Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) imempata bosi mpya, Diwani Athumani Msuya, ambaye wiki iliyopita aliteuliwa na kuapishwa na Rais John Magufuli kushika wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa idara hiyo.

Kabla ya uteuzi huo, Kamishna Msuya alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Kamishna Msuya amechukua nafasi ya Dk. Modestus Kipilimba ambaye atapangiwa kazi nyingine.

Kamishna Msuya katika utumishi wake kwenye Jeshi la Polisi ameshika vyeo na nyadhifa mbalimbali, ikiwemo kuwa msaidizi binafsi (Aide –de-camp) kwa kifupi ADC  ‘bodyguard’ wa IGP Omari Mahita.

Mwaka 2008, Msuya alipandishwa cheo kutoka Mrakibu wa Polisi (SP) kuwa Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) na baadaye kuteuliwa kuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya (RCO).

Aprili 2010 alipandishwa cheo kutoka Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) kuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) na kubaki na majukumu yake yaleyale ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya.

Novemba 2010,  IGP Said Mwema alimpangia majukumu mapya ya kuwa Kamanda wa Polisi (RPC) wa Mkoa wa Shinyanga kuchukua nafasi ya ACP Daudi Siasi.

Mei 2012 alihamishwa kutoka Shinyanga kurudi Mbeya kuendelea na majukumu yake kama Kamanda wa Polisi (RPC) wa Mkoa wa Mbeya.

Novemba 2013, Rais Jakaya Kikwete alimpandisha cheo kuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) kutoka Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP). Alidumu katika cheo hicho kwa wiki mbili tu, na Desemba 2013, Rais Kikwete alimpandisha tena cheo kuwa Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) na kumteua kuwa Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai.

Mwaka 2014 alibadilishiwa majukumu kutoka Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai na kuwa Kaimu Kamishna wa Kamisheni ya Intelijensia ya Jinai, hiyo ilikuwa ni baada ya mabadiliko ya muundo ndani ya Jeshi la Polisi.

Machi 2015, Rais Kikwete alimteua Kamishna Msuya kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuchukua nafasi ya Isaya Mungulu ambaye alistaafu.

Novemba 2016, Rais John Magufuli alitengua uteuzi wake katika nafasi ya DCI na kumteua kuwa Katibu Tawala (RAS) Mkoa wa Kagera.

Miaka miwili baadaye, yaani mwaka 2018, Rais Magufuli alimteua kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) huku akichukua nafasi ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo Valentino Mlowola ambaye aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba.

Kamishna Msuya amehudumu katika nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru kwa siku 371, sawa na mwaka mmoja na siku sita.

Septemba mwaka huu, Rais John Magufuli akamteua kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), kuchukua nafasi ya Dk.  Kapilimba.

Kamishna Msuya ni kachero, msomi wa sheria, anafahamika kwa kuwa na msimamo usioyumba na mnyenyekevu, hilo limethibitika katika nafasi alizoshika katika utumishi wake wa umma.

Katika kipindi cha mwaka mmoja aliohudumu akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, amesimamia mageuzi makubwa na kuisuka upya taasisi hiyo ambayo ni mhimili muhimu sana katika misingi ya utawala bora.

Punde baada ya kuingia katika ofisi hiyo yenye Makao Makuu yake Upanga, jijini Dar es Salaam, alianza kwa kufumua safu ya viongozi wa juu wa taasisi hiyo, lengo likiwa ni kuipa nguvu inayostahili ofisi hiyo nyeti.

By Jamhuri