“Kazi ya kuunganisha na kusambaza mabomba ya kusafirisha gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam imefikia hatua ya kuridhisha. Kazi hiyo inafanywa na  mashirika yenye uzoefu mkubwa kimataifa, ambayo ni Shirika la Teknolojia na Mendeleo ya Petroli la China (CPTDC), Kampuni ya Kutengeneza Mabomba ya China (CCP), Worley Parsons Limited na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC). Tayari mpaka sasa kilomita 142 kati ya 542 zimekamilika. Mradi huo unaotarajiwa kukamilika Desemba mwakani na utakuwa na mitambo ya kisasa.”

Hayo yamezungumzwa na Katibu Mkuu wa Wizara Nishati na Madini, Eliakim Maswi,  katika ziara iliyofanyika Novemba 7 hadi 9, mwaka huu, iliyotokana na wadau wa maendeleo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Banki ya Dunia (WB) na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) kutaka kuona utekelezaji wa mradi huo na iwapo kilichozungumzwa na Maswi katika warsha ya kujitathmini kwa utekelezaji wa mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).

Katika ziara hiyo, Maswi amewaambia wadau kuwa hatua za ujenzi wa mradi huo zimegawanyika katika sehemu mbili. Hatua ya kwanza ni kutandaza mabomba na kazi hiyo inatarajiwa kumalizika Julai mwakani, na hatua ya pili ni kujenga kituo cha kusafisha gesi asilia cha  Madimba, mkoani Mtwara, kisha kuisafirisha hadi Dar es Salaam – unaotarajiwa kukamilika Desemba mwaka kesho.

“Katika gesi kuna mambo mengi. Kwanza ni kuitafuta, sasa tumeipata halafu kuna uchimbaji. Hapa tunalenga mchakato wa kuchimba visima, na jinsi ya kuitoa gesi kutoka katika hifadhi yake na kuileta katika uso wa dunia na tumeanza na inatumika pale Ubungo. Sasa tupo katika mchakato wa kuzalishaji, usafishaji, usindikaji wa gesi asilia na usafiri hapa Madimba ndiyo mahali muhimu. Bila hapa hakuna gesi Dar es Salaam,” amesema Maswi.

Amesema mradi huo unamilikiwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Tanzania na ndiyo mradi mkubwa kuliko yote katika ya miradi iliyowahi kufanywa na Serikali.

Amesema kituo hicho kitakuwa cha kisasa na kina mashine zote zitakazokuwa zikisafisha gesi inayotoka katika visima na kuisafirisha hadi Dar es Salaam. Kituo hiki kitakuwa na vyumba 86, ofisi, viwanja ya michezo, bwawa la kuogelea na mahitaji mengine muhimu, hali itakayowapa  wafanyakazi morali na hawatakuwa na mawazo ya kwenda mjini.

Maswi ameridhishwa na kasi ya kazi zinayofanywa na kampuni hizo na kuwataka Watanzania kuwa na imani nazo. Awali shughuli hiyo ilitakiwa kukamilika Januari, 2015, sasa inatarajiwa kumalizika Desemba mwakani kutokana na kuwapo kwa vifaa vya kisasa na imara kutoka Kampuni ya China Petroleum Pipeline (CPP) wanaofanya kazi ya kulitandaza bomba hilo.

Mabomba yanayotandazwa ni imara na yanaweza kudumu kwa zaidi ya miaka 70 iwapo yatatunzwa vizuri, na kwamba Serikali itahakikisha inayafuatilia vizuri na kuhakikisha hayachafuki.

“Uunganishwaji unafanywa na mitambo ya kisasa kabisa na hapo bomba linapochimbiwa ndiyo hapohapo uunganishaji unafanyika na mabomba yatakayolazwa baharini yataunganishwa huko huko,” amesema.

Kwa mabomba yatakayokwenda baharini, uzito wake ni mkubwa zaidi ikilinganishwa na mabomba yanayotumika nchi kavu kwa kuwa yatakayolazwa baharini yatawekewa zege maalumu.

