Kwa kipindi cha wiki tatu kumekuwa na vuguvugu la mgogoro kuhusu Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida (Ilongero).

Mgogoro huu unahusu hasa wapi yajengwe Makao Makuu ya Wilaya ya Ilongero. Uliibuka kuanzia tarehe Oktoba 28, 2016 baada ya Baraza la Madiwani  wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, kwa usiri mkubwa kupitisha azimio la kujenga Makao Makuu ya Halmashauri katika Kijiji cha Kinyamwambo, Kata ya Merya karibu na barabara kuu iendayo Babati na Arusha.

Azimio la Baraza la Madiwani lilipitishwa katika mazingira ya usiri mkubwa na kimyakimya kupindua uamuzi uliokwishafanyika serikalini kupitia ngazi zote za wilaya, mkoa na TAMISEMI.

Baada ya kutoa utangulizi hapo juu, sasa nitajikita kufanya uchambuzi ili kuwasaidia wadau wengine ambao hawajui ukweli wa jambo hili ili kuondoa ushabiki usiokuwa na tija.

Mgogoro huu wa makao makuu ya wilaya umeibua makundi mawili- kundi la kwanza linalalamika makao makuu yajengwe Mji Mdogo wa Ilongero kama ilivyoamuriwa na Serikali; na kundi la pili linatetea makao makuu yajengwe Kijiji cha Kinyamwambo, Kata ya Merya (hawa wanavutia kwao bila kujali hujuma kufanyika) na kumeibuka mabishano makali kupitia majukwaa ya Singida mtandaoni.

 

Kwanini makao makuu?

Lengo la kujenga makao makuu ya halmashauri ni kutokana na sababu kwamba ofisi za sasa za Halmashauri ya Wilaya ya Singida zipo ndani ya eneo la Manispaa ya Singida Mjini. Halmashauri ya Wilaya ya Singida kuwa na ofisi za utawala nje ya eneo lake la utawala imesababisha usumbufu kwa wananchi wa Singida Kaskazini kwa muda mrefu kwa kuwa huduma za kiutawala zipo mbali na hivyo inaweka umuhimu wa kujenga makao makuu ya Halmashauri ndani ya eneo lake la utawala.

 

Historia kuhusu wilaya za Mkoa wa Singida

Mnamo Novemba 10, 2006 Serikali ya Mkoa wa Singida kupitia Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC)  ilifanya mgawanyo wa wilaya saba (7) na kuamua kila wilaya wapi yajengwe makao makuu ya halmashauri na baadaye kupitishwa na TAMISEMI. Mgawanyo wa wilaya na makao makuu yake ni kama ifuatavyo :

1: Wilaya ya Mkalama -makao makuu yajengwe Nduguti

2: Wilaya ya Iramba- makao makuu yajengwe Kiomboi

3: Wilaya ya Itigi- makao makuu yajengwe Itigi

4: Wilaya ya Manyoni- makao makuu yajengwe Manyoni

5: Wilaya ya Ilongero – makao makuu yajengwe Ilongero

6: Wilaya ya Ikungi -makao makuu yajengwe Ikungi

7: Wilaya ya Singida – makao makuu yajengwe Singida

Kamati ya RCC Mkoa wa Singida iliamua kwa kuzingatia mapendekezo ya Mabaraza ya Madiwani na mapendekezo ya Kamati za Ushauri za Wilaya (DCC) toka pande zote kwa kuzingatia utaratibu wa kisheria.  Ikumbukwe kwamba RCC ni chombo cha juu cha uamuzi ndani ya mkoa husika kabla jambo halijaenda ngazi za juu serikalini.

 

Utekelezaji wa kila wilaya

Baada ya kupitishwa hili suala la mgawanyo wa wilaya, kila wilaya ilijielekeza kutekeleza maagizo ya Serikali kupitia TAMISEMI ikiwa ni pamoja na jina la wilaya na ujenzi wa makao makuu ya halmashauri.

Wilaya zifuatazo kupitia Mabaraza ya Madiwani walitekeleza kama ifuatavyo:

 1: Wilaya ya Manyoni

2: Wilaya ya Itigi

3: Wilaya ya Mkalama

4: Wilaya ya Iramba

5: Wilaya ya Ikungi

6: Wilaya ya Singida (Manispaa)

 Wilaya pekee ambayo haijatekeleza uamuzi wa serikali hadi muda huu ni Wilaya ya Ilongero ambayo kwa sasa wanaiita Halmashauri ya Wilaya ya Singida; na bado imejibana Singida Mjini huku ikiwahudumia wananchi wa Singida Kaskazini.

