.Adai moto aliowasha hauzimiki mpaka kieleweke 2015

.Asema anaumizwa kuteketea mamilioni Bunge la Katiba

.Atamba ipo siku polisi watazitambua haki za Watanzania

 

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema anashangazwa na vigogo wa Jeshi la Polisi kufanya hila za kumkabili, ilhali wanaona namna Watanzania walivyodhulumiwa haki yao kupitia Bunge Maalum la Katiba.

“Moto wangu wa kudai haki za Watanzania uko palepale mpaka pale polisi watakapoona ninachokifanya ni haki kwa jamii ya Watanzania,” amesema Mbowe alipozungumza na gazeti hili Alhamisi saa 1.30 jioni.

Ilikuwa ni baada ya kiongozi huyo wa Kambi ya Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB), kumaliza shughuli zake ambako siku hiyo pia alihojiwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kutoa maneno ya uchochezi akihamasisha Watanzania kugoma kufanya kazi na kuandamana kupinga kuendelea kwa Bunge Maalum la Katiba.

“Hivi ikitokea siku tutaulizwa! Eeh! kwamba mlifanya nini kuokoa mamilioni ya fedha yanayoteketezwa pale Dodoma kwenye Bunge la Katiba? Tukiwa kama chama kikuu cha upinzani tutajibu nini?” alisema Mbowe, alipozungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam.

Alisema kwamba vyama vya upinzani wa kweli vinapoona mambo hayaendi sawa serikalini, lazima kupaza sauti, na ndicho kinachofanywa sasa na vyama vya upinzani wa kweli, ambavyo kwa sasa vinaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Mbowe alisema kwamba wanachokifanya polisi kwa sasa ni kusikiliza tu amri kutoka kwa wakubwa, lakini Chadema pamoja na washirika wake — Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi, NLD na DP “ni kutetea haki za wananchi.”

“Polisi wanakamata na kuhoji, lakini wanasahau kwamba nyuma yao wako watu wanaowategemea kama vile baba, mama, mke au mume, watoto, kaka au dada ambao si mapolisi…

“…Fedha wanazolipa kodi zinapotea pale Dodoma, hatuwezi kuacha mambo yakiharibika pale na kukaa kimya, tutaendelea kupaza sauti, kupinga anachokifanya Sitta (Samuel) [pale Dodoma],” anasema Mbowe.

Kama ambavyo Mbowe anaungwa mkono na chama chake ambako Ofisa Habari wa chama hicho, Tumaini Makene, ambaye mbali ya kulaani, alisema kwamba ratiba ya maandamano ya chama chake yapo palepale.

Mbowe alisema: “Ipo siku polisi watajua ninachokifanya,” alisema Mbowe, ambaye siku hiyo alipohojiwa, lakini polisi walitumia nguvu za ziada kuwapiga na kuwararua waandishi wa habari waliojitokeza kuripoti kilichokuwa kinajiri kwenye Makao Makuu ya Jeshi hilo.

Polisi waliwapiga waandishi wa habari wakiwa kazini na asasi mbalimbali za kijamii zimejitokeza kulaani vikali na Chadema ikisisitiza kutositisha mpango wao wa kuandamana nchi nzima kupinga kuendelea kwa vikao vya Bunge Maalum la Katiba.

Mbowe alikuwa anahojiwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kutokana na kauli aliyoitoa ya kuitisha maandamano nchi nzima yasiyo na kikomo kupinga kile kinachoendelea bungeni Dodoma.

Wanahabari ambao walipigwa siku hiyo ni Josephat Isango wa Gazeti  Tanzania Daima; Shamimu Ausi wa Gazeti Hoja na Mpigapicha wa magazeti ya Serikali (TSN), Yusuf Badi, ambao walijeruhiwa. Isango alijeruhiwa mguuni na Ausi usoni karibu na jicho.

Waandishi hao wamepigwa ikiwa imepita siku chache tu tangu kufanyika mkutano wa mashauriano kati ya vyombo vya dola na waandishi wa habari wakati Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mohamed Gharib Bilal, aliyeonya vyombo hivyo kufanya kazi kwa kushirikiana bila kukwaruzana kwa lengo la kudumisha amani.

Matamko ya kulaani yametoka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ambako Mwenyekiti wake, Absalom Kibanda, alimtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, kulifumua jeshi hilo na kuliunda upya. Kauli hiyo iliungwa mkono na Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga.

1036 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!