“Mabomba yatakayokwenda kulazwa baharini yatakuwa na uzito wa zaidi ya tani 10 baada ya kuwekewa zege ambapo kwa sasa yana uzito wa tani tatu,” amesema Maswi.

Mabomba yatakayolazwa bahari yatakuwa katika urefu wa kilomita 25 hadi 30 na hadi sasa kazi inaendelea vizuri.

Maswi amesema bomba hilo litakapokamilika uzalishaji wa umeme utaongezeka kutoka megawati 1,500 zilizopo hadi megawati 3,000 mwaka 2015 na kuanza kuuza umeme utakaokuwa wa ziada kwa nchi jirani. Kuhusu suala la ajira, amesema mradi huo tayari umezalisha ajira. Magari ya Watanzania yapatayo 45 yamepewa kazi ya kusafirisha mabomba huku Watanzania wengine wakiajiriwa katika kazi zinazoendelea.

Mradi huo ni wa kipekee na una umuhimu mkubwa kwa uchumi wa Tanzania, kwani kupitia mradi huo Tanzania itaweza kuwa na viwanda vingi na kuongeza ajira. Mradi utasaidia kutunza mazingira kwa kuwa badala ya kuendelea kukata miti kwa ajili ya mkaa na kuni, Watanzania watatumia gesi asilia kupikia.

Baada ya kukamilika, kampuni hiyo ya China itaendesha mitambo kwa muda wa miaka miwili na kisha watakabidhiwa wataalamu wa Kitanzania. Tayari baadhi ya vijana Watanzania wamepelekwa China na Brazil kusoma taaluma ya gesi.

Ulinzi wa bomba

Maswi amesema Serikali itaanzisha kikosi maalumu cha ulinzi ndani ya wizara kulinda bomba hilo, kitakachojumuisha wanausalama kutoka katika taasisi mbalimbali za usalama nchini. Kwa sasa bomba hilo linalindwa na Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Ulinzi wa Mazingira kinachoongozwa na George Mayunga.

Mtaalamu Mwandamizi wa Nishati kutoka Benki ya Dunia, Dk. Natalia Kulichenkoa, ambaye alifika kwa ajili ya kuona utekelezaji wa mradi huo, amesema mradi huo ni mkubwa na unatekelezwa kwa ufanisi mkubwa na vifaa vilivyotumika ni imara.

Dk. Kulichenkoa amesema kuwa sasa ni jukumu la Watanzania kuchangamkia fursa kwa kuwa mradi huo ni mkubwa na si vema kuwaachia Wazungu kuendelea na kazi hiyo, ilhali Watanzania wakigeuka watazamaji.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Symthies Pangisa, amesema pamoja na matatizo yaliyojitokeza awali kwa sasa wananchi wa mkoa huo wameanza kuelewa umuhimu wa gesi. Mkoa umeweka mikakati ya kuhakikisha wananchi wanafaidika na rasilimali hiyo kwa kuwekeza katika elimu.

“Mheshimiwa Katibu Mkuu hadi sasa tunajitahidi kuwekeza katika elimu. Tumehakikisha kuwa chuo chetu cha VETA kinatoa elimu kwa ajili ya vijana wetu ili waweze kushiriki katika ujenzi wa Mtwara na vile vile kujiingizia kipato,” anasema.

Pangisa pia amesema idadi ya watu wanaoingia na kutoka Mtwara imeongezeka, hali inayowalazimisha kuangalia upya mpangilio wa ramani wa mkoa huo.

Amesema wageni wengi wamekuwa wakitaka kuwekeza katika biashara ya hoteli, nyumba za kulala wageni na nyumba za kuishi, hivyo wameiagiza Idara Ardhi  ya Halmashauri hiyo kuangalia upya ramani ya mkoa na kuifanyia marekebisho.

