* Asema yeye kuwa Waziri wa Katiba na Sheria anajiona kama samaki aliyetumbukizwa majini

 

Wakazi wa Jimbo la Nachingwea mkoani Lindi, wana kila sababu ya kujivunia bahati ya wabunge wao kuteuliwa na Rais kuongoza wizara mbalimbali hapa Tanzania. Edgar Maokola-Majogo, aliyeliongoza jimbo hilo kwa kipindi cha miaka 30, pamoja na wizara nyingine, alipata kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, kitengo cha Kupunguza Umaskini na Kuratibu Mashirika yasiyo ya Kiserikali na Waziri wa Nishati na Madini.

Baada ya Maokola-Majogo kustaafu siasa mwaka 2005, Mathias Meinrad Chikawe, ambaye kwa sasa ni Waziri wa Katiba na Sheria, alishika hatamu ya kuliongoza jimbo hilo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

 

Kilichomshawishi Chikawe

Katika mahojiano maalum na JAMHURI Dar es Salaam wiki iliyopita, Waziri Chikawe ambaye kitaaluma ni mwanasheria, anasema alianza kunusa siasa mwaka 1999 wakati akifanya kazi katika Tume ya Marekebisho ya Sheria Tanzania (TLRC).

 

“Nikiwa pale kwenye tume [TLRC] ndiyo nikashawishika kujihusisha na siasa kwa vitendo, na Kikwete [Jakaya Mrisho Kikwete] alipoanza kusikika ndipo nami nikashawishika. Nilikutana naye akanitia moyo,” anasema Chikawe na kuendelea:

 

“Mwaka 2000 nilikwenda kuwania ubunge wa Nachingwea, lakini nikashindwa katika kura za maoni [ndani ya CCM], ila kura nyingi nilizopata zilinitia moyo. Hata Maokola-Majogo aliyenishinda alitikisika.

 

“Baada ya hapo ndiyo nikasema kumbe hili jambo linawezekana, na wananchi wakawa wananitia moyo, si kwamba Maokola-Majogo ni mbaya, lakini kwa sababu walikuwa wamemchoka.”

 

Kitendo cha kuungwa mkono na wananchi wengi kilimwongezea Chikawe ujasiri kiasi cha kujitosa tena kwenye kinyang’anyiro cha ubunge wa Nachingwea katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2005.

 

Mwaka huo, pengine baada ya kusoma alama za nyakati, Maokola-Majogo alitangaza kung’atuka siasa, hivyo hakujitokeza kuomba kuteuliwa na CCM kugombea ubunge katika jimbo hilo. Hatua hiyo ilimpatia Chikawe nafasi nzuri zaidi ya kutwaa ushindi.

 

“Katika uchaguzi ule [wa 2005] nilishinda kwa kupata asilimia 85 za kura za jumla, nikaingia [bungeni] nikiwa na nguvu,” anasema Chikawe na kuongeza:

“Kuanza tu [ubunge] Rais [Rais Kikwete] akaniteua kuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria chini ya Waziri kamili, Dk. Mary Nagu. Baadaye Rais akafanya mabadiliko na kuniteua kuwa waziri kamili wa wizara hii.

 

“Mwaka 2010 nikarudi kugombea [ubunge], wananchi wakasema bado wana imani na mimi, wakanichagua kwa kura nyingi.

 

“Niliporudi bungeni Rais akaniteua kuwa Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, (Utawala Bora), nikawa pale Ikulu na yeye, tukaendelea vizuri hadi mwaka 2012 aliponitoa pale akanirudisha tena Wizara ya Katiba na Sheria wakati vuguvugu la mabadiliko ya Katiba limeshaanza.”

 

Lengo lake kisiasa

Waziri Chikawe anasema lengo kuu la yeye kujiingiza katika siasa ni kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya huduma duni za umeme, maji, barabara na umaskini yaliyokuwa yanawakabili wakazi wa Jimbo la Nachingwea.

 

“Kabla sijaenda kugombea ubunge, kila nilipopata nafasi ilikuwa lazima niondoke Dar es Salaam kwenda Nachingwea kusalimia wazazi wangu, ndipo nikawa ninashuhudia kero zinazowakabili wananchi kule.

 

“Umeme ulikuwa kero, unakatika ovyo, maji ni shida, watu walikuwa wanachota maji machafu kwenye visima, nilikerwa pia na hali ya umaskini wa wananchi. Nikasema labda ninaweza kufanya kitu kikaleta mabadiliko kule,” anaeleza.

 

Mafanikio anayojivunia jimboni

“Mafanikio ni makubwa. Mwaka 2005 nilipochaguliwa kuwa mbunge, Nachingwea yenye wakazi 187,000 ilikuwa na shule za sekondari tatu, hospitali mbili, vituo vya afya viwili, umeme ulikuwa ni mjini tu na barabara zote zilikuwa za vumbi,” anasema Chikawe na kuendelea:

 

“Lakini mpaka sasa mradi wa maji uliogharimu Sh bilioni 31 umekamilika, watu wanatumia hayo maji, tatizo la uhaba wa maji limepungua Nachingwea.”

