Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Kagera, Jamal Malinzi, amewataka Watanzania kuiunga mkono  Taifa Stars iweze kushinda katika mchezo kuwania tiketi ya  kufuzu Kombe la Dunia unaotarajiwa kufanyika Machi 24, mwaka huu.

Timu hiyo inayofundishwa na kocha Kim Poulsen, inazidi kupanda chati kisoka kadri siku zinavyosonga mbele hali inayowapa Watanzania matumaini mazuri.


Akizungumza na JAMHURI juzi, Malinzi amesema Watanzania wanatakiwa kuacha mambo na kuelekeza akili na  nguvu zao katika kusaidia timu hiyo iweze kushinda mechi hiyo.


“Mimi kwa sasa sitaki kuzungumzia uchaguzi wala nini bali nawashauri kitu kimoja Watanzania, tuache mambo yote mfano uchaguzi na mawazo yetu tuelekeze katika kupata ushindi dhidi ya Morocco,” amesema.


Stars inapambana na Morocco ikiwa kichwa mbele baada kupata ushindi dhidi ya Mabingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika, Zambia kabla ya taji hilo kwenda kwa Timu ya Tifa ya Nigeria.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kampuni ya Bia ya Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Kilimanjaro inashika nafasi ya 124 kwenye chati ya ubora wa soka kimataifa wakati Zambia inashika nafasi ya 39.


Staars iliifunga Zambia Desemba 22, mwaka jana kwa bao lililofungwa na Mrisho Ngasa, na katika mechi nyingine Stars ikaichapa Cameroon 1-0  katika mechi ya  kirafiki ya Kimataifa iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.


Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na waamuzi kutoka nchini Rwanda, bao la Stars lilifungwa na Mbwana Samatta anayecheza soka katika Klabu ya TP Mazembe ya DR Congo.


Cameroon inashika nafasi ya 67 kwa ubora wa soka duniani, ushindi huo unawapa ari wachezaji wa Taifa Stars katika mechi ya Machi 24 dhidi ya Morocco katika mbio za kuwania tiketi ya Kombe la Dunia zitakazopigwa mwakani nchini Brazil.


Katika kundi lake, Stars inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi tatu ikitanguliwa na Ivory Coast yenye pointi nne huku nafasi ya tatu ikishikwa na Morocco yenye pointi mbili na Gambia inaburuza mkia kwa pointi moja.


Baada ya kucheza na Morocco kwenye Uwanja wa Taifa, mechi itakayofuata itakuwa zamu ya Taifa Stars kuwafuata wakali hao kwa mechi ya Juni 7, mwaka huu mjini Rabat.


Kisha Taifa Stars itarejea nchini kujipanga kwa mechi nyingine ya marudiano dhidi ya Ivory Coast itakayochezwa Juni 14, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.


Mechi ya mwisho kwa Stars katika kampeni hiyo, itakuwa Septemba 6,  itakapowafuata Gambia watakaokuwa nyumbani, itakuwa ikitaka kulipa kisasi cha kufungwa 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa.


1162 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!