaji na watumishi wa Mungu”, inaweza kunishawishi kubadili msimamo hasi niliyoanza kuujenga juu ya watu hawa.

 

Hawa wanaojiita watumishi wa Mungu ni “wasanii” tu. Wanajitahidi kulitumia jina la Mungu kuwapa watu matumaini yasiyowezekana. Wanatumia mazingaombwe kuwaaminisha watu kuwa Mungu ana nguvu za ajabu zinazoweza kumaliza matatizo yao pasi na wao kuhangaika!

 

Sina hakika, lakini jambo hili tunapaswa kulichunguza kuanzia kwenye ofisi inayotoa usajili wa madhehebu haya. Nasema hivyo kwa sababu usajili wa makanisa haya unafanywa kwa kasi na kwa idadi mtu unayoweza kujiuliza, kulikoni?

 

Mara kadhaa tumesikia polisi wakipelekwa kulinda au kukagua maeneo fulani fulani ili baadaye kinachopatikana kiweze kufikishwa kwa wakuu wao. Wanaopangwa sehemu nono kama za mizani, vituo vya mabasi na kwenye doria ni wale wanaopeleka makusanyo ya kuvutia! Haya mambo yanazungumzwa, na kwa kweli yapo.

 

Isije ikawa mambo kama hayo yapo pia katika ofisi inayotoa usajili wa makanisa haya. Yawezekana mtoa usajili akawa na fungu lake analopata kutoka kwa “wachungaji na watumishi wa Mungu”.

 

Baadhi ya matapeli wameona kuwa njia nzuri na sahihi ya kupata fedha au utajiri wa haraka haraka ni kupitia kwenye shida za watu. Wapo watu tunaowatambua kuwa hawana mizizi ya kiimani, lakini ghafla wameweza kuanzisha makanisa na sasa ni matajiri wa kutupwa. Ukwasi wao unathibitishwa na namna wanavyolipa mamilioni ya shilingi kwa ajili ya vipindi vyao kuweza kuonekana kupitia runinga.

 

Kipindi cha dakika 30 au saa moja katika runinga kinagharimu fedha nyingi mno. Fedha hizi hazitoki mahali pengine isipokuwa kwa waumini, na mara kadhaa kwenye biashara haramu kama za mihadarati. Hapa ikumbukwe kuwa wapo walioamua kutumia makanisa kama ngao ya kuendesha biashara hizo chafu.

 

Kuna watumishi wa Mungu walioamua kutenga viti makanisani kwao kulingana na hadhi na kiasi cha sadaka na misaada mingine kutoka kwa waamini wao.

Wale wenye ukwasi wanapewa nafasi za mbele, na mara kadhaa hata viti wanavyokalia ni tofauti na vya makabwela wenye sadaka zisizo za noti.


Hapa ndipo kunakojitokeza maswali mengi. Tangu lini kanisani kukawa na utaratibu kama wa kwenye ukumbi wa starehe au uwanja wa mpira? Tangu lini kanisani kukawa na utaratibu unaofanana na wa jukwaa la siasa? Hivi mbele ya waamini wa Mungu kuna VIP?

 

Jambo jingine linalotia shaka na kuthibitisha kuwa kinachotafutwa na watu hawa ni fedha, ni uamuzi wa wao kutanguliza mbele namba za M-Pesa, TigoPesa, Airtel Money, na kadhalika. Mara kadhaa wanapoendesha vipindi kwenye runinga, chini huweka namba ambazo mtu anayeguswa au anayehitaji upako anapaswa kuzitumia kupeleka fedha.

 

Katika redio kuna mahubiri yanayoendeshwa. Wasikilizaji twatakiwa tutume fedha kwa njia hiyo ya kieletroniki au kwa posta. Tunaambiwa kuwa fedha/sadaka hizo zikipokewa kwa mtumishi wa Mungu hutakatisha maombi na kufanya yapokewe mbinguni! Kwa maneno mengine ni kwamba kama kuna mtu ana imani ya kuponywa, lakini akawa hana uwezo wa kifedha, basi Mungu hatapokea na kummalizia shida zake! Hii ni sanaa tu.

