TFDA yataja ilivyoruhusu nchini

Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) imeendelea kupiga marufuku vipodozi vyenye viambato (ingredients) vyenye sumu inayoathiri afya ya binadamu.

TFDA inayofanya kazi chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, pia imeendelea na jitihada za kuelimisha jamii kuhusu madhara ya kiafya, yasababishwayo na matumizi ya vipodozi hivyo ili wananchi watambue na kufanya uamuzi makini wakati wa kununua na kutumia vipodozi.

Taasisi hiyo ndiyo yenye dhamana ya kusimamia udhibiti wa ubora na usalama wa ufanisi wa vyakula, dawa za mitishamba, vipodozi na vifaa tiba hapa nchini.

Kifungu cha 88 (a) cha Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Sura 219, kinakataza kutengeneza, kuuza au kusambaza vipodozi vyenye viambato vyenye sumu ambayo huleta athari kwa watumiaji.

Lengo kuu la TFDA ni kulinda afya za wananchi dhidi ya madhara yanayoweza kujitokeza katika matumizi ya bidhaa inazodhibiti. Inatekeleza dhima hiyo kwa kuzuia athari zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya vyakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba.

Dira ya TFDA ni kuwa taasisi bora katika udhibiti wa vyakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba barani Afrika ifikapo mwaka 2015. Falsafa ya mamlaka hiyo ni kutoa huduma za udhibiti katika kulinda afya ya jamii na mazingira kwa kutumia wafanyakazi wenye ujuzi na ari ya kazi.

Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo, anasema Mamlaka hiyo inadhibiti ubora na usalama wa vipodozi kwa kufanya tathmini na uchunguzi wa kimaabara kabla ya kusajili vipodozi hapa Tanzania. Anaongeza kuwa mamlaka hiyo pia hufanya ukaguzi katika vituo vya mipakani na maduka ya jumla ya vipodozi kuhakikisha vilivyo salama ndivyo vinavyoruhusiwa kuuzwa katika soko la Tanzania.

Anasema mamlaka hiyo ina wataalam waliobobea katika uchunguzi wa usalama na ubora wa bidhaa inazozidhibiti. Wataalamu hao ni pamoja na wafamasia, wataalam wa chakula, wakemia, wataalam wa maikrobiolojia na mafundi sanifu maabara.

 

Viambato vilivyopigwa marufuku

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu huyo, viambato vyenye sumu vilivyopigwa marufuku kuuzwa na kutumika hapa nchini ni bithionol, hexachlorophene, mercury compounds, vinyl chloride na zirconium.

Viambato vingine vilivyopigwa marufuku ni halogenated salicylanilides, chloroquinone, steroids, chloroform, chlofluorocarbon propellants na methyelene chloride.

Vipodozi vilivyopigwa marufuku

Sillo anataja vipodozi vilivyopigwa marufuku na TFDA hadi kufikia Juni, 2013 kuwa ni krimu na losheni zenye kiambato cha hydroquinone.

Anataja baadhi ya krimu zenye kiambato cha hydroquinone ni Mekako, Claire, Rico Complexion, Princess, Mic, Extra Clear, Shirley, Kissy-Medicated Beauty, Lolane, Binti Jambo, Care Plus Fairness, Topiclear na Cleartone Skin Toning.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu huyo wa TFDA, pia krimu zenye misuguano (hormones in steroids) zimepigwa marufuku. Krimu hizo ni pamoja na Amira, Jaribu, Fair & Lovely Super, Age Renewal, Mediven, Musk-Clear, Miss Caroline, Movate, Top Lemon, Topifram na First Class.

Losheni zilizopigwa marufuku kuingizwa, kuuzwa na kutumika hapa nchini ni pamoja na Peau Claire Body, Tura, Super Max-Tone, Clear Essence Skin Beautifying Milk, G & G Dynamiclair, G & G Teint Uniforme, Dawny-Lightening, Maxi White na Bioclare Lightening.

“TFDA pia imepiga marufuku jeli zenye kiambato cha hydroquinone ambazo ni Body Clear, Top Clear na Ultra Clear,” anaongeza.

Hali kadhalika, jeli zenye ‘steroids’ zikiwamo Fashion Fair, Hot Movate, Hyprogel, Secret, Peau Claire, Prosone, TCB, Demo, Ultimate Lady, Regge Lemon, Skin Success, Skin Fade, Ultra na Soft & Beautiful zimepigwa marufuku hapa Tanzania.

Pia sabuni ya maji ya kujipaka, Peau Claire Lightening Body Oil, Body Clear Medicated Antiseptic, Blackstar, Lady Claire, M.G.C Extra Clear, Ultra Clear na Top Beauty Complexion zimepigwa marufuku baada ya kubainika zina kiambato cha sumu cha hydroquinone.

