Ndugu Rais  na wana wote wa nchi hii mama yetu ni mmoja tu, naye ni mama Tanzania. Nchi yangu kwanza, umoja na mshikamano katika mama huyu ndiyo mwamba wetu. Maandiko yanasema mwenye busara na hekima akitaka kujenga nyumba, hujenga nyumba yake juu ya mwamba ili hata mvua na upepo zikivuma, nyumba haitetereki.
Bali amekosa busara na hekima mtu yule ambaye atajenga nyumba yake juu ya mchanga, kwa maana utakapopiga upepo wa kusi na kisha ule wa kaskazi ukaipiga nyumba ile katika pande zake zote nne, nyumba yake haitasimama sababu ameijenga juu ya mchanga. Ndugu Rais nchi yetu Tanzania ndiyo mama yetu wote.

Hakuna aliyechagua mwenyewe kuzaliwa katika nchi hii. Wote tupo hapa kwa utashi tu wa yeye aliye juu, naye ndiye alituumbia katika nchi hii kwa usawa na utimilifu. Hakuna aliye bora kuliko wengine na kwasababu hiyo, baba mwema, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alitulea katika sala kuwa, ‘Binadamu wote ni sawa!’
Wanaonichoma mkuki moyoni ni wale ambao bado wanaimba kama kasuku kuwa nchi yetu ni kisiwa cha Amani. Tanzania ya kisiwa cha amani ilikwisha kwenda.
Imebaki tu katika kumbukumbu ziletazo majonzi. Upo utulivu ambao nao unaning’inia katika uzi mwembamba, baadhi ya waheshimiwa wameapa hawatikiswi huku wakitikisika hovyo kama utete dhaifu.
Baba, kama kukubali ushauri ni kuyumbishwa ikikupendeza, na iwe hivyo, lakini kama kuna ukweli ambao umejidhihirisha kwangu katika umri huu nilionao, ni ule usemao ‘hasira, hasara’. Hasira ni ulevi! Ni kama uchochezi kutaka kuthibitisha kwa kupima mkojo ni kutaka kuthibitisha upunguani alionao mpimaji.

Ndugu Rais tunaelekea 2020, mwaka wa uchaguzi mkuu. Kwa mazingira ambayo tumejitengenezea wenyewe, yale ya bahati mbaya (kama yapo) ambayo yangetokea wakati wa uchaguzi mkuu huo, yataanza mwaka 2019 kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.
Mwaka huo, wote waliofungiwa, zuiliwa, katazwa au nyimwa haki yao yakufanya demokrasia, kamba zilizotumika kuwafungia zitajifungua zenyewe, siyo kwa matakwa ya waliozuia bali ni fursa itakayokuwa imejitokeza kulingana na katiba ya nchi.

Wale wanaodhani walikuwa wamenyimwa sauti sasa watataka waseme tena waseme zaidi. Ya kusema watakuwa nayo mengi kwasababu labda bila kujitambua kuzuiliwa kwao tena kwa muda mrefu kuliwapa fursa ya kuyakusanya mengi.
Wakuwasikiliza watakuwa wengi zaidi pia kwasababu nao watakuwa ‘wamewamiss’ kwa muda mrefu. Waliokuwa na fursa ya kusema siku zote wasijeshangaa kukosa wakuwasikiliza kwa maana watakuwa wamekwisha kuyasikia yao yote.
Na wakuchokwa watakuwa tayari wamekwisha chokwa! Watu hupenda nyimbo mpya bwana, ndugu Rais baadhi ya wenzetu wameanza kufilisika.
Wanayashikilia yale ambayo Baba wa Taifa aliyaita ya kijingajinga, kama vile ukabila, ukanda, udini, uchama na vitu kama hivyo. Ieleweke kuwa mama Tanzania ndiye anayetuunganisha sisi wote, nchi haijengwi na mtu mmoja wala na kikundi fulani.
Hujengwa kwa umoja na mshikamano wa wananchi katika ujumla wao. Bila kuwa wamoja haya unayoyaifanyia nchi hii hata kama yangekuwa ni ya kushangaza sawa na kuing’oa milima, baada ya wewe kupita nayo yatapita kama moshi upitavyo baada ya moto kuzimwa.
Kuna watu umewakalia kooni wanaona siku haziendi, wasiokupongeza au kukusifia wala usiwalaumu kwasababu hilo ni jambo la hiari, lakini wao kukiri kuwa ufanyayo ni mema na makubwa ni lazima kwasababu kwa kufanya hivyo tu ndiyo watakuwa wanajionyesha kuwa na wao ni timamu!
Ndugu Rais, kuna wenzetu ambao hawaishi hapa kwetu akiwamo dada Tausi Likokola, mwanamitindo anayefanyia shughuli zake Marekani.
Simfahamu lakini tumeambiwa ni Mtanzania ambaye amewahi kushiriki maonyesho makubwa ya mavazi duniani kama vile yale ya Gucci, Escada, Tomy Hilfiger na Christian Dior? Amesema, “Nilikuwa Tanzania wakati aliyekuwa waziri wa Habari, utamaduni na michezo Nape Nnauye
aliposhurutishwa kurudi ndani ya gari wakati akijaribu kuzungumza na waandishi wa habari. Tukio hilo lilikuwa baya zaidi niliposhuhudia akionyeshwa bastola. Ni nini hiki kinachotokea kwa Tanzania yangu? Amani imeenda wapi?”

