Kama tujuavyo Bunge la Mabadiliko ya Katiba limekumbwa na vurugu na misukosuko kiasi cha kutia aibu Taifa letu.

Nashindwa kusema Bunge hilo liliendelea kujadili Rasimu ya Katiba kwa ukaidi wa nani. Maana wakati wote magenge mbalimbali  ya watu waliendelea kudai Bunge hilo lisitishe shughuli zake, hasa baada ya wabunge wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kususia Bunge hilo.

Japokuwa si rahisi kutaja mambo yote yaliyosababisha Bunge  la Katiba kukumbwa na vurugu na misukosuko, jambo moja  ni wazi. Mchakato wa Katiba haukuandaliwa vizuri au kwa umakini.

Hapa hatuna sababu hata ndogo ya kutilia shaka lengo la Rais Jakaya Kikwete  la kuanzisha mchakato wa katiba. Rais Kikwete alianzisha mchakato wa mabadiliko ya Katiba kwa lengo zuri kabisa la kuwaachia Watanzania Katiba bora ambayo  wangeikubali wananchi walio wengi. Maana hakuna kitu kinachokubalika na watu wote.

Lakini kama yalivyo mambo mengine nchini kwetu Tanzania, malengo yetu ni mazuri wakati wote lakini  utekelezaji ni mbovu wakati wote pia.  Kwa kifupi waliopanga ratiba ya utekelezaji wa mchakato wa Katiba hawakuwa makini, hawakufanya kazi nzuri.

Kwa hiyo, Rais Kikwete hataweza kutuachia  Katiba mpya kama alivyokusudia. Katiba, kama mwongozo wa utawala, ni kitu muhimu sana. Ni sheria mama  au sheria kuu ya nchi.

Lakini haikushughulikiwa kwa umakini ili nchi iwe na utawala bora.

Kwanza kabisa idadi ya watu waliounda Bunge la Katiba ilizidi watu 600. Idadi hii ni kubwa mno  kwa mambo mawili. Kwanza, idadi  kubwa  mno ya wajumbe wa Bunge la Katiba ilisababisha wajumbe wengine kutochangia  mawazo yao juma zima. Kwa kuwa hawakuwa na jambo la kufanya walimaliza  juma zima  wakizomea. Wasingeweza kukaa kimya juma zima.

Pili, wajumbe wa Bunge la Katiba waliokaa kimya wakati wote waliendelea kupokea posho ya shilingi 300,000 kwa siku. Kwa hiyo, tuliendelea kuwalipa  mshahara watu ambao  hawakuwa wafanyakazi. Juu ya yote, idadi kubwa  mno ya wajumbe wa Bunge la Katiba ilisababisha wajumbe wengine kuwa watoro.

Halafu aina ya wajumbe walioteuliwa kuingia kwenye Bunge la Katiba pia ilibidi iangaliwe kwa umakini. Walijaa wanasiasa zaidi kuliko wataalamu. Ni kweli hii si mara ya kwanza kwa nchi yetu Bunge kujadili Katiba ya nchi.  Mwaka 1962 Bunge la Tanganyika lilijadili na kupitisha sheria iliyofanya Tanganyika kuwa Jamhuri yaani nchi inayoongozwa na rais. Tanganyika ikawa Jamhuri  Desemba  9, 1962, Rais  wake akiwa Mwalimu Julius Nyerere.

Mwaka 1965 Bunge la Tanzania lilijadili na kupitisha  sheria iliyofanya Tanzania nchi ya chama kimoja. Tanzania ikaanza kufuata rasmi mfumo wa chama kimoja  Julai 1,1965. Mwaka 1992 Bunge la Tanzania lilijadili na kupitisha sheria iliyorejeshea nchi mfumo wa vyama vingi.  Tanzania ikawa rasmi  nchi ya mfumo wa vyama vingi  kuanzia Julai 1,1992.

Ni vyema tukazingatia kwamba nyakati zote hizo mijadala ndani ya mabunge ya Katiba  iliendeshwa kwa utulivu. Sababu yake moja kubwa ni kwamba Tanzania ilikuwa nchi ya chama kimoja. Kwa hiyo, walikuwa wamoja lakini kulikuwa na kasoro zake.

Kasoro moja kubwa ya Katiba hizo zilizopitishwa wakati wa mfumo wa chama kimoja  ni kwamba wajumbe wa Bunge la Katiba wote  walikuwa wa chama kimoja. Walitumia fursa hiyo  kupitisha mambo ya kujipendelea na ya kulinda maslahi ya chama chao.

Chukua, kwa mfano, Katiba ya Kudumu ya mwaka 1977 tunavyotaka kubadilisha  ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 1992 ili kuruhusu mfumo wa vyama vingi.

Kwanza sheria  ya vyama vingi ilivyotungwa  mwaka 1992  ilizua watu binafsi  kugombea udiwani, ubunge na urais. Pili, sheria hiyo ilikataza Tume ya Uchaguzi kuhojiwa na kufikishwa  mahakamani. Tatu  sheria  hiyo pia ilikataza ushindi wa Rais kuhojiwa  mahakamani. Kwa hiyo, nchi ya Bunge la chama  kimoja mambo yalipita kiulaini kabisa.

Leo mambo ni tofauti, katikati ya mfumo wa vyama vingi  hakuna  Bunge linaloweza kupitisha sheria yoyote kiulaini. Ni muhimu kuzingatia pia kwamba Bunge la vyama vingi wabunge wanatawaliwa zaidi na ushabiki wa kisiasa kuliko maslahi ya Taifa.

Kwa hiyo, Bunge la Katiba lilipoanza Februari 18 mwaka huu,  ilitokea misuguano iliyotokana na  ushabiki wa kisiasa. Lakini baada ya watu wa UKAWA  kususia Bunge hilo  wakidai kuwa walikuwa wanatetea katiba ya wananchi, wabunge wa chama tawala walitumia nafasi hiyo kupitisha mambo ya kujipendelea na kujiandalia mazingira ya  kuendelea kuwa  wabunge bila kubughudhiwa.

Kwa hiyo, walifuta kipengele katika  Rasimu  ya Katiba kilichotaka wapiga kura wamwajibishe mbunge asiyefaa wakati wowote hata kabla ya uchaguzi. Wametaka pia ubunge usiwe na kikomo baada ya Rasimu  ya Katiba kutaka mtu aliyewahi kuwa mbunge  kwa vipindi vitatu vya miaka mitano mitano asigombee tena ubunge.

Wajumbe wa chama tawala wanataka  ubunge uwe ajira  yao ya maisha, wanataka wafe na ubunge! Basi ili kupata Katiba bora isiyopendelea chama  chochote cha siasa, ilitakiwa Katiba ijadiliwe na kupitishwa na wataalamu ambao si wanasiasa na ambao si mashabiki  wa vyama vya siasa  moja kwa moja.

Ilitakiwa wajumbe wa Bunge wawe  mawakili wa Serikali na mawakili wa kujitegemea. Hao wangeweza kutuletea Katiba bora isiyotegemea upande wowote. Wala tusingehitaji kupata kura ya maoni.

Kasoro nyingine iliyojitokeza katika  mchakato wa Katiba ya Tanzania ni ratiba ya mchakato huo kukosa kutoa nafasi  kwa wajumbe wa Katiba kufanyiwa semina nzuri elekezi. Chukua, kwa mfano, ukurasa wa kwanza kabisa  wa Rasimu ya Katiba kuna taarifa iliyotolewa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Januari 22, 2014. Taarifa hiyo inasomeka ifuatavyo:-

Toleo hili la Rasimu  ya Katiba (la pili) linachapishwa kwenye Gazeti  la Serikali kwa mujibu wa kifungu cha 20 (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, sura ya 83, na itawasilishwa kwenye Bunge  Maalum la Katiba, kwa ajili ya KUJADILIWA NA KUPITISHWA.”

Kama wajumbe wa Bunge la Katiba wangeelimishwa vya kutosha kwamba  Bunge lilikuwa ilimeitwa ili  kujadili na kupitisha Rasimu ya Katiba, huenda  watu wa UKAWA wasingesusia Bunge kwa madai kwamba walikuwa wanatetea katiba  ya wananchi. Walishindwa kuelewa  mambo mawili.

Kwanza, kwamba Bunge halikuitwa kwa lengo la kupitisha kila kitu moja kwa moja bila kujadiliwa. Shughuli ya kwanza ya Bunge ilikuwa kujadili. Na katika kujadili kwa uadilifu mkubwa kwa maslahi ya Taifa hakukosekani  kukuta maeneo ya kuongeza  au kurekebisha kabla ya kupitishwa kuwa sheria.

Kwa maana hiyo kama wajumbe wa UKAWA  na Jaji mstaafu Joseph Warioba  wangezingatia kuwa Bunge halikuitishwa  kwa lengo la kupitisha moja kwa moja  maoni ya wananchi bila kujadiliwa,  wasingelalamikia kuongezwa au kurekebishwa  maeneo mbalimbali ya katiba.

Pia wangejua kuwa halikuwa jukumu la Bunge  kutoa Katiba ya wananchi moja kwa  moja. Katiba ya wananchi  ingepatikana baada ya wananchi kupiga kura ya maoni.

Huko nyuma nimedokeza kwamba Rasimu ya Katiba ilipaswa kujadiliwa kwa uadilifu mkubwa na kwa maslahi ya Taifa, ukweli ni kwamba baada ya wajumbe  wa UKAWA kususia Bunge  la Katiba wajumbe wa chama  tawala hawakujadili Rasimu ya Katiba kwa uadilifu mkubwa na kwa maslahi ya Taifa.

Kuna uadilifu gani mnapotaka msiwajibishwe na wapiga kura  na mnapojiongezea miaka saba ya kuendelea na ubunge? Na tangu lini  kujipendelea kumekuwa  sehemu ya uwadilifu?

Halafu  tuangalie suala la kura ya maoni. Wenzetu hawawezi kuitisha kura ya maoni na mambo ambayo ni mchanganyiko wa mambo mengi, wanaitisha kura ya maoni  ya kukubali au kukataa jambo moja.

Kwa mfano, ukiitisha kura ya maoni  ya kuwataka wananchi  waamue kama wanataka muungano au hawataki ni sawa kabisa. Hilo ni jambo moja. Kadhalika ukiitisha kura ya maoni  ya  kuwataka wananchi waamue kama  wanataka Serikali mbili  au tatu ni sawa. Hilo pia ni jambo moja.

Lakini si sahihi  kuitisha kura ya maoni  inayowataka wananchi  waamue suala la muungano, idadi ya Serikali, madaraka ya Rais, maadili ya uongozi  na utumishi  wa umma, miiko ya uongozi wa umma, haki za binadamu, wajibu wa raia, wajibu ya mamlaka ya nchi, uraia katika Jamhuri ya muungano, madaraka ya Bunge, madaraka ya mahakama na kadhalika.

Mambo yote haya hayakuhitaji kupigiwa kura isipokuwa kama kutakuwa na kijitabu ambacho kitakuwa na vifungu ambavyo mpiga kura atatakiwa kuandika NDIYO au HAPANA au vinginevyo.

Huwezi kumtaka mtu apige kura moja kwa jambo fulani ambalo ni mchanganyiko wa mambo mengi tofauti. Unataka akubali au akatae yote kwa mpigo?

Halafu kuna jambo lingine ambalo waliomba ratiba ya mchakato wa Katiba hawakuliona jambo hilo ni hili hawakupanga Bunge la Katiba lingefika mwisho namna gani. Matokeo yake baadhi ya watu walimtaka Rais asitishe Bunge ilidhihirika kuwa Rais hakupewa madaraka hayo.

Ni katika mazingira hayo yote tunaweza kukubaliana kwamba mchakato wa Katiba haukuandaliwa kwa ufanisi. Nani anabisha?

1206 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!