• Mabishano, matusi vyakwamisha kikao
  • Polisi washindwa, Meya atumia mabaunsa

Ni dhahiri kuwa sasa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza hapakaliki. Mgogoro baina ya Meya Henry Matata na madiwani watatu aliowafukuza, unazidi kufukuta na kuhatarisha maendeleo ya wananchi.

Katika tukio lisilo la kawaida, Meya huyo na madiwani Marietha Chenyenge wa Kata ya Ilemela, na Abubakar Kapera wa Kata ya Nyamanoro (Chadema), walipimana nguvu kwa mabishano yaliyohusisha matusi ya nguoni na kukwamisha kikao cha Baraza la Madiwani, kilichokuwa kimeandaliwa kujadili mipango ya maendeleo ya wananchi.

Tukio hilo lilijiri kwenye ukumbi wa mikutano wa manispaa hiyo, Jumanne iliyopita, baada ya Chenyenge na Kapera kuvamia na kulazimisha kushiriki kikao kama madiwani halali.

Kitendo hicho kilimkasirisha Matata na kumlazimu kuomba msaada wa askari polisi kuwaondoa madiwani hao, waliokuwa tayari wamevaa majoho (sare) husika na kuketi vitini kwa kujichanganya na madiwani wengine kadhaa ukumbini.

Hata hivyo, askari polisi aliyeitwa hakuweza kuwatoa madiwani hao ukumbini zaidi ya kutaka busara itumike kuepusha malumbano zaidi baina ya Meya na madiwani hao.


Huku akionekana kuhamaki, Matata alisema madiwani hao hawana uhalali wa kushiriki kikao kama madiwani, kwani alishawafukuza pamoja na Diwani wa Kirumba, Dany Kahungu, kutokana na kosa la kutohudhuria vikao vitatu mfululizo vya Baraza la Madiwani bila taarifa.


Meya ambaye ni Diwani wa Kata ya Kitangiri kwa tiketi ya Chadema, alisema kifungu namba 18 cha Kanuni za Halmashauri za Manispaa, kinampa mamlaka ya kuamuru kuondolewa kwa watu wanaofanya vurugu katika kikao anachokiongoza.

Hata hivyo, baada ya kuona askari polisi anakuwa mzito kuchukua hatua ya kuwaondoa madiwani hao ukumbini, Matata alitishia kuita mabaunsa wake watekeleze amri yake hiyo bila kusita.


Kwa upande wao, Chenyenge na Kapera walisema wamelazimika kuhudhuria kikao hicho bila mwaliko baada ya kuona wamesimamishwa udiwani kwa muda wa miezi tisa kinyume cha kanuni za uendeshaji wa Serikali za Mitaa.


“Tuambie kwanini sisi si madiwani, mwambie Pinda [Waziri Mkuu, Mizengo Pinda] aje atutoe, kwani ndiye amesema turudi tuwakilishe wananchi,” Chenyenge alimjibu Meya Matata.


Matata alijibu kauli hiyo ya Chenyenge kwa kusema, “Halafu hata askari [polisi] wakishindwa mabaunsa watawatoa na kuwatupa nje.”


Kwa mujibu wa madiwani hao, kitendo cha Meya kuwafukuza udiwani kimesababisha shughuli za maendeleo ya wananchi kukwama katika kata zao, kutokana na kukosa usimamizi wao. Walimshutumu Meya wakidai ameigeuza Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kuwa mali yake binafsi na kwamba amekuwa kinara wa kufukuza madiwani na watumishi katika manispaa hiyo.


Walalamikia kitendo cha mamlaka husika kushindwa kuchukua hatua ya kuitisha uchaguzi mdogo wa kata za Ilemela, Nyamanoro na Kirumba kama imeshindikana kuwarejeshea udiwani.


Kapera alimtupia lawama Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akimtuhumu kwamba ameshindwa kuingilia kati kupata ufumbuzi wa mgogoro huo.


Chenyenge yeye alisisitiza kwamba kwa kuwa Serikali imeshindwa kuingilia kati mgogoro huo, ataendelea kushirikiana na wenzake kuhudhuria vikao vya Baraza la Madiwani mpaka kieleweke.


Diwani wa Kata ya Pasiansi, Rose Brown, nusura anunue ugomvi baada ya kumkaripia Meya kutokana na kitendo cha kutoa matusi ya nguoni dhidi ya Chenyenge.


