Mashabiki wa soka sasa wamegeukia michuano ya Kombe la Chalenji, itakayoanza kutimua vumbi kwenye Uwanja wa Namboole, Kampala nchini Uganda, Jumamosi wiki hii.

Tanzania inapeleka timu za Kilimanjaro Stars ya Tanzania Bara na Zanzibar Heroes ya Zanzibar, fursa ambayo ikitumiwa vizuri inaweza kulileta kombe hilo nyumbani.


Tayari Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen, amesema Kundi B linaloijumuisha timu yake ni gumu. Timu nyingine za kundi hilo ni Sudan, Burundi na Somalia.


Amesema Sudan ndiyo inaongoza kwa ubora wa viwango vinavyotolewa na Shirikisho la Kandanda Duniani (FIFA) katika kundi hilo, ikifuatiwa na Burundi, Tanzania na Somalia.

“Ninachokifanya (sasa) ni kuiandaa kikamilifu timu yangu kwenda Uganda kukabiliana na wenzetu na kupata ushindi,” amesema kocha huyo raia wa Uholanzi.


Kim Poulsen alichukua nafasi hiyo kumrithi Jan Poulsen aliyetimuliwa baada ya timu hiyo kuendelea kudidimia kisoka kwa kasi zaidi.


Kabla ya Jan, Kilimanjaro Stars na timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) zilikuwa zikinolewa na kocha Mbrazili, Marcio Maximo, kuanzia mwaka 2006 hadi 2010 alipomaliza mkataba wake na kurudi kwao.


Katika kipindi chake hicho cha miaka minne, soka la Stars lilibadilika na kuanza kushinda mechi kwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya miaka 12, ikaanza kuwa tishio kwa kutoka sare hata na vigogo vya kandanda Afrika zikiwemo Ivory Coast na Cameron, hatua ambayo ilirejesha uzalendo wa nchi kwa mashabiki.


Pia Maximo aliiwezesha Tanzania kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN), zilizofanyika nchini Gabon mwaka 2009. Ilipata nafasi hiyo baada ya kuzikosa kwa ncha ya kidole Fainali za Kombe la Afrika (AFCON) ya mwaka 2008 zilizoandaliwa kwa pamoja na Nigeria na Ghana.


Michuano ya Chalenji mwaka huu, itamalizika Desemba 8, ambapo bingwa mpya atapatikana baada ya mtifuano mkubwa wa siku 15 mfululizo ukishirikisha timu 12.


Mbali ya timu za Kundi B ambazo ni Tanzania Bara, Kundi A linaundwa na mataifa ya Uganda, Kenya, Ethiopia na Sudan Kusini inayoshiriki kwa mara ya kwanza tangu ijitenge kutoka Sudan na kuwa taifa huru, Julai 9, mwaka jana.


Kundi C linaundwa na timu za Rwanda, Zanzibar, Eritrea na Malawi iliyoomba kushiriki michuano hiyo. Kulingana na ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Kandanda Afrika na Kati (CECAFA), Ethiopia na Sudan Kusini ndizo zitafungua michuano, zikifuatiwa na Uganda na Kenya kuingia, mechi ambazo zote zitachezwa siku ya ufunguzi, Jumamosi wiki hii.


Jumatano iliyopita, Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) ilicheza kujipima nguvu na Kenya (Harambee Stars) kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza, ilikopiga kambi kabla ya safari ya kuelekea Kampala, keshokutwa, Alhamisi.


Katika mechi hiyo, Kilimanjaro Stars ilishinda bao 1 – 0 lililofungwa na beki Aggrey Morris ambaye aliunganisha kichwa mpira wa kona uliopigwa na beki Amiri Maftaha katika dakika ya saba, bao lililodumu kwa muda wote wa dakika 90 za mchezo huo.


Kikosi cha Kilimanjaro Stars kilichopo kambini kinaundwa na makipa Juma Kaseja wa Simba na Deogratius Munishi ‘Dida’ wa Azam FC. Wachezaji wengine na vilabu vyao vikiwa kwenye mabano ni mabeki Kelvin Yondani (Yanga), Aggrey Morris na Erasto Nyoni (Azam FC), Issa Rashid (Mtibwa Sugar), Nassoro Masoud ‘Cholo’, Shomari Kapombe na Amiri Maftaha (Simba).


Viungo ni Frank Domayo (Yanga), Salum Abubakari ‘Sure Boy’ (Azam FC), Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Ramadhani Singano na Mrisho Ngassa (Simba), Athuman Idd na Shaban Nditi (Mtibwa Sugar).


Washambuliaji ni simon Msuva (Yanga), John Bocco ‘Adebayor’ (Azam FC), Christopher Edward (Simba), Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo).


By Jamhuri