Maambukizi ya ugonjwa wa malaria katika Mkoa wa Mwanza yanazidi kuiweka jamii ya mkoa huo hatarini.

Kwa sasa Mkoa wa Mwanza una kiwango cha asilimia nane ya maambukizi ya ugonjwa huo ikiwa ni juu ya kile cha taifa ambacho ni asilimia saba.

Ugonjwa huo unaosababisha vifo vya mamilioni ya watu ulimwenguni ni dhoruba inayoiandama dunia licha ya kuwapo kampeni ya muda mrefu kuutokomeza.

Uchunguzi uliothibitishwa na mamlaka za serikali unasema kuwa Wilaya ya Ukerewe ndiyo inayoongoza kwa kuwa na asilimia 51 ya maambukizi ya malaria mkoani Mwanza.

Wilaya ya Misungwi ni asilimia 38 huku Halmashauri ya Buchosa – Wilaya ya Sengerema ikiwa na asilimia 34 ya maambukizi ya ugonjwa huo wa malaria.

Kulingana na uchunguzi, uwezo mdogo wa kiuchumi baina ya wananchi ni sababu mojawapo inayochangia kushamiri maambukizi haya.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza imekiri eneo lake la utawala kuwa na asilimia nane ya maambukizi ya malaria, juu zaidi ya kiwango cha taifa.

Tayari imeanzisha kampeni ya kuhamasisha mpango wa vyandarua shuleni, ngazi ya mkoa ili kuinusuru jamii katika  athari za usalama wa afya zao.

Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Boniphace Magembe, amesema kulingana na kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo wilayani Ukerewe kuna umuhimu kwa serikali kupeleka ndege maalumu za kunyunyizia dawa za kuua mbu.

“Elimu ya namna ya kujikinga na malaria isiishie kwetu viongozi tu. Mashirika yanayohusika kutoa elimu yafike kwa wananchi wenyewe. Ukerewe ina visima 38 vya maji vinavyokaliwa na wananchi. Nadhani iwepo njia mbadala ya kuua hawa mbu,” amesema mkuu huyo wa wilaya.

“Tuletewe helikopta inyunyizie na kuua mbu maeneo yote na masalia yake,” amesisitiza DC Magembe.

Shirika la PSI na Amref Health Africa – Tanzania yamejielekeza kwenye mapambano hayo ili kuinusuru jamii dhidi ya athari za malaria.

DC Magembe amesema Wilaya ya Ukerewe inayozungukwa na maji kwa asilimia 90 inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa boti za kusafirisha raia majini (Ambulance Boat).

Hivi karibuni Rais John Magufuli alitoa Sh milioni 200 kwa ajili ya utengenezaji wa boti moja wilayani humo.

“Tuna bajeti ya Sh bilioni 42. Tuna boti moja tu na hii ndiyo inaelekea kukamilika matengenezo yake. Ukerewe tunahitaji boti si chini ya tano. Tukipewa hizi boti tutawafikia kwa urahisi wananchi kutoa elimu, katika kilometa 6,800 zinazounda wilaya yangu,” amesema Magembe ambaye pia kitaaluma ni mwalimu.

Malaria ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea vinavyoenezwa na mbu jike aina ya ‘anofelesi’ aliyeathiriwa. Wajawazito na watoto wamo katika hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu.

Dalili za malaria huanza kuonekana siku 10 hadi 15 baada ya kung’atwa na mbu mwenye maambukizi. Dalili za mwanzo ni homa, kichwa kuuma na mwili kuhisi baridi.

Kwa watoto wenye ugonjwa huo hupata dalili mojawapo ya hizi. Upungufu wa damu, kushindwa kupumua vizuri au malaria kupanda kichwani.

Inashauriwa kila mtu kupima kabla ya kuanza kutumia dawa, kwani dalili hizo zinaweza kuonekana kwenye magonjwa mengine pia.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amewahi kukaririwa akisema malaria inachangia asilimia 30 ya homa zote Tanzania.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dk. Philis Nyimbi, amesema wastani wa kila dakika moja mtu hufariki dunia kwa malaria.

“Tanzania inachangia asilimia 70 ya vifo vya watu vitokanavyo na malaria ulimwenguni. Naelekeza vyandarua visifugiwe kuku. Visitumike kuvua samaki,” Dk. Nyimbi ameeleza.

Mpango wa serikali unaelekeza kuwa ifikapo mwaka 2020/2030 ugonjwa wa malaria utakuwa umetokomezwa.

Ripoti za serikali zinawataja mama na watoto kuwamo hatarini zaidi nchini na Bara la Afrika kwa ujumla.