“Unajua sasa Mtwara si kama ile ya miaka iliyopita, ni Mtwara mpya. Watu wanatafuta viwanja kwa kasi, wanataka kujenga. Sasa tumewaangiza maofisa mipango miji kuhakikisha wanapanga mji upya na kuchora ramani ya miji kwa kuangalia uwiano wa watu na ofisi za kiutendaji zisikae mahali pamoja, hatutaki kuwe kama kwenu Dar es Salaam  kwenye foleni kutokana na ofisi zote kuwa sehemu moja.

“Mambo yamebadilika kwa sasa, kiwanja kilichokuwa kinauzwa Sh milioni 1 sasa hupati kwa bei hiyo, kimefikia Sh milioni 10. Mambo yamebadilika sana kutokana na gesi asili,” amesema Pangisa.

Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Msoko, Abdallah Ulega,  amesema wilaya yake imejipanga vyema kuhakikisha vijana wa wilaya yake wananufaika na bomba hilo.

“Tunajitahidi kuhakikisha tunawapa vijana wetu elimu. Elimu itakayowawezesha kupata ajira mradi huu utakapokamilika. Pia tuna mpango wa kuanzisha Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kitakachotoa elimu ya ufundi kwa vijana wetu. Tunawasisitiza wazazi kuwapeleka watoto wao shule. Hili tunasisitiza mno hatuna mchezo nalo,”  amesema Ulega.

 

Akizungumza na JAMHURI, Juma Ibrahim Chilumba, mkazi wa Mkoa wa Mtwara, amesema mwanzoni hakujua umuhimu wa mradi huo, lakini sasa amefahamu ni jinsi gani wananchi wa mkoa huo wanavyoweza kufaidika na gesi.

“Ndugu, mwanzo hatukujua jinsi ya kutafuta fedha, ndiyo maana ikatokea vurugu zile lakini sasa ni mtaji tu. Ona kule ulikosema umetoka (Mabimba) watu wameuza kuku, mbuzi hadi wamekwisha lakini zamani thubutu… huwezi uza hivyo, ilikuwa ni ngumu mno. Sasa wenzetu kutoka mikoa ya jirani ndiyo wanauza na kupata utajiri baada ya kuku wetu na mbuzi  kuisha sisi tupo tu.

“Kwa hapa mjini watu wanajenga nyumba kila baada ya mwezi. Wanakuja Wazungu na Wachina wa gesi, wanakulipa fedha ya mwaka [pango] wengine miaka miwili unatafuta kiwanja kingine na kujenga nyumba nyingine kisha unapangisha tena kwa Wazungu, tatizo ni mtaji tu,” amesema Chilumba.

Amesema  maradi huo wa gesi umesababisha idadi ya watu kuongezeka, hatua inayofanya hali ya biashara kubadilika na kuwa juu. Vijana wengi sasa wanabaki katika mkoa huo badala ya kukimbilia katika miji iliyoendelea.

Historia ya gesi Tanzania

Gesi iligunduliwa mwaka 1982 na kampuni ya uchimbaji wa mafuta ya Agip, ambapo lengo lake ilikuwa ni kutafuta mafuta na badala yake wakakuta gesi. Mwaka 2004 Kampuni ya Artmus wakakiendeleza kisima cha kwanza kilichochimbwa ndani ya bahari. Hadi sasa kuna kampuni 18 za utafiti wa gesi nchini, ambapo kati ya hizo kampuni nne zinatafiti baharini na 14 zipo nchi kavu.

Kuna visima 63 vilivyotokana na utafiti huo, ingawa hadi sasa ni visima sita tu vinavyozalisha gesi hiyo. Katika uchimbaji huo, Kampuni ya British imefanikiwa kuchimba visima vinne, ambavyo vyote vina gesi, Kampuni ya Petroplus haijafanikiwa kupata gesi, Statoil imepata visima viwili.