Sabuni zenye kiambato cha zebaki (mercury) na michanganyo yake nazo zimepigwa marufuku na TFDA. Baadhi ya Sabuni hizo ni Movate, Miki, Jaribu, Binti Jambo, Amira, Mekako, Rico, Tura, Acura, Elegance, Fair Lady, Maxi-Tone, Margostara, Rusty-Whitening na Emani Naturally Pearls.

Vile vile kipodozi cha kuzuia harufu (antiperspirant) chenye ‘aluminum zirconium compound’ kimepigwa marufuku na TFDA. Kitaalamu kipodozi hicho kinafahamika kama triple dry antiperspitant.

Kipodozi kingine kilichopigwa marufuku hapa Tanzania ni kile cha kupunguza unene chenye kiambato kitokanacho na mmea unaojulikana kitaalamu kama phytolacea spp.

Pia vipodozi vyenye kiambato cha ‘steroid’ vikiwamo fair & white serum exclusive whitenizer, maxi white, maxitone cleansing milk, avordem, niomre, nyala, Si Claire, cute press, white SPA Rose na white SPA UV.

Vipodozi vingine vilivyopigwa marufuku ni vile vinavyotokana na mmea aina ya ‘arctostaphylos UVA URSI (bearberry extract)’ vyenye ‘hydroquinone’ na ‘abutin’ na vyenye kiambato cha Tin Oxide kinachosababisha muwasho kikitumiwa karibu na macho.

Sillo anaongeza kuwa kipodozi chenye kiambato cha ‘malic acid’ kinachochubua seli za ngozi na kusababisha weupe, nacho kimepigwa marufuku kuingizwa, kuuzwa na kutumiwa nchini. Kipodozi hicho kinafahamika kama AHA Whitening Cream.

“Kipodozi cha nywele chenye kiambato cha ‘cannabium root extract’apocynum, pia kipodozi kinachotokana na ‘tussilago farfara’ na vipodozi vyenye viambato vya dawa za tiba kama vile bleu cap na marhaba vimepigwa marufuku,” anasema.

Matumizi mabaya ya dawa

Miongoni mwa viambato vilivyopigwa marufuku vilivyobainika kutumiwa kimakosa kama vipodozi ni aina ya steroids ambavyo kimsingi ni dawa.

 

Viambato hivyo ni pamoja na clobetasol na betamethasone vinavyopatikana kwenye dawa aina ya Movate, Betacor-N, Diproson, Gentrisone, n.k. Bidhaa hizo haziruhusiwi kutumika kama vipodozi, badala yake zinastahili kutumika kama dawa za cheti kwa wagonjwa wa ngozi kwa kufuata maelekezo ya daktari na mfamasia.

Dawa nyingine zilizopigwa marufuku zinazotumika kimakosa kama vipodozi ni za kuongeza makalio na maziwa. Dawa hizo zimepigwa marufuku baada ya kusadikiwa kwamba husababisha madhara kwa watumiaji, ikiwa ni pamoja na kumweka mtumiaji katika hatari ya kupata ugonjwa wa kansa.

Madhara ya viambato sumu

Madhara yatokanayo na matumizi ya vipodozi vyenye viambato vya sumu ni kupata mzio wa ngozi na athari kwenye ngozi inapopata mwanga wa jua. Athari hizo husababishwa na kiambato sumu kiitwacho bithional.

Kwa mujibu wa Mkutubi Mwandamizi wa TFDA, James Ndege, madhara ya kiambato sumu kijulikanacho kama hexachlorophene, ni kupenya hadi kuingia kwenye mishipa ya fahamu na kusababisha ugonjwa, hasa kichwani. Pia husababisha ugonjwa wa ngozi na kuiathiri mtu anapokuwa juani.

Kwa watoto wachanga, hexachlorophene huathiri ubongo. Vile vile husababisha ngozi kuwa laini kiasi cha kukaribisha ugonjwa wa fangasi au maambukizo ya vimelea vya maradhi.

TFDA inataja madhara ya zebaki kuwa ni pamoja na kuharibu ngozi, ubongo, figo na viungo mbalimbali vya mwili. Mama mjamzito akitumia vipodozi vyenye zebaki humwathiri mtoto tumboni, ikiwa ni pamoja na kusababisha azaliwe akiwa na mtindio wa ubongo.

Matumizi ya zebaki husababisha pia ngozi kuwa laini na mabaka meusi na meupe. Husababisha pia mzio wa ngozi na muwasho, ugonjwa wa mishipa ya fahamu na madhara ya upofu, uziwi na upotevu wa fahamu mara kwa mara.

Vinyl chloride: Hiki ni kiambato chenye sumu kinachosababisha magonjwa ya kansa ya ini, ubongo, mapafu na mfumo wa damu. Sumu yake pia humsababishia mtumiaji kuumwa kichwa, kuhisi kizunguzungu na kupoteza fahamu. Kiambato sumu aina ya zirconium husababisha kansa ya ngozi na mapafu.

Athari kubwa za kiambato sumu aina ya halogenated salicylanilide katika afya ya binadamu ni ugonjwa wa ngozi na mzio wa ngozi mara inapopata mwanga wa jua.

