Moja ya hukumu murua kabisa kutolewa na mahakama ya juu kabisa nchini Kenya hivi karibuni, inahusu Mfuko wa Jimbo kwa kutamka pasipo kumung’unya maneno kuwa ni haramu kwa mbunge kugeuka mtendaji wa fedha za umma.

Majaji wa Mahakama ya Rufaa ya Kenya wametamka kuwa Sheria ya Mfuko wa Jimbo (Constituency Development Fund Act), ya mwaka 2003 inakiuka Katiba ya nchi ambayo imeweka mipaka ya madaraka kwa mihimili mitatu ya dola; yaani Serikali, Bunge na Mahakama.

Majaji wote (rejea Daily Nation Novemba 25, 2017) wakatangaza kuwa mbunge hapaswi kufanya kazi za utendaji kwa kuendesha pesa za mfuko wa jimbo. Hilo ni jukumu la mhimili mwingine wa dola- Serikali.

Kwa uamuzi huo wa Mahakama, wabunge wamepokwa majukumu ya kusimamia fedha za Mfuko wa Jimbo ambazo zimerejeshwa kwa Serikali za Mitaa.

Itakumbukwa kuwa Bunge la Tanzania kwa kuiga Sheria ya Mfumo wa Jimbo ya Kenya, mwaka 2009 lilipitisha Sheria ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Jimbo licha ya kupingwa vikali mashirika ya hiari kwamba sheria hiyo ilikuwa inakwenda kinyume cha matakwa ya Katiba inayoweka mipaka ya dhima miongoni mwa mihimili mitatu  ya dola – Serikali, Bunge na Mahakama.

Rais mstaafu, Jakaya Kikwete aliridhia sheria hiyo kwa madai kwamba itawasaidia wabunge kuondoa kero za wananchi. Lakini, wanaharakati walikwenda mbali kwa kudai kuwa licha ya kukiuka Katiba, Sheria ya Mfuko wa Jimbo ilikuwa inahalalisha ubaguzi wa kisiasa na kuchochea rushwa kwani kwa silika ya mwanasiasa, atatumia mfuko huo kujikweza yeye mwenyewe na chama chake mbele ya wapigakura na wakati huo huo kuwatenga wapinzani wake ndani na nje ya chama.

Mantiki ya kutenganisha majukumu hayo ni kuona kuwa shughuli za kiutendaji zinafanywa na Serikali wakati Bunge linatunga sheria na kuisimamia Serikali. Kwa upande wake Mahakama imepewa jukumu la kutafsiri sheria.

Mbunge anapogeuka kuwa mtendaji maana yake ni kwamba anaacha jukumu la kuisimamia na kuiwajibisha Serikali kwa niaba ya wananchi na badala yake anaingia jikoni mwenyewe.

Lakini vibaya zaidi, ni ule ukweli kwamba Sheria ya Mfuko wa Jimbo inajenga tashwira ya ubaguzi na upendeleo. Mfano mzuri umeelezwa na mwandishi Joe Khamis katika kitabu chake cha The Great Political Betrayal (Usaliti Mkubwa wa Kisiasa) kwa kutolea mfano wa Kenya.

Khamis aliyepata kuwa Mbunge wa Jimbo la Bahari nchini Kenya, anatoa mfano wa mbunge wa moja ya majimbo maskini sana yaliyoko kaskazini mashariki mwa Kenya.

Kwa kutumia Mfumo wa Jimbo, mbunge huyo alianzisha kampuni yake binafsi ya ujenzi na kuipa kandarasi ya kujenga barabara zote katika jimbo lake. Akaanzisha kampuni nyingine na kuipa zabuni ya kusambaza vifaa vya elimu kwenye shule za umma katika jimbo. Zaida ya hapo akaanzisha kampuni nyingine nayo akaipatia zabuni ya kushona sare za wanafunzi na watumishi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati. Vile vile akaanzisha kampuni ya kusambaza vyakula na kuipa zabuni ya kuhudumia shule zote za bweni na kutwa.

Kwa staili hii, karibu shughuli zote za kiuchumi zikawa mikononi mwake. Hatma ya jimbo ikawa kwake. Mbunge akatoa ajira kwa watu wengi na umaarufu wake ukazidi. Lakini ikizingatiwa kwamba Kenya ni nchi ya ukabila, waliofaidika na ajiri hiyo ni wale tu wa kabila lake na kisha wanachama na wafuasi wa chama chake.

