Malele aendelea kuteseka Muhimbili

Maendeleo ya matibabu ya Mohamed Malele aliyetangaza siri za mtandao unaodaiwa kuhusika kumuua Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, ni kitendawili.

Jeshi la Polisi lilimpeleka Malele kutibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) takriban miezi miwili iliyopita akidaiwa kuwa mgonjwa wa akili, ingawa mwenyewe akana kwamba si mgonjwa.

Malele mwenyewe amepata kusema, “Kabla ya kuletwa huku maaskari waliniuliza ‘umewahi kuugua?’ Nikasema sijawahi kuugua, lakini wamenileta hospitali.

 

“Nikawauliza humu hospitali mtanisaidiaje, wakasema wewe nenda hospitali, tuna shaka na wewe utakuwa umetumwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Huku naletewa dawa natumia kila siku.

“Mama alikuja kutoa maelezo kwamba mimi si mgonjwa, na mimi niliwaeleza mbona nilichokisema mlichunguza mkakuta ni kweli, lakini wapi.”

JAMHURI lilifanya juhudi za kutaka kujua maendeleo yake hospitalini hapo, lakini uongozi wa Idara ya Maradhi na Afya ya Akili ulikataa kuweka bayana suala hilo kwa saabu za kimaadili.

Daktari Bingwa wa Maradhi ya Afya ya Akili wa MNH, Frank Masao, amesema kitendo cha kueleza maendeleo ya ugonjwa wa Malele kwa mtu asiye mzazi wake ni kinyume cha maadili ya utabibu.


“Mojawapo ya miiko yetu ya kazi ni kutoongea habari za ugonjwa wa mtu. Tulikula kiapo cha kulinda haki ya mgonjwa.

“Kuhusu Mohamed [Malele] siwezi kuongea chochote kwa sababu nalinda haki yake ya msingi,” amesema Dk. Masao.

Hata hivyo, bila kutaja aina ya ugonjwa, amesema “Malele ni mgonjwa, ndiyo sababu yuko hapa hospitalini.”

Wakati Dk. Masao akisisitiza suala la kulinda siri ya ugonjwa wa mtu, Jeshi la Polisi lilimtangaza Malele kuwa ni mgonjwa wa akili.

Dk. Masao amesema kwamba hata kitendo cha kumwita mtu kichaa ni sawa na kumtukana, kumnyanyapaa na kumdhalilisha mbele ya jamii.

Alipotakiwa kueleza ni hatua gani zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya watu wanaotangaza magonjwa ya watu, Dk. Masao amesema, “Tunashauri taratibu za kisheria zichukuliwe dhidi ya wanaotangaza ugonjwa wa mtu.”

Kwa upande mwingine, Dk. Masao amesema kwamba si watu wote wanaopelekwa hospitalini wakidaiwa ni wagonjwa wa akili hukutwa na maradhi hayo.

Ametumia nafasi ya mahojiano maalumu na JAMHURI kutoa wito kwa jamii kuhakikisha hawatangazi magonjwa ya watu kuepuka kukiuka haki za msingi za wagonjwa.

“Tusihukumu kabla ya kuthibitisha,” amesema Dk. Masao huku akisisitiza kuwa hata madaktari waliopima na kuthibitisha ugonjwa hawapaswi kuutangaza.

Kijana Malele ana siri nzito juu ya mtandao mpana wa mauaji ndani ya Jeshi la Polisi unaohusisha watumishi wengine kutoka vyombo vya ulinzi na usalama, wafanyabiashara na wanasiasa.

Habari za karibuni zinasema kwenye orodha ya aliowataja kwenye mtandao wa uhalifu, wamo wabunge. JAMHURI inaendelea kuyahifadhi majina yao kwa kuwa haijafanikiwa kuzungumza nao.

 

Mtandao huo unatajwa na Malele kwamba ndiyo uliohusika kumuua Kamanda Barlow usiku wa kuamkia Oktoba 13, mwaka jana katika eneo la Kitangiri jijini Mwanza wakati akimrejesha nyumbani Mwalimu Doroth Moses, aliyekuwa naye katika kikao cha harusi.

Malele alikamatwa Mei 10, mwaka huu, katika lango la Bunge mjini Dodoma wakati akiwatafuta wabunge awape siri za kundi hilo la mauaji ambalo yeye anasema alikuwa mfuasi wake.


 

1034 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!