Wakuu wa wilaya za Kwimba, Ukerewe, Misungwi, Magu, Sengerema, Ilemela na Nyamagana  wiki iliyopita walikutana jijini Mwanza kujadili mpango wa vyandarua shuleni ngazi ya mkoa.

Kikao hicho kiliitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, chini ya washirika wake PSI na Shirika la Afya la Amref Africa – Tanzania.

Katika kukabiliana na ugonjwa huo wa malaria, zaidi ya vyandarua 1,260,000 vimepangwa kugawiwa na serikali kwa wanafunzi shuleni.

George Kabulika, mratibu wa mpango wa vyandarua shuleni amethibitisha kwa kusema vyandarua hivi vitaanza kugawiwa mwezi huu.

Kwa mujibu wa Kabulika, wiki moja au mbili zitatumika kukamilisha Mchakato huo wa ugawaji wa vyandarua kwa wanafunzi shuleni.

Mikoa ya Kigoma, Geita, Kagera na Mwanza inalengwa katika mradi huo wa vyandarua zaidi ya 1,260,000 unaosimamiwa na serikali.

Ofisa Kitengo cha Udhibiti wa Malaria katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mponeja Peter, amesema dhamira ya serikali ni kuuondoa ugonjwa wa malaria.

“Mkoa wa Mara una asilimia 11, Geita asilimia 17 na Tabora asilimia 12. Malaria haikubaliki,” amesema na kusisitiza kuwa kila kaya ijilinde na mbu waenezao malaria kwa kuwa na vyandarua, pamoja na kuharibu madimbwi ya maji yanayoasisi mazalia ya wadudu hao.

Wakati serikali ikijiimarisha kimkakati kukabiliana zaidi na ugonjwa huo, Shirika la Amref limetiliana saini makubaliano ya utekelezaji wa mradi wa usafi wa mazingira Nyamagana na Ilemela.

Mradi huo unalenga kuigeuza takataka kuwa fursa kiuchumi, ukilenga kuboresha mazingira kwa watu wenye vipato vya chini katika Manispaa ya Ilemela na Nyamagana.

Mikakati hiyo inajumuisha ile ya Malengo Endelevu ya Millenia (SDGs 2030) ambapo katika mradi huo unaowalenga mama na vijana, utainua vipato vya raia.

Meneja Miradi ya Programu ya WASH wa Shirika la Amref Tanzania, Mturi James, katika hili amesisitiza udhibiti wa kimazingira.

“Jamii itapata elimu ya kutumia takataka kutengeneza mkaa, kinyesi kutengeneza mbolea na gesi,” James amekaririwa.

Ofisa huyo wa Amref ameshauri uongozi wa halmashauri za Nyamagana na Ilemela mkoani Mwanza kusimamia vema maridhiano hayo.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema malaria bado inaua mtoto mmoja aliye chini ya umri wa miaka mitano kila baada ya dakika mbili.

Mwaka 2015 WHO ilibaini ‘kesi’ za ugonjwa huo zipatazo milioni 214 na vifo 438,000, vifo 306,000 vilikuwa vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Pia, inakadiria kuwa asilimia 43 ya watu walio katika hatari ya kupata ugonjwa wa malaria hawana vyandarua na dawa za kuua mbu katika makazi yao. Hadi kufikia mwaka 2015, nchi 91 duniani zilikuwa na maambukizi ya malaria.

Hata hivyo, kati ya mwaka 2010 na 2015, maambukizi ya malaria yalipungua kwa asilimia 21 ulimwenguni. Bara la Afrika lilikuwa linabeba asilimia 90 ya kesi zote za ugonjwa huo.

WHO imewahi kukaririwa ikisema asilimia 92 ya vifo vyote vinatokana na maambukizi ya ugonjwa huo wa malaria.

Akiwa Mjini Geneva nchini Uswisi, Mkurugenzi wa Mpango wa Kimataifa wa Malaria, Pedro Alonso, aliiambia dunia kuwa: “Mwaka 2016 ulipata visa milioni 216 vya malaria, huku vifo 445,000 viliripotiwa kutokana na ugonjwa huo hatari.” Hiyo, kati ya mwaka 2015 na 2016, viliongezeka vifo vya watu 7,000.

Wito unasisitizwa kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) kuchukua hatua za haraka, kurejesha vita dhidi ya malaria katika mstari unaotakiwa.

Kuimarishwa kwa vita dhidi ya ugonjwa huo pia nchini, kutaharakisha kufikiwa lengo namba tatu la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) la kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.

680 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!