Anafafanua kuwa mradi huo umewezesha mji wa Nachingwea na vijiji tisa kuwa na uhakika wa huduma ya maji safi ya bomba na kwamba Rais Kikwete ameahidi kwenda kuuzindua wakati wowote akipata nafasi.

 

“Ninajivunia juhudi zangu hizo na ninamshukuru Rais kwa kunisaidia kutafuta ufumbuzi wa tatizo la uhaba wa maji Nachingwea. Pia ninamshukuru Mwandosya [Profesa Mark James Mwandosya] naye alinisaidia sana kufanikisha mradi huo,” anasema Waziri Chikawe.

Kikwete alipata kuwa Katibu wa CCM Wilaya ya Nachingwea. Profesa Mwandosya ambaye kwa sasa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Asiye na Wizara Maalum, alipata kuwa Waziri wa Maji.

 

Pia tumefanikiwa kuchimba mabwawa matano ya maji, kila moja linahudumia vijiji vinne na tumechimba visima virefu saba vya maji,” anaongeza Chikawe.

Kuhusu umeme, Waziri Chikawe anasema amejitahidi kupunguza kwa kiwango kikubwa tatizo lililokuwapo.

 

“Siku hizi kule Nachingwea unaweza kukaa wiki nzima bila kuona umeme umekatika na wananchi wengi, hasa vijana wanatumia fursa hiyo kuanzisha na kuendesha miradi mbalimbali ya uzalishaji mali,” anasema.

 

Kwa mujibu wa waziri huyu, chanzo cha umeme huo ni gesi inayovunwa katika Mkoa jirani wa Mtwara. Akizungumzia barabara, Chikawe anasema, “Sasa kwa mara ya kwanza, wananchi wa Nachingwea wanaona lami, tumejenga barabara ya lami yenye urefu wa kilomita tano.”

 

Kwa upande wa sekta ya afya, mbunge huyu wa Nachingwea anasema ameweza kuishawishi Serikali kwa kushirikiana na wananchi hadi kufanikisha ujenzi wa zahanati 28 katika kata 28, na kwamba juhudi zinafanyika kuwezesha ujenzi wa zahanati nyingine nne katika kata nne zilizosalia.

 

Sekta ya elimu, kwa mujibu wa Chikawe, nayo haijaachwa nyuma katika Jimbo la Nachingwea. “Tumefanikiwa kujenga shule ya sekondari katika kila kata na jitihada za kuboresha zaidi elimu zinaendelea,” anasema.

 

Mtazamo wa Waziri Chikawe ni kwamba uboreshaji wa huduma za jamii ni chanzo cha kupiga vita umaskini miongoni mwa wakazi wa Jimbo la Nachingwea.

 

Mafanikio anayojivunia wizarani

Chikawe anaelezea pia kuridhishwa kwake na jinsi anavyomudu majukumu katika Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na viongozi wengine.

 

“Ninamudu majukumu vizuri, nina Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Jaji Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wote tunashirikiana vizuri, tunajivunia tunachokifanya,” anasema.

 

Waziri huyu anataja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika wizara hiyo kutokana na juhudi zake kwa kushirikiana na viongozi wengine kuwa ni kuongezwa kwa bajeti ya sekta ya sheria.

 

“Kwa mfano, Mahakama na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali vimeboreshewa incentive (marupurupu). Pia tumeanzisha Law School (Shule ya Sheria) jijini Dar es Salaam na Rais anatarajiwa kuizindua hivi karibuni,” anathibitisha.

 

Anaongeza kuwa Wizara ya Katiba na Sheria chini ya uongozi wake imefanikiwa kuwezesha ujenzi wa Mahakama Kuu katika mikoa ya Kagera na Shinyanga.

 

“Mwaka huu pia tumejipanga kuanzisha ujenzi wa Mahakama Kuu katika mikoa mitano, bajeti ipo na imeshapitishwa, tunaishukuru ofisi ya Hazina inatuelewa. Tunataka kila mkoa uwe na Mahakama Kuu.

 

“Pia sisi kama Wizara ya Katiba na Sheria tunasimamia mchakato wa mabadiliko ya Katiba. Tume ya Warioba [Jaji mstaafu Joseph Sinde Warioba – Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba] inaendelea vizuri,” anasema.

 

Ataja changamoto

Waziri Chikawe anataja changamoto kuu zinazomkabili kama mbunge wa Nachingwea kuwa ni kuongeza juhudi za kuboresha huduma za jamii kama vile elimu, maji, afya, umeme na barabara.

 

“Kuna changamoto nyingine ninaiona, unaweza ukawajengea wananchi barabara na shule, lakini kama hujawapa pesa baadhi ya wananchi wanaweza wasiridhike. Lakini mimi ninaamini kuwa kazi ya mbunge ni kutafuta maendeleo ya umma, si ya mtu binafsi,” anasema na kuongeza:

 

“Pia kiwango cha rushwa kinakatisha tamaa, ni kikubwa, kwa sababu ukitaka ardhi mtu anaomba rushwa, ukitaka shule mtu anaomba rushwa. Hata kule mahakamani mambo hayoko very clean (shwari sana). Lakini mapambano yanaendelea.