Kwa upande mwingine, kiambato cha hydroquinone husababisha muwasho na mzio wa ngozi, kansa, kuchubuka kwa ngozi na kusababisha mabaka meusi na meupe.

Kadhalika, kiambato aina ya steroids cha kundi la homoni, husababisha madhara mbalimbali yakiwamo ugonjwa wa ngozi, chunusi, kulainisha ngozi kupindukia, kuchelewesha kidonda kupona na magonjwa ya moyo.

Chloroform ni kiambato chenye sumu ambacho husababisha kansa ya utumbo mpana na kibofu cha mkojo. Husababisha pia ugonjwa wa akili na mishipa ya fahamu, ngozi kuungua, maumivu makali, ngozi kuwa nyekundu na kuota vipele.

Madhara kwenye mishipa ya fahamu yanayosababisha mtu kutopumua vizuri husababishwa na kiambato chenye sumu kijulikanacho kama chlorofluorocarbon (halogenated chlorofuoroalkanes).

Kiambato sumu aina ya ethylene chloride husababisha kansa, madhara kwenye mishipa ya kati ya fahamu, ini na mishipa ya moyo.

Vipodozi vilivyoruhusiwa

TFDA imehalalisha vipodozi zaidi ya 900 katika makundi ya krimu na losheni kuigizwa, kuuzwa na kutumia hapa Tanzania.

Baadhi ya vipodozi vinavyotambuliwa na Mamlaka hiyo ni 4-u, beauty natural honey, boss, burgess & finch, cocoa butter, daily repair, eye therapy, furaha, goldy beauty, high potency multi-vitamin, Johnson, joy skin, lady Diana, limara, natrodale arnica, nomarks, nivea, papaya na pecos.

Vipodozi vingine vilivyoruhusiwa ni PH 5.5 aqueous, aloe vela, avon herbal, blue lady, clean comb, BIO Valley Sun, vital, venus, vestline, holotropic, jambo, jergens, jumbo, lakme peach milk, neucare vitamin E, pamamas, pond, royal, solea, St. Ives Aloe Vera, sweet heart, tea tree, vatiny, zawadi, mandara, GNLD, henna wax na kempinski.

Vingine ni balsam, coconut, black rose, makini, taft range, peacock, herbal shampoo, morgans pomade, motions, hair works, Revlon, lotta, porosity, ultra girl, poly tint no. 38, young color excel, duke textrurizing, pressol, SAS, afro, madame, podoa, TCB natural – hair food, VO5 Advance na Yolanda.

Pamoja na madhara ya kiafya yaliyotajwa hapo juu, pia kuna madhara ya kiuchumi yanayotokana na matumizi ya vipodozi visivyo bora na salama. Ofisa Uhusiano wa TFDA, Gaudensia Simwanza, anataja madhara ya kiuchumi yanayosababishwa na matumizi ya vipodozi hivyo kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa gharama za matibabu kwa waathirika na lishe kupungua kwa watoto na familia kutokana na fedha nyingi kutumika kununua vipodozi au mikorogo.

Kutokana na madhara ya kiafya na kiuchumi yanayosababishwa na matumizi ya mikorogo na vipodozi vyenye viambato sumu, TFDA imeweka mifumo ya udhibiti wa vipodozi kuhakikisha vinavyotumiwa na wananchi ni bora na salama, havina madhara kwa afya za watumiaji.

Simwanza anafafanua kwamba mifumo ya udhibiti inajumuisha usajili wa vipodozi, udhibiti katika uingizaji, ukaguzi, ufuatiliaji na utoaji wa vibali vya biashara ya bidhaa hizo.

Takwimu za TFDA zinaonesha kuwa aina 250 za vipodozi zimebainika kuwa na viambato sumu na kwamba kuna dalili za idadi hiyo kuendelea kuongezeka kila uchunguzi wa kimaabara utakapokuwa unafanywa.

Ni kwa sababu hiyo, TFDA inatoa wito wa jumla kwa wananchi kwa jumla kujiepusha na matumizi ya vipodozi vilivyopigwa marufuku kuepuka madhara ya kiafya yanayosababishwa na bidhaa hizo.

Kwa upande mwingine, ofisa uhusiano huyo anawakumbusha wafanyabiashara ya vipodozi kuhakikisha wanapeleka taarifa za bidhaa wanazouza katika ofisi ya TFDA kwa ufuatiliaji zaidi. Anasisitiza kuwa vita dhidi ya matumizi ya vipodozi visivyo salama si jukumu la TFDA pekee bali ni la kila Mtanzania.

“Tunaomba wananchi kutoa ushirikiano katika kutoa elimu kuhusu madhara yatokanayo na matumizi ya vipodozi visivyo salama ili kulinda afya ya jamii kwa ujumla. Kwa pamoja tupambane na bidhaa duni na bandia ili kulinda afya zetu,” anasisitiza.


7272 Total Views 1 Views Today
||||| 4 I Like It! |||||
Sambaza!