Songosongo kuna gesi inayochimbwa yenye futi za ujazo 105 ambazo zinatumika kuzalisha umeme katika kituo cha Ubungo. Nishati ya gesi asilia mara nyingi hutumika kwa ajili ya joto, kupika, uzalishaji wa umeme, kuendeshea mitambo na magari, huku asilimia nyingine ikitumika kuzalisha mbolea.

Miaka 500 Kabla ya Kristo (B.C) Wachina walivumbua jinsi ya kutumia gesi kwa matumizi yao kwa kutafuta ni wapi inapatikana. Baada ya kufanikiwa kuipata walitengeneza vipande vya mianzi na kufanya mfano wa mabomba ya kusafirisha gesi asili na kutumia kwa ajili ya matumizi yao binafsi. Walitumia gesi asilia kwa ajili ya kuchemsha maji ya bahari  ambapo walitenganisha chumvi na maji na kuyafanya kuwa maji safi ya kunywa baada ya kuondoa chumvi.

Uingereza ilikuwa nchi ya kwanza kufanya biashara  ya gesi asilia. Mwaka 1785, gesi ya asili zinayozalishwa kutokana na makaa ya mawe ilitumiwa kama mwanga majumbani na mitaani. Kwa mara ya kwanza gesi ilitumika nchini Marekani mwaka 1816 katika mitaa ya miji ya Baltimore, Maryland. Gesi asilia iligunduliwa na kutambuliwa Marekani mapema mwaka 1626, kutokana na mpelelezi kutoka Ufaransa baada ya kuvuja katika Ziwa Erie.

Mwaka 1859 Kanali Edwin Drake (zamani kondakta wa Reli) alichimba kisima cha kwanza kilichokuwa na urefu wa futi 69 chini ya ardhi. Baadhi ya viwanda viliweka imani na kisima hicho kuwa ulikuwa mwanzo wa matumizi ya gesi katika viwanda vya Marekani. Lilijengwa bomba lililopitisha gesi lililokuwa na kipenyo cha inchi mbili na umbali wa maili tano na nusi kutoka katika Kijiji cha Titusville, Pennsylvania.

Ujenzi wa bomba hilo ulitoa mwanga kuwa gesi asilia inaweza kutolewa kwa usalama na kwa urahisi kutoka ardhini na kuwa chanzo kizuri cha matumizi mbalimbali. Mwaka 1821, William Hart alikuwa na nia ya dhati  kupata gesi asilia hivyo alichimba kisima cha futi 27 katika Mji wa Fredonia, New York. Hart, ambaye amekuwa akitambulika kama baba wa gesi asilia nchini Marekani, alianzisha kampuni ya kwanza ya  gesi nchini humo.

Bila miundombinu ya mabomba ilikuwa vigumu kusafirisha gesi kwa umbali mrefu kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. Mwaka 1885,  Robert Bunsen aligundua chombo ambacho alikiita Bunsen burner. Alitengeneza chombo hicho ili kitumike kuchanganya gesi asili na hewa ya oxygen na kupata uwiano wa mwanga, kutengeneza moto na kuwa salama kwa kupikia.

Ugunduzi wa Bunsen burner ulifungua fursa mpya kwa matumizi ya gesi katika Bara la Amerika na duniani kote. Ugunduzi wa kifaa joto cha thermostatic ulirahisisha msisimko mkubwa katika gesi asilia. Hivyo mwaka 1891 bomba la urefu wa maili 120 la gesi asilia lilijengwa kutoka Kisima cha Indiana katika Jiji la Chicago.

Pamoja na kuwapo kwa bomba hilo bado usafirishaji wa gesi haukukidhi mahitaji ya walaji. Hakuna jambo lolote muhimu lililofanyika hadi mwaka 1920. Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia uzinduzi wa uchomeleaji kutengeneza mabomba ulishika kasi na ufuaji wa vyuma vya mabomba imara ulifanywa. Baada ya vita ujenzi wa bomba la gesi uliimarika katika miaka ya 1960 na kuruhusu ujenzi wa maelfu ya maili za mabomba ya gesi yalijengwa Marekani.

