Moja ya mijadala mikubwa iliyotoka siku chache zilizopita hapa nchini ni hatua ya Marekani kupitia kwa Waziri wake wa Mambo ya Nje, Mike Pompeo, kumzuia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuingia nchini humo kwa tuhuma za uvunjifu wa haki za binadamu. 

Katika taarifa yake Pompeo anasema wanao ushahidi wa kutosha wa Makonda kukiuka haki za binadamu, pia kuzorota kuheshimu haki za binadamu na kukosekana kwa utawala wa sheria nchini Tanzania.

Mjadala huu kuhusu Makonda unaendeleza hali ya kiongozi huyo kijana kutokauka kwenye vyombo vya habari. Makonda ni mmoja wa watu ambao jina lake limekuwa likitajwatajwa sana kwenye vyombo vya habari.

Kwangu mimi Makonda ni mmoja wa viongozi wenye tamaa na hamu kubwa sana ya kuona maendeleo yanapatikana nchini. Hilo linathibitishwa na yale ambayo Makonda anayafanya. Kila mara amekuwa mbunifu wa mambo yanayolenga kutafuta suluhu ya matatizo yanayowakabili watu anaowaongoza. Ni Kiongozi hasa aliye na kiu ya maendeleo.

Haiba na hulka hiyo hajaianza leo, ni tangu akiwa UVCCM. Kama kijana alipambana sana kuisaidia nchi iende mbele na mpaka alipoingia serikalini ameendelea kuwa hivyo. Amekwisha kuanzisha mipango mingi ikihusisha kuwasaidia wajane, kina mama waliotelekezwa, watoto, walemavu, walimu na makundi mengi kwenye jamii.

Makonda aliibua mpaka mambo yaliyohatarisha uhai wake, lakini kwa sababu ya mapenzi na uzalendo wake mkubwa kwa nchi aliyasimamia na kuyafanya bila woga.

Licha ya yote, Makonda amekuwa akiangushwa sana na aina ya mbinu na mtazamo wa kuyafikia anayoyataka ama anachokiamini. Leo ana msuguano na Marekani, taifa kubwa na lenye nguvu ulimwenguni, huku rais akiwa amemlaumu na kumlalamikia mara kadhaa hadharani kwa baadhi ya vitu kutokwenda sawa kwenye eneo lake. Kama kijana mwenye kesho nyingi, bado anahitaji kujifunza na kujisahihisha ili awe bora zaidi.

Makonda bado ana safari ndefu sana kwenye uongozi. Mabadiliko ni kitu cha msingi sana kwa binadamu yeyote. Makonda ni kiongozi mzuri sana lakini kama ikimpendeza baada ya zuio hili la Marekani ajaribu kuondoa baadhi ya makandokando yafuatayo yanayotia doa uongozi wake.

Kwanza, ajaribu kuacha kutoa kauli tata. Makonda amekuwa akiingia sana kwenye mijadala kwa kutoa kauli na maneno ambayo yanakuwa hayana picha na haiba nzuri kwa jamii. Kuna mifano kama kauli kuhusu Wachaga aliyoitoa wakati wa msiba wa mzee Reginald Mengi. Makonda pia aliwahi kuingia kwenye mgogoro na Spika wa Bunge na Bunge lenyewe kwa kauli zake tata.

Ana kauli tata nyingi sana na zisizohesabika zilizoacha mijadala mikubwa sana hapa nchini. Kama kiongozi mwenye mvuto anatakiwa awe mwangalifu wa kile anachokisema, kwani mijadala inayotokana na kauli zake wakati mwingine inaharibu haiba yake kama kiongozi.

Pili, apunguze kugawa fedha ovyo. Makonda ameacha mijadala mizito ktokana na tabia yake hiyo. Wengi wakijiuliza anakozipata fedha hizo, hasa ukilinganisha na kipato cha mkuu wa mkoa.

Ningemshauri kama ana marafiki wengi wa ndani ama nje wanaompa misaada, basi aanzishe mfuko maalumu ambao utaendeshwa na watu wengine, yeye akiwa msimamizi tu. Hii itamsaidia kuondoa hisia mbaya dhidi ya fedha anazozigawa.

Tatu, apunguze kutekeleza mipango mingi kwa wakati mmoja. Waswahili tuna msemo kuwa, mshika mawili moja humponyoka, na msemo mwingine; mtaka nyingi nasaba hupata mingi misiba.

Makonda anapaswa kuwa na mpango mahususi wa utekelezaji wa yale anayopenda kuona yanatokea katika jamii. Asiwe na tamaa ya kutaka kutatua matatizo yote katika jamii inayomzunguka mara moja. Kwa kufanya hivyo hatafanikiwa.

Amekwisha kuanzisha mambo mengi sana Dar es Salaam tangu awe mkuu wa mkoa. Vizuri sana. Lakini ili afanikiwe ni lazima awe na mpango wa utekelezaji.

Hili linamuathiri sana kwenye ufanisi wa hayo yote na ndiyo maana hata rais amekwisha kumlalamikia hadharani mara kadhaa kwa miradi mingi ya msingi na kimkakati mkoani mwake kukwama. Unakumbuka jinsi rais alivyong’aka kuhusu kuchelewa kwa utekelezaji wa mradi wa Coco Beach na machinjio ya Vingunguti?

Nne, nimuombe sana kiongozi wangu Makonda aache kujikweza. Kujimwambafai hakufai. Hili liliwahi kusemwa hata na mlezi wake, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ali, kwa vijana kukosa maadili. Kujimwambafai kunaonekana kupitia kauli na matendo pia.

Nilimsikia hadharani Makonda akitamka kwa madaha kwamba hata nani aloge yeye ataendelea kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Hizi si kauli nzuri kutoka ndani ya kinywa cha kiongozi, hasa ukizingatia kuwa nafasi aliyonayo ni uteuzi unaofanywa na mtu mwingine.

Bahati nzuri Makonda ni mpenzi na kondoo mzuri sana wa bwana. Amshirikishe Mungu kwa kila jambo analotaka kulifanya kupitia uongozi wake na maisha yake. Naamini atafanikiwa zaidi ya hapo. Rais ameonyesha imani na uvumilivu mkubwa sana kwake, anahitaji kweli kumlipa kwa kumsaidia kazi.

Mwisho kabisa, nimuombe Makonda kulimaliza suala lake na Marekani kidiplomasia na kiakili zaidi. Mambo ya kujimwambafai na kutuna yasiwepo hapa. Marekani ni taifa kubwa sana, kwa ‘level’ yake na ‘level’ ya taifa letu zima hatuna kiburi cha kutunishiana misuli na Marekani.

Bwanku ni mchambuzi wa masuala ya kijamii anayesoma Chuo Kikuu Dodoma.

0657475347

By Jamhuri