Mfanyabiashara Steven Buhanza anailalamikia Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, kwa kile anachodai imeuza shehena ya mbao zake ilhali kesi ikiwa haijatolewa uamuzi.

Buhanza, mmiliki wa Kampuni ya Ntiyonza Company Limited ya Dar es Salaam, alikamatwa Oktoba 30, 2012 wilayani Tunduru, akituhumiwa kuingiza nchini mbao zenye thamani ya Sh milioni 87.5; ingawa yeye mwenyewe anasema thamani halisi ni Sh milioni 154.

Anasema alikamatwa licha ya kuwa na nyaraka zote halali zinazomruhusu kufanya biashara hiyo.

“Mahakama ya Wilaya ilinitia hatiani, lakini nilipokata rufaa katika Mahakama Kuu Kanda ya Songea hukumu ilitenguliwa kwa sababu jaji aliona mwenendo wake haukuwa sahihi. Akaamuru kesi irejeshwe Mahakama ya Wilaya kwa ajili ya kuanza kusikilizwa upya.

“Wakati wote huo shehena ya mbao zangu ilikuwa bado ipo, lakini nashangaa kesi ikiwa imeanza upya, mbao zote zineuzwa,” anasema Buhanza.

 

Mambo yalivyokuwa

Buhanza anasema alishitakiwa katika Mahakama ya Wilaya ya Tunduru katika kesi Na. 168/2012 kwa makosa matatu ya kughushi nyaraka, kuwasilisha nyaraka za kughushi na kukutwa na mbao bila kibali halali.

“Kesi ilisikilizwa hadi hatua ya utetezi, Hakimu Mkazi Nyalanda aliyekuwa akisikiliza akafariki dunia. Akaletwa mwingine ambaye akatoa hukumu ya kwanza na kunitia hatiani kifungo cha miaka miwili jela.

“Nikakata rufaa katika Mahakama Kuu Songea. Mahakama Kuu ikapitia kesi na Desemba 31, 2015 Jaji Chikoyo aliona upungufu mkubwa kwenye uendeshaji wa shauri. Akabaini vipengele vya sheria havikuzingatiwa. Akafuta hukumu, akafuta mwenendo mzima wa kesi. Akaamuru kesi irudi Mahakama ya Tunuru kwa hakimu mpya.

“Wakati huo hadi Januari 2016 mbao zote 2,317 zilikuwa zipo pamoja na za washitakiwa wengine.

“Shauri likarudi Mahakama ya Wilaya kwa Hakimu Mkazi Barthy na kupewa namba 9/2016.

“Shauri limeendelea kusomwa bila wakili wa Serikali kufika mahakamani, lakini akafika Januari 14, 2016. Aliyefika ni Wakili Mfadhiwi wa Serikali anayeitwa Mkude. Mashitaka yakasomwa na nikapata dhamana.

“Wakatakiwa mashahidi, hawakuwapo. Kesi ikapangwa Machi 31, 2016. Siku hiyo Mahakama ikafuta mashitaka, lakini wakati natoka nje ya Mahakama nikakamatwa tena na kuwekwa rumande.

“Siku iliyofuata nikafikishwa mahakamani na kufunguliwa kesi ya jinai Na. 38/2016 wakati ukweli ni kuwa Mahakama Kuu iliamuru kesi isikilizwe upya.”

Buhanza anasema wakati akifunguliwa kesi hiyo ya tatu, Serikali Wilaya ya Tunduru ikaamua kutaifisha mbao zake na kuzitumia kutengeneza madawati.

Alipoulizwa alijuaje mbao hizo zilitumika kutengeneza madawati, Buhanza aliionesha JAMHURI nakala ya barua iliyoandikwa na Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tunduru, Agnes Hokororo, ya Februari 13, mwaka huu kwenda kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Tina Sekambo.

Katika barua hiyo, DC alikuwa akihimiza utengenezaji madawati katika kata za Mlingoti Mashariki, Nanjoka, Majengo, Mchangani na Nakayaya.

Buhanza anasema kinachomsumbua sasa ni kuwa kutokana na uamuzi wa kuuzwa kwa mbao zake, ni kama viongozi wa Serikali katika Wilaya ya Tunduru wanajua hukumu itakayotolewa.

“Nina imani kubwa na Mahakama, lakini kwanini mbao zangu ziuzwe wakati Mahakama bado inaendelea kusikiliza kesi? Je, wao tayari wanajua matokeo ya kesi? Mbao si kitu cha kuoza kama vizibiti vingine, kulikuwa na sababu gani ya kuuza mbao wakati kesi ikiwa haijatolewa uamuzi?” Anahoji.

Anasema asingeweza kuwa na shaka kama uamuzi huo ungekuwa umetolewa na Mahakama, lakini chombo hicho cha utoaji haki hadi mbao zinauzwa kilikuwa hakijatoa uamuzi wa aina yoyote.

“Hizi mbao nilizipata kihalali, zilikuwa na nyundo halali, sasa kama zimeuzwa si ina maana ushahidi umepotezwa? Kwanini hazikuachwa zitumike kama kielelezo hadi kesi itakapoisha? Hukumu ya kwanza ilisema zitaifishwe, lakini Mahakama Kuu ikatengua uamuzi huo na ndiyo maana niliamini Serikali ingeendelea kuheshimu uamuzi wa Mahakama hadi hapo kesi iliyo mbele itakapomalizika,” anasema Buhanza.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tunduru, Sekambo, ameulizwa na JAMHURI na kusema hana taarifa ya kukamatwa na hatimaye kutaifishwa kwa mbao hizo.

“Mimi sina taarifa, mtafute DC, mimi siwezi kukumbuka kwa sababu maelekezo ninayopewa ni mengi kwa hiyo siwezi kukumbuka. Nafikiri ni vizuri ukamtafuta DC ukaongea naye,” amesema.

DC Hokororo hakuweza kupatikana baada ya kupewa taarifa kuwa yuko likizo.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Tunduru ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Chande Nalicho, alipoulizwa na JAMHURI, alijibu kuwa mwenye kuweza kulizungumza jambo hilo ni Katibu Tawala wa Wilaya  (DAS) ya Tunduru, Lingo Ghaid.

Kwa upande wake, Ghaid, alipoulizwa hakutaka kuingia kwenye undani wa suala hilo akisema kufanya hivyo ni kuheshimu shauri ambalo lipo mahakamani.

“Kitu kikiwa mahakamani wengine hatuzungumzi mpaka kiishe, lakini mbao hizi ni za mwaka sijui 2011 (kesi ni ya mwaka 2012), kwa hiyo kuna mambo mengi yamejitokeza hapo.

“Kesi ilipoisha walikata rufaa, yupo huyo (Buhanza) na wengine sijui sita; walitiwa hatiani, lakini katika rufaa ikaonekana mtiririko wa hukumu haukwenda sawa. Makakama Kuu ikaamuru kesi irudiwe upya katika Mahakama ile ile. Hadi sasa siwezi sema zaidi kwa sababu kesi ipo mahakamani.

“Hizo mbao michakato ni mingi, zipo wanazopewa Magereza na sasa sijui yupi yupi na kipi ni kipi,” anasema.

Ghaid anahitimisha kwa kuthibitisha kuwa mbao zinazodaiwa na Buhanza kwamba zimeuzwa, si kweli.

“Mimi nasema zipo, in which quantity (kwa idadi gani) sijui, hizo ni support evidence kwa hiyo zipo,” anasema.

Lakini kwa upande wake, Buhanza anasema mbao hazipo kwani tayari zilishatumiwa kutengeneza madawati kama ilivyoamuriwa na DC Hokororo.

1636 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!