 

Kwanini wilaya ya Ilongero haijatekeleza?

Sababu pekee na ya kweli kabisa iliyotufikisha hapa ni maslahi binafsi ya genge hatari la viongozi (lobbyists)  wanaotumia pesa chafu kurubuni kila mtu ilimradi afuate matakwa yao.  Bahati mbaya sana kinara wa genge hili hatari ni kiongozi aliyepigiwa kura na wananchi ili asimamie maslahi ya wananchi wa Singida Kaskazini.

Genge hili hatari limekamata ngazi zote za uamuzi ndani ya Chama Cha Mapinduzi na Serikali ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida; na sasa kuna taarifa linajipenyeza ndani ya Serikali ya Mkoa wa Singida. Tangu mwanzo genge hili halikupenda makao makuu yajengwe Ilongero, likachelewesha utekelezaji (delaying tactics) ili wawe na nguvu kwenye Baraza la Madiwani wafanye mapinduzi ili makao makuu ya wilaya yakajengwe sehemu wanayoitaka, hasa maeneo karibu na Mgori, Ngimu, Merya, na Itaja.

Ghafla wakageuza ajenda kwa ujanja kwamba makao makuu ya wilaya yaliamuriwa yajengwe Tarafa ya Ilongero na haikutajwa kata au kijiji yatakapojengwa.  Wakatengeneza mkakati maalumu kupeleka Kijiji cha Kinyamwambo, Kata ya Merya mpakani kabisa mwa Tarafa ya Ilongero na Tarafa ya Mgori.

Genge hili hatari kila wakati wa uchaguzi ukiwadia linahakikisha madiwani wote wanaogombea ni watiifu kwao- hupewa msaada wa kifedha ili washinde na baadaye watii matakwa yao kwenye uamuzi mbalimbali unaohusu Halmashauri ya Wilaya ya Singida.

 

Mwito wangu kwa viongozi wa Serikali

Natoa mwito kwa viongozi wa Serikali- Wilaya na Mkoa wa Singida walioteuliwa na Rais John Magufuli,  kuwatumikia wananchi wa Singida waenende na watende kuendana na kasi ya Mheshimiwa Rais kuwa serikali hii ni ya wananchi wanyonge inayosimamia maslahi mapana ya wananchi, na siyo watu wachache wenye fedha.

Viongozi wa serikali mkiingia kwenye mtego wa genge hatari linalotumia pesa chafu kurubuni kila mtu ilimradi afuate matakwa ya kundi hilo, itakuwa ndio mwanzo wa usaliti kwa wananchi wa Singida na hakika maendeleo itakuwa ni ndoto ya sahau.

 

Mwito wangu kwa baraza la madiwani

 Hakika mmedhihirishia umma wa wananchi wa Singida Kaskazini kuwa Baraza lenu ni baraza kibogoyo kuliko mabaraza yote yaliyopita tangu tupate Uhuru. Baraza lenu limewekwa mfukoni na uamuzi wenu unaendeshwa kwa rimoti. Wananchi watakuwa sahihi kutokuwa na imani na Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Singida kwa kuwa hamsimamii matakwa ya wananchi wenu.

Kwanini hamkuwashirisha wananchi kabla ya kwenda kwenye Baraza kufanya uamuzi mkubwa wa kupindua uamuzi uliokwishafanyika?

Kwanini, baada ya kupitisha azimio lenu la kujenga Makao Makuu ya Halmashauri katika Kijiji cha Kinyamwambo hamjaenda kwa wananchi kuwaeleza mlichoamua?

Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Singida  mjitafakari upya na mkumbuke mlitumwa kusimamia maslahi mapana ya wananchi wa Singida Kaskazini.

 

Mungu huyu ni wa wote.

Nawasilisha.

 

Mwandishi wa makala hii, Alfred Ringi Nyalandu, ni msomaji wa JAMHURI. Anapatikana kupitia simu: 0713 272 701.

3585 Total Views 8 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!