Chama cha Soka mkoani Kagera kimewaondoa wasiwasi mashabiki wa mchezo huo mkoani humo kuhusu kasoro za Uwanja wa Kaitaba, kikisema unafanyiwa marekebisho uweze kutumika wakati wa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara zitakazoanza hivi karibuni Agost 24 mwaka huu.

Uwanja wa Kaitaba umekuwa ukitumiwa na timu ya soka ya Kagera Sugar ya mkoani humo, katika mechi zake za Ligi Kuu kama uwanja wa nyumbani kwa takriban miaka 20 sasa.

 

Hivi karibuni, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia kamati yake inayoshugulikia masuala ya Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, ilitangaza kuufungia uwanja huo kutokana na kilichotajwa kuwa haukidhi viwango vya kutumika katika mechi za ligi hiyo.

 

Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi, Wallace Karia, alisema kasoro za uwanja huo ziliwekwa bayana baada ya viongozi wa kamati hiyo akiwamo Mkurugezi wa Ufundi wa TFF, Sunday Kayuni, kwenda mjini Bukoba kukagua uwanja huo.

 

Kayuni aliwahi kuwa Kocha Mkuu wa Kagera Sugar wakati huo ikiitwa  RTC Kagera, na Uwanja wa Kaitaba ndiyo uliokuwa ukitumiwa na timu hiyo.  Kasoro zilizotajwa na TFF ni uwanja huo kutokuwa na urefu unaotakiwa na kwamba una vipimo tofauti vya ukubwa wa magoli yake.

 

Akizungumza na JAMHURI jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Kagera, Jamal Malinzi, amesema taratibu za kurekebisha uwanja huo zimekwishaanza na kuwa marekebisho yatafanyika muda wowote kuanzia sasa, ili kutoa fursa kwa uwanja huo kutumiwa na Kagera Sugar katika mechi za Ligi Kuu kama ilivyokuwa imezoeleka.

 

“Uwanja utafanyiwa marekebisho na mipango imeanza tayari tunasubiri kumalizika kwa fainali za Kombe la Kagasheki tarehe 17, mwezi huu, na baada ya hapo tutarekebisha, ni kasoro chache tu ambazo hazitachukua muda mrefu,” alisema Malinzi.

 

Katika hatua nyingine, Malinzi alisema viwanja vingi vya soka hapa nchini vimekuwa katika mazingira mabovu kutokana na gharama za utunzaji wa viwanja hivyo kuwa kubwa.

 

“Matatizo ya viwanja yapo na si kwa Kaitaba peke yake, viwanja vingi viko katika hali isiyoridhisha na hasa katika eneo la dimba. Unajua kutunza uwanja ni gharama kubwa, ndiyo maana hali inakuwa hivi, lakini pia kuna haja ya wamiliki wa viwanja hivyo kuhakikisha vinakuwa katika hali ya kuridhisha ili kuondoa matatizo ya hapa na pale,” alisema.

 

Nyasi za viwanja mbalimbali vya timu 14 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania inatarajiwa kusagika, wakati timu hizo zitakapowasha moto  kuanza Agosti 24. Kagera Sugar watasafiri hadi Mbeya kumenyana na Mbeya City iliyopanda Ligi Kuu msimu huu.

1113 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!