 

Mwenye kanisa ndiye kila kitu. Hakuna mahali, hasa kwenye fedha ambako anawashirikisha wengine. Mara kadhaa tumeona makanisa haya ni mali binafsi za mwenye kanisa, mkewe na familia yake.

 

Tuangalie maisha wanayoishi hawa watumishi wa Mungu. Maisha yao ni ya kifahari mno. Juzi tumeoneshwa kwenye mitandao nyumba anamoishi mmoja wa watumishi wa Mungu katika eneo la Mbezi, Dar es Salaam.


Kwenye ufunguzi kawaita baadhi ya maskini. Akawaandalia chakula na vinywaji. Wakati wao wakimsifu mchungaji kwa kujenga nyumba kubwa na ya kifahari, sidhani kama wote wana vibanda vya kuishi au kama wamelipa kodi ya pango.

 

Watumishi hawa wamekuwa wafanyabiashara wakubwa. Kwa bahati nzuri au mbaya ni kwamba hawalipi kodi, kwa hiyo miradi yao yote wanaiendesha bila kulipa kodi kwa kigezo kwamba ni ya kanisa! Wanaingiza magari bila kuyalipia ushuru kwa mgongo wa kanisa. Wapo wanaoingiza vifaa vya ujenzi kwa njia hiyo hiyo. Wanajitwalia mashamba makubwa makubwa.

 

Lakini kwanini hali hii ya kuwapo makanisa inazidi kushamiri? Kwa hakika hali hii si hapa Tanzania tu, bali katika maeneo mengi duniani, hasa yenye watu maskini waliokata tamaa. Watanzania wengi wamekata tamaa ya kufanikiwa katika maisha. Hali hii imewafanya wengi wetu tuwe wepesi wa kuamini kuwa njia za miujiza zinaweza kutukomboa kutoka katika lindi la ufukara na matatizo ya kila aina.

 

Jamii inayoweza kuamini kuwa kwa kusali pekee Mungu anaweza kushusha neema zake, hata kuifanya iweze kula na kuishi kwa raha; jamii hiyo inakuwa imeshakata tamaa.

 

Miaka kadhaa iliyopita tumeshuhudia kundi la waamini likiweka kambi nje ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini, likiamini kuwa litasafiri hadi Ulaya kueneza Injili kwa mataifa! Jambo la kustaajabisha ni kwamba kundi hilo liliaminishwa kwamba linaweza kwenda Ulaya na kwingineko duniani kwa miujiza, yaani bila kuwa na hati za kusafiria wala tiketi za ndege!

 

Lakini hatimaye tumeona polisi wakitumika kuwaondoa waamini hao. Bado wapo wanaoamini kuwa safari yao itawezekana tu.

Huko ni kuchanganyikiwa. Ufukara uliopindukia, kukosa kazi, kukosa matumaini ya kuiona kesho, ndoto za kuwa na maisha bora na kukata tama, kunaweza kuwa moja ya vyanzo vya hali hii tunayoiona hapa.

 

Hawa wanaojiita watumishi wa Mungu ni kama binadamu katika kijiji wanaofurahia mawindo ya nyumbu waliokimbia hifadhini kwa sababu ya ukame.

Nyumbu wanapoingia kijijini kwa matarajio ya kupata maji na malisho hudakwa na wanakijiji wenye shauku ya kula nyama.

 

Vivyo hivyo, hawa watumishi uchwara ni kama wanakijiji wanaosubiri nyumbu (watu wenye matatizo) ili kupitia matatizo waliyonayo waweze kujinufaisha.

Ndiyo maana hakuna mahali popote katika kanisa ambako mtumishi ameweza kukataa sadaka hata kama inatoka kwa maskini wa kupindukia!


Pengine sasa ni wakati mzuri kwa wanasaikolojia kuwasaidia Watanzania kutambua kuwa maisha bora hayawezi kuletwa kwa maombi kutoka kwa matapeli.


Maisha bora ni matokeo ya kujibidiisha, kutokata tamaa na kuepuka njia za mkato. Taifa ambalo watu wake wamekata tamaa litakuwa Taifa lenye makanisa mengi yakiwamo ya matapeli. Tutafakari.

By Jamhuri