Kuwafundisha watoto kumcha Mungu ni dhana nzuri inayowajenga katika maadili ya kuwawezesha kufanikiwa maishani, amesema Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Dk. Reginald Mengi.

Amefafanua kwamba kumcha Mungu kunamfanya mtoto kuwa mwema, mkweli na mwaminifu, tabia ambazo ni nyenzo muhimu katika kufikia mafanikio ya kiuchumi na kijamii.

“Ni jambo la msingi kwa mzazi kumwandaa mtoto aweze kufanikiwa maishani. Kumfundisha mtoto amweke mbele Mwenyezi Mungu kutamfanya awe mnyenyekevu, mkweli na mwaminifu ili hata akikopa arudishe, maana hakuna anayetaka kufanya biashara na mtu mwongo na anayejivuna,” amesisitiza.

Dk. Mengi ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, katika hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa shindano la Tweet na Mengi kwa mwezi uliopita. Alianza kudhamini shindano hilo Juni, mwaka jana.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti Mtendaji huyo wa IPP, wazazi pia wanapaswa kuwafundisha watoto kujenga tabia ya kujiendeleza kwa kupata mawazo ya wengine badala ya kujiamini kwamba wanajua kila kitu.

Wakati huo huo, Dk. Mengi amewahimiza vijana kuwa na macho yanayoona fursa za ajira, badala ya kuishia kulalamika na kusubiri kuajiriwa na Serikali.

“Mimi ninaamini fursa za ajira zipo ila watu wengi wanakosa macho ya kuziona. Ukosefu wa ajira utapungua kama tutakuwa na macho yanayoona fursa za shughuli mbalimbali.

“Lakini pia watu waache kuogopa na kubagua kazi. Jiamini kuwa unaweza. Mwenyezi Mungu hawezi kukuleta halafu akwambie huwezi. Kusema kwamba huwezi unamkosea Mungu, ni dhambi,” amesema Dk. Mengi.

Katika hafla hiyo, Abnery Mwogela aliibukwa mshindi wa kwanza wa mashindano hayo na kuzawadiwa Sh milioni moja, akifuatiwa na Shilla Samson aliyezawadiwa Sh 500,000 na Gerald  Nyaissa aliyepata Sh 300,000.

Swali la “tweet” bora la Aprili, mwaka huu liliuliza; “Mzazi afanye nini kumwandaa mtoto kufanikiwa kiuchumi?”

Mwogela alijibu swali hilo kwa kusema, “Mzazi amwandae mwanaye kuishi kwa kujiamini, kuthubutu, kuanza kufanya anachodhani ni vema akifanye kwa wakati huo kiuchumi.”

Mshindi wa pili, Samson, alijibu “Mzazi amwandae mtoto katika mambo makuu manne; elimu, kupenda kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na kupenda kumcha Mungu.”

Kwa upande wake, mshindi wa tatu, Nyaissa, alisema “Kila siku mzazi mnong’oneze mwanao; “Mungu anawapa matajiri saa 24 kwa siku sawa na anazokupa wewe. Zitumie saa hizo kwa taifa.”

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utawala na Ujasiriamali, Dk. Donath Olomi, alitaja swali la mwisho linaloshindaniwa Mei, mwaka huu kuwa linasema, “Eleza ulivyotumia ama utakavyotumia wazo lako/la wengine lililotolewa katika mashindano haya kujijenga kiuchumi.”

Lengo la Dk. Mengi kuanzisha mashindano hayo ni kupata mawazo bora yanayoweza kusaidia wananchi kujijenga kiuchumi na kupunguza umaskini miongoni mwao.

Vigezo vinavyotumika kupata washindi ni upya wa wazo, uwezekano wa kutekelezeka katika mazingira ya hapa Tanzania na jinsi lilivyoelezwa kwa ufasaha.

Mwisho wa shindano hilo unatoa nafasi ya uandaaji wa kitabu kitakachokuwa na mawazo bora yaliyoshinda kwenye shindano la Tweet na Mengi, utakaodhaminiwa na Dk. Mengi ili kuwapa Watanzania fursa ya kuyasoma na kuyatumia katika kubuni na kuanzisha miradi ya kujijenga

By Jamhuri