“Wewe mbona una kiherehere sana? Mimi sina ugomvi na wewe. Nina ugomvi na madiwani niliowafukuza pamoja na uongozi wa Chadema Taifa,” Matata alimjibu Brown.


Baada ya mabishano yaliyodumu kwa takriban nusu saa, Meya alisimama na kutamka maneno ya kufungua kikao hicho, huku akirejea kanuni za kudhibiti vurugu vikaoni na muda huo huo akatamka maneno ya kukiahirisha.


“Ninatamka kwamba kikao hiki kimefunguliwa. Kifungu namba 18 cha Kanuni za Halmashauri kinanipa mamlaka ya kuamuru watu wanaofanya vurugu kikaoni waondolewe ukumbini.


“Baada ya kusema hayo kikao hiki kimeahirishwa rasmi na tumeona hakuna chombo cha Serikali kinachotulinda,” alisema Matata na kuondoka ukumbini.


Katika mahojiano na JAMHURI ofisini kwake, Meya Matata aliwashutumu askari polisi akidai walichangia kukwamisha kikao hicho kwa kushindwa kuwaondoa madiwani waliokivamia.


“Polisi walionekana kuwa wazito. Walitakiwa wawatoe madiwani wale ukumbini. Kuahirisha kikao ni hatari kwa maendeleo ya wananchi,” alisema Matata na kuendelea:


“Polisi wameshindwa kazi, lakini sitakubali kuona polisi wanaendelea kushindwa kazi siku zote kikaoni, kwani mimi pia nitaleta mabaunsa wangu watakaokuwa wanakaa ndani (kikaoni).


Alipoulizwa sababu za yeye kutoa matusi ya nguoni dhidi ya Diwani Chenyenge, Matata alisema,

 

“Polisi walaumiwe kuruhusu tukatukanana na fujo vikaoni.”


JAMHURI ilipohoji sababu ya kujiandalia kundi la mabaunsa kwa ajili ya ulinzi binafsi na kuwapeleka katika jengo la ofisi za manispaa, Matata alisema:


“Mabaunsa wakija watatusaidia, hawaji kupiga watu, watakuja kutoa watu wanaofanya fujo kwa sababu polisi wameshindwa. Mwafaka wa suala hili ni kuweka mabaunsa.”


Alipotakiwa kueleza uelewa wake kuhusu mgogoro huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Francis Damian, alisema suala lao linashughulikiwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, na kwamba madiwani waliofukuzwa hawakutakiwa kushiriki kikao hicho.


Damian alisema kutokana na vurugu zilizojitokeza, ofisi yake haitalipa posho iliyokuwa imeandaliwa kwa ajili ya wajumbe wa kikao hicho.


Alisema vurugu zimempa changamoto ya kushirikiana na viongozi wengine kujipanga kuhakikisha usalama unatawala katika vikao vijavyo.


Kuhusu kundi la mabaunsa linalotangazwa na Meya, Damian alisema; “Siyo utaratibu kuweka mabaunsa kulinda usalama hapa Manispaa.”


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ernest Mangu, alipoulizwa suala la askari polisi kushindwa kutuliza vurugu katika kikao hicho, na kitendo cha Matata kupeleka mabaunsa wake katika manispaa, alisema; “Mimi siko huko, niko Dar es Salaam, muulize RCO (Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa).” Hata hivyo, RCO hakupatikana kuzungumzia suala hilo.


Mkuu wa Operesheni za Chadema Kanda ya Ziwa, Tungalaza Njungu, aliiambia JAMHURI kwamba bado Chadema inatambua uhalali wa madiwani waliofukuzwa na Meya na kwamba wana haki ya kuhudhuria vikao vya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kuwakilisha wananchi.


“Tutatumia sheria kushughulikia suala hili na tutatumia mikutano ya hadhara kuishitaki Serikali kwa wananchi,” alisema Njungu.


Awali Diwani wa Kata ya Kirumba, Dany Kahungu (Chadema), alifuatana na madiwani wenzake, Chenyenge na Kapera kwa ajili ya kushiriki kikao hicho, lakini alipopata taarifa za uwepo wa askari polisi na mabaunsa wa Meya aliondoka eneo la Manispaa kukwepa shari.


 

By Jamhuri