Maisha yamebadilika sana kutokana na ugonjwa huu wa corona. Si maisha tu, bali pia tamaduni, mazoea na tabia za jamii. Hakika hili litapita, lakini litaacha nyuma yake kumbukumbu kadhaa mbaya na nzuri.

Kwa miaka mingi Wakristo duniani wamekuwa wakitumia maji ya baraka kwa namna mbalimbali kama kisakramenti kimojawapo, kwa Wakatoliki, katika kujitakatifuza wakati wakiingia au kutoka kanisani.

Sasa Wakatoliki nchini wamelazimika kubadili na kuacha (kwa muda) mazoea hayo kutokana na corona wakitekeleza agizo au maelekezo kutoka TEC.

Lakini hali ni tofauti kwa waumini wa Parokia ya Karoli Lwanga, Yombo Dovya jijini Dar es Salaam kwani huduma hii (kuchovya maji ya baraka mlangoni) imeendelea hata nyakati hizi za corona.

Ni ukaidi au kutozingatia maelekezo ya TEC na serikali? Kwa mujibu wa Paroko wa kanisa hilo, Padri Camillius, si ukaidi ila ni ubunifu uliopo parokiani kwake.

“Usafi, hasa wa mikono, ni muhimu katika mapambano na corona. Tumezingatia hilo na kwa miaka mitatu sasa waumini wetu hawachovyi maji ya baraka kwenye bakuli au kisima mlangoni,” anasema Padri Camillius.

Hili limewezekanaje? Jibu ni rahisi tu. Ubunifu. Milango yote minne katika kanisa hilo vipo vifaa ‘vya kisasa’ kwa ajili ya maji ya baraka ambavyo muumini hapaswi kuchovya mkono au kidole ili kujitakatifuza.

“Vimetengenezwa kitaalamu vikizingatia ‘hygiene’ (usafi) ya hali ya juu. Maji yanatiririka na mtu hawezi kuacha ‘gems’ (vijidudu vya maradhi) ndani na kusababisha uwezekano wa kumuambukiza mwingine! Tunachosisitiza kwa waumini ni kutokugusa mdomo wa kifaa hiki,” anasema.

Muonekano wa kifaa hicho ni wa kuvutia na kwa hakika kinaongeza nakshi kwenye milango ya kanisa. 

Kwa sasa Kanisa la Mtakatifu Karoli Lwanga si pekee jijini hapa linalotumia kifaa hicho, kwani tayari Kanisa la Mt. Peter, Oysterbay limeanza matumizi hayo wiki kadhaa zilizopita, likiwa ni la tatu baada ya Kanisa la Yohane wa Mungu la Yombo Vituka.  

“Nitafurahi sana iwapo watu watakuja kujifunza kwetu wabadili mazoea (ya kuchovya maji ya baraka kwenye bakuli). Kiafya si sahihi hata kama hakuna corona,” anasema Padri Camillius.

Kwa hakika mazoea ya Wakatoliki kuchovya maji kwa sasa yanapaswa kusahaulika na kufungua ukurasa mpya kwa kuanza kutumia kifaa hicho kinachotoa matone ya maji yanayotosha muumini kutumia kujitakatifuza.

Lakini liturjia inasemaje kuhusu hili? “Hakuna tatizo. Liturjia haipingani na matumizi ya kifaa hiki. Hata kipindi hiki utakuta ‘sanitizer’ za umeme milangoni. Liturjia haisemi kitu,” anasema Padri Camillius.

Maji ya baraka yalianza kutumiwa rasmi na kanisa miaka mingi na kuanzia karne ya tisa Kanisa Katoliki lilianza kunyunyizia waumini maji hayo kabla ya kuingia kanisani, kisha likaweka mabeseni (visima) kwa ajili ya waumini kuchovya maji na kujitakatifuza kabla ya ibada ya misa.

Mwishoni mwa karne ya 19 wataalamu wa afya walihoji usalama wa matumizi ya maji hayo kwa waumini wengi (wote) yakiwa ndani ya mabakuli milangoni. 

Mwaka 1995, wataalamu hao waliyapima maji ya baraka yaliyokuwa kwenye mlango wa kanisa la Sassari, Italia, na kukuta vimelea kadhaa vya maradhi baada ya muumini mmoja aliyekuwa na vidonda vya moto kupata maambukizi kutoka kwenye maji hayo.

Ubunifu huu ulioanzia Yombo Dovya unatoa nafasi kwa Kanisa Katoliki duniani kuondokana na mazoea na kuja kujifunza Tanzania, ikiwa ni moja ya matukio chanya ya mlipuko wa corona. 

JAMHURI kwa kushirikiana na Padri Camillius linamtafuta mbunifu wa kifaa hiki aweze kueleza kwa kina nini kilimsukuma kufikia uamuzi huo.

Inafahamika kuwa mbunifu huyo ni mzee wa kanisa hilo la Yombo Dovya.

1562 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!