Dk. Kamani: Mahakama isiwe juu ya sheria nchini

Mbunge wa Busega mkoani Simiyu Dk. Titus Kamani (CCM), amependekeza pamoja na mambo mengine, Katiba mpya idhibiti uhuru wa Mahakama na kuruhusu uundaji chombo maalumu cha kuwabana wahujumu uchumi.

Akizungumza na JAMHURI Dar es Salaam juzi, Dk. Kamani amesisitiza kuwa mabadiliko ya Katiba ni fursa nzuri ya kuondoa upungufu uliopo katika Mahakama na utaratibu wa kuwashughulikia wahujumu uchumi.

Uhuru wa Mahakama

“Uhuru wa mahakama uangaliwe upya katika Katiba mpya kwa kuwekewa udhibiti ili kuondoa mwanya wa kutoa hukumu zinazominya haki za watu.


“Serikali inapokiuka taratibu inashitakiwa, Katiba ijayo iweke mfumo wa kuidhibiti Mahakama ili nayo iweze kuhojiwa na mamlaka ya juu pale inapofanya uamuzi kichume cha maadili ya Taifa.


“Wakati mwingine Mahakama zinatumia uhuru wake kufinyanga haki za watu katika hukumu kutokana na msukumo wa rushwa. Zisipokuwa na mamlaka ya kuzihoji zinaweza kuwa na udikiteta,” anasema mbunge huyo.

Wahujumu uchumi

Dk. Kamani anaona utaratibu wa sasa wa kushughulikia wahujumu uchumi una upungufu unaochangia kudumisha tatizo hilo nchini.


Anapendekeza Katiba mpya iruhusu uanzishaji wa Mahakama Maalumu ya kushughulikia wahujumu uchumi kuokoa rasilimali za Taifa.


“Kwa mfano, mtu anakamatwa akiwa na nyara za Serikali, fedha chafu [alizojipatia kwa njia haramu] lakini vyombo vya sheria vinasema lazima vifanye upelelezi na kesi hizo zinachukua muda mferu kabla ya kutolewa hukumu.


“Kufanya upelelezi juu ya mtuhumiwa wa uhujumu uchumi aliyekamatwa akiwa na kidhibiti ni kutoa mwanya wa rushwa, na mara nyingi kesi za aina hiyo zimekuwa zikiishia kutupiliwa mbali na washitakiwa kuachiwa huru. Ni vigumu kumaliza tatizo hilo kwa utaratibu huo.


“Mahakama maalumu ya wahujumu uchumi itasaidia kupanua wigo wa mashitaka dhidi ya watu wa aina hiyo. Ethiopia inafanya hivyo na inafanikiwa kwa hilo.


“Mahakama hiyo ipewe nguvu ya kuhakikisha kwamba wahujumu uchumi wanaokamatwa wakiwa na vidhibiti wahukumiwe kifungo mara moja kisha upelelezi ufanyike kwa kuwasaka na kuwakamata washirika wao. Tukifanya hivyo watu hawatachezea mali za umma,” anasisitiza.


Anaeleza kuwa tatizo la uhujumu uchumi wa nchi kupitia idara, taasisi, mashirika na kampuni za umma likikomeshwa litatoa mwanya wa kukuza uchumi wa Taifa kwa kasi ya kuridhisha.


“Ethiopia mtu akikamatwa akiwa na kidhibiti cha uhujumu uchumi anahukumiwa papo hapo, hakuna suala la kwamba ngoja kwanza tufanye upelelezi kama ilivyo hapa Tanzania. Unafanya upelelezi gani zaidi wakati mtu amekutwa akiwa na kidhibiti?” anahoji Dk. Kamani.

Tume ya maadili

Dk. Kamani anapendekeza Katiba mpya pia uruhusu kuundwa kwa Tume Maalumu itakayokabidhiwa mamlaka ya kudhibiti na kusimamia maadili ya wananchi wote badala ya iliyopo sasa inayosimamia maadili ya viongozi wa umma.


“Tume iliyopo sasa inachunguza maadili ya viongozi wa umma tu wakati suala la maadili linawahusu watu wote hata wa kawaida katika jamii.


“Siku hizi kuna mmomonyoko wa maadili katika jamii, uadilifu na uwajibikaji umepungua hata kwa watu wa kawaida kwa sababu wamewekwa kando katika suala la maadili. “Kutokana na hali hiyo baadhi ya matajiri wanatumia fedha zao kuvuruga upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii zikiwamo za afya na elimu,” anasema.

Uzembe wa kutofanya kazi

“Ningependa suala hili lionekane kwenye Katiba ijayo, kwamba kuwepo na msukumo wa kuwabana watu kufanya kazi kwa sababu kuna watu wenye uwezo wa kufanya kazi lakini wanakwepa wajibu huo.


“Ninasema hivyo kwa sababu baada ya kuona hakuna mtu wa kuwabana, baadhi ya wananchi wenye uwezo wa kufanya kazi wamebweteka, wamejikita katika vitendo vya kuombaomba na kushinda wakicheza kamari kwa kutumia pool, karata na bao.


“Huu ni uzembe ambao haupaswi kupewa nafasi katika nchi yetu yenye changamoto kubwa ya kupambana na umaskini na kuinua kipato cha wananchi.


“Katiba mpya itamke wazi kwamba ni wajibu wa kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi kuwajibika kufanya kazi, vitendo vya kamari na ombaomba vidhibitiwe visiwe utamaduni katika nchi yetu,” anasema Dk. Kamani.

Benki ziwajali wazawa

Suala la benki kutoa kipaumbele kwa wazawa katika utoaji mikopo ya kibiashara linatajwa na mbunge huyo wa Busega kuwa ni miongoni mwa mikakati inayoweza kupunguza umaskini nchini.

Dk. Kamani anaeleza kutofurahishwa na dhana iliyojengeka katika benki nyingi ya kutoa kipaumbele cha kuwapatia wawekezaji wa kigeni mikopo ya kibiashara huku wakiwageuzia kisogo wazawa.


“Katiba mpya iwe na kipengele kitakachozibana taasisi za fedha zisiendelee kuwatajirisha wawekezaji wa kigeni kwa kuwapatia mikopo ya kibiashara kuliko wazawa.


“Wawekezaji wa kigeni nchini wakipata faida wanazipeleka katika mataifa yao lakini wazawa wakikopeshwa mitaji ya kuanzisha na kuendeleza biashara zao faida itabaki hapa hapa Tanzania. Suala hili ni muhimu kuzingatiwa kwenye Katiba mpya,” anaongeza.

Utajiri wa wazawa

Kasumba ya watu wenye uwezo mkubwa wa kiuchumi kuitwa mafisadi kinamkera Dk. Kamani kiasi cha kufikia hatua ya kupendekeza dhana hiyo ifafanuliwe katika Katiba mpya kuimarisha upendo na mshikamano nchini.


“Tanzania siku hizi ndiyo nchi pekee ambako mtu akitajirika anatanzamwa kama fisadi hata kama inajulikana wazi kuwa ameupata utajiri kwa njia halali. Hii ni dhana mbaya.


“Cha ajabu ni kwamba wakati ikiwa hivyo kwa mzawa, kwa mwekezaji wa kigeni ni tofauti. Yeye hutazamwa kama mtu ayepata utajiri kwa njia halali hata kama sivyo. Katiba mpya ifafanue utajiri wa watu ili kuepusha kila tajiri kuitwa fisadi.


“Kitendo cha kuwaona matajiri kama mafisadi kinawakatisha wengine tamaa ya kuongeza juhudi za kujiinua kiuchumi,” anasisita mbunge huyo.


By Jamhuri