Baada ya matumizi ya gesi kuwa rahisi, matumizi mapya ya gesi asilia yaligunduliwa. Matumizi hayo ni ya vifaa vya nyumbani kama vikanza (heaters) vya kuchemshia maji na oven. Viwanda navyo vilianza kutumia gesi asilia kwa ajili ya kuzalisha bidhaa zinazotokana na mimea. Pia gesi ilitumika kuchemsha mashine zilizokuwa zikitumia kuwasha majenereta ya umeme. Uboreshaji katika usafirishaji wa gesi umefanya bidhaa hiyo kupatikana kirahisi.

Mwaka 1938, Serikali ya Marekani ilianzisha sekta ya gesi asilia. Wakati huo, wajumbe wa Serikali hawakuwa na imani na sekta hiyo kutokana na ukiritimba. Walihofu wananchi kudhulumiwa kutokana na kuwa bidhaa hiyo ilikuwa na bei ya juu kuliko kipato cha Wamarekani wengi kuwa duni.

Kutokana na umuhimu wa matumizi ya gesi hiyo, sheria ya gesi asilia ilitungwa. Sheria hiyo iliweka kanuni na vikwazo juu ya gesi kulinda walaji.

Kampuni zinazojenga bomba hili zina uzoefu mkubwa. Kampuni Mabomba ya  China Petroli (CPP) ilianzishwa mwaka 1973, ikiwa ni mahususi katika utafutaji wa madini, uhandisi, ushauri, miundombinu, ununuzi, ujenzi na usimamizi. Ni kampuni ya kimataifa ya muda mrefu na ina uzoefu mkubwa katika masuala ya gesi, imekuwa ikisimamia ujenzi wa usafirishaji wa mabomba, vifaa kama matangi ya ukubwa wa kati na mkubwa ya kuhifadhi gesi.

Tayari imefanya miradi mikubwa katika nchi za Kuwait, Tunisia, Sudan, Libya, Malaysia, Kazakhstan na Msumbiji.

 

Shirika la Teknolojia na Maendeleo ya Petroli (CPTDC)  inayomilikiwa na Shirika la Taifa la Petroli la China (CNPC), nalo linajishughulisha na kuuza petroli na kusambaza vifaa vya ujenzi.

CPTDC ilianzishwa mwaka 1987 na  kuanza kuuza bidhaa nje ya China kuanzia mwaka 1992. Kila mwaka inapata mikataba yenye thamani ya dola bilioni 5 za Marekani. CPTDC imetoa bidhaa na huduma zake kwa nchi 78 duniani.

CPTDC inalenga kuboresha maendeleo mara sita  ya uwezo wake na imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika biashara hiyo. Imejiimalisha kibiashara katika nchi za Mashariki ya Kati, Asia ya Kati, Russia, Afrika, Marekani, Mashariki ya Mbali, Asia-Pasifiki na nchi nyingine ulimwenguni. Lina masoko katika taasisi 67 katika nchi 51.

Worley Parsons Limited ilianzishwa mwaka 1971 na ina uzoefu wa hali ya juu katika kushauri masuala ya gesi. Makao makuu yake yako nchini Australia na inatoa huduma za ushauri wa rasilimali na sekta za nishati na viwanda na pia inatoa huduma za bima.

Julai mwaka huu, Worley Parsons imeshinda mkataba wa kiwanda cha Samsung katika kubuni na uhandisi, kuhifadhi uzalishaji.

Kampuni hiyo ina matawi katika nchi za Australia/New Zealand, Afrika, Canada, China,  Ulaya, Amerika ya Kusini, Mashariki ya Kati, Kusini na Mashariki ya Asia na Marekani. Pia  ina wafanyakazi makini 38,700 katika ofisi 165 ndani ya nchi  43 duniani kote.


2075 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!