Mawaziri wa JPM na mbio za sakafuni

Kasi ya mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tano chini Rais Dk. John Pombe Magufuli inatia shaka. Bila shaka, baadhi yao wanaonekana kutafuta sifa ambazo hawastahili. Hawa wanaongozwa na hofu ya kutimuliwa kazi.

Tangu walipoapishwa Desemba 12, mwaka huu, mawaziri hawa hawakai ofisini na kazi yao ni kufanya ziara za kushtukiza kwa taasisi zilizo chini yao, wakifuatilia utendaji na huduma zitolewazo kwa wananchi na kutoa matamko mbalimbali.

Kwa kasi waliyoanza nayo ambayo inaelezwa kwamba ni kujaa nidhamu ya woga, mara baada ya kuapishwa, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na Naibu wake, Hamis Kigwangalla, hawakwenda ofisini na badala yake waligawana ziara za kushtukiza – mmoja akielekea Hospitali ya Amana na mwingine Mwananyamala kukagua huduma zinavyotolewa.

Mawaziri karibu wote wamefanya ziara hizo za kushtukiza katika taasisi zinazowahusu na baadhi yao kutoa maagizo makali yaliyoambatana na kuwasimamisha kazi watendaji walioonekana na makosa. Hawa wanajaribu kwenda na desturi ambayo haikuzoeleka katika awamu zilizopita.

Wanatafuta kwenda kasi ya Rais Magufuli na Waziri Mkuu, Majaliwa, lakini baadhi yao hawafanyi utafiti wa kina kuhusu tuhuma zinazowakabili watendaji wanaodaiwa kuwa ni wazembe na mafisadi, na hizi ni dalili za kutaka waonekane wanafanya kazi.

Sitaki kuwavunja moyo mawaziri hawa. Lakini ninachosema ni kwamba maagizo mengi ni ya kukurupuka na pengine kuonesha mapema kwamba wameshindwa majukumu yao na kuongeza wingi wa majipu kuliko kazi ya kuyatumbua.

Tatizo kubwa linalosababisha wafanye kazi kwa nidhamu ya woga ni uongozi wa mazoea, Serikali za kirafiki tangu awamu ya pili hadi ya nne iliyomaliza muda wake na kuliua Azimio la Arusha lililohubiri miiko ya uongozi kwa kuanzisha na Zanzibar ambalo nalo limeyeyuka.

Kuwa na ziara za kushtukiza kunapaswa kuakisi uadilifu wa kiongozi mwenyewe na uhakika wa kile wanachokichunguza ama kukihoji kwa watendaji wa Serikali kuhusu utekelezaji wa majukumu yao badala ya kutumia nguvu nyingi.

Pamoja na kuwapongeza kwa kuthubutu kwenda sambamba na kaulimbiu ya Rais Magufuli ya ‘hapa kazi tu’ hata hivyo wanapaswa kuelewa kwamba utendaji kazi kwa mazoea ndiyo uliokuwa chanzo cha umaskini kwa Watanzania na maovu mengine yaliyokuwa yakifanywa na baadhi ya watendaji kwa kigezo cha kufahamiana na viongozi waandamizi wa Serikali zilizopita.

Kwa upande mwingine, nimefurahishwa na utendaji  wa Naibu Waziri  wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Kigwangalla mwishoni mwa wiki iliyopita kwa kuwafungia nje ya geti watumishi wa wizara hiyo waliochelewa kazini na kuahidi kwamba kitendo hicho kitakuwa endelevu.

Dk. Kigwangalla alifika ofini kwake saa 1:05 asubuhi na moja kwa moja alianza kukagua daftari la mahudhurio linalotumiwa na wafanyakazi wa wizara hiyo na kubaini kwamba wengi walikuwa hawajafika.

Ilipofika saa 1:32 alimwamuru askari aliyekuwa akilinda geti hilo kufulinga na asiruhusu mtumishi yeyote kuingia ndani, hata wale walioletwa kwa magari nao walizuiwa pamoja na magari nje geti na pia kumwamuru Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wizarani hapo kumpelekea vitabu vya mahudhurio ya vitengo vyote ili avikague.

Kwa kuwabana wazembe maofisini iwe kwa taasisi zote kutokana na kukithiri kwa uzembe kwa Watanzania wengi ambao nao ni chanzo kikubwa cha umaskini. Watanzania kwa asilimia kubwa ni wavivu na wazembe ambao mafanikio ya maisha yao ni ‘upigaji dili’ kama hao wanaoitwa majipu yanayopaswa kutumbuliwa.

Nakumbuka baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, Halmashauri ya Jiji la Mbeya ilikumbwa na kashfa ya ufisadi wa ukwapuaji wa fedha katika akaunti ya jiji hilo ambazo zilidaiwa kusaidia uchaguzi kwa CCM. Hali kama alivyoikuta Rais Magufuli kwenye kibubu chetu cha Taifa baada ya Uchaguzi Mkuu uliopita.

Nakumbuka, aliyekuwa mkurugenzi wa jiji hilo wakati huo, Willson Kabwe, alianza mkakati wa kukusanya mapato kwa kuweka nidhamu kwa watumishi na kuondoa uzembe.

Alikuwa anawahi ofisini na kuwadhibiti maofisa wazembe na wachelewaji. Walisaini daftari la mahudhurio ofisini kwake na ilipotimu saa 1:30 walioingia kwa kuchelewa aliwakata mshahara kulingana na siku walizochelewa katika mwezi.

Kwa utaratibu huo hakuna ofisa aliyekubali kuchelewa kazini, walitimua mbio kuwahi bila kujali mwenye cheo au mhudumu wa ofisi, na kazi iliyofuata ni kuwadhibiti wapiga dili na mapato yakaongezeka.

Tangu alipohamishwa kutoka Jiji la Mbeya, sifa za utendaji wa mkurugenzi huyo zilitoweka naye, akazolewa na utawala dhaifu awamu ya nne uliozalisha viongozi, watendaji hadi wafagizi wa ofisi wapiga dili.

Nachelea kuwapongeza na kuwapa sifa mawaziri hawa wa ‘Mr hapa kazi tu’ kwani mbio zao zinaonekana wazi kuwa za sakafuni, wataishiwa na pumzi tu kama huyu jamaa aliyekuwa akiongoza Jiji la Mbeya.