 

“Tumewaongezea watu wa Mahakama marupurupu ili wafanye kazi vizuri. Tunaendelea kupambana kuwezesha uboreshaji wa bajeti za sekta zote zilizo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria.”

 

Kwa upande mwingine, Waziri Chikawe anasema kitendo cha Rais kumteua kuwa Waziri wa Katiba na Sheria kinamfanya afarijike zaidi kwa kuwa kitaaluma yeye ni mwanasheria.

 

“Mimi ni mwanasheria, ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, ninajisikia vizuri, niko kwenye sekta yangu, mimi kuwa hapa [Wizara ya Katiba na Sheria] ni kama umemtumbukiza samaki kwenye maji. Ninajivuna kuwa nimefanya something (kitu fulani) kwa ajili ya maendeleo ya sekta yetu,” anaeleza.

Ndoto yake

“Mimi ni mwanasiasa, ndoto ya mwanasiasa siku zote ni kuendelea mbele. Maisha ya mwanasiasa yanatawaliwa na vitu vitatu. Kwanza ni matakwa yako mwenyewe, pili ni matakwa ya watu unaowaongoza na tatu ni majaliwa ya Mwenyezi Mungu.

 

“Ninaweza nikataka mimi, wananchi wakakataa, wananchi wanaweza kutaka Mungu akakataa. Ukikubali hali hiyo hakuna shida.

 

“Kwa hiyo, mimi kama mwanasiasa ni mtu wa kwenda mbele. Ndoto yangu ni kuendelea for at least ten years (kwa angalau miaka kumi), bado nina nguvu na moyo wa kuwatumikia wananchi,” anaeleza Waziri Chikawe.

 

Wito wake

Kiongozi huyu wa Wizara ya Katiba na Sheria anatumia nafasi ya mahojiano na JAMHURI pia kutoa wito kwa viongozi na wanachama wa CCM kuboresha ushirikiano na kujiimarisha katika sera na hoja za kisiasa.

 

Kwa upande mwingine, anatoa wito kwa viongozi na wanachama wa vyama vya siasa vya upinzani dhidi ya CCM kujenga utamaduni wa kuchangia mawazo yatakayoiwezesha Tanzania kusonga mbele katika suala zima la maendeleo.

 

“Wapinzani wasaidie kujenga kuliko kubomoa,” anasisitiza Waziri huyu wa Katiba na Sheria.  Kadhalika, anasema Serikali haina budi kuendelea kujitambua kuwa ipo kwa ajili ya kuwahudumia Watanzania walioikabidhi madaraka.

 

“Mfano, minister (waziri) ni servant (mtumishi), viongozi sisi kazi yetu ni kuwatumikia wananchi, Serikali nayo kazi yake ni kuwahudumia wananchi wake. Serikalini si mahali pa kwenda kutafuta fedha, na viongozi tusiwe mabosi bali tuwe watumishi,” anasisitiza.

 

Anaiambia nini jamii? “Wito wangu kwa jamii nzima ni kwamba kila mtu anapoamka afanye yanayowezekana kwa siku hiyo na ayafanye vizuri ayamalize, kwa sababu jana haipo na kesho haipo, ipo leo na leo ndiyo siku ya kufanya kila kitu. Nchi yetu itaendelea tukifanya hivyo, mimi ninafanya hivyo.”

Chikawe alikosoma

 

Mathias Meinrad Chikawe anasema alizaliwa mwaka 1951. Alipata elimu ya awali (chekechea) katika Shule ya St. Josephs Convent ya jijini Dar es Salaam mwaka 1958.

 

Alipata elimu ya msingi shuleni hapo kati ya mwaka 1959 na 1965 kabla ya kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule hiyo hiyo mwaka 1966 hadi mwaka 1969 alipohitimu kidato cha nne.

 

Kati ya mwaka 1970 na 1971 alipata elimu ya sekondari ya juu (kidato cha tano na cha sita) katika Shule ya Mkwawa iliyopo mkoani Iringa. Mwaka 1972 alijiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Ruvu, kabla ya kuchaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hadi mwaka 1975 alipohitimu digrii ya sheria.

 

“Mwaka huo huo wa 1975 mara baada ya kuhitimu chuo kikuu niliajiriwa katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, huku nikipata mafunzo ya vitendo pia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Shirika la Sheria Tanzania na Chuo cha Siasa Kivukoni hadi mwaka 1976 nilipohitimu nikaajiriwa rasmi na kupangiwa kazi katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” anasema Chikawe.

 

Baadaye alihamishwa kwenda kuwa Mwanasheria wa Wizara ya Kilimo, akiwasaidia John Malecela na Joseph Mungai katika kipindi cha miaka 10 kabla ya kuhamishiwa Ikulu ambako alifanya kazi kati ya mwaka 1985 na 1998, kabla ya kuanza kujitosa kwenye siasa mwaka 1999. Huyu ndiye Mathias Meinrad

1384 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!