Akaendelea, “Nadhani uelekeo wetu si mzuri. Yako mengi ninayoweza kueleza ambayo yamenisukuma kutoa msimamo wangu huu. Tanzania inahitaji shule bora, huduma bora za afya na miundombinu. Dunia inaona
kinachoendelea, tusiende huko!”
Alinikumbusha nguvu ya uwaziri wa Mambo ya Ndani aliyokuwa nayo Augustino Lyatonga Mrema. Aliposema siku saba, zilikuwa siku saba. Aliposema watuhumiwa wamfuate kwa wazazi wake kule Kiraracha, walimfuata. Tulilala huku madirisha yetu yakiwa wazi maana amani ilitapakaa! Huyu wa sasa aliagiza mtu yule akamatwe.

Sijui huu ni mwezi wa ngapi toka atoe agizo hilo! Na sijui kama yeye mwenyewe anakumbuka kuwa alitoa agizo la kukamatwa mtu yule? Agizo la mheshimiwa likipuuzwa wananchi watamheshimuje? Wananchi wanapotupuuza nakutuona ni wa burebure, tusikimbilie kuwalaumu! Tujiulize, ni kwa kiasi gani sisi tumeziheshimu kauli zetu?

Tausi alisema, “Natambua kazi inayofanywa na serikali ya kusafisha rushwa na kuwapa Watanzania maisha bora, lakini maisha ya Watanzania hayawezi kuwa bora kama watu hawatapewa uhuru wa kujieleza!”
Anasema alisikitishwa sana na kitendo cha Mwanasheria Fatma Karume kuzuiwa kuzungumza na waandishi wa habari.
Akaona kwa mshangao magereza kutumika kuwatisha watu badala ya kuwahifadhi wafungwa! Ndugu Rais mabaya tunayoyaona yakitokea kwa wenzetu kila uchaguzi mkuu unapojiri tuyatumie kujifunza na kukiri kuwa sisi hatuko kisiwani!
Uchaguzi Mkuu wa Kenya wa Mwaka 2007 ulifuatiwa na vurugu za kumwaga damu zilizowaacha mamia wakiwa wamepoteza maisha yao huku maelfu wakiachwa bila makazi.
Uchaguzi mkuu wa 2017 unafanyika leo, huku Christopher au kama alivyozoeleka kuitwa Chris Msando wa IEBC, (Independent Electoral and Boundaries Commission) tukiwa hatunaye hapa duniani.
Ripoti ya kitabibu inathibitisha kuwa Chris Msando alikufa kwa kunyongwa! Uchaguzi umemtoa roho! Hata kwa wale tunaowadhania kuwa wameendelea, udhalimu huu ungalipo! Tumeona uchaguzi mkuu wa Marekani ukimwacha aliyekuwa Mkurugenzi wa FBI, James Comey akifutwa kazi na Rais wa nchi hiyo Donald Trumph. Ndugu Rais sisi ni watoto wa mama mmoja tusifike huko!

PASCHALLY MAYEGA
SIMU:     0713334239

2689 Total Views 1 Views Today
||||| 2 I Like It! |||||
Sambaza!