Rais John Magufuli amefuta agizo la kutofungishwa ndoa kwa watu wasiokuwa na vyeti vya kuzaliwa kuanzia Mei mwaka huu lililotolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Waziri wa Katiba na Sheria Dk. Harrison Mwakyembe. 

Rais Magufuli amewatoa hofu Watanzania na kuwataka kuendelea na utaratibu wa kuoa na kuolewa kama kawaida na iwapo kuna kifungu chochote cha sheria kinachomlazimisha mtu awe na cheti cha kuzaliwa ndipo aoe ama aolewe basi atamuelekeza Dk. Mwakyembe apeleke Bungeni kikarekebishwe. 

Akizungumza na Waandishi wa habari mkoani Dodoma wiki iliyopita, Rais Magufuli amesema serikali haiwezi kuruhusu sharti hilo kutumika kwa kuwa litawanyima haki ya kuoa na kuolewa Watanzania wengi ambao hawana vyeti vya kuzaliwa huku utaratibu wa kupata vyeti hivyo ukiwa bado unakabiliwa na changamoto nyingi kwa wanaohitaji. 

Amesema idadi ya Watanzania walio na vyeti vya kuzaliwa ni chini ya asilimia 20 huku wengi wao wakiwa ni wananchi waishio vijijini ambako ni vigumu kupata vyeti hivyo na wengine wakiwa wamezaliwa kabla ya kuanza kutolewa kwa vyeti vya kuzaliwa nchini mwaka 1961. 

Pamoja na hayo, Rais Magufuli amewataka wanasheria kuziangalia vizuri sheria zinazohusiana vizazi na vifo na kuoa na kuolewa ili zisilete mkanganyiko kwa wananchi na kwamba watanzania waendelee kupata vyeti vyao vya kuzaliwa kama kawaida na amewataka viongozi wote kuwahamasisha wananchi kuwa na vyeti hivyo. 

Dk. Mwakyembe akiwa ziarani mkoani Morogoro, alinukuliwa akisema kuanzia Mei Mosi, mwaka huu, watu hawataruhusiwa kuoana bila kuwa na vyeti vya kuzaliwa na kwamba serikali imeamua kufanya hivyo ili kupata takwimu sahihi za wananchi wake zitakazosaidia kupanga mipango ya kimaendeleo sanjari na kuzuia wageni kuingia nchini kinyemela.

 Nasema kwa hili la Dk. Mwakyembe, limeonesha kutokuwepo kwa mawasiliano mazuri ndani ya serikali. Hali hiyo inaweza kusababisha mkanganyiko miongoni mwa wananchi.

 Kama viongozi wetu wanaona ni sawa kuiongoza nchi bila kuwa na mipango madhubuti yenye kuchochea kasi ya maendeleo ya Watanzania, lakini pia inaonesha kukatika kwa mawasiliano serikali, kiasi cha Rais Magufuli kuingilia kati.

 Haiwezekani kila mmoja atoe maagizo na amri kali kwa wananchi na nyingine zikibeba kila aina ya chuki kwa baadhi ya watu kwa sababu ya tofauti za kisiasa, kiimani.

 Matibu Kata, Tarafa, Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa Mkuu wa Kituo cha Polisi, na wengine kwa kutumia mwanya wa ukiukaji wa Katiba wamekuwa wakitoa maagizo ya kukamatwa na kuwekwa mahabusu baadhi ya watu kwa makosa mengine ambayo hayana mashiko.  

 Kutokana na agizo la Dk. Mwakyembe ambalo huenda lilikuwa na nia njema ya kupambana na ndoa za utotoni au zaidi ya hapo kama yalivyo madai yake; kosa linalojitokeza ni kutowasiliana kabla ya kutoa kauli hiyo bila kukubaliana na mawaziri wenzanke na kufanya uchunguzi wa kina.

 Viongozi wetu wanapaswa kuelewa kwamba nchi haiongozwi kwa mlolongo wa matukio tu yanayofurahisha na kuwapumbaza wananchi wanaokabiliwa na hali ngumu za maisha kila kukicha.

 Nchi yetu sasa inaonekana kuwa ya matukio tu, tulianza na kupambana na dawa za kulevya na kukamata wanaodaiwa kujihusisha na matumizi ya dawa hizo, vyeti vya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda, pombe za viroba na sasa marufuku ya Mwakyembe iliyopata pigo baada ya kufutwa na Mkuu wa Nchi.  

By Jamhuri