Upande wa Utetezi katika kesi iliyokuwa ikimkabili Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Joseph Mbilinyi “Sugu” na Katibu wa Kanda ya Nyasa, Emmanuel Msonga umekata rufaa kupinga hukumu ya kwenda jela miezi mitano iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mbeya jana, Jumatatu Februari 26.

Wakili wa washtakiwa hao, Peter Kibatala amesema kuwa hawakuridhika na uamuzi wa mahakama hiyo uliotolewa na Hakimu Mfawidhi Mkazi, Michael Mteite na kuelezea azma yao ya kukata rufaa pamoja na kuwaombea dhamana wateja wao.

Washtakiwa kwa pamoja wamekutwa na hatia ya kutumia maneno ya fedheha dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Mwenge Desemba 31, mwaka jana.

Akirejea mwenendeo mzima wa kesi na ushahidi uliotolewa, Hakimu Mtetite amesema washtakiwa kwa pamoja wamekutwa na hatia.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili Mkuu wa serikali Joseph Pande umeieleza Mahakama kuwa hawana kumbukumbu ya washtakiwa kutenda kosa la aina yoyote.

Lakini akaiomba Mahakama itoe adhabu kali kwa kuwa aliyefedheheshwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Peter Kibatala akishirikiana na Profesa Abdallah Safari na Faraji Mangula umeiomba Mahakama kuwapunguzia adhabu wateja wao kwa kuwa wamekaa mahabusu takribani mwezi mmoja

Mbali na kifungo wameiomba mahakama kuzingatia kuwa mshtakiwa namba moja ni Mbunge na endapo atafungwa kifungo kinachozidi miezi sita watakaoathirika ni wananchi wa jimbo lake.

Kibatala akaikumbusha Mahakama kutoa adhabu mbadala kutokana na washtakiwa wote kuwa na familia na wana watoto wachanga wanaowategemea.

Baada ya kusikiliza pande zote mbili Mahakama ikatoa adhabu ya kifungo cha miezi mitano jela na adhabu hiyo ianze kutekelezwa mara moja.

1766 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!