Tafsiri ya kisiasa hapa ni kwamba, mbunge huyo alitumia fedha za Serikali kujijengea uhalali wa kisiasa wa kuchaguliwa tena na tena kutokana na kutoa ajira. Hakuna namna ambayo raia mwingine angeweza kushindana na mbunge huyu wakati wa uchaguzi. Hali kadhalika, kwa kutumia fedha za umma, mbunge alikijengea chama chake uhalali wa kuchaguliwa dhidi ya vyama vingine. Kama hiyo haitoshi, mbunge huyu aligeuka mtendaji badala ya kuwa mdhibiti wa fedha za umma. Ndio maana rushwa imetamalaki nchini Kenya!

Tahadhari kama hizo ndizo zilizotolewa na wanaharakati wa Tanzania wakati wa kupinga uanzishwaji Sheria ya Mfuko wa Jimbo pasipo mafanikio.

Uzoefu katika nchi mbalimbali umeonyesha kuwa matumizi ya mifuko hii, hugubikwa na ushawishi mkubwa wa wabunge ambao huwa na sauti kubwa ya jinsi na namna ya kugawa fedha kwenye miradi.

Wakati fedha za Mfuko wa Jimbo nchini Tanzania huingizwa kwenye akaunti ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya jiji, manispaa, mji au wilaya husika, mambo ni tofauti huko Kenya. Nchini Kenya fedha za Mfuko wa Jimbo hutumwa moja kwa moja kwenye akaunti ya mbunge. Hali ni hiyo hiyo huko Uganda na hata Visiwani Zanzibar ambako pia Baraza la Wawakilishi lilipitisha Sheria ya Mfuko wa Jimbo.

Washawishi wa utawala bora, wanasema ni makosa kwa wabunge kujiingiza katika uendeshaji wa fedha za miradi ya maendeleo na kuacha dhima ya kuisimamia na kuiwajibisha Serikali.

Mno zaidi ni kwa mbunge anapotengewa fedha azitumie kisiasa inaua maana nzima ya utawala wa bora, uwazi, uwajibikaji na kugawana madaraka. Uzoefu kutoka katika nchi zenye mifuko hiyo kuanzia Ghana, Uganda, Zambia hadi Nigeria unaonyesha kuwa  wanachofanya wabunge ni kuzielekeza fedha hizo kwenye miradi iliyoko maeneo yale ambayo wao na vyama vyao wanakubalika. Maeneo ambayo hawapendwi huambulia patupu. Njia nyingine, ni kutumia fedha hizo kuwarubuni wapinzani wao ndani na nje ili wawaangukie wakati wa uchaguzi. Lugha rahisi hapa ni kuwa wanawanunua au kuwahonga!

Hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Juu kabisa nchini Kenya, ni moja ya hukumu zenye maono mapana na yenye maslahi mapana ili dhana ya kutenganisha mihili ya dola – Serikali, Bunge na Mahakama iweze kutekelezeka.

Hukumu hiyo kama ilivyokuwa uamuzi wa kutengua matokeo ya uchaguzi wa rais, ni changamoto/funzo kwa mahakama za Tanzania. Tangu lini mbunge akawa mfadhili ya miradi ya maendeleo? Ni kwa kiasi gani Mfuko wa Jimbo umeboresha maisha ya watu kwenye majimbo ya uchaguzi?

Ni kweli, upo umuhimu wa kupeleka fedha kwenye halmashauri na kwenye majimbo kwani ndiko waliko watu. Swali ni kwa nini Serikali iwagawie wabunge mafungu ya fedha? Uzoefu umeonyesha kuwa inapotokea kwamba majimbo yanasigana na misimamo ya wabunge na vyama vyao, wananchi huachwa solemba!

Mipango ya maendeleo ni suala la kitaifa. Kama kweli nchi inataka maendeleo sawia nchini kote, wabunge si jawabu la azma hiyo. Hii ni kwa sababu siyo siku zote malengo ya wanasiasa na vyama vyao yanaendana na matakwa ya wananchi.

Hali kadhalika, Mfuko wa Jimbo unaua dhana nzima ya kutenganisha majukumu miongoni mwa mihimili mitatu ya ya dola na kuimarisha uwajibikaji.

Ni vema wabunge wakaendelea kuisimamia Serikali na vyombo vyake kutimiza wajibu wake kwa kuisakama kwa maswali kwa niaba ya wapigakura wao. Wabunge waendelee na majukumu ya kuwapigania wapigakura wao kupitia mipango ya maendeleo iliyo rasmi na kurekebisha sera ya sheria zinazosimamia miradi ya maendeleo na siyo kuingia jikoni!

2670 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!