Mpunga unapotaka kuupata mchele wake lazima uutwange. Kamwe usitarajie kupata mchele bila ya chuya na chenga baada ya kutoa pumba. Vyama vyetu vya siasa vinafanana na mpunga. Iwe CCM, CUF, ACT-Wazalendo, TLP, Chadema na kadhalika vina mchele, chuya na chenga. Kwa vipi?

Maneno hayo niliyatamka wiki iliyopita na leo narudia kuyatamka nikiwa na madhumuni ya kuweka msisitizo si katika mpunga kupata mchele, chuya na chenga, hapana. Ni katika vyama vya siasa nchini mwetu ambako tunapata wanachama na viongozi mithili ya mchele, chuya na chenga.

Chama cha siasa ni kama nafaka ya mpunga. Chama hicho kiwe maarufu au la. Kinaposhamiri na kutikisa nchi katika itikadi, falsafa na sera zake, kinabeba na kukumbatia wanachama walio katika makundi matatu. Makundi hayo nayafananisha na mchele, chuya na chenga baada ya kupata elimu ya siasa na itikadi ya chama.

Ndani ya chama cha siasa kuna wanachama wa ukweli na wanaoamini na kuzingatia itikadi ya chama chao. Wanachama hawa huwa ndiyo viongozi waaminifu na bora wanaoieleza na kuitetea itikadi na falsafa ya chama chao. Kauli na vitendo vyao havina dosari zaidi ya upendo, amani na uongozi bora. Asili yake ni mafundisho ya chama.

Hili ndilo kundi ninalolifananisha na mchele safi uliopatikana baada ya mpunga kutwangwa ndani ya kinu na kupatikana pia pumba, chuya na chenga. Pumba hutupwa. Mchele hutumika kwa mapishi aina aina iwe ubwabwa, wali, pilau au biriani.

Katika kupata wanachama safi (mchele) bado hupatikana wanachama ndume (chuya) ambao kwa mtazamo wa haraka utaamini wapo safi kumbe sivyo. Mafunzo ya itikadi na falsafa waliyopata ndani ya chama ni bure.

Wanachama hawa hupenda sana madaraka (uongozi) na hujifanya wanyenyekevu, wakarimu na wacheshi, kumbe ni walaghai. Wao hupenda sana kuwa karibu na wanachama safi katika kila shughuli za chama. Ni sawa na tabia ya chuya kuwa karibu na mchele. Haitoki mpaka ichaguliwe na kutupwa na muhitaji wa mchele safi.

Kundi la pili ni la wanachama ndume (chuya) Hawa wasipopata mahitaji yao (mamlaka na fedha) huwa tayari kusaliti na hata kuhama chama, huku wakilalama kila mahala wameonewa, wamedhalilishwa na wamefedheheshwa. Hawa si watu wema hata chembe. Watu hatari katika chama. Chuya (ndume) huharibu mapishi na ladha ya chakula.

Kundi la tatu ni la wanachama chenga. Hawa si wakweli wa kauli wala wa vitendo kwa chama chao cha siasa. Ni wachache lakini ni wakorofi. Ni wadogo wa madaraka na wengine ni waupe pe. Lakini ni watu hatari. Wachonganishi na mashabiki wa mambo. Walitakalo hulifanya.

Chenga hupoteza sanaa ya upishi na ladha ya chakula – wali, pilau na biriani. Lakini chenga hizo hufaa kwa matumizi ya kuchoma vitumbua na aina nyingine ya kuoka mikate. Wanachama chenga katika chama huwa mstari wa mbele kuhamasisha na kupambisha mambo ya chama mbele ya vyama vingine vya siasa.

Nasema ndani ya vyama vyetu vya siasa hapa nchini tuna wanachama na viongozi mithili ya mchele safi. Tuna wanachama na viongozi mithili ya chuya na tuna wanachama na viongozi mithili ya chenga. Mchanganyiko huu kwa wanasiasa una mushkeli na ndiyo maana mara kwa mara migongano ya kisiasa hutokea na watu kufarakana.

Angalia matukio yanayotokea katika vyama vya CUF, Chadema, CCM, ACT-Wazalendo na fukuto la joto linalotokea katika chama cha NCCR-Mageuzi. Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wameliona hilo na wameanza kushughulikia ili kuweka chama sawa.

CCM wanafanya mabadiliko. Chadema wanatahadharisha wanachama na viongozi wafanye kazi na kuhoji wakiwa na ‘evidence’ na hoja kuntu, wasiwe watu wa mahakamani kwa makosa ya kuropoka jukwaani na mitandaoni – huu ni muda wa kazi. Vyama hivyo vimejitambua na kujikosoa.

CUF mjitazame kwa mapana na marefu yake juu ya yale ya uanachama na uongozi wenu hauna mchele, chuya na chenga?  Kama hauna vipi mgawane ofisi, mkimbiane kama paka na panya, mpigane mahakamani ilhali mnashindwa kutimiza ahadi zenu kwa wanachama kushika madaraka ya nchi? Vipi msiungane baada ya kufanyiana usaliti ndani ya chama?

Vyama ambavyo sikuvitaja vijitazame pia na kuanza kujitakasa na kujiweka sawa. Huu ndiyo wakati mzuri wa kuvisafisha vyama kwa kufanya mikutano ya ndani ambayo inaboresha utendaji wa kazi za chama. Namalizia kwa kuvitakia vyama vyote vya siasa na wasomaji wa makala za FASIHI FASAHA heri na fanaka ya Mwaka Mpya wa 